Hatma ya Raila Odinga kwenye siasa za Kenya

waterproof

JF-Expert Member
Aug 14, 2020
387
348
Tangu kuwepo kwa ushirikiano kati ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga mnamo Machi 9, 2018, kumekuwepo na maswali chungu nzima kuhusu hatma ya kisiasa ya Bw. Raila Odinga katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022 nchini Kenya.

Wengi wamekuwa wakikisia na kujaribu kuweka kwenye mizani suala la iwapo Bw. Raila Odinga atakuwa kwenye debe mwaka wa 2022 kuwania Urais kwa mara ya tano.

Matamshi ya hivi karibuni ya Naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee na ambaye pia ni mwandani wa Rais Kenyatta na Katibu Mkuu wa chama kikuu cha wafanyikazi nchini Kenya (COTU) Francis Atwoli yanaonekana kuchochea fikra hizi ingawa kinara wa chama cha ODM mwenyewe hajalivalia njuga suala hili.

Wendani wengi na wafuasi wa kiongozi wa upinzani Bw. Raila Odinga wanaamini kwamba ni yeye tu anayeweza kumshinda Naibu Rais William Ruto, ambaye uhusiano wake na Rais Kenyatta umeendelea kudorora miezi ya hivi karibuni, kwenye uchaguzi wa 2022.

"Ikiwa kuna mtu ambaye anaweza kumsimamisha huyu mtu (Ruto) kutokuwa Rais, ni aliyekuwa Waziri Mkuu. Hakuna mwingine yeyote." Bw. Murathe amenukuliwa akisema mara kwa mara.

Itakumbukwa kwamba Naibu Rais, William Ruto alikuwa akiandaa mikutano mingi ya kisiasa ambayo wengi walioona kama yenye kujitafutia umashuhuri kwa jukwa la kisiasa nchini Kenye na kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.

Miezi ya hivi karibuni, Bw. Murathe na Seneta wa Siaya James Orengo pia wamekuwa wakitoa matamshi kama haya ya kumuunga mkono Bw. Odinga kungangania Urais huku wakisema kuwa Rais Kenyatta na Bw. Odinga walikuwa wakiunda muungano ambao ungepelekea kinara wa chama cha ODM kupambana na Naibu Rais William Ruto kwenye uchaguzi mkuu ujao nchini Kenya.

Kinara wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, kinara wa Maendeleo Chap Chap, Alfred Mutua, pia wametangaza azma zao za kuwania Urais.
Bw. Murathe amekuwa akieleza kwamba ushirikiano kati ya Rais Kenyatta na Raila Odinga ni jambo muhimu kwa taifa la Kenya na ni kitovu cha msingi wa maendeleo makubwa ya kisiasa nchini kwa miaka 50 ijayo nchini Kenya.

Jambo hili limeonekana kuashiria kwamba mradi wa BBI na ushirikiano kati ta Rais Kenyatta na Bw. Odinga tangu mwaka wa 2018 umekuwa na malengo ya kisiasa.
Odinga anafaa kustaafu siasa Kenya?
Wasifu wa Raila Odinga, kiongozi wa upinzani Kenya

Kuna dalili ambazo zimekuwa zikionyesha kuwa ushirikiano baina ya Rais Kenyatta na Bw. Odinga haukuwa bure tu bali malengo ya muda mrefu.

Odinga
Kwanza, tangu ushirikiano wake na Rais Uhuru Kenyatta kuanzia Machi 9, mwaka wa 2018, imekuwa bayana kwamba Bw. Odinga ana wadhifa na nafasi maalum kwenye serikali ya Kenya hasa ikizingatiwa uhusiano wake wa karibu na Rais Uhuru Kenyatta ambao umezaa mpango wa maridhiano wa BBI.

Kuna ishara kwamba BBI ni mhimili mkubwa katika uhusiano wa wawili hao. Kabla ya majilio ya Covid-19, wawili hawa walikuwa wakifanya mikutano ya kiasiasa pamoja na kuonyesha ishara za kushirikiana pakubwa kwenye shughuli za siasa zao.

Katika mikutano hiyo, Bw. Raila Odinga alikuwa akisherehekewa sana kama mwanasiasa shupavu na wakati huo huo kumlinganisha na kumuumbua Naibu Rais Dkt. William Ruto, na kuwashusha wanasiasa wengine kihadhi kama walio wachanga sana kwenye siasa za Kenya wakilinganishwa na Raila Odinga.

Kwa upande wake Naibu Rais, William Ruto amekuwa akiendelea na kampeini zake akiwashawishi Wakenya kuhusu azma yake ya kuwania Urais mwaka wa 2022.

Pili, tangu kuingia kwake kwenye ulingo wa siasa za Kenya, Bw. Raila Odinga hajawahi kuonekana kuwa na nguvu za kisiaza kama zile alizonazo sasa kupitia uhusiano huu.

Kwa hakika, kiongozi huyu wa upinzani hajawahi kuwa na uwezo mkubwa na ushawishi serikalini nchini Kenya hata wakati alipokuwa Waziri Mkuu katika serikali ya Rais Mwai Kibaki, ama alipokuwa waziri mara mbili, ama hata alipokuwa katibu mkuu wa chama tawala cha Kanu.

Kihistoria, katika siasa za Kenya, tangu uhuru, hakujawahi kuwepo na mwanasiasa ambaye hajachaguliwa ambaye amewahi kuwa na nguvu na ushawishi mkubwa serikalini miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu kama alivyo Bw. Odinga.

Itakubukwa kwamba Bw. Raila Odinga alikuwa na umashuhuri mkubwa miezi ya kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2007 ambao ulikumbwa na vita vya ndani kwa ndani na baadaye kuwepo mshirika kama waziri mkuu katika serikali iliyoundwa baadaye, chini ya Rais Mwai Kibaki. Wakati huo, alikuwa akishidana na Rais aliyekuwa mamlakani, Mwali Kibaki. Tofauti na ilivyokuwa wakti huo, sasa Rais aliyepo mamlakani ndiye mshirika wake na mwendani wake mkuu.

Pia, kando na Raila, hakuna mwanasiasa yeyote nchini Kenya ambaye hajachaguliwa ambaye amewahi kuwa na ushawishi bila kuwa na afisi kikatiba na muundo msingi vyote ambavyo vinalipwa na ushuru wa Wakenya. Bw. Raila anayafanya haya. Zaidi ni kwamba, ni bayana kwamba afisi ya Raila Odinga, inashauriwa na kutoa ushauri na mawaziri, na wafanyikazi wengine wakuu serikalini kuhusiana na miradi mbali mbali nchini Kenya. Pia, Bw. Odinga huwaagiza wakuu hawa na mawaziri kama kwamba yeye ndiye mkuu wao. Hali hii, bila shaka, ina baraka za Rais Kenyatta. Hii inaonyesha kwamba, ikiwa atawania Urais nchini Kenya mwaka wa 2022, basi atakuwa mmoja kati ya wale ambao tayari wanaelekeza Kenya na siasa zake.

Au tuseme, labda hii ndiyo BBI, gari la kisiasa la Bw. Odinga la kumpeleka ikuluni?
Aidha, nguvu na haiba za kiti cha Urais zimetumika kikatiba na kisiasa, kichinichini na wazi, ili kurahisisha kazi ya kutafuta Urais kwa Raila Odinga

Masuala ya mradi wa BBI na ushirikiano kati ya Rais Kenyatta na Bw. Odinga ndilo lililopelekea kutengana kisiasa kati ya Rais Kenyatta na naibu wake, Dkt William Ruto. Kutokana na haya, wendani na marafiki wa kisiasa wa Bw. Ruto wameondolewa kwenye nyadhifa zao katika bunge la kitaifa na kwenye seneti.

Hali hii imepelekea Naibu Rais kuonekana kunyanganywa nguvu za kimamlaka na kisiasa huku ukuruba kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ukiendelea kunawiri. Rais Kenyatta mwenyewe amenukuliwa mara nyingi akimsifu na kumpa sifa nyingi na kueleza kuwa bila Bw. Odinga, Kenya haingekuwa na amani iliyonayo.

Huku Naibu Rais William Ruto akiwa amewekwa kando katika maamuzi muhimu na shughuli za serikali ikiwemo kwenye baraza la mawaziri, mikutano ya kisiasa, maamuzi muhimu, Raila Odinga anaonekana wazi kuwa mwenye wadhifa mkubwa serikalini, labda chini tu ya Rais Kenyatta.

Pia, ni bayana kuwa kufika mwaka wa 2022, Mpango wa Rais Uhuru Kenyatta na malengo yake hayatakuwa yamefikiwa. Kwa sababu hii, njia ya pekee ya kuhakikisha kuwa malengo haya yatafikiwa, inavyobainika, ni kuhakikisha kuwa kuna uhusiano mzuri kati ya jamii za Agikuyu na Luo, uhusiano ambao uliharibika wakati babake alipomsaliti babake Raila, Jaramogi.

Jamii ya Agikuyu imekuwa kimkataa Bw. Odinga kisiasa ingawa babake alikataa kuwa waziri mkuu wakati wa ukoloni, akisisitiza kuwa hakungekuwepo na uhuru nchini Kenya bila kuachiliwa kwa Kenyatta ambaye alikuwa kizuizini.

Kutokana na haya, Rais Kenyatta anaonekana kutaka kulipa jamii ya waluo 'deni la kisiasa' ambalo babake alipata kwa kumsaliti Jaramogi.

Suala linguine ambalo litaonyesha mwelekeo wa kinyanganyiro cha mwaka wa 2022 ni kura ya maamuzi ambayo haijulikani iwapo itakuwepo au la na itafanyika lini. Bw. Odinga na Rais Kenyatta wamekuwa wakishikilia kwamba kura hii itakuwepo. Ikiwa na wakati kura hii ya maamuzi ambayo itakuwa na msingi wake kwenye BBI itafanyika, matokeo yake yatakuwa kipimo yakini kuelekea kinyanganyiro cha uchaguzi wa mwaka wa 2022.

Hii ni kwa sababu, matokeo yake huenda yakaamua mfumo wa serikali ambao utakuwepo hata kabla ya uchaguzi wa mwaka wa 2022. Kwa sababu hii, huenda serikali ya mseto ikaundwa na ikifanyika hivi, Bw. Odinga atakuwa kifua mbele kuelekea uchaguzi wa 2022.

Kwa sasa, kuna mengi yanayoendelea kufanyika katika siasa za Kenya na yatasaidia sana katika kufikia uamuzi wa iwapo Raila Odinga atawania Urais mwaka wa 2022 au la.
 
Safari hii hatufanyi makosa.. hatuwezi kuchagua wale ambao wanatafuna nchi wao na famila zao na kuacha maelfu ya wakenya wamejichokea kwa njaa

Husler Ruto anatosha 2022.
 
Huyo Mutua ana kitu inaitwa Maendeleo Chap Chap? Kumbe ndo maana anabishana sana na sera za serikali ya Tanzania adharani. Anaonekana ana lugha flani tata.
 
Safari hii hatufanyi makosa.. hatuwezi kuchagua wale ambao wanatafuna nchi wao na famila zao na kuacha maelfu ya wakenya wamejichokea kwa njaa

Husler Ruto anatosha 2022.
Una his I ruto hatoweza kufanya anachofanya Kenyatta now.
 
Ruto sio mwizi kama uhuru, anajali watu wote..he only care for kenyans and its prosperity.. unlike those two looters who care about their pocket.
Kwa ruto nae is ones of members of government in kenya so me nadhani kundi Leo ni moja tu
 
Ruto ni mtu makini.. ndio maana uhuru anamuogopa..venye akiwa prezo ata confsicate zile hela zote kaibia wakenya.
Hana huo ujanja Ruto bila Uhuru SI kitu. Coalition ya Sasa Ni Uhuru+Gideon Moi (KANU, Rift Valley)+Raila (Nyanza, Pwani +Mandera& Garissa).
**Gideon anam-replace Ruto kwenye siasa za ukanda Wa Rift Valley.
NB:Kutoboa Siasa za Kenya Lazima ufanye Coalition na Kikuyus (Central), Nyanza (Luo) na Pwani (Mombasa, Kwale, Taveta, Kilifi)
 
Hana huo ujanja Ruto bila Uhuru SI kitu. Coalition ya Sasa Ni Uhuru+Gideon Moi (KANU, Rift Valley)+Raila (Nyanza, Pwani +Mandera& Garissa).
**Gideon anam-replace Ruto kwenye siasa za ukanda Wa Rift Valley.
NB:Kutoboa Siasa za Kenya Lazima ufanye Coalition na Kikuyus (Central), Nyanza (Luo) na Pwani (Mombasa, Kwale, Taveta, Kilifi)

Wizi wa uhuru na genge lake umetosha.. wakenya tunataka ruto saiv
 
Back
Top Bottom