Amicus Curiae
JF-Expert Member
- Sep 12, 2012
- 4,800
- 6,280
"Kamati kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi hakiwezi kuepuka
lawama. Lakini kuilaumu Kamati Kuu ni kukiri kwamba sasa Chama Cha Mapinduzi kina
kansa ya uongozi ambayo isipotibiwa itakiua Chama kizima. Pengine kwa nchi yetu hii
lisingekuwa jambo la kutisha kama tungekuwa tumeanza kuona chama kizuri cha upinzani
ambacho kinaweza kuiongoza nchi hii badaIa ya CCM. Hakijaonekana bado. Chama Cha
Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake,
mazoea ya watu, na ubovu wa vyama vya upinzani, kinaweza kuendelea kuchaguliwa na
Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza. wakachoka, wakasema,
"potelea mbali:" wakachagua Chama chochote, ili mradi tu watokane na kansa ya uongozi
wa CCM. Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa nchi yetu unataka yasemwe"-Hayati Mwl Nyerere
"Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi isingekuwa ni
jambo la kutisha sana kama tungekuwa tumeanza kuona kizuri cha upinzani kinachoweza
kuiongoa nchi yetu badala ya CCM. Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliofanya
nikapendekeza tuanzishe mfumo wa vyama vingi. Nilitumaini kuwa tunaweza kupata chama
kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza nchi yetu badala CCM au ambacho
kingekilazimisha Chama Cha Mapmduzi kusafisha uongozi wake kwa kuhofia kuwa bila
kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao"-Hayati Mwl Nyerere
Maneno hayo hapo juu yanapatikana katika ukurasa wa 42 na ule wa 45 katika kitabu cha Mwl kiitwacho UONGOZI WETU NA HATIMA YA TANZANIA alichokiandika mwaka1994 lakini baada ya kukipeleka kwa wachapishaji (Mkuki na Nyota), Serikali ilikataa kisichapishwe ikabidi Mwl akakichapishe Zimbabwe. Alipokileta nchini ili kukisambaza Seriakali ikakipiga 'ban'; ingawa wapo wajanja wachache waliopata nakala ya Kitabu hicho.
Mwl alipofariki mwaka 1999, mwaka 2010 Serikali ikatengeneza CHAPISHO LA KIZAZI KIPYA kwa kuyaondoa maneno yote ambayo yalionekana ni sumu kwa CCM. Sitakuwa na maneno mengi, nitakachofanya ni kuwapa nukuu tu ili mjue yanayotokea sasa yalitabiriwa na Mwl takribani miaka 18 iliyopita.
Katika ukurasa huo wa 45 mpaka ukurasa wa 46 Mwl anaendelea kusema....
"Lakini bado sijakiona chama makini cha upinzani; wala,dalili zozote za kuondoa kansa ya
uongozi ndani ya CCM. Bila upinzani mzuri wa nje, na bila demokrasia halisi ndani ya Chama
Cha Mapinduzi, Chama hili kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu. Kwa hali yetu
ya kisiasa ilivyo nchini, hili si jambo la kutarajia bila ya hofu na wasi wasi!
Wazalendo Watanzania hawana budi wapende kuona demokrasia halisi ndani ya Chama Cha
Mapinduzi: Hii ina sura mbili".
"Kwanza, ni lazima kurudisha tena uhuru na utaratibu wa kujadili masuaIa yote makubwa na
kufikia uamuzi baada ya mjadala.
Viongozi wetu hivi sasa wanaogopa kutumia nguvu za hoja ili kutoa maamuzi muhimu. Kwa
sasa wanatumia hila zaidi kuliko hoja; vitisho kwao ni mbinu rahisi zaidi kuliko adha
ya kutumia akili na kupata hoja safi ya kumjibu mpinzani katika mjadala. Viongozi hawa
wakipewa nafasi watatumia hoja ya nguvu tu; na hawatakuwa na haja ya kutumia akili.
Kichini chini baadhi yao tayari wameanza kutumia hoja ya vitisho. Na kama tukiacha
utamaduni wa woga ukazagaa tutakuwa tunakaribisha udikteta".
"........ Washindania urais wapo, tena moto moto. Chama kinajua
hivyo, na wananchi wanajua hivyo. Chama Cha Mapinduzi hakina budi kitafute utaratibu
mzuri wa kuwashindanisha wataka urais hawa kwa njia ya wazi wazi. Tutafanya makosa
makubwa tukikubali kuteua mgombea urais kwa kutumia mzengwe. Njia ya mzengwe
ilitufaa tu wakati tulipokuwa hatuna washabiki wa urais. Na inaweza kufaa kama mnataka
kumteua mwenzenu ambaye mnaamini kuwa ndiye anayefaa, lakini hapendi misukosuko ya
kushindania uongozi".
Hivi Mwl Nyerere ni mzimu unaoishi? Nimebahatika kupata nakala ya hiki kitabu. Ukikisoma chote hutashangaa yanayotukia sasa.
Mungu Ibariki Tanzania.