Hii si vita ya Dk. Slaa pekee, ni yetu sote | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Hii si vita ya Dk. Slaa pekee, ni yetu sote

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BAK, May 6, 2009.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  May 6, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,550
  Likes Received: 81,990
  Trophy Points: 280
  Hii si vita ya Dk. Slaa pekee, ni yetu sote

  Mwandishi Wetu

  Tanzania Daima~Sauti ya Watu

  INASIKITISHA kuona viongozi wa ngazi za juu serikalini, hususan baadhi ya mawaziri wakisaidiana na baadhi ya wabunge wanaojifanya wako bungeni kuwawakilisha wananchi kutoka majimboni mwao, kumbe wako pale kwa masilahi yao binafsi.

  Ni mawaziri wanaojifanya kuzungumza kwa niaba ya serikali, serikali kwa niaba ya wananchi.

  Ni jambo la ajabu kabisa kusikia katika nchi yoyote ile duniani akatokea mtu mmoja anaewapigania wanyonge dhidi ya ufisadi wa watu wachache, ghafla mtu huyo aonekane ni adui mkubwa wa wananchi hao hao anaowapigania.

  Hapa inadhihirisha vita anayoipigania mpambanaji huyu ilikuwa haiungwi mkono na kundi linalojifanya liko pale bungeni kuwapigania wananchi wao.

  Kumbe liko pale kujipigania lenyewe na familia zao, ndugu na marafiki zao.

  Kamwe hawawezi kutuaminisha wako pale kwa masilahi ya wananchi wao.

  Tujikumbushe kuhusu wabunge wetu wakati wanaingia bungeni mwaka 2006.

  Kabla hata ya kuanza kazi iliyowapeleka pale walianza kwa kudai nyongeza ya mishahara.

  Wananchi na wanaharakati wote nchi nzima walikipinga kitendo kile, wengi waliamini zoezi lile lilisitishwa.

  Lakini kwa matukio ya hivi karibuni yanavyojieleza, zoezi lile lilitekelezwa kimya kimya kwa kuwaongezea wabunge mishahara.

  Hilo linaweza kuthibitishwa kwa jinsi wabunge walivyotaharuki mwenzao mmoja Dk. Wilibrod Slaa, Mbunge wa Karatu alivyowaelezea wananchi wa jimboni kwake akiweka bayana kiasi wanacholipwa na kusema mishahara yao wabunge ni mikubwa sana na inafaa ipunguzwe.

  Kutokana na hali hiyo kumeibuliwa hoja ya kutaka serikali iwachukulie hatua kali, ikiwa ni pamoja na kuwashitaki wale wote wanaotumia nyaraka za siri za serikali kwa manufaa ya kujipatia umaarufu wa kisiasa, kama ambavyo hao wenye kumtuhumu mpiganaji wetu wanavyodai.

  Mtazamo wangu hapa, mlengwa moja kwa moja ni Dk. Slaa. Serikali imepanga vilevile mikakati ya kutaka kuwabaini ni maofisa gani serikalini wanaozitoa hizo nyaraka za siri na kuwapatia hao wanaozifanyia kazi.

  Kwa kuwa mtazamo huu haukulenga kuongelea nyaraka za siri hasa, bali ni hiyo mishahara ya wabunge na viongozi wa ngazi za juu serikalini.

  Ebu tuangalie ni kitu gani hasa kimewafanya wabunge wataharuki walivyosikia taarifa za mishahara na posho zao zikiwekwa hadharani?

  Wametukumbusha kile walichokuwa wakikililia tangu walivyoingia bungeni mwanzoni mwa utawala wa Awamu ya Nne kuhusu nyongeza za mishahara yao.

  Wanadiriki kutamka wazi kwamba mishahara yao ni midogo ukilinganisha na mishahara ya wabunge wa mabunge mengine.

  Hoja ya ajabu kabisa, hoja za wabunge bungeni na hata nje ya Bunge.

  Wabunge wanaotaka kutambulishwa kwa majina ya vyeo vyao vya kisomi kama vile Profesa, Dk. na siku hizi hata wengine wanataka kutambulishwa kwa kuanza na taaluma zao, mfano mara nyingi tunasikia Injinia, kwani ukiitwa Mh. Mbunge fulani hautatambulika?

  Basi na wahasibu nao watambulishwe kwa kuanzia na Mhasibu Mh. Buhari Choka Mbaya, Mkandarasi fulani, Msanifu Majengo fulani, Mwalimu fulani n.k.

  Mtazamo wangu ni kwamba wabunge wa namna hiyo waache ulimbukeni.

  Kwanza wewe kama injinia unafanya nini bungeni? Wabunge wa namna hiyo si walipaswa kwenda kuitumia taaluma yao muhinu sana kuiletea nchi maendeleo mijini na vijijini?

  Kwa nini wasiende wakasimamie ujenzi wa mabarabara, kufufua viwanda vyetu, mashule, hospitali n.k. badala ya kwenda kuzilaza taaluma zao muhimu sana bungeni?

  Ndiyo maana wananchi wanasema baadhi ya wabunge wamefuata na wako pale kwa masilahi yao binafsi.

  Kuna hoja ya wabunge kupenda kulinganisha mishahara yao na wabunge wa nchi nyingine.

  Kwa nini hawatumii nafasi hiyo wao kama wawakilishi wa wananchi kulinganisha mishahara ya askari, walimu, madaktari, wauguzi na watumishi wengine serikalini kwa kulinganisha na wa nchi nyingine?


  Mishahara ya watumishi wa umma imekuwa ikilalamikiwa sana lakini wabunge hawa hawalioni hilo, wanajali masilahi yao tu.

  Mbona hawatuambii ubora wa uchumi, ukubwa wa nchi, idadi ya watu wa hizo nchi wanazojilinganisha nazo na kadhalika?

  Wanataka mishahara yao kuwa siri, wananchi wasijue, kwa kuwa wakijua watataharuki.

  Wabunge wanaendelea kumtuhumu Dk. Slaa kwa kusema anawachonganisha na wapiga kura wao.

  Niwaulize wabunge wa jinsi hiyo, hivi hao wapiga kura wenu ni wa aina fulani ya watu mmewaseti, mnapanga nini cha kuwaambia ili mradi hawavurugi wala kuingilia masilahi yenu?

  Kwa hiyo mnawaumiza walipa kodi halafu hamtaki wajue, sasa wamejua, mnasema mnachonganishwa nao?


  Hivi ni kosa gani kwa walipa kodi kujua mnalipwa kiasi gani? Achilia wabunge, wananchi pia wanataka kujua rais wa nchi analipwa kiasi gani kwa mwezi.

  Na ni gharama kiasi gani zinatumika kumkimu awapo madarakani kwa siku, wiki mwezi na hata mwaka, au anaposafiri nje au ndani ya nchi, ni kiasi gani cha fedha hutumika?

  Kwa mtazamo wangu, ziko gharama nyingi zimejificha hazionekani wala kujulikana, ikiwa ni pamoja na marupurupu.


  Na rais huwa anatumia kiasi gani pindi anapomaliza kipindi chake cha utawala wa miaka tuseme kumi? Ni haki yetu sisi walipa kodi kufahamu.

  Mtazamo wangu ni kwamba gharama za rais ziwekwe bayana ikiwa ni pamoja na wananchi wajulishwe gharama za makamu wa rais, waziri mkuu, mawaziri, manaibu mawaziri, makatibu wakuu na manaibu wao.

  Na hata wakurugenzi wa idara mbalimbali, wakuu wa majeshi, wakuu wa mikoa na wilaya.

  Hata Mwanasheria Mkuu wa serikali na watumishi wengine wa vyeo vya juu serikalini na taasisi za umma akiwemo Gavana wa Benki Kuu.

  Ni haki ya walipa kodi kujua, na kwa njia hiyo angalau kutasaidia kujua baadhi tu ya matumizi ya serikali tunayoambiwa kila siku haina fedha lakini hakuna aliye tayari kutaja au kueleza ukweli fedha zinatumika vipi, manake hicho ndicho wabunge, mawaziri na viongozi wengine serikalini wanataka kibakie kuwa siri.

  Tangu lini matumizi ya fedha za walipa kodi yakawa siri? Wananchi wanahitaji kujua kodi wanazolipa pamoja na umaskini walionao zinatumika namna gani.

  Hapa bado hatujahoji fedha zinazopelekwa kwenye miradi mbalimbali, hapana, tujue mishahara yao tu na fadhila zingine zinazowazunguka ikiwemo matibabu, elimu kwa watoto wao kama anastahili, gharama za nyumba, simu, maji, umeme, magari, mafuta gharama za safari, vikao mbalimbali nk.


  Nakumbuka kipindi kile cha uchaguzi wa mwaka 1995 katika baadhi ya mikutano yake, Augustine Mrema wakati ule akiwa NCCR Mageuzi alitamka juu ya viongozi waliokuwa wakilipwa fedha nyingi serikalini.

  Alisema Mwanasheria Mkuu wa serikali kipindi hicho alikuwa akipokea sh mil. tisa kwa mwezi, sasa cha kujiuliza, leo ni zaidi ya miaka 13 imepita, mwanasheria atakuwa akipokea kiasi gani?

  Kwa mtazamo wangu, sisi wananchi tungependa kujua zaidi kuhusu mishahara ya wabunge, maana kilichotamkwa ni mshahara tu, bado kuna posho nyingine nyingi wanazozipata lakini hazijawekwa wazi.

  Katika Bunge la bajeti la mwaka jana 2008/9, kulikuwa na hoja iliyokuwa ikijadiliwa na wabunge ya kutaka wakatiwe bima za maisha wao na familia zao, sijui suala hilo limefikia wapi, linaweza likapitishwa tena katika usiri kama huu huu wa mishahara ulivyotekelezwa ili wananchi wasijue.

  Angalia ubinafsi wa wabunge wanaojifanya wako pale kuwawakilisha wananachi wakati wako pale kujiwakilisha na kujipigania wenyewe.

  Kama ambavyo tumesikia mishahara ya wabunge, vipi hao wabunge ambao ni mawaziri?

  Wanapokea mishahara miwili? Je, hao ambao kote huko wako na kwenye bodi mbalimbali wapo na wanajilipa vinono inakuwaje?

  Ikiwa hali ndiyo hiyo, mtumishi mmoja wa umma au serikali anajinyakulia zaidi ya sh milioni 15 kwa mwezi na huku serikali hiyo iliyomwajiri inatangaza baa la njaa, kwa wananchi wake maskini wa kutupwa.


  Hivi inaingia akilini mwetu na kwa wanaotutizama hususan hao tunaowakimbilia kila siku kwenda kuomba?

  Mtazamo wangu ni kwamba wenye taarifa zaidi zinazoitwa siri zinazohusu mishahara na marupurupu mengine ya aina ya viongozi wa ngazi za juu serikalini na taasisi za umma wazianike hadharani wananchi wapate kujua ukweli wa usemi usemao ukila na kipofu usimshike mkono.

  Hakika kama tutafanikiwa kukigeuza hicho kinachoitwa kuwa ni siri, hususan linapokuja suala la matunizi ya fedha za umma kuwa wazi na tukafanikiwa kudhibiti hali hiyo kwa kuungana na shujaa Dk. Slaa na wapiganaji wengine, ni lazima tutafanikiwa na maendeleo yatapatikana.

  Hapa wameguswa wabunge tu, wako watumishi wengi serikalini na taasisi za umma hawajaguswa, hakika na wenyewe watakapoguswa watahamaki, hao ni pamoja na mawaziri, ndiyo maana wanataka matumizi yao na mishahara iwe siri.

  Huwezi kudhibiti kitu usichokijua, hivyo wahusika wote kwa pamoja watafanya kila wawezalo matumizi hayo yasijulikane.

  Wanatuficha sisi walipa kodi tusijue kodi zetu zinatumikaje.

  Vita hii si ya Dk. Slaa pekee, ni yetu sote, tumuunge mkono kwa nguvu zote.
   
 2. D

  Diana Member

  #2
  May 6, 2009
  Joined: Apr 29, 2009
  Messages: 9
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  I don't think why those people don't fill ashamed of themselves, due to this mess, using the money of hard working people who especial get a very low wage of sallary and been deducted 13% amount of their money, and them whom they called themselves leader taking without fear of God!! Now it's time to speak out!!! but then who will going to hear our voice???? this is the qns to ask ourself!! Mafisadi wameanzia huko ngazi za juu so without God nothing will change, tupate viongozi toka kwa Mungu!? watakaokuwa na hofu ya Mungu, Our trust to JK was danganya toto??? Poor Tanzanian!!! this is too bud
   
Loading...