Hatma ya fao la kujitoa kujulikana leo | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Hatma ya fao la kujitoa kujulikana leo

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Mamboleo, Oct 30, 2012.

 1. M

  Mamboleo Member

  #1
  Oct 30, 2012
  Joined: Oct 15, 2008
  Messages: 69
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 15
  Hatma ya fao la kujitoa kujulikana leo


  Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika
  Serikali itawasilisha tamko la kuruhusu fao la kujitoa katika Mkutano wa Tisa wa Bunge, unaotarajia kuanza leo mjini hapa.

  Hatua hiyo imetokana na baadhi ya wabunge na wananchi kulalamikia Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2012 inayozuia mwanachama kunufaika na fao la kujitoa hadi atakapofikisha umri wa kustaafu kwa hiari wa miaka 55 ama kwa lazima wa miaka 60.

  Taarifa kutoka ndani ya serikali, ilibainisha kuwa serikali itawasilisha tamko hilo na hivyo kufuta barua ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Irene Isaka.

  Katika barua hiyo, Isaka alibainisha kuwa serikali imefuta fao hilo la kujitoa na kuzuia wanachama kuchukua mafao yao hadi wanapofikisha umri wa kustaafu.

  "Serikali imeona kisheria haiwezekani kumzuia mfanyakazi kujitoa kwenye mfuko wowote hivyo imeamua kuwasilisha taarifa yake rasmi ya kufuta muswada wake iliokuwa iuwasilishe, ambao ulionekana una mapungufu na hivyo kuifuta barua ya SSRA," kilisema chanzo cha taarifa hiyo bila kufafanua zaidi.

  NIPASHE ilipomtafuta kwa njia ya simu Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka, na Naibu wake, Dk. Makongoro Mahanga, ili kufafanua hawakupatikana.

  Awali, Ofisa Habari wa Bunge, Prosper Minja, alipotakiwa kueleza kuhusiana na shughuli zitakazofanyika katika Mkutano wa Bunge unaoanza leo, aliwataka waandishi wa habari kusubiri hadi leo jioni.

  Katika mkutano wa Nane wa Bunge la Bajeti, Mbunge wa Kisarawe, Suleiman Jafo (CCM), aliwasilisha hoja binafsi bungeni ya kutaka Bunge liazimie kuiagiza serikali ile muswada wa marekebisho ya sheria hiyo kwa dharura na kufuta barua ya kuzuia fao la kujitoa iliyotolewa na SSRA.

  Jumatano wiki iliyopita wabunge wakiwa katika vikao vya kamati jijini Dar es Salaam, walipewa muswada wa serikali wenye lengo la kufanyia marekebisho sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2012, lakini marekebisho hayo yalihusu Mfuko wa PPF pekee.

  Kwa mujibu wa Jafo, muswada huo waliopelekewa ulikuwa na upungufu na hivyo, kuitaka serikali kuufanyia marekebisho na pia kuuleta kwa hati ya dharura kama walivyokubaliana katika azimio hilo la Bunge.

  Awali, Jafo aliwasilisha muswada binafsi bungeni wa kutaka sheria hiyo, hususan kipengele chake kinachomtaka mfanyakazi kupata mafao yake baada ya kufikisha umri wa kustaafu kwa hiari miaka 55 au 60 kirekebishwe.

  Jafo, ambaye alizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi Ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam Oktoba 16, mwaka huu, alisema alifikia uamuzi huo baada ya kuona kukiwa hakuna dalili kwa serikali kuwasilisha bungeni muswada wa marekebisho ya sheria kama ilivyoahidi.

  Hatua hiyo ya Jafo, ilichukuliwa siku moja baada ya Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, kuwasilisha kwa Katibu wa Bunge kusudio la kuwasilisha muswada binafsi wa sheria hiyo kwa hati ya dharura.

  Jafo akizungumzia hatua hiyo ya Mnyika, alisema mbunge huyo (Mnyika) anadandia hoja hiyo kwa kuwa ni yake (Jafo).

  Hata hivyo, wakati Jafo akisema hayo, Oktoba 8, mwaka huu, Waziri Kabaka, aliliambia NIPASHE kuwa mchakato wa kusahihisha sheria hiyo kabla ya kupelekwa bungeni, umefika mbali na kwamba, muswada wa marekebisho ya sheria hiyo utawekwa hadharani kupitia Bunge kwa kuwa ndilo lililoagiza suala hilo kufanyika.

  Hoja ya kutaka suala hilo lijadiliwe upya ilitolewa na Jafo bungeni Julai 25, mwaka huu, na kuungwa mkono na wabunge.

  Hoja ya Jafo ilitokana na kuwapo kwa taarifa kuwa zaidi ya wafanyakazi 600 katika migodi minane nchini wameacha kazi huku wengine zaidi ya 4,000 wakiwa tayari wamewasilisha barua za kuacha kazi kutokana na sheria hiyo.

  Minja alisema jana Kamati ya Uongozi chini ya Mwenyekiti, Spika wa Bunge, Anne Makinda, imeshakaa na kupanga shughuli za Bunge.

  Alisema leo baada ya kumalizika kipindi cha maswali na majibu, kutafanyika vikao vya kamati mbalimbali za Bunge na kamati za vyama vya siasa na baadaye wabunge wataelezwa ratiba ya shughuli za Mkutano wa Tisa wa Bunge la Kumi.


  CHANZO: NIPASHE
   
Loading...