Haya ndio mambo ya kuzingatia unapomchagulia mwanao shule

Ferruccio Lamborghini

JF-Expert Member
Apr 15, 2020
1,664
2,517
Dar es Salaam. Mwanzo wa mwaka unapokaribia wazazi wengi huanza kutafuta shule bora kwa ajili ya watoto wao kujiunga ili wajiendeleze kielimu.

Wakati huu ndio ambao wazazi hulazimika kuwapeleka watoto katika shule tofauti kufanya mitihani ya kujiunga, hasa wale wa kidato cha kwanza.

Hapa wazazi hutumia fedha nyingi bila kujali, ila anachotaka ni kuhakikisha mwanawe apate shule bora kwa ajili ya elimu bora.

Wengi huwapeleka watoto wao kutokana na sifa husika za shule, mazingira, ufundishaji, nidhamu lakini kubwa linaloangaliwa ni ufaulu wa shule husika.

“Mimi niko tayari kulipa gharama yoyote ili mwanangu asome shule nzuri itakayomfanya kufaulu mitihani yake, kwa kuwa huo ndio mwanzo wa mafanikio yake kimaisha,” anasema Digna Sikomele, mkazi wa Tabata.

Anasema licha ya yeye kusoma shule za umma hadi kufika chuo, lakini anatamani watoto wake wasome shule binafsi.

“Shule nyingi za binafsi wanajua wanachokifanya, ufuatiliaji wa watoto na hata ufundishaji wao, jambo linalofanya watoto wafaulu masomo yao,” anasema Digna.

Mawazo kama ya Digna hulazimisha wazazi, hasa wale ambao watoto wao huingia kidato cha kwanza kwenda shule tofauti kuchukua fomu na watoto wao kufanya mitihani ya majaribio.

“Mpaka tunapata shule tumeshafanya interview (usaili) kwenye shule nne, tulilipa hela ya fomu lakini hatukubahatika na hizo ndiyo zilikuwa chaguo la kwanza,” anasema mzazi aliyejitambulisha kwa jina la Dionis.

Mtafiti wa Masuala ya Elimu, Muhanyi Nkoronko anasema wazazi wanapaswa kuangalia shule wanayompeleka mtoto itamsaidia kupata maarifa, ujuzi na kukua kiakili.

“Pia, shule lazima iwe na walimu wa kutosha, mazingira mazuri ya kujifunzia na kumuandaa mtoto kimasomo na maisha ya baadaye.

“Lakini katika dunia ya leo ni vyema kuangalia malengo pia na namna soko linavyokwenda, ni bora kuangalia kama shule hiyo inakuza ujuzi na maarifa yatakayomfanya awe bora zaidi atakapomaliza masomo yake,” anasema Nkoronko.

Licha ya hayo, wazazi wengi huangalia sifa moja pekee ya shule kuwa na uwezo wa kufaulisha wanafunzi wengi bila kuangaliwa wanasomaje hadi wanaweza kufaulu.

“Pia, aangalie shule ambayo haitakuwa na mazingira yanayomfanya mtoto aweze kutoka kama ni ya bweni, ina mazingira wezeshi ya mtoto kufanya vizuri kupata maarifa,” anasema Nkoronko.

Anasema mienendo ya shule pia inatakiwa kuchunguzwa ili mzazi asije kumpeleka mtoto katika shule ambazo adhabu zake ni viboko.

Dk Luka Mkonongwa, ambaye Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) anasema mazingira ya shule ni kitu cha kwanza cha kuzingatia, yawe rafiki kwa mwanafunzi na kufahamu vyema mfumo wa shule.

Hapo anamaanisha kuwa baadhi ya shule mifumo yake ni ya dini huku ikiwa na misimamo mikali, hivyo ni vyema aangalie kama inaendana na mtoto wake.

“Wazazi wanatakiwa kutofautisha suala la shule na umaarufu wa shule husika, asifuate shule kwa sababu ni maarufu, bali aangalie elimu inayotolewa pale ni ya aina gani,” anasema Dk Mkonongwa.

Anasema zamani kulikuwa na shule zenye majina makubwa na wazazi bila kuzingatia sifa za shule walipeleka watoto wao na hawakupata kile kilichotarajiwa.

Mwalimu John Julius kutoka Shule ya Sekondari Tubuyu anasema mbali na ufaulu, ni vyema mzazi akaangalia pia shule ambayo inawalea watoto katika misingi mizuri, ikiwamo ile ya dini.
Hiyo ni kutokana na ukuaji wa sayansi na teknolojia unaoathiri ukuaji wa watoto wengi ikiwa watakuwa hawana watu wa kuzungumza nao kwa ukaribu.

Anasema mazingira mazuri ya kujifunzia, maabara kwa wale wa sekondari ni muhimu ili mtoto aweze kusoma kuendana na matamanio yake.

“Lakini wakati akiangalia yote haya, mzazi anatakiwa kuchagua shule ambayo si ya gharama itakayomshinda, kama anaona hawezi shule za Serikali zipo nzuri na zinafundisha vizuri ampeleke hata huko,” anasema Julius.

Pia, anasema baadhi ya shule za binafsi zina mazingira mazuri lakini zipo kibiashara zaidi bila wazazi kutambua.

Mwalimu Neema Kitandu kutoka Shule ya Sekondari Kingolwira anasema ufikaji wa shule ni kitu cha kuzingatiwa kwa wanafunzi wanaosoma kutwa.

“Kama ni daladala anatumia basi akishuka afike kirahisi, kama ni gari la shule linampitia basi lifike pia karibu na makazi na muda uwe rafiki kuondoa usumbufu kwa mtoto kwa kuwahi kuamka sana au kuchelewa kufika nyumbani.

“Hili linamfanya mtoto kuchoka na kukosa muda wa kujisomea na kila anaporudi nyumbani hutamani kulala,” anasema Neema.

GHARAMA.
Kuhusu gharama za shule husika. anasema ni vyema wazazi waangalie wanavyoweza kumudu gharama si katika mwaka wa kwanza wa masomo pekee. bali hadi mwanafunzi atakapomaliza masomo.

“Siku hizi elimu imekuwa biashara, watoto wengi wamekuwa wakianza shule baadaye wanahamishiwa shule nyingine, hivyo ni vyema kufanya tathmini kabla ya kumuanzisha mtoto.

“Kitendo cha kumhamisha mtoto kwenda shule nyingine kinaathiri kujifunza kwake, kwa kuwa lazima aanze kuzoea mazingira mapya, aanze kuzoea walimu wapya, mwishowe anapata matokeo mabaya,” alisema Dk Mkonongwa.

Nkoronko ambaye ni Mtafiti wa masuala ya elimu, anasema mzazi aangalie uwezo wake wa kumudu gharama ili kumwezesha mtoto kupata maarifa na elimu yake kwa kipindi chote cha masomo, huku akishauri mzazi kutompeleka mtoto shule ambayo baadaye inaweza kumshinda kulipa.

Nicodemus Shauri, ambaye ni Meneja Programu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet) anawataka wazazi kufanya machaguo ya shule kutokana na uwezo wao wa kifedha.

“Pia, waangalie shule wanazofundisha vizuri kwa sababu mzazi anajua mwanawe anataka nini, inakuwa ni rahisi kufanya chaguo la shule,” alisema Shauri.

Mwalimu Neema pia anasema kama mwanafunzi anatumia gari la shule, mzazi anapaswa kuhakikisha gharama zake anazimudu ili kuepusha usumbufu anaoweza kuupata mtoto.

AFYA.
Mara zote mzazi anajua mazingira gani ni rafiki kwa mwanawe na yapi si rafiki.

Kwa sababu baadhi ya watu mazingira ya joto au baridi kali si rafiki, hivyo ni vyema badala ya kumlazimisha mtoto kusoma katika shule iliyopo eneo ambalo unajua haendani nalo kiafya, ukampeleka ambako hatopata matatizo.

Anasema ukilazimisha kisa shule inafaulisha, inaweza kumuathiri.

“Hili huweza kusababisha mtoto akawa mtu wa kujiuguza kila siku, yupo hospitali kila baada ya muda fulani, mwishowe anapata matokeo mabaya,” anasema Dk Mkonongwa.

©Mwananchi
 
habari njema yenye elimu ndani yake inatukumbusha wazazi mambo ya msingi kwa watoto wetu
 
Back
Top Bottom