Haijathibitishwa
- Tunachokijua
- Kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006, kifungu cha 26, Benki Kuu ya Tanzania ndiyo chombo chenye jukumu la kutoa sarafu na noti halali (legal tender) zinazotumika nchini. Katika kutekeleza jukumu hili Benki Kuu hutoa noti na sarafu zenye uwiano mzuri wa thamani (denominations) unaozingatia uwezekano wa zile zenye thamani kubwa kuweza kugawinyika katika zile zenye thamani ndogo.
Sheria ya benki kuu ya mwaka 2006 inaweka wazi kuwa Utengenezaji wa noti au sarafu hutumia miundo na alama ambazo ni lazima zipitishwe na waziri wa fedha. Wakati wa kutoa noti na sarafu, Sheria hii inaitaka Benki kuu kutoa tangazo katika Gazeti la serikali kuhusu makundi ya fedha na sifa zingine za noti na sarafu kabla ya kusambazwa kwa matumizi.
Noti ya shilingi elfu kumi ambayo sasa inatumika katika mfumo wa malipo ni toleo la mwaka 2010 ikiwa ni baada ya toleo la mwaka 2003.
Mnamo tarehe 08/02/2024 Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Vijana Ng’wasi Kamani Bungeni jijini Dodoma, aliyetaka kujua ni lini Serikali itaweka kumbukumbu ya kudumu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka picha yake kwenye fedha za Nchi na kutambua mchango wa Rais wa kwanza Mwanamke Tanzania
Waziri Mkuu, Majaliwa Alisema serikali imeupokea na itaujadili ushauri wa kuweka kumbukumbu ya kudumu kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hasssan kwa kuweka picha yake kwenye fedha za Tanzania ikiwa ni heshima ya kuwa na Rais wa kwanza Mwanamke anayefanya kazi nzuri na kutambua utendaji wake.
Kumekuwepo na taarifa ikionesha mfano wa noti ya shilingi elfu kumi ambayo imekuwa ikisambaa mtandaoni huku ikiwa na picha ya Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Rais wa awamu ya sita Samia Suluhu Hassan. Noti hiyo imekuwa ikisambazwa mtandaoni na huku ikielezwa kuwa inatarajiwa kutumika hivi karibuni kwa ajili ya malipo halali ya fedha za kitanzania.
Taarifa hiyo inayosambaa mtandaoni inapatikana hapa na hapa.
Uhalisia wa jambo hili ni upi?
Ufuatiliaji wa kina uliofanywa na JamiiCheck umebaini kuwa taarifa hiyo si ya kweli kwani umebaini madhaifu kadhaa katika noti hiyo ikiwemo kukosewa kwa neno ‘Shillings’ ambalo limeandikwa ‘shilings’
Aidha, utaratibu wa kisheria unaitaka Benki kuu kuchapisha tangazo kwenye gazeti la serikali juu ya kutoa noti au sarafu mpya kabla ya kuanza kwa matumizi jambo ambalo halijafanyika kwa noti hiyo inayosambaa mtandaoni.
Hata hivyo kupitiaa kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii Benki kuu ya Tanzania imekanusha hiyo taarifa na kwamba si taarifa ya kweli ni vema ikapuuzwa huku naye waziri wa fedha Dr. Mwigulu Nchemba kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X amekanusha uwepo wa taarifa hiyo na kuwa si ya kweli.