Hii ndiyo nguvu kubwa iliyopo ndani yako ambayo ukiijua na kuanza kuitumia utakuwa na maisha bora sana

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,897
3,337
“Matatizo yote ya binadamu chanzo chake ni mtu kushindwa kukaa peke yake kwenye chumba bila ya kuwa na kitu cha kufanya.” Hii ni kauli ambayo ilitolewa na mwanahisabati, mwanafalsafa na mwandishi Blaise Pascal mwaka 1654.

Unaweza kusema kauli hiyo ni ya zamani na haina ukweli kwenye zama tunazoishi sasa. Lakini utakuwa umekosea sana, kwa sababu utafiti uliofanyika mwaka 2014, umeweza kudhibitisha kauli hiyo.

Mwaka 2014 kulifanyika utafiti ambapo watu walipewa jukumu moja tu, kukaa kwenye chumba peke yao na kufikiri. Chumba hicho hakikuwa na kitu chochote kile, bali nyaya za umeme ambazo mtu akizishika anapigwa shoti na kuumia.

Kabla ya kuingia kwenye chumba hicho, watu waliulizwa kama wapo tayari kushika nyaya hizo za umeme na kupigwa shoti, wote walisema hawapo tayari kuzishika.

Hivyo waliwekwa kwenye chumba hicho na kuachwa, kwa dakika 15 mpaka 25 bila ya kitu cha kufanya, bali kufikiri tu.

Baada ya kuachwa kwenye chumba hicho kwa muda, asilimia 67 ya wanaume na asilimia 25 ya wanawake walizishika nyaya za umeme na kupigwa shoti.

Tena wengine walifanya hivyo zaidi ya mara moja. Waendeshaji wa utafiti huu walijumuisha kwamba, watu huwa hawapo tayari kukaa bila ya kuwa na kitu cha kufanya, watafanya hata kitu kinachowadhuru lakini siyo kukaa kwa upweke.

Rafiki, hili halishangazi, kwa sababu zama tunazoishi sasa, ni zama zenye kelele ya kila aina. Simu janja tunazotembea nazo kila mahali, ni chanzo kikuu cha usumbufu kwenye maisha yetu.

Ukiwa umekaa karibu na mtu na simu yake ikaita, utaangalia na yako pia. Ukipata dakika chache za kuwa mpweke, haraka sana utakimbilia kuangalia simu yako, kuingia mitandaoni, kufuatilia habari na kadhalika.

stillness is the key.jpg


Matatizo makubwa uliyonayo kwenye maisha yako, ni matokeo ya kushindwa kukaa peke yako kwenye eneo tulivu na kufikiria bila ya kuwa na usumbufu wa aina yoyote ile.

Huu ni ukweli ambao wengi hawajawahi kupata nafasi ya kuujua, lakini wewe umepata nafasi hiyo leo, hivyo itumie vizuri.

Ipo nguvu moja kubwa sana iliyopo ndani yako, ambayo ukiijua na kuanza kuitumia, utaweza kutatua kila aina ya tatizo ulilonalo, itaweza kuzuia usitengeneze matatizo mapya na itakuwezesha kuwa na maisha bora na yenye utulivu mkubwa.

Nguvu hiyo ni muhimu sana kwenye zama tunazoishi sasa, zama ambazo tumezungukwa na usumbufu mpaka kwenye vitanda vyetu.

Hivi unaweza kuamini kwama zaidi ya asilimia 90 ya watu wanalala na simu zao, tena zikiwa wazi na hivyo kuruhusu usumbufu wowote kuwafikia, hata kama wamelala?

Na je unajua asilimia zaidi ya 80 ya watu kitu cha kwanza wanachofanya wanapoamka ni kuangalia simu zao, kujua nini kimeendelea duniani ili wasipitwe?

Unaweza kuona hayo ni maendeleo, lakini kwa hakika siyo maendeleo, ni kinyume kabisa na maendeleo, ni mtu kujirudisha nyuma, kwa sababu mtu anaianza siku akiwa amevurugwa badala ya kuianza siku kwa utulivu ambao utamwezesha kufanya makubwa.

Nguvu kubwa ambayo unakwenda kujifunza hapa ni UTULIVU, kuweza kukaa peke yako eneo tulivu na kufikiri, bila ya kuruhusu usumbufu wowote ukuondoe kwenye utulivu wako.

Hii ni nguvu kubwa mno, ambayo tayari ipo ndani yako, unachopaswa kujua ni jini ya kuifikia na kuanza kuitumia.

Mwandishi Ryan Holiday kwenye kitabu chake kipya kinachoitwa STILLNESS IS THE KEY amejadili kwa kina sana kuhusu dhana hii ya UTULIVU, ametuonesha jinsi ambavyo ni muhimu, jinsi ambavyo viongozi wakubwa, watu wa dini, falsafa na hata waliofanikiwa sana waliweza kutumia nguvu hii ya utulivu kufanya makubwa.

Ukiangalia Falsafa zote kubwa duniani na hata wanafalsafa wakubwa, walikuwa na utaratibu wa kutenga muda wa kukaa peke yao bila ya kuruhusu usumbufu wowote na kufikiri kwa kina.

Hata kwenye dini kubwa duniani, mfano Ukristo, Uislamu na Ubudha, wale ambao dini hizi zimeanzishwa kupitia wao, walipenda kupata muda ya kuwa peke yao. Yesu (Ukristo), Mohamad (Uislamu) na Gautama (Ubudha) katika vipindi vyao, walikuwa na utaratibu wa kuyaacha mazingira yao, kuwaacha wafuasi wao na kwenda milimani au msituni peke yao na kupata muda wa kuwa tulivu, kufikiri na kutafakari kwa kina.

Ni katika nyakati hizo za UTULIVU na kutafakari ndipo viongozi hao waliweza kupata ufunuo na uamsho ambao umekuwa msingi wa dini hizo.

Nguvu hii pia ipo ndani yako, lakini umeidumaza kwa sababu kila siku umekuwa unakimbia mazingira yanayokuacha wewe na fikra zako tu.

Kwenye kitabu chake Ryan anatuambia UTULIVU ni ufunguo wa vitu vingi sana kwenye maisha, baadhi ya vitu hivyo ni kama;

Kufikiri kwa umakini na kwa ufasaha.

Kuweza kuuona mchezo mzima pale unapokuwa na ushindani.

Kufanya maamuzi magumu.

Kudhibiti hisia zako.

Kuweza kuyajua malengo sahihi kwako.

Kuweza kukabiliana na hali zenye msongo mkubwa.

Kuweza kuimarisha mahusiano yako na wengine.

Kujijengea tabia bora.

Kuongeza ufanisi na uzalishaji wako.

Kuweza kufurahia hali unayopitia, bila ya kujali ni hali gani.

Utulivu ni ufunguo wa kila kitu kwenye maisha, hakuna kitu chochote ambacho ufunguo huu hauwezi kufungua pale kinapokuwa kimefungwa.

Kama unataka kuwa mzazi bora, msanii bora, mfanyakazi bora, mfanyabiashara mwenye mafanikio, mwekezaji mkubwa, mwanamichezo mkubwa, mwanasayansi bora au hata kuwa mtu bora, ufunguo pekee unaoweza kuutumia kufika huko ni UTULIVU.

Jijengee tabia ya kuwa na muda wa utulivu kwenye kila siku yako, muda ambao unakaa wewe peke yako na mawazo yako, na hakuna usumbufu wowote unaokuwa karibu na wewe katika wakati huu.

Hili ni zoezi gumu sana katika zama hizi, lakini linawezekana kama ukiamua, anza na muda mdogo kama wa dakika 15 mpaka 30, kisha endelea kuongeza muda huo kadiri unavyokwenda. Mwanzoni litakuwa zoezi gumu sana, utakapokaa tu utaanza kufikiria vitu vingi ambavyo ungeweza kuwa unafanya, mambo mazuri yanayoendelea mtandaoni ambayo yanakupita, lakini usiruhusu hayo yakuondoe kwenye utulivu wako.

Anza zoezi hili na utaona jinsi ambavyo maisha yako yataanza kubadilika na kuwa tulivu na bora zaidi. Msongo utapungua, wasiwasi na mashaka ya kupoteza vitu yataondoka kabisa na utajiona unayaendesha maisha badala ya maisha kukuendesha wewe.

Kwenye uchambuzi wa kitabu cha juma hili, tutakwenda kujifunza kwa kina kutoka kwenye kitabu hiki cha STILLNESS IS THE KEY, tutaona jinsi ya kupata utulivu wa AKILI, ROHO na MWILI, kuna hatua mbalimbali za kuchukua ili kupata utulivu kwenye maisha yetu kwa kuanzia maeneo hayo matatu yanayotengeneza utu wetu.


Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.
 
Mada nzuri. Unaweza kujaribu kuwa pekee yako sehemu tulivu na kwa utulivu cha kushangaza mawazo yatakayokuwa yanazunguka kichwani maisha kwa ujumla mara unaweza ukipata hela utafanya hili mara lile. Ghafla mawazo yanahamia kwa extended family yaani vurugu kichwani baada ya nusu saa unajikuta kichwa kimejaa. Daah
 
Kuna muda mtu unaweza kukaa pekee ili uwe creative.. huo ndio muda wa kujenga dunia yetu,ndio mafanikio ya mawazo yalipolala pia Ni charge ya akili kabla ya kukutana na jamii.
Kabia,
Mwandishi mmoja amewahi kusema kama kungekuwa na instagram enzi za Newton huenda asingeweza kugundua nguvu ya mvutano ya dunia. Maana wakati amekaa kwa utulivu chini ya mti na kuona tunda linadondoka chini, ndiyo alijiuliza kwa nini linadondoka chini na lisiende juu. Lakini kwa ulimwengu huu wa sasa, mtu akikaa mahali akili yote ipo kwenye simu. Ni vigumu sana kupata mawazo mazuri kwenye zama hizi kama mtu hutaweka juhudi.
 
Nadhani kilicho katika Mada kinafanana na kufanya meditation

Mada nzuri ahsante mleta Mada
Ni kweli,
Meditation(Tahajudi) ni sehemu ya utulivu, lakini siyo kila utulivu ni meditation.
Unaweza kukaa peke yako na mawazo yako lakini siyo kwa lengo la kufanya meditation.
Kwa sababu lengo kuu la meditation ni kudhibiti mawazo yako kwa kuyaelekeza eneo moja ili kupata utulivu wa akili.
Lakini kwenye utulivu mwingine unaweza kuruhusu mawazo yako yazurure yawezavyo, au ukawa unatafakari mambo ya nyuma.
 
Mada nzuri. Unaweza kujaribu kuwa pekee yako sehemu tulivu na kwa utulivu cha kushangaza mawazo yatakayokuwa yanazunguka kichwani maisha kwa ujumla mara unaweza ukipata hela utafanya hili mara lile. Ghafla mawazo yanahamia kwa extended family yaani vurugu kichwani baada ya nusu saa unajikuta kichwa kimejaa. Daah
Hilo ni zeri, kwa sababu linaibua vitu ambavyo vipo ndani yako na unaweza kukabiliana navyo. Kwa sababu mara nyingi tumekuwa tunakimbia matatizo yaliyo ndani yetu kwa kujiweka kwenye usumbufu. Sasa unapoweka usumbufu pembeni na kukabiliana na uhalisia, utaweza kuona hatua sahihi ya kuchukua.
 
Mada nzuri,nitaiongeza hii kwenye ratiba yangu ya kila siku,sasa sijui hapa nianze na lipi,yaani lipi liwe la kwanza na lipi liwe la mwisho.Mimi nikiamka nimejiwekea utratibu sifungui simu yangu zaidi ya kuanza na kusoma Bible,at least chapter 3,then nafanya maombi atleast nusu saa,then ndio nafungua simu yangu,sasa nataka niongeze hii ya kuwa na utulivu wa nusu saa,nipe ushauri nianze na lipi,nianze na utulivu kwanza au utulivu uwe wa mwisho...?
 
Ni kweli,
Meditation(Tahajudi) ni sehemu ya utulivu, lakini siyo kila utulivu ni meditation.
Unaweza kukaa peke yako na mawazo yako lakini siyo kwa lengo la kufanya meditation.
Kwa sababu lengo kuu la meditation ni kudhibiti mawazo yako kwa kuyaelekeza eneo moja ili kupata utulivu wa akili.
Lakini kwenye utulivu mwingine unaweza kuruhusu mawazo yako yazurure yawezavyo, au ukawa unatafakari mambo ya nyuma.
Nakubaliana nawe
 
Mada nzuri,nitaiongeza hii kwenye ratiba yangu ya kila siku,sasa sijui hapa nianze na lipi,yaani lipi liwe la kwanza na lipi liwe la mwisho.Mimi nikiamka nimejiwekea utratibu sifungui simu yangu zaidi ya kuanza na kusoma Bible,at least chapter 3,then nafanya maombi atleast nusu saa,then ndio nafungua simu yangu,sasa nataka niongeze hii ya kuwa na utulivu wa nusu saa,nipe ushauri nianze na lipi,nianze na utulivu kwanza au utulivu uwe wa mwisho...?
Ingawa sijaulizwa Mimi ila hili liweke mwisho, ratiba yako iko vzr nimeipenda
 
Ukikaa peke yako mara nyingi ni mawazo ya madeni tuu na jinsi gani ya kudeal na michepuko ya mzee ukichoka hayo unawaza siku ukifa itakuwaje lol utaiachaje familia yako.😊😀
 
Mada nzuri,nitaiongeza hii kwenye ratiba yangu ya kila siku,sasa sijui hapa nianze na lipi,yaani lipi liwe la kwanza na lipi liwe la mwisho.Mimi nikiamka nimejiwekea utratibu sifungui simu yangu zaidi ya kuanza na kusoma Bible,at least chapter 3,then nafanya maombi atleast nusu saa,then ndio nafungua simu yangu,sasa nataka niongeze hii ya kuwa na utulivu wa nusu saa,nipe ushauri nianze na lipi,nianze na utulivu kwanza au utulivu uwe wa mwisho...?
Vizuri mkuu kwa utaratibu huo mzuri ambao umekuwa unaufanya kwenye asubuhi yako.
Huwa nashauri kila mtu atenge masaa mawili ya kwanza kwenye siku kwa ajili yake yeye mwenyewe,
Nusu saa ya kwanza anafanya sala au tahajudi,
Nusu saa ya pili anaandika malengo yake, mipango ya siku pamoja na kupata muda wa kuwa tulivu na kutafakari.
Nusu saa ya tatu kusoma kitabu au kitu chochote kwa maendeleo binafsi.
Na nusu saa ya nne kufanya mazoezi ya viungo.
Kama masaa mawili haiwezekani basi saa moja unaigawa kwa dakika 20 au 15.
Kila la kheri.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom