Hii ndio sababu kwanini utaoa/olewa na mtu asiye sahihi

Underthesea

JF-Expert Member
Jul 8, 2021
327
882
(usomaji wa dakika 7)

Wangapi wanaweza kukiri kuwa wanahisi wameoa/wameolewa na mtu asiye sahihi?
images (67).jpeg


Basi mimi nipo hapa kutoa ushauri nasaha pamoja na faraja kwenu.

Unajua watu wengi tuna hasira tulizozibeba ndani yetu juu ya mahusiano yetu ya kimapenzi, jinsi mahusiano yetu yalivyoenda.

Leo kazi yangu ni kugeuza hasira hiyo kuwa huzuni. Ukiweza kugeuza hasira kuwa majonzi, unakuwa umepiga hatua kisaikolojia.

Mara nyingi huwa tunafikiri mtu mwenye hasira ni mtu flani muovu, au mtu mwenye kukata tamaa kirahisi. Si kweli!! Ukichunguza vizuri utagundua kuwa ndani ya mtu ambaye hukasirika mara kwa mara, kuna mtu flani mwenye matumaini makubwa! Yaani matumaini huzaa hasira!

images (85).jpeg


Fikiria mtu ambaye hupiga kelele kila akitafuta funguo zake, au akiwa amekwama kwenye foleni barabarani. Mtu huyo huonyesha kuwa na Imani (ingawa ya kizembe) ya dunia ambayo funguo huwa hazipotei na barabara ziko wazi tu muda wote.

Kwahiyo ili tupunguze hasira tuliyonayo juu ya mahusiano yetu inabidi tupunguze baadhi ya matumaini tuliyonayo juu ya mapenzi.

Ni vigumu sana kupunguza matumaini hayo kwasababu kwanza kuna biashara nyingi zilizoundwa kwa ajili ya kuongeza matarajio yetu juu ya mapenzi.

Mwanafalsafa mmoja mjerumani Theodore Adorno miaka ya 60 alisema "Mwanaume wa hatari kuliko wote Marekani ni Walt Disney" (producer mkubwa wa filamu za vibonzo). Adorno alisema hivyo kwasababu alimuona Disney kuwa wakala mkuu wa matumaini kupitia filamu zake, kwahiyo alikuwa wakala wa hasira na wa uchungu.

images (66).jpeg


Kwahiyo mwanafalsafa huyo aliona ni kazi ya wanafalsafa kuua matumaini ya watu taratibu, kitu ambacho ndo nitafanya hapa sasa hivi.

Kama kichwa kinavyosema, Kwanini Utaoa/olewa na Mtu Asiye Sahihi? au inawezekana ushaoa/olewa na mtu huyo tayari.

Kwanza tambua ni kuwa si jambo baya sana kwasababu wote hapa hatutapata mtu sahihi, sanasana tunaweza kupata anayeridhisha (good enough), na utakuwa umefanikiwa, kama tutakavyoona baadae.

Sababu ya kutopata mtu sahihi kama tulivyokuwa tunategemea wakati tunakua, wakati wa utineja wakati tunatafakari mapenzi, ni kuwa sisi ni viumbe wa ajabu. Tunaweza tusitoke nje na kufanya vitu vya ajabu au vya hatari lakini bado sisi kisaikolojia ni wa ajabu.

images (80).jpeg



Na huwa hatutambui jinsi tulivyo wa ajabu hadi baadae saana, ambapo tutaanza kujielewa na kuona jinsi ilivyo ngumu kuishi na sisi.

Wangapi humu wanahisi wao ni watu rahisi kuishi nao?? Wengi watasema wao ni wa rahisi kuishi nao lakini ukweli ni kuwa sisi sote ni wagumu. Na ni kwasababu sisi ni Binadamu!

Huwa kuna ukuta flani wa ukimya unaotuzunguka unaofanya iwe vigumu kwetu kujua ni nini kuhusu sisi kinachofanya iwe ngumu kuishi na sisi.

Marafiki hawataki kutuambia, wanaona ah kwanini nijisumbue me nataka ku enjoy basi. Marafiki wetu wanazijua zaidi kasoro zetu kuliko sisi na walizijua ndani ya dakika kumi tu ya kuanza urafiki. Mtu mliyekutana tu msiyejuana anaweza kujua kasoro zako haraka kuliko ambavyo wewe utajijua ndani ya miaka 40 ya maisha yako.

images (77).jpeg


Uwezo wetu wa kutambua kasoro zetu ni mdogo sana.

Wazazi wetu nao hawatuambii. Wametuona tangia wachanga wanajua sana tuna matatizo gani lakini ah wanatupenda sana kwanini watuambie.

Ma Ex ndo kabisa. Hawa ndo vyanzo muhimu sana. Wanajua kabisa una matatizo gani. Saa nyingine mnaachana tu kwa amani na hatokwambia una matatizo, lakini jua kuwa aliona matatizo mengi sana akasema tu ngoja nijiondokee ya nini kujisumbua kuanza kumuelezea matatizo yake.

images (86).jpeg



Kwahiyo Kuna habari fulani, ukweli fulani ambao unajulikana huko duniani lakini hauko ndani yako, huujui, hivyo tunaenda huko duniani tukiwa na uwezo mdogo sana wa kutambua tuna kasoro gani.

Unajua sisi sote ni waraibu (addicts). Sipendi kufafanua uraibu kwa kutaja kitu unachotumia mfano madawa ya kulevya. Inabidi uraibu ufafanuliwe upya.

Uraibu ni tabia ambazo zinajitokeza kwasababu unashindwa kukaa peke yako, na mawazo yako na hisia zako zinazokuwepo ukiwa peke yako, ambazo hukufanya uwe na wasiwasi (uncomfortable).

Kwahiyo unaweza kuwa na uraibu na kitu chochote mradi kinakengeusha fikra kutoka kwako.

Na Kwa teknolojia na vikengeusha fikra vya siku hizi, unaweza kujihakikishia kabisa kuwa unaweza kuishi maisha yako yote bila kuwa na muda wa kuwa peke yako kabisa!

images (87).jpeg



Na hili ni TATIZO linaloathiri uwezo wako wa kutengeneza mahusiano na mtu mwingine, kwasababu huwezi kutengeneza mahusiano mazuri na mtu mwingine kabla hujajijua mwenyewe.

Moja ya sababu kwanini Mapenzi ni magumu kwetu ni kwasababu yanahitaji tufanye kitu kimoja kigumu ambacho hatutaki kufanya. Nacho ni kumfuata binadamu mwenzio na kumwambia "Nakuhitaji", "Nisingeweza kuishi bila wewe", "Mimi ni dhaifu mbele yako".

images (89).jpeg


Na ndani yetu huwa kuna msukumo unaotufanya tujizuie, tuwe wakakamavu, tujihami na tusionyeshe udhaifu wetu kwa mtu mwingine.

Wanasaikolojia wanasema kuna aina mbili za muitikio ambao watu huonyesha wakijikuta kwenye hali hatari ambapo wanahitaji wawe dhaifu sana (vulnerable) na kujionyesha kwa mtu mwingine.

Muitikio wa kwanza, mtu anakuwa anajiambatisha kwa wasiwasi (Anxiously attached). Yaani badala ya kusema maneno kama "Nakuhitaji", "Nakutegemea", anapeleka mambo kiutaratibu (procedural). Atasema "Umechelewa dakika 10" au "Uchafu huu unahitaji kutolewa nje", yaani anaanza kuwa mkali. Lakini anachotaka kusema hasa ni "Bado unanijali?" Lakini hataki kutamka maneno hayo, badala yake anakuwa mkali na kumpeleka mambo kiutaratibu (procedural).

images - 2021-11-21T135520.428.jpeg


Muitikio wa pili, mtu anakuwa anakwepa/anaepuka (avoidant), hasa kwa aina ile ya watu wanaopenda kujichanganya na watu (outgoing). Yani wakati ule ambapo ndo anamuhitaji mtu, atajifanya hamuhitaji. Wakati anajihisi dhaifu atajifanya yuko busy na kusema kuwa hana shida yoyote. Yani huficha kabisa kuwa anamuhitaji mwenzake, na mwenzake sasa hupata viulizo na kuwaza ikiwa mtu huyo ni wa kuaminika, basi mahusiano yanakuwa ya kutoaminiana.

images (72).jpeg


Kwahiyo tunakuwa tunaendeleza tabia za kutothubutu kufanya kile hasa tunachopaswa kufanya, ambacho ni kusema tu kuwa "ingawa mimi ni mtu mzima, Nina ndevu, nimeishi miaka mingi, Nina urefu wa zaidi ya futi 6 n.k, lakini ndani mimi ni mtoto mdogo, na ninakuhitaji, kama mtoto anavyomuhitaji mzazi wake."

images (88).jpeg

Maneno hayo ni ya kujishusha sana kiasi kwamba hatuthubutu kuyatamka, hivyo hatuthubutu kukabiliama na changamoto hiyo ya Mapenzi.

Kwa kifupi hatujui kupenda. Na wote tungehitaji kwenda kwenye shule ya Mapenzi. Unaweza kushangaa, shule ya Mapenzi? Mapenzi si ni ya asili!?

images (90).jpeg


Hapana! Mapenzi ni ufundi. Ufundi unaopaswa kufundishwa. Na ni ufundi ambao jamii imekataa kuuona kama ufundi. Tunaambiwa tufuate tu hisia zetu. Lakini tukiwa watu wa kufuata hisia zetu, tutakuwa tukifanya makosa siku zote.

Kwani Mapenzi ni nini? Kwanza tujue kuna Kupenda na Kupendwa.

images (74).jpeg


Wote tunaanza kwa kujua kupendwa ni nini, na ndo penye raha. Unaletewa chakula, unaulizwa shule ilikuwaje n.k., na ndo tunakua tukifikiri mahusiano ya utu uzima yatakuwa hivyo. Hilo ni kosa linaloeleweka lakini ni kosa kubwa sana, kwani inatufanya tusione upande wa pili ambao ni Kupenda.

Kupenda ni nini? Kupenda ni kuwa na utayari wa kuelewa tabia za mtu zisizovutia ili kupata sababu zenye fadhili zinazosababisha tabia hizo. Yaani, Kupenda ni kuwa mwenye ukarimu na mwenye hisani katika kumuelewa mtu (generosity and charity of interpretation).

Wengi wetu tuna uhitaji mkubwa wa Kupendwa. Yani tunahitaji tufanyiwe wepesi maana tabia zetu huwa ni ngumu kuelewa kiasi kwamba tusingekuwa tunafanyiwa wepesi tusingeweza kuwa na mahusiano yoyote.

images (91).jpeg


Huwa hatuwazi kuwa huo ndio Upendo lakini kiini cha upendo ndio hicho, utayari wa kuelewa tabia za mtu.

Ambacho huwa tunashindwa kutambua ni kuwa mtu tunayeweza kumpenda ni mchanganyiko tata wa mazuri na mabaya.

Mwanasaikolojia Melanie Klein miaka ya 60 alikuwa anatafiti jinsi watoto wanavyojifunza kuhusu mahusiano kupitia wazazi wao. Alisema kuwa watoto wachanga huwa hawamuoni mzazi kama mtu mmoja. Huwa wanamgawanya kuwa mzazi mzuri na mzazi mbaya. Hii huendelea hadi mtoto anapofikia takriban miaka minne anapogundua kuwa kumbe hawa watu wawili ni mtu mmoja, ambapo huanza kuwa na hisia mchanganyiko na kuona kuwa kumbe anaweza kumchukia mtu na kumpenda pia, na hakuna tatizo.

images (95).jpeg


Melanie aliona hii ni hatua kubwa ya ukuaji wa kisaikolojia, ambapo hatumuoni mtu kuwa tu "mzuri sana, wa ajabu sana, wa kufurahisha sana" au kuwa tu "mbaya sana, mwenye kunikatisha tamaa, mwenye kuchukiza".

Kila tunayempenda lazima atatukatisha tamaa. Huwa tunaanza kwa kumuwazia mtu mazuri tu na kuishia kumuona kama mtu mbaya kabisa.

Ukomavu wa kisaikolojia ni kujua kuwa hamna mashujaa na waovu tu kati yetu, bali sote ni mchanganyiko tata wa mazuri na mabaya.

images (100).jpeg


Upendo sio tu kupendezwa na sifa nzuri, bali pia ni kuvumilia udhaifu, na kutambua kuwa mtu anaweza kuwa na hisia mchanganyiko.

Sababu ya sisi kufanya makosa katika kuchagua wenzi ni kuwa tuliambiwa tufuate hisia na mioyo yetu. Tuliambiwa tusiwaze sana! Ingawa hamna kitu kama "kuwaza sana", lakini kuna "kuwaza vibaya".

Tatizo linakuja, jinsi tunavyopenda tukiwa watu wazima inategemea sana na matukio ya utotoni. Tulivyokuwa tunajifunza kuhusu Upendo, hatukujifunza tu kupitia matendo ya ukarimu na huruma na wema. Tulijifunza pia kupitia mapitio mengine tuliyopitia kama kukatishwa tamaa, kudhalilishwa, kutendewa kwa ukali, kugombezwa, kufanywa kujihisi mdogo n.k.

images (98).jpeg


Yani mambo tuliyojifunza kuhusu Upendo yalichanganywa kwa namna fulani na mateso. Kinachotokea tukiwa watu wazima ni kuwa, tunaenda tukifikiri tunatafuta mtu atupe furaha, lakini kumbe tunaenda tukitafuta mtu tunayehisi tunamjua (familiar). Na tatizo la kile tunachokijua (familiarity) ni kuwa kimechanganywa kwa namna fulani na mateso.

Ndomana rafiki yako anaweza kukuunganisha na mtu ambaye mwenyewe unakubali anavutia ni mtu poa tu, lakini ukakataa kuendelea na mahusiano kwasababu unahisi tu kuna kitu hakipo sawa. Ukweli ni kuwa tunakuwa tu tumegundua kuwa mtu huyu hawezi kututesa namna tunavyohitaj kuteseka ili tuhisi kuwa Upendo huo ni wa kweli.

images (99).jpeg

Kwahiyo tunakuwa hatutafuti tu Upendo bali tunatafuta "kuteswa" kwa namna ambayo tunaijua (familiar).

Hali hii hupunguza kwa kiwango Kikubwa uwezo wetu wa kuchagua mwenza sahihi.

Sababu nyingine itakayotufanya tukose mwenza sahihi ni kuwa tunaamini kuwa kadri mwenza anavyokuwa wa sahihi kwetu, basi ndo haja ya kujielezea inavyopungua, kwamba huhitaji kumuelezea unachowaza, unachohisi, unachotaka, kisichokufurahisha n.k. Yani kama ambavyo mtoto hahitaji kujielezea kwa mzazi wake, basi mpenzi wa kweli anapaswa kujua kilicho akilini mwako.

Hilo ni kosa kubwa sana ambalo binadamu hufanya, kufikiri mwingine atajua unachowaza bila wewe kusema. Na ikija kwenye Mapenzi ndo kabisa, tuna hamu kubwa ya mpenzi wetu kutuelewa bila sisi kusema chochote. Mwisho wake ni tabia ya Kununa.

images (81).jpeg


Jambo la kushangaza kuhusu Kununa, ni kuwa huwa tunawanunia watu ambao tunaamini walipaswa kutuelewa lakini kwasababu fulani wameamua wasituelewe. Ndomaana huwa tunawanunia watu tunaowapenda na tunafikiri wanatupenda.

Mwenzako naye akiona umenuna atauliza shida nini? Utasema hamna kitu. Atakwambia no hauko sawa. Utasema mimi niko sawa kabisa, halafu uende chumbani ujifungie asiingie. Yote kwasababu unahisi mpenzi wako anapaswa kujua unachohisi na kujua wewe ni nani.

Hii ni sumu kwa uwezo wetu wa kutengeneza mahusiano ya kudumu! Usipojieleza, hutoeleweka!

images (68).jpeg


Mzizi wa Penzi zuri na Ndoa nzuri ni uwezo wa kuwa mwalimu mzuri. Haijalishi unafanya kazi gani, tunapaswa kujifunza kufundisha, yaani Ufundi wa kutoa wazo kutoka kichwa kimoja hadi kingine kwa njia ambayo litakubalika.

Wengi wetu sio walimu wazuri, maana huwa tunafundisha tukiwa tumechoka, tukiwa tunaogopa; tunaogopa nini? Tunaogopa kuoa/olewa na mjinga, ndomana tunaishia kuwagombeza "HIVI HUELEWI.....".. na ukishaanza kumdhalilisha tu au kumfanya ajihisi mdogo, kamwe hatoweza kuelewa unachotaka aelewe.

images (75).jpeg


Ili ufundishe vizuri inabidi u relax, inabidi uelewe kuwa mpenzi wako anaweza asikuelewe, na inabidi muwe na utamaduni wenu kama wenzi ambapo kila mmoja anaweza kumfundisha mwenzake na kujifunza pia.

Na hii inanileta kwenye sababu nyingine kwanini unaweza kuwa kwenye mahusiano yasiyo na furaha, kwamba kila mwenzako atakapokuambia kitu kukuhusu ambacho hakikukupendezi na hukupa wasiwasi basi unahisi mwenzako anakushambulia.

Hakushambulii! Anataka uwe mtu bora zaidi. Na huwa hatuamini kama hii Ina kazi kwenye Mapenzi. Tunafikiri kwenye Upendo wa kweli mtu anapaswa akukubali mzima mzima ulivyo. Hapana. Huo sio Upendo. Tunapaswa kukubali kuelimishwa.
images (71).jpeg


Je, kuna tumaini?

Mwanasaikolojia Donald Winnicott ndiye aliyekuwa na msemo "anayeridhisha" (good enough). Wazazi walikuwa wakimfuata na kumuelezea kuwa wanajihisi kuwa sio wazazi wazuri, watoto wao wana shida hii na ile. Akawa anawajibu tu ninyi ni wazazi wenye kuridhisha (good enough parents). Na hii iliwapa tulizo wazazi waliokuwa wanataka kila kitu kiende kwa ukamilifu (perfectionists).

Uzuri hamna yeyote aliyekamilika kwahiyo hatuhitaji ukamilifu, na kutaka ukamilifu kutatuletea jambo moja tu, Upweke. Hauwezi kupata ushirika (company) na ukamilifu. Kuwa na ushirika humaanisha kushauriana kuhusu (negotiate) kasoro zenu kila siku.

Vipi kuhusu kutopatana (Incompatibility)? Wote humu hatupatani, lakini ni kazi ya Upendo kuweka nafasi kwa neema (graciously accommodate) kwa ajili yetu wenyewe na kwa ajili ya tofauti zetu. Kupatana ni matokeo ya Upendo!

images (70).jpeg


Wote hapa tuna "type" zetu, ambazo huja na matatizo yake. Labda ana kiburi. Labda hajui kujielezea. Ukweli ni kuwa huwezi kubadilisha "type" yako. Unachoweza kufanya ni kubadilisha jinsi unavyokabiliana na "type" yako uliyoipata.

Tangu utoto tumejitengenezea wenyewe namna ya ku deal na hizi "type" zetu. Labda mzazi alikuwa asiye na ukaribu basi tungepiga kelele na kufanya fujo kupata attention. Fujo kama hizo hazitasaidia kwenye utu uzima zaidi ya kuleta matatizo.

Suluhisho ni kutafuta njia za kikomavu za kukabiliana na changamoto wanazokuja nazo hawa "type" zetu. Hayo yatakuwa mafanikio makubwa!

images - 2021-11-21T135313.285.jpeg


Mwisho, tambua umuhimu wa kuzingatiana (compromise).

Najua ungeona aibu kumtambulisha mwenzio na kusema "Jamani huyu ndiye mchumba wangu. Wakati namchagua Nimemzingatia (compromise). Kwasababu mimi mwenyewe sina mvuto kiivyo, Nina matatizo mengi, pia kichwa yangu dk mbili mbele, na kusema ukweli nilikosa tu mtu mwingine, lakini hata huyu yuko poa tu."

images - 2021-11-21T140116.236.jpeg


Lakini tuna compromise katika kila nyanja ya maisha yetu, hakuna sababu ya kuacha ku compromise kwenye Mapenzi.

Ku compromise ni Uungwana (Noble). Utasikia "yule baba kabaki tu kwaajili ya watoto"! mbona hiyo ni sababu nzuri kabisa ya kubaki!!

Bila shaka utaoa mtu asiye sahihi na kufanya maamuzi yasiyo sahihi kwenye maeneo mengi maishani, nawe utafanya hivyo kwakuwa ni binadamu.

Mwanafalsafa Kierkegaard (Karne ya 19) alisema:
"Oa, na utajuta. Usioe, na utajuta. Oa Usioe bado utajuta.
Ucheke upumbavu wa dunia, utajuta. Lia juu ya upumbavu wa dunia, utajuta.
Ucheke upumbavu wa dunia au lia juu ya upumbavu wa dunia, utajuta vyote.
Jinyonge, utajuta. Usijinyonge, utajuta. Jinyonge au usijinyonge vyovyote utajuta."

Na hicho ndicho kiini cha falsafa zote!

images (83).jpeg


-----
Picha kwa hisani ya Google
 
Huyo alikuwa Alain de Botton, mwanzilishi wa The School Of Life, ambao ni kundi la wanasaikolojia, wanafalsafa na waandishi waliojitolea kusaidia watu waishi maisha tulivu na yenye ustahimilivu kupitia filamu, vitabu, tiba za kisaikolojia, madarasa ya mitandaoni, michezo n.k

 
Aliyesoma mpaka mwisho asamarize pls
Mwanafalsafa Kierkegaard (Karne ya 19) alisema, "Oa, na utajuta. Usioe, na utajuta. Oa Usioe bado utajuta. Ucheke upumbavu wa dunia, utajuta. Lia juu ya upumbavu wa dunia, utajuta. Ucheke upumbavu wa dunia au lia juu ya upumbavu wa dunia, utajuta vyote. Jinyonge, utajuta. Usijinyonge, utajuta. Jinyonge au usijinyonge vyovyote utajuta." Na hicho ndo kiini cha falsafa zote!
 
Mwanafalsafa Kierkegaard (Karne ya 19) alisema, "Oa, na utajuta. Usioe, na utajuta. Oa Usioe bado utajuta. Ucheke upumbavu wa dunia, utajuta. Lia juu ya upumbavu wa dunia, utajuta. Ucheke upumbavu wa dunia au lia juu ya upumbavu wa dunia, utajuta vyote. Jinyonge, utajuta. Usijinyonge, utajuta. Jinyonge au usijinyonge vyovyote utajuta." Na hicho ndo kiini cha falsafa zote!
Hata hii siwezi maliza kusoma maana inakera hahahaaaa
 
Aliyesoma mpaka mwisho asamarize pls
Manzi wako aliyetafuna pesa zako na akiba yako ya mwezi mzima katika hiki kipindi cha uhaba wa maji na kero ya tanesco na geto hajatokea afu simu zako hapokei,

Mdau anashauri uwe mpole na umtumie ujumbe politely useme......"ingawa mimi ni mtu mzima, Nina ndevu, nimeishi miaka mingi, Nina urefu wa zaidi ya futi 6 n.k, lakini ndani mimi ni mtoto mdogo, na ninakuhitaji, kama mtoto anavyomuhitaji mzazi wake."

Yeah lakini naye lazima ajue kutafsiri mambo, haiwezekani mtoni kuna mamba kibao halafu unamsubiri ng'ambo
 
Mi mwathirika wa hii kitu aisee nlienda kusini mke akae da kaskazini afu kwa mbaaaaaali tunaambiana njoo tuoane, tukaoana kila mtu akarudi sehem yake yaan kaskazini na kusini
 
Manzi wako aliyetafuna pesa zako na akiba yako ya mwezi mzima katika hiki kipindi cha uhaba wa maji na kero ya tanesco na geto hajatokea afu simu zako hapokei,

Mdau anashauri uwe mpole na umtumie ujumbe politely useme......"ingawa mimi ni mtu mzima, Nina ndevu, nimeishi miaka mingi, Nina urefu wa zaidi ya futi 6 n.k, lakini ndani mimi ni mtoto mdogo, na ninakuhitaji, kama mtoto anavyomuhitaji mzazi wake."


Yeah lakini naye lazima ajue kutafsiri mambo, haiwezekani mtoni kuna mamba kibao halafu unamsubiri ng'ambo
Asante kwa kicheko Mkuu
 
Mi mwathirika wa hii kitu aisee nlienda kusini mke akae da kaskazini afu kwa mbaaaaaali tunaambiana njoo tuoane, tukaoana kila mtu akarudi sehem yake yaan kaskazini na kusini
Nimetoka kapa. Ongeza maelezo ya kutosha kusoma dakika 2.
 
Back
Top Bottom