Harakati za Ukombozi wa Tanzania na Mustakabali wake

Jul 16, 2012
55
43
UKOMBOZI ni kitu kimoja cha ajabu sana, napenda kukiita cha ajabu kwa sababu wakati watu wengine wanajitahidi kuleta ukombozi wapo wengine wanaojaribu kuzuia ukombozi. Sababu zinakuwepo nyingi lakini katika akili ya kawaida kabisa na ya kibinadamu kama utazuia ukombozi wa watu au vitu basi akili yako itakuwa ina walakini.

Nchi yetu TANZANIA na nchi nyingine duniani inawezekana katika bara hili la Afrika au mabara mengine ya dunia zimepitia hatua mbalimbali za ukombozi, hatua hizi zote zikiwa na lengo la kuleta haki zilizo sawa kwa watu wote.

Wakati wa ukoloni mkongwe ilikuwa ni rahisi kwa viongozi wa ukombozi wa kipindi kile kuweza kuwaonyesha wananchi wao adui yao mkubwa wanayepambana naye kwamba ni mkoloni mweupe ambaye anatokea Ulaya, na kwa wananchi walio wengi ilikuwa rahisi kumtambua kwani MKOLONI MWEUPE (alas: Mzungu) alikuwa anaonekana hata kwa macho tu, na watu wale wajinga wa kipindi kile ambao walikuwa wanatumika na wakoloni weupe kuweza kuwasaliti au kushirikiana na mkoloni mweupe kuwakandamiza wenzao walikuwa wanaonekana ni VIBARAKA WABAYA katika jamii iliyokuwa inawazunguka, na vibaraka hao kwa ujinga wao walikuwa wanajiona kwamba wao ni wateule katika tawala zile bila kufahamu kuwa walikuwa ni MBWA TU WA KUTUMWA na watawala wale na walikuwa wanakula makombo tu ya chakula kinachoanguka kutoka kwenye meza za mabwana zao, vibaraka hao walikuwa wanavimba vichwa vyao kwa fadhila za kijinga kabisa ambazo mtu mwenye akili timamu usingeweza kuamini kwamba zinalingana na usaliti waliokuwa wanaufanya.

Nchi yetu (Taifa letu) ya TANZANIA haijatengwa katika harakati za ukombozi, kama nilivyoelezea hapo awali harakati hizi zimeanza hata kabla ya nchi yetu kupata uhuru na bado zinaendelea kwani bado haki haipo kwa kila mtu, harakati hizi huwezi kuzizuia hata kidogo iwapo haki inakuwa hakuna, ni ujinga usiothimilika kuweza kufikiria kwamba kuna siku harakati za ukombozi zitaweza kuisha, sana sana zitazidi kuongezeka.

Changamoto inayozikuta harakati za ukombozi wa nchi yetu kwas asa ni kumtambua adui tunayepambana naye, kwani adui amegeuka kutoka MKOLONI MWEUPE kuwa MTANZANIA MWEUSI ambaye sio rahisi kumtambua kwani wengi wetu tunamuona ni mwenzetu kama sisi tulivyo, Mtanzania huyu mweusi ndiye tuliyemkabidhi dhamana ya kututoa pale tulipo (JANGWANI) na kutupeleka nchi ya ahadi (ASALI NA MAZIWA), Mtanzania huyu mweusi ameona kwamba safari ya pamoja inachelewa hivyo ameamua yeye pamoja na vibaraka wake kutangulia nchi hiyo ya asali na maziwa na kisha kuhuisha juhudi zozote zitakazopelekea walio wengi kufika huko, anataka abaki siku zote yeye peke yake na wateule wake wachache na familia zao ili waweze kuishi maisha ya peponi na kubaki wakitushangaa kwamba tunatakia nini kuingia nchi hiyo wakati Jangwani tunaweza kuishi tu, OLE WAO WATU HAO, nasema Ole Wao, kwani harakati za ukombozi siku zote haziwezi kuisha, OLE WAO NA VIBARAKA WAO, wao wenye kuwasaliti ndugu zao wanyonge, kwani saa ya ukombozi ikifika tutawafunga mawe mazito shingoni na kuwatumbukiza baharini.

Tulikuwa tukishangaa filamu mbalimbali za ukombozi katika harakati za kupigana dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika ya Kusini zikionyesha jinsi Waafrika weusi (VIBARAKA) walivyokuwa wakiwasaliti Waafrika wenzao na kutoa siri za vita ya ukombozi kwa adui yao ambaye ni utawala dhalimu wa Makaburu kwa fadhila za kijinga kabisa, inawezekana zile ni filamu tu lakini nataka kujiaminisha kwamba mambo kama hayo yaliweza kweli kutokea kwani tukiangalia mwenendo wa mambo ulivyo katika nchi yetu tunaona jinsi ambavyo wenzetu wachache wanavyotumika na Watawala kuvunja nguvu juhudi za ukombozi, maswali la kujiuliza; Je vibaraka hawa hawaoni jinsi wanavyotumiwa na watawala dhalimu kuteketeza/kuharibu juhudi za kumkomboa Mtanzania masikini ambaye kikubwa anachokitaka ni mahitaji yake muhimu ya maisha na haki yake kama raia?

Je Vibaraka hawa hawatambui kwamba Watawala wanaowapigania wanawalipa ujira mdogo sana ambao ni sawa sawa na makombo yanayondoka mezani ukilinganisha na utajiri ambao wao wanajilimbikizia?

Je vibaraka hawa hawatambui kwamba juhudi hizi za ukombozi zina nia ya kuwakomboa wao, familia zao, ndugu zao na Watanzania wenzao wote kwa ujumla ? Je vibaraka hawa wanakuwaje na upeo mfupi wa mawazo kuweza kutambua kwamba tawala dhalimu wanazozipigania zinawadhamini tu pale wao wanapokuwa na manufaa kwao, pindi thamani yao inapokuwa imeisha hawataweza kudhaminiwa tena na watatupwa nje/jalalani kama chumvi isiyokuwa na ladha?

Sasa najiuliza, ujira huu wa Makombo ya Mezani ndio kweli unakufanya uwasaliti ndugu zako?

Nimejikuta nachukua nafasi kubwa kuongelea habari za vibaraka kwa sababu vita vingi vya ukombozi huwa zinakwamisha na vibaraka kwani vibaraka huwa wanapandikizwa na tawala dhalimu kwenye vikundi vya ukombozi ili kuvunjwa nguvu za ukombozi na bila ya wao tawala hizi zisingeweza kuwepo madarakani.

Yapo mataifa ambayo yalifikia mahali raia wake waliishiwa uvumilivu na wakaingia barabarani au msituni ili kuendeleza harakati hizi za ukombozi kwa kumwaga damu hadi ukombozi ukapatikana, tunashukuru kwamba raia wetu bado wana uvumilivu wa kuweza kudai ukombozi wao kwa NJIA YA AMANI kabisa ya SANDUKU LA KUPIGIA KURA.

Lakini jambo la kushangaza kabisa ni upofu walio nao viongozi wetu na vibaraka wao wa kutosoma alama za nyakati na kufahamu kwamba midhali hakuna HAKI harakati hizi huwezi kuzizuia,zitazidi kuendelea hadi hapo HAKI ITAKAPOPATIKANA.

Ningependa nitoe mifano michache ya viongozi ambao walishindwa kusoma alama za nyakati na matokeo yake ni kwamba wameishia mahali pabaya, tuchukue mifano ya viongozi wawili wa nchi za kaskazini mwa bara la Afrika, Hayati Kanali Muamar Gadaffi wa Libya na Hosni Mubarak wa Misri, kama miaka mitano nyuma wangepata wazo la kupumzika kuongoza mataifa yao na kuruhusu chaguzi huru basi naamini sasa hivi wangekuwa ni viongozi wastaafu wanaoheshimika katika mataifa yao, lakini viongozi hawa walitamani bado kuendelea kutawala jambo ambalo limepelekea mustakabali ambao naamini sio mzuri katika maisha yao, Yako wapi leo mahekalu aliyojenga Hayati Gadafi? Wako wapi leo watoto wa Hayati Gadafi na familia zao? Je ni nani leo kati yetu sisi wapumbavu wa dunia ya tatu anafahamu mahali ambapo mwili wa Hayati Gadafi umezikwa?

Je viongozi wetu na vibaraka wao ndio wanavyotaka maisha yao na ya familia zao yaishie hivyo? Nionavyo mimi nafasi ya kujirudi na kukaa pembeni kwasasa wanayo na gharama wanayotegemea kuilipa kwasasa ni ndogo kuliko wakisuburi NGUVU YA UMMA iwaweke pembeni, kwani kitakachowatokea baada ya hapo ni kilio na kusaga meno, utajiri wote wanaojilimbikizia watanyang'anywa, wao wenyewe wataishia gerezani na familia zao zitaishi ukimbizini.

NISINGEPENDA NIJE KURUDIA MANENO YANGU HAYA, MWENYE MASIKIO YA KUSIKIA NA ASIKIE.​
 
Back
Top Bottom