HEKAYA ZA MLEVI: Ukitaka kumfundisha chizi, nawe jifanye chizi

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Apr 29, 2016
20,744
25,445
Tulikuwa na mwalimu pekee katika Shule ya Chekechea iliyomilikiwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC). Mwalimu alikuwa ni mama mnene, wenyewe tulimwita ‘bibi’. Alitupokea na kutukagua, na kila mmoja alifagia kwenye kiunga chake ambacho pia kilikuwa na bustani ya maua.

Sasa tulikuwa tayari kuingia darasani. Tulijikumbusha a, e, i, o, u za jana, tukaimba kidogo na kupata uji wa bulga. Baadaye tulichezea mpira wa karatasi, magari ya waya, na michezo kama rede, komborela, namtafuta rafiki, baishoo, ukuti, kula mbakishie baba na kadhalika.

Kama kawaida ya watoto, kuna wababe na wanadiplomasia. Ilimlazimu mwalimu kuingilia kati amani ilipovurugwa. Mtoto alipomsugua konzi mwenzie, mwalimu aliamua ugomvi kwa adhabu ndogo, aliamuru mkorofi kusafisha kiunga cha mnyonge. Alikuwa zaidi ya mwalimu kwetu.

Siku moja mtoto aliyekuwa na pigo za El Shababi alimtwanga konzi zito mtoto wa kike. Darasa zima lilishtuka kwa kishindo cha konzi. Ilikuwa almanusura mtoto azirai, alikata sauti kwa nusu dakika hivi kabla hajalipua kilio.

Mwalimu alimtazama kijana mbabe. Nadhani alitathmini adhabu gani itamtosha maana kila siku alifanya tukio kama hili. Siku chache zilizokuwa zimepita alibamiza kichwa cha mwenzie sakafuni hadi kumtoa damu puani kwa sababu ya ugomvi wa goroli.

Mwalimu alionekana kuchoshwa hasa baada ya kukaona kabinti kadogo kakibebeshwa dharuba isiyo ya rika lake bila kosa. Aliingia ofisini, akatoka kavalia suruali ya mazoezi. Akambeba mwamba yule kwa mkono mmoja na kumtupia kwenye uwanja wa tifutifu:

“Kila siku unaonea wenzio, leo mimi na wewe tunapigana ‘ndundi’ hadi mwisho”. Mtoto aliogopa. Kila alipotaka kukimbia mwalimu alimdaka na kumdondosha mchangani, tulicheka na kumzomea hadi akapandwa jazba

Akamvamia mwalimu na kuning’inia mguuni, mwalimu akamtikisa dogo akaramba mchanga, mashabiki tukahesabu “moja… mbili… tatu…” akainuka kabla ya kumi na kuendelea, kwa mara ya kwanza tulimwona akilia.

Ilikuwa burudani ya kipekee lakini tangu siku hiyo kijana hakuthubutu kuwadunda wenzie kama ngoma maana alijua angekutana na mtemi wake. Halafu tena hakupenda kudhalilishwa na kuchekwa hadharani hata na watoto wanyonge wake.

Nikilikumbuka tukio hilo napata picha ya ugumu wa kufundisha watoto. Mtoto wa chekechea hana mgawanyo wa rika wala kazi. Ukiacha mama, kila aliyebaki kwake ni rafiki anayefanana na mwenzie. Huko kwa wenzetu watoto huwaita baba zao kwa majina (Tom, Ben n.k.)

Mtoto wa umri huu utambuzi wake wa mema na maovu ni sawa na ziro. Ukimkenuza meno atakupenda, ukimsagisha meno au kumtoa chozi atakuona kama mbu wa dengue.

Mtoto wa enzi zile aliyetabaruku kitandani alipelekwa kwa mzee Totolala, akatiwa kwenye kikapu na kutembezwa mtaa mzima. Kama atarudia basi huyo alihitaji uchunguzi maalum wa dakitari. Mtoto wa mtaani pamoja na jeuri yake yote, alipokumbuka timbwili la totolala alijua kuwaamsha wakubwa wampeleke maliwato.

Nadhani saikolojia ya mwalimu wetu ilikuwa hivyo, alikuwa rafiki. Lakini ukileta undava naye anakuletea, hutapasuka ila hautarudia. Ni tofauti na mwalimu anayechapa au kutoa adhabu za kuchimba visiki. Ukuaji wa mtoto kuelekea utu uzima ni mtaala muhimu zaidi maishani. Akitoka chekechea ataanza shule ya msingi, sekondari na chuo akijitayarisha kuingia kwenye kazi. Hapa kijana anaweza kuongoza maisha yake.

Kwenye mfululizo huu mtoto huweza kupotezwa na kitu kidogo sana. Kama vile mkondo wa maji utokao kwenye chemichemi ukipindishwa, ndivyo anavyoweza kuondoka katika malengo kusudiwa na kushindwa kuendesha maisha yake ukubwani. Tumewaona wengi walioyumbishwa na mifarakano ya kifamilia au kuondokewa na wazazi/walezi.

Wapo waliopotezwa na ujana ikiwemo utumiaji bangi, pombe na dawa za kulevya na kinadada walioathirika na mimba za utotoni. Lakini wengine waliweza kuvurugwa hata na kupindwa kwa mitaala yao. Si makosa yao, bali mitaala hutembea bega kwa bega na maisha yao ya kila siku, unapomwambia “Kiswahili lugha ya Taifa” halafu ukamwekea tangazo la ‘Speak English Only’ shuleni unaweza kumchanganya.

Unategemea nini unapomhamisha mtoto English Medium kwenda Shule ya Kata (au kinyume chake)? Ni lazima hili lifanywe chini ya uangalizi maalum tena wa kitaalamu. Ndiyo maana sikuunga mkono walimu wa sekondari kufundisha shule za msingi.

Wapo wanaodhani shule za msingi zingepata faida kuwa na walimu wenye digrii za kufundisha sekondari. Lakini walimu hutofautiana mbinu za ufundishaji toka wakiwa vyuoni. Katika mtazamo wa kawaida ni sawa na kuyatumia magari makubwa yasafirishayo makontena nchi za nje yabebe abiria mijini.

Hebu vuta picha walimu hao wangepelekwa kufundisha Chekechea. Hakika yule mtoto gaidi kama angebahatika kurudi kwao angerudi na mkono mmoja! Kufundisha watoto wadogo kunataka nawe ujifanye mtoto.


Credit : Hekaya Za Mlev
 
Back
Top Bottom