Hatupaswi kulaumiwa kwa chochote Kufeli kidato cha nne 2010 | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Hatupaswi kulaumiwa kwa chochote Kufeli kidato cha nne 2010

Discussion in 'Jukwaa la Elimu (Education Forum)' started by kilimasera, Feb 26, 2011.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  Feb 26, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  BARAZA la Mitihani la Taifa (Necta), limepuuza lawama zinazoelekezwa kwake kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne ya mwaka 2010, likieleza kuwa halipaswi kulaumiwa huku Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Dk Joyce Ndalichako akisema kuna tatizo kubwa kuliko inavyodhaniwa na kutaka mamlaka husika zichunguze chanzo cha matokeo hayo.

  Dk Ndalichako aliliambia Mwananchi katika mahojiano maalum hivi karibuni kuwa, ili kubaini chanzo cha kufanya vibaya kwa wahitimu wa kidato cha nne mwaka jana, mamlaka husika zichukue hatua ikiwa ni pamoja na kuchunguza chanzo cha matokeo hayo kuwa mabaya.

  “Nasisitiza, katika matokeo ya mwaka 2010 ya mitihani ya kidato cha nne, baraza (Baraza la Mitihani) tunajitoa kabisa, hatupaswi kulaumiwa kwa chochote maana sisi tulifanya kazi yetu kwa mujibu wa sheria na kutekeleza wajibu wetu ipasavyo,”alisema Dk Ndalichako.

  Alisema badala ya wadau wa elimu kuitupia lawama Necta kuwa inahusika na kufeli kwa wananfunzi hao, mamlaka husika ziunde chombo huru cha kuchunguza mchakato mzima wa mitihani hiyo na kutoa taarifa kwa umma kuhusu chanzo cha wanafunzi kufanya vibaya.

  “Mimi nadhani kuna tatizo kubwa kuliko tunavyofikiria, hapa lazima ufanywe utafiti wa kitaalamu,"alisema Dk Ndalichako

  Kauli ya Dk Ndalichako imekuja wakati tayari Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imeonyesha nia ya kufanya utafiti wa kina kujua chanzo cha wanafunzi hao wa kidato cha nne kufanya vibaya kupita kiasi katika mitihani ya kuhitimu elimu ya sekondari iliyofanyika nchini mwishoni mwa mwaka jana.

  Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Hamis Dihenga alisema utafiti huo unaweza kuanza mwanzoni mwa Machi mwaka huu ukihusisha wizara yake, Ofisi ya Waziri Mkuu -Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na vyuo vya ualimu nchini.

  Akiwa mjini Morogoro Februari 16 mwaka huu, Profesa Dihenga alisema yapo majibu mepesi yanayoonyesha kuwa wanafunzi hao wamefeli kutokana na uhaba wa walimu, uhaba wa maabara na vitabu, lakini akasema ni vema taasisi hizo pamoja na wizara yake ikafanya utafiti wa kina na kuwa na majibu ya kitaalamu.

  Matokeo ya kidato cha nne mwaka 2010 yanaonyesha kuwa kiwango cha ufaulu kimeshuka kwa asilimia 22 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2009.

  Taarifa ya Dk Joyce Ndalichako wakati akitangaza matokeo hayo ilisema asilimia 50.40 ya watahiniwa wote, wamefaulu, ikimaanisha kwamba waliofeli ni asilimia 49.60 ambapo wasichana waliofaulu ni 69,996 sawa na asilimia 43.47 na wavulana ni 107,025 sawa na asilimia 56.28.

  “Mwaka 2009 watahiniwa waliofaulu walikuwa sawa na asilimia 72.51 ya watahiniwa waliofanya mtihani huo,” alisema Dk. Ndalichako.

  Kufuatia matokeo hayo, badhi ya wadau wa elimu wakiwemo wasomi, wanasiasa na mashirika ya kijamii na wananchi kwa ujumla wao, waliyaita matokeo hayo kuwa ni “janga la kitaifa” hivyo kutoa wito kwa wasimamizi wa sekta ya elimu nchini kuchunguza chanzo cha tatizo hilo, lakini pia kuchukua hatua ili lisiotokee tena.

  Vimbwanga vya watahiniwa………
  Katika mahojiano na Mwananchi, Dk Ndalichako alisema wasahihishaji wa mitihani ya kidato cha nne mwaka 2010 walikutana na vioja mbalimbali ambavyo si vya kawaida, kuliko ambavyo imewahi kutokea katika miaka iliyopita.

  Miongoni mwa mambo ambayo si ya kawaida kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu huyo wa Necta ni pamoja na baadhi ya shule kutofaulisha mwanafunzi hata mmoja, watahiniwa kuandika matusi katika karatasi za majibu, idadi kubwa ya watahiniwa kutoandika chochote na wengine kuchorachora katika karatasi hizo za majibu.

  Alisema hata wao (Necta) walishtuka wakati wakisahihisha mitihani hiyo, baada ya kubaini kwamba baadhi ya shule hazikufaulisha mwananfunzi hata mmoja jambo ambalo si la kawaida.

  “Mimi nadhani kuna tatizo kubwa kuliko tunavyofikiria, hapa lazima ufanywe utafiti wa kitaalamu kwani unapokuwa na asilimia 20 ya shule wanafunzi wameandika namba tu kwenye kijitabu cha majibu na kuondoka bila kujibu swali hata moja basi hapo sijui mlitaka mimi au baraza (Necta) tufanye nini?,” alihoji Ndalichako huku akionyesha baadhi ya karatasi hizo.

  Mwananchi lilishuhudia baadhi ya karatasi za majibu ambazo watahiniwa hawakuandika chochote pamoja na vijitabu vya majibu ambavyo karatasi zake zilikuwa zimechorwachorwa maandishi yasiyoeleweka.
  Alisema miaka iliyopita kulikuwa na matukio kama hayo lakini, mwaka huu yameongezeka, ikiwa ni pamoja na wanafunzi wengi kuandika majibu sahihi, lakini kinyume cha swali lilivyouliza.

  “Katika mtihani wa mwaka 2009 kulikuwa na mtahiniwa mmoja tu aliyeandika matusi, lakini mwaka huu wameongezeka na wamekuwa wanne..,”alisema Katibu Mtendaji huyo wa Necta.

  Usahihishaji wa Mitihani………
  Kuhusu taratibu za usahihishaji wa mitihani, Dk Ndalichako alisema taratibu ni zile zile zinazotumika miaka yote na kwamba hakuna mabadiliko yoyote katika mchakato huo ikilinganishwa na miaka mingine.

  Alisema lazima ijulikane kwamba pamoja na idadi ya watahiniwa kuongezeka, muda wa kutunga mitihani, kusahihisha na hata kutoa matokeo haubadiliki hivyo kilichofanywa na Necta katika usahihishaji ni kuongeza idadi ya wanaosahihisha mitihani na si kuongeza muda.

  “Mtihani huu wa kidato cha nne wa 2010 tulikuwa na 'markers' (wasahihishaji) 4,546 ikilinganishwa na mwaka 2009 ambapo tulikuwa nao 3089 na tuliongeza wasahihishaji zaidi ya 1,400 kwa kuzingatia ongezeko la watahiniwa,”alifafanua Dk. Ndalichako.

  Kwa mujibu wa takwimu za Necta, mwaka 2010 kulikuwa na watahiniwa kidato cha nne 441,426 ikilinganishwa na watahiniwa 339,925 mwaka 2009, sawa na ongezeko la watahiniwa 101,501.

  Katibu Mtendaji huyo wa Necta alibainisha kuwa utaratibu wa kusahihisha mitihani ni ule wa ‘conveyer belt’ ambao unamruhusu mwalimu mmoja kusahisha swali moja tu kisha na kumpasia msahihishaji mwenzake.

  “Utaratibu huu unalenga kuepuka uonevu unaoweza kuwakuta watahiniwa, kwa sababu kuna walimu wengine ni ‘strict markers’ (wasahihishaji wanaozingatia jinsi jibu lilivyo tu na si vinginevyo) na wengine ni ‘liberal markers’, (wasahihishaji wanaoweza kutoa alama kwa mtazamo kwamba mtahiniwa alikuwa akielekea kwenye jibu),” alifafanua.

  Alisema katika chumba cha kusahihisha mitihani pia wanakuwepo ‘checkers’ (wakaguzi) ambao pia wana wajibu wa kukagua iwapo usahihishaji, uwekaji wa alama na ujumlishaji wake umefanyika kwa usahihi, na kwamba pale wanapobaini kasoro yoyote, karatasi husika hurejeshwa kwa msahihishaji aliyekosea ili kuondoa kasoro hiyo.

  “Tuko makini katika usahihishaji na pale inapobainika kwamba makosa katika kusahihisha yanatoka kwa mtu yule yule kila wakati, basi huyo huwa tunamwondoa mara moja katika timu ya wasahihishaji wetu,”alisisitiza.

  Ufafanuzi wa Dk Ndalichako katika suala hilo ni kama jibu kwa Chama na Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi nchini (Tamongsco), ambacho mwanzoni mwa mwezi huu kilitoa tamko la kupinga matokeo ya mtihani huo wa kidato cha nne wa mwaka jana kwa madai kwamba “ulisahihishwa kwa muda mfupi”, hali iliyochangia matokeo mabaya kwa wahitimu.

  Katibu wa Tamongsco, Benjamin Nkonya alisema chama chake kinapendekeza “usahihishaji mpya” wa mitihani hiyo, jambo ambalo Dk Ndalichako alisema haliwezekani kwani hakukuwa na kasoro zozote katika usahihishaji.

  Utunzi wa Mitihani…………..
  Kuhusu utunzi wa mitihani, Dk Ndalichako alisema, walitumia mitaala ya masomo iliyopitishwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania.
  Alisema kwa mujibu wa maoni ya wasahihishaji wa mtihani wa mwaka jana wa kidato cha nne, hata kiwango cha ugumu wa mtihani huo hakitofautiani sana na mtihani wa mwaka 2009.

  “Kila tunapomaliza kusahihisha huwa tunapata maoni ya wasahihishaji kwa njia ya questionnaire (hojaji), ambapo masomo 39 kati ya 46 ya mwaka jana, wasahihishaji wanasema 'level of difficulcy' (kiwango chake cha ugumu) kilikuwa sawa na mitihani ya mwaka juzi,”alisema Ndalichako na kuongeza:

  “Kwa masomo sita kiwango cha ugumu kilikuwa chini kuliko cha mwaka juzi, na ni somo moja tu la 'physical education' (elimu mazoezi na michezo) ambalo wasahihishaji walisema lilikuwa gumu kuliko mtihani uliotangulia”.

  Alisema kutokana na maoni hayo, Necta inaamini kwamba mtihani ulitungwa sawa na mitihani mingine kwani wasahihishaji ni walimu kutoka shule za sekondari za serikali na za binafsi.

  “Hawa ni walimu kutoka shule za serikali na zile za binafsi, sasa iweje leo hawa wamiliki wa shule za binafsi walalamikie baraza?, Mimi nasema hatupaswi kulaumiwa,” alisema.

  Sababu za wanafunzi kufeli
  Kuhusu idadi kubwa ya wanafunzi kufeli mtihani huo, Dk Ndalichako alisema Necta hawawezi kufahamu sababu hizo moja kwa moja, lakini akabanisha kuwa inawezekana “watahiniwa hawakuwa wameandaliwa vizuri”.

  “Kama mwanafunzi anaingia darasani kufanya mtihani na anaandika namba ya mtihani tu halafu anakusanya, hapo utasema nini? Ni dhahiri kwamba huyu (mtahiniwa) hakuwa na kitu cha kuandika, hakuandaliwa vizuri,” alisema na kuongeza kuwa huenda kulikuwa na maandalizi hafifu kwa watahiniwa kiasi cha kushindwa kuandika chochote.

  Ndalichako alionekana kukwepa kuzungumzia wingi wa sekondari za kata kama sababu ya kufeli kwa wananfunzi, badala yake alisisitiza ufanyike uchunguzi ili kupatikana kwa majibu yatakayowezesha utatuzi wa suala hilo.

  "Hata shule ambazo zilikuwa zikifanya vizuri, baadhi yake zimefanya vibaya hivyo kwenda kwenye conclusion (hitimisho) la moja kwa moja kwamba shule mpya ndizo zimechangia matokeo kuwa mabaya nadhani siyo sahihi,"alisisitiza.

  Alisema sababu nyingine inayoweza kuwa ilichangia matokeo hayo mabaya ni udanganyifu, kuvuja na wizi wa mitihani ya darasa la saba ulitokea mwaka 2006.

  Alisema kwa bahati mbaya wanafunzi hao hao ni wale ambao hawakuchujwa kidato cha pili, kufuatia serikali kufuta mtihani huo mwaka 2008.

  “Mwaka ule wa 2006 tulilazimika kutoa (special provision) mtihani maalum kwa baadhi ya watahiniwa kutokana na udanganyifu uliojitokeza, nakumbuka mfano mkoani Dodoma mtihani wa Kiingereza ulirudiwa katika shule 52,” alisema Dk Ndalichako na kuongeza:

  “Sasa inawezekana, nasema inawezekana ikawa sababu ambayo pia imechangia wanafunzi kufeli sana mwaka huu, maana hatuwezi kujua kwamba wengi waliofaulu kuingia kidato cha kwanza kupitia mtihani ule, walifanya udanganyifu”.

  Alisema mwaka huo wa 2006 katika wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro shule nyingi zilifanya vizuri lakini ulibainika udanganyifu wa hali ya juu kwani wanafunzi walikosa maswali yale yale na makosa yalikuwa yakifanana.

  Aliongeza kuwa wananfuzi hao walipopewa mtihani mwingine ni asilimia 11 tu ya watahiniwa waliofaulu na kwamba uchunguzi ulibaini kuwa wahusika wa kuvuja kwa mitihani hiyo walikuwa ni wakuu wa shule, waratibu wa elimu kata na maofisa elimu.

  “Wengi wanafanya hivi ili wilaya zao zisionekane kuwa zimefanya vibaya, sasa hapa ndipo tunaposema kwamba lazima tusaidiane kwani athari zake zinaweza kuwa ndio hizi tunazoziona, kuwa na matokeo mabovu ya kidato cha nne,”anasema Dk Ndalichako.
   
 2. G

  Gad ONEYA JF-Expert Member

  #2
  Feb 26, 2011
  Joined: Oct 26, 2010
  Messages: 2,641
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 135
  I concur with huyu mama! Wanafunzi wengi hawajiandai vizuri kwaajili ya mitihani, licha ya kutoandaliwa na walimu! Wazazi pia waepuke kutoa pesa kuwanunulia watoto wao mitihani!
   
Loading...