Hatua za haraka zinahitajika kukabili upotoshaji huu

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
KWA muda mrefu kumekuwa na madai ya kuwepo kwa taarifa na matangazo kutoka nchi jirani ya Kenya, ambayo pamoja na kutangaza utalii wa nchi hiyo, lakini kwa namna moja ama nyingine yamekuwa yakipotosha kwa kutangaza baadhi ya rasilimali za Tanzania kuwa zipo nchini humo.

Tabia hiyo ya kujimilikisha rasilimali hizo, hasa zile muhimu ambazo pamoja na kuipatia sifa nchi, lakini ni vivutio vikubwa kwa sekta ya utalii, imedumu kwa muda mrefu, ambapo hata Serikali yenyewe kuna kipindi ilibidi ichukue hatua ya kufafanua kuhusu rasilimali hizo.

Rasilimali ambazo nchi hiyo kupitia taarifa na matangazo yake, imekuwa ikijimilikisha kwa jamii kubwa za kimataifa ni pamoja na kudai kuwa Mlima Kilimanjaro uko nchini Kenya pamoja na mbuga ya Serengeti.

Katika matangazo hayo, nchi hiyo ilibainisha wazi kuwa mlima huo uko Kenya pamoja na mbuga ya wanyama ya Serengeti, ambayo nchini humo huitwa Mbuga ya Mara. Hata hivyo, baada ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Bodi ya Utalii kuingilia kati suala hilo, nchi hiyo ilibadilisha tangazo hilo na sasa limebaki kuwahimiza watalii watembelee Kenya ili wauone mlima huo.

Wakati bado suala hilo likiwa halijapatiwa ufumbuzi wa kutosha, hivi karibuni kumezuka mzozo na malumbano katika mitandao ya kijamii bado ya Watanzania na Wakenya kuhusu hoja hiyo ya nchi ya Kenya kujimilikisha rasilimali za Tanzania, wakiwemo wana muziki wanaofanya vizuri.

Sakata hilo liliibuka baada ya kusambaa kwenye mitandao hiyo ya kijamii video inayomuonesha mwanadada raia wa Kenya, Rosemary Odinga akidai kuwa Fuvu la Mtu wa Kale liligunduliwa Olduvai Gorge iliyopo nchini Kenya.

Mwanadada huyo alikuwa akihutubia katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa uliofanyika jijini New York. Aidha, kabla ya kutokea sakata hilo lililozua mjadala, siku kadhaa zilizopita katika mitandao hiyo, pia ilizagaa taarifa inayodaiwa kutolewa na mmoja wa watumia mitandao nchini Kenya, ikitangaza ‘single’ mpya ya muziki kati ya mwanamuziki wa Afrika Kusini, AK na wa Tanzania, Nasib Abdul maarufu kama Diamond Platnumz.

Katika taarifa hiyo, ilidai kuwa singo hiyo imeongoza kwa kuangaliwa na kufikisha mashabiki zaidi ya milioni na kudai kuwa AK ameshirikiana na Diamond Platnumz, ambaye ni rapa wa Kenya.

Ukweli ni kwamba, taarifa hiyo ya mwanadada Odinga na taarifa hiyo kuhusu Diamond, iliamsha hasira za watanzania na kudai kuwa sasa Wakenya wanapotosha kwa makusudi kuwa Oldupai Gorge iko kwao na Diamond ni Mkenya, ili kujitangaza na kuongeza zaidi utalii. Diamond ni mwanamuziki wa Tanzania anayefanya vizuri kwa sasa katika Afrika na dunia kwa ujumla baada ya kujinyakulia tuzo kadhaa za kimataifa.

Oldupai Gorge ni eneo la kiakiolojia linalopatikana katika mkoa wa Manyara nchini Tanzania, ambalo lipo katika Hifadhi ya Ngorongoro na karibu na Hifadhi ya Serengeti. Ni mahali ambapo zamadamu, viumbe wa kale waliokaribiana na mwili wa binadamu, waliishi tangu miaka milioni mbili iliyopita.

Katika eneo hili mwanaakiolojia Mary Leakey ndipo alipogundua fuvu la kichwa la kiumbe wa kale wa jamii hiyo la Paranthropus boisei (pamoja na mumewe alimuita kwanza Zinjanthropus) ambalo lipo katika makumbusho ya Dar es Salaam.

Ni wazi kuwa kwa haya yanayotokea haitoshi tu kwa Serikali na watanzania kwa ujumla, kukanusha taarifa hizi pekee, bali kunahitajika hatua za haraka za kuihakikishia dunia kuwa vivutio hivi na wanamuziki wetu wanaofanya vizuri ni vya Tanzania.

Mamlaka husika lazima zitambue kuwa biashara haiishii kwenye bidhaa bora tu, bali inakwenda zaidi ya hapo ikiwemo ubunifu. Hivyo ni vyema zikatumia mbinu mpya za kuhakikisha dunia inatambua wazi kuwa rasilimali za Tanzania, zinapatikana Tanzania na si kwingine.
 
Back
Top Bottom