Haya ndio Maoni ya Rais JK kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya

bibikuku

JF-Expert Member
Feb 16, 2011
832
195
SALAMU ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA TUME YA KATIBA, 03 JUNI, 2013, DAR ES SALAAM

Ndugu Wananchi;


Leo ni siku muhimu sana katika historia ya nchi yetu. Mchakato wa kutengeneza Katiba mpya ya nchi yetu umefikia hatua muhimu sana. Sasa tunayo Rasimu ya Katiba kwa kila mmoja wetu kuona na kutoa maoni.


Kwa niaba yangu na kwa niaba yenu Watanzania wenzangu wote napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi na shukrani zangu za dhati kwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Mheshimiwa Joseph Sinde Warioba na Wajumbe wote wa Tume kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya na kutuwezesha kupata Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Wanastahili shukrani na pongezi kwa sababu natambua kuwa kazi yao haikuwa rahisi hata kidogo. Kwanza, kwamba nchi yetu ni kubwa hivyo kuzunguka karibu pande zote ni shughuli pevu. Pili, kwamba kusikiliza maelfu ya wananchi wa Tanzania waliojitokeza kutoa maoni yao kuhusu Katiba wanayoitaka ni kazi kubwa sana. Na hasa tunapotambua ukweli kwamba watu wana hulka tofauti na uwezo tofauti wa kuelewa na kujieleza. Si ajabu pia kwamba katika baadhi ya maeneo walikutana na watu waliohitaji wakalimani.
Ndugu Wananchi;


Pengine kazi iliyokuwa ngumu zaidi kwa Wajumbe wa Tume, ilikuwa ile ya kuchambua maoni na mapendekezo yote lukuki yaliyotolewa na kuamua yale ya kupendekeza yaliyojumuishwa katika Rasimu waliyoitangaza leo. Ndiyo maana Wajumbe wa Tume wanastahili shukrani na pongezi maalum zinazokwenda pamoja na pole nyingi.

Tunawapongeza kwa umahiri wao kwani matokeo ya kazi yao ni ya kiwango cha hali ya juu. Tunawapongeza kwa moyo wao wa ustahamilivu, uvumilivu, kujituma na uzalendo uliowawezesha kukamilisha kazi kwa wakati muafaka na kwa ufanisi mkubwa.


Ndugu zangu, Watanzania wenzangu;


Tume imemaliza kazi yake ya msingi ya kutayarisha Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kinachofuatia sasa ni kazi ya Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba na wananchi kuijadili Rasimu hiyo na kutoa maoni na mapendekezo yao kuhusu namna ya kuiboresha Rasimu hiyo. Baada ya hapo Tume itatengeneza Rasimu ya Mwisho ya Katiba itakayofikishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba kwa ajili ya kujadiliwa na kufanyiwa maboresho kadri wajumbe watakavyoona inafaa. Kisha hapo, Rasimu ya Katiba itakayotokana na mjadala na marekebisho ya Bunge Maalum itafikishwa kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho kupitia kura ya maoni.


Nawaomba Watanzania wenzangu, tuitumie vizuri nafasi hii kutoa maoni yetu yatakayoboresha Rasimu hiyo ili hatimaye tupate Katiba nzuri yenye maslahi kwa nchi yetu na watu wake. Katiba ambayo itatetea Taifa letu kwa miaka mingi ijayo kwa umoja, amani, upendo, mshikamano na maendeleo.


Ndugu wananchi;


Najua, kama tunavyojua sote, kuwa wakati wa kutoa maoni washiriki walitoa mapendekezo mengi na ya namna mbalimbali. Baadhi ya mapendekezo yamejumuishwa na mengine hayamo katika Rasimu ya Katiba.

Nawaomba wale ambao maoni na mapendekezo yao hayamo wasifadhaike wala kukasirika. Naomba sote tutambue kuwa si kila wazo au pendekezo lililotolewa na kila mmoja wetu lingeingizwa.

Ukweli ni kwamba haiwezekani tuwe na Katiba ambayo mapendekezo ya kila mtu yamejumuishwa. Kama ingekuwa hivyo tungekuwa na kitabu kikubwa mno cha Katiba ambacho kingekuwa hakibebeki kwa uzito na wala hakisomeki kwa urahisi kwa sababu ya kuwa na maelfu ya kurasa. Vile vile ingeweza hata kuwa taabu kueleweka kwa sababu ya kuwepo mawazo mchanganyiko na mengine yakiwa yanakinzana.


Nawaomba mtambue na kuthamini jitihada kubwa waliyofanya Wajumbe wa Tume ya kuunganisha mawazo na mapendekezo mbalimbali na kuja na Rasimu waliyotuletea siku ya leo.


Ndugu wananchi;


Nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitawashukuru wananchi wenzetu wote waliojitokeza kutoa maoni yao kwenye mikutano na kwa njia nyinginezo mbalimbali. Aidha nawashukuru Maafisa wa Tume na Serikali waliofanikisha mchakato huu tangu mwanzo mpaka sasa. Napenda, vile vile kuwashukuru Wabunge kwa kupitisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyotuwezesha kufikia hatua hii ya leo.

Nawashukuru sana viongozi na wanachama wa vyama vya siasa na asasi za kiraia kwa ushirikiano wao na maoni yao muhimu yaliyoboresha Sheria hiyo. Ndugu zetu wa vyombo vya habari nao tunawashukuru kwa kuelimisha jamii. Wote nawaomba tuendelee kushirikiana na kushikamana katika hatua zinazofuata mpaka tukakapofikia mwisho wa safari yetu na kupata Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotokana na maoni yetu na ushiriki wetu.


Ndugu wananchi;


Naomba nimalize kwa kuwasihi Watanzania wenzangu tuwe wastahimilivu na watulivu katika kujadili mapendekezo ya Tume yaliyomo katika Rasimu ya Katiba Mpya. Tusiwe na jazba wala hamaki kwa mapendekezo yaliyotolewa. Kama tulivyosikia na kama tutakavyosoma katika Rasimu, baadhi ya mapendekezo ya Tume yakikubaliwa yatabadili sura ya nchi yetu hususan muundo wa Muungano wetu na jinsi ya kuendesha baadhi ya mambo yetu muhimu.

Mambo yatakuwa tofauti na ilivyo sasa au na jinsi tulivyozoea kwa miaka mingi. Baadhi yetu tunaweza kushtuka au hata kuhamaki na kuhamanika. Nawasihi msiwe hivyo wala msifanye hivyo.


Tusiikasirikie wala kuilaumu Tume ya Katiba. Tuliwapa kazi ya kusikiliza maoni na kutoa mapendekezo. Wametimiza wajibu wao. Wajibu wetu sisi sasa ni kutoa hoja za kuboresha kilichopendekezwa kama tunacho. Tushiriki kwa ukamilifu kutoa maoni yetu kwa mujibu wa utaratibu utakaowekwa na Tume. Katika kufanya hayo naomba tuongozwe na maelekezo mazuri aliyoyatoa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipokuwa Rais kwa Maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje mara baada ya nchi yetu kupata Uhuru kuwa; “Toa Hoja Usipige Kelele” – Argue Don’t Shout. Nawaomba tupime na kupimwa kwa uzito wa hoja tutakazozitowa.


Ndugu zangu, Watanzania wenzangu,


Tukifanya hivyo tutakamilisha mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa salama na amani na mafanikio ya hali ya juu. Dunia itatupongeza, itashangaa na kutamani kuja kujifunza kutoka kwetu. Wakati hayo yakitokea tuweze kusema kwa kujidai kuwa “Usione vinaeleza vimeundwa” na waundaji si wengine bali ni sisi Watanzania: mimi na wewe.


Mungu Ibariki Afrika


Mungu Ibariki Tanzania.
 

Zinedine

JF-Expert Member
Apr 9, 2011
1,188
0
Rasimu ya Katiba nimeisoma hii nimeishindwa ndefu sana,
maoni yangu haya
16(1) Kuhusu kutangaza mali kwa mtumishi wa Umma; napendekeza kuwa Kiongozi wa Umma atangaze mali na thamani siku 30 kabla ya kuwa kiongozi na wali SI siku thelethini baada ya kuwa kiongozi. Hii maana yake kama kuna mtu mwenye hoja za ya msingi ya kupinga uhalisia/ufichaji wa mali/thamani ya mtumishi mtarajiwa aweze kuwasilisha pingamizi au hoja, kwani kutaja mali baada ya kuwa kiongozi kutaleta tabu ya kumvua madaraka au gharama za kumvua madaraka pindipo ikibainika kwamba kiongozi huyo alitangaza mali/thamani zake kiuongo isivyo kweli/. Ikumbukwe hapa lengo si tu kutangaza kama ilivyo sasa bali pia uchunguzi ufanyike wa kubaini uhalisia na uhalali wa mali hizo/thamani na ikiwa amezipata kihalali au kimagendo, na pia atangaze kama ni mfanyabiashara na atangaze biashara zake na awe tayari kupitia kampuni yake kukaguliwa hesabu za biashara yake ili mwisho wa siku tujue thamani ya mali zake baada ya kutumikia uongozi zinaendana na chumo lake. Tukifanya hivi tutapata viongozi ambao kweli wazalendo kwani wasio wazalendo wataogopa wakijua kuwa mwisho wa kubainika kwa uongo wao ni confiscation ya mali zake. Pliiiiiiiiiiiz; Lakini akishaingia katika uongozi atalindwa na sheria nyingi za uongozi na ugumu wa kufanyiwa assessment ya haki. Hata hivyo hii natumaini kuwa kifungu hiki kitawagusa watumishi ambao ni highly personnel, hivyo kuteuliwa/kuchaguliwa kwao kazini hakutakuwa na haraka na hakutazuia watanzania wengine wasijue wamuhoji kama si muadilifu
 

Mwana Mpotevu

Platinum Member
Sep 7, 2011
3,295
1,500
Nina Mawili kuhusu JK

1. Nasubiri atangaze kusimama kwa muda kwa mchakato wa katiba ya Muungano na atangaze kuanza kwa mchakato mpya wa katiba ya Tanganyika kwanza ili tukishapata katiba ya Tanganyika ndipo tuje tuendelee na mchakato wa hii katiba ya Muungano.

2. Naanza kuhisi kuwa Prof. Lipumba was right kuwa JK ataongezewa muda wa kukaa madarakani na hataondoka 2015 sababu lazima mchakao uchukue muda mrefu kuliko ilivyodhaniwa. Mchakato wa katiba ya Tanganyika haujaanza na haijulikani utaanza lini ukizingatia kuwa lazima tujue namna gani tutakuwa na Bunge la Bara, Rais wa Bara, Mfumo wa mahakama wa bara na mengineyo mengi.

Just thinking aloud!
 

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
98,478
2,000
Mie pia sijapata nafasi ya kuisoma. Nimeona Mbunge kama utendaji wake ni finyu basi wapiga kura wa jimbo lake wanaweza kumvua Ubunge. Hili pia lingewekwa kwa Rais kwamba kama Rais utendaji wake ni hovyo kama huyu Kikwete basi Bunge lipige kura ya maoni kama linakubali utendaji wake au la. Kama hili lingekuwepo ndani ya katiba ya sasa labda DHAIFU angekuwa history miaka mingi iliyopita. Halafu Wabunge kuruhusiwa kuwa Bungeni kwa awamu tatu ni muda mrefu sana, nao wangepewa awamu mbili tu kama Rais. Kisha hili la mikataba ambalo linaitafuna Taifa sijui kama nalo limo katika hii rasimu kama halipo basi nalo liwekwe ili mikataba yote ya Tanzania iweze kujadiliwa kwa kina Bungeni ili kuhakikisha inakuwa na maslahi kwa Tanzania na Watanzania na kuepuka mikataba fisadi kama ya Rada, Richmond, uchimbaji dhahabu, mikataba yote na Wachina n.k.
 

dada jane

JF-Expert Member
Dec 8, 2011
565
0
Nakubaliana na Pasco wa jf alivyosema kuwa JK ana "sense of humour" ila saa nyingine daa!
 

bibikuku

JF-Expert Member
Feb 16, 2011
832
195
Nina Mawili kuhusu JK

1. Nasubiri atangaze kusimama kwa muda kwa mchakato wa katiba ya Muungano na atangaze kuanza kwa mchakato mpya wa katiba ya Tanganyika kwanza ili tukishapata katiba ya Tanganyika ndipo tuje tuendelee na mchakato wa hii katiba ya Muungano.

2. Naanza kuhisi kuwa Prof. Lipumba was right kuwa JK ataongezewa muda wa kukaa madarakani na hataondoka 2015 sababu lazima mchakao uchukue muda mrefu kuliko ilivyodhaniwa. Mchakato wa katiba ya Tanganyika haujaanza na haijulikani utaanza lini ukizingatia kuwa lazima tujue namna gani tutakuwa na Bunge la Bara, Rais wa Bara, Mfumo wa mahakama wa bara na mengineyo mengi.

Just thinking aloud!
Hili limenigusa sana
 

Capt Tamar

JF-Expert Member
Dec 15, 2011
9,915
2,000
Bado sijaona utaratibu wa kuwapta wakuu wa mikoa/wilaya,mkono wa rais bado ni mrefu kupindukia,unaanzia juu kuzunguka chini kisha unarudi juu,hii ni hatari dhahri,mwenyekiti wa tume HURU ya uchaguzi kuwa appointed na rais/mwenyekiti wa chama ni janga jingine,ngoja tuone awamu hii kama kuna atakayekumbuka kulizungumzia hilo bila kwikwi.
 

Mwana Mpotevu

Platinum Member
Sep 7, 2011
3,295
1,500
Hili limenigusa sana
Mkuu bibikuku hapa vovyote iwavyo, JK ni Rais hadi 2016 and above ikiwezekana maana mchakato wa katiba ya Tanganyika ukitangazwa lazima ituchukue walau miaka miwili hivi na hadi sasa haijulikani mchakato ukaanza lini.

Hatuwezi kupitisha katiba ya Muungano bila ya kuwa na Tanganyika au Tanzania Bara kama alivyoiita Warioba et al. Kwahiyo lazima mchakato huu ufikie hatua usimamishwe kwa muda na mchakato mwingine uanze upya kabisa kutafuta katiba ya Bara. Zenji wanayo sio issue sana kwao ni swala la amendments tu.

Kwa ufupi tusahau kuwa na Katiba mpya ya Muungano 2014 hata kama itatokea miujiza!
 
Last edited by a moderator:

tenende

JF-Expert Member
Jan 10, 2012
6,554
1,195
Nina Mawili kuhusu JK


2. Naanza kuhisi kuwa Prof. Lipumba was right kuwa JK ataongezewa muda wa kukaa madarakani na hataondoka 2015 sababu lazima mchakao uchukue muda mrefu kuliko ilivyodhaniwa. Just thinking aloud!
MUNGU tuepushie janga hili!
 

Capt Tamar

JF-Expert Member
Dec 15, 2011
9,915
2,000
Kugawa tisheti na kanga nk wakati wa uchaguzi kuainishwe rasmi na katiba kama kitendo cha rushwa kama zilivyo rushwa nyingine,Mwenge wa uhuru utupiliwe mbali!!! Matumizi ya mali za serikali kwa shughuli za kichama na binafsi yadhibitiwe,mali zilizochumwa na serikali kipindi cha chama kimoja ziainishwe rasmi kuwa mali za umma,mfano viwanja vya wazi na vya michezo,wakuu wa mikoa na wilaya wasipewe haki ya kutumia vyombo vya dola watakavyo,kuwe na tume huru ya bei,utaratibu wa kuwapata jaji mkuu,mwanasheria mkuu uwe competitive zaidi ya huu wa kumchomoa pale na kumchomeka hapa,naaaaaaaaa
 

Nduka

JF-Expert Member
Dec 3, 2008
8,509
2,000
Nina Mawili kuhusu JK

1. Nasubiri atangaze kusimama kwa muda kwa mchakato wa katiba ya Muungano na atangaze kuanza kwa mchakato mpya wa katiba ya Tanganyika kwanza ili tukishapata katiba ya Tanganyika ndipo tuje tuendelee na mchakato wa hii katiba ya Muungano.

2. Naanza kuhisi kuwa Prof. Lipumba was right kuwa JK ataongezewa muda wa kukaa madarakani na hataondoka 2015 sababu lazima mchakao uchukue muda mrefu kuliko ilivyodhaniwa. Mchakato wa katiba ya Tanganyika haujaanza na haijulikani utaanza lini ukizingatia kuwa lazima tujue namna gani tutakuwa na Bunge la Bara, Rais wa Bara, Mfumo wa mahakama wa bara na mengineyo mengi.

Just thinking aloud!

Kuna siku usipokuwa na yale magwanda yako unakuwa na akili sana. JK hadi 2017
 
Top Bottom