Hapo zamani za kale: Historia ya Mwalimu Thomas Staudtz Plantan na Clement Mohamed Mtamila

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,787
30,080
HAPO ZAMANI ZA KALE: HISTORIA YA MWALIMU THOMAS SAUDTZ PLANTAN NA CLEMENT MOHAMED MTAMILA

Ulikuwa ukiingia nyumbani kwa Mwalimu Thomas Plantan Mtaa wa Masasi kitu kimoja ambacho kitakushangaza ni "trophy," vichwa vya wanyama vilivyotundikwa katika ukumbi mzima wa nyumba yake.

Nyumba ya Thomas Plantan ilikuwa na haiba kwa urefu wake wa kwenda juu na upana wa ukumbi wake huu ambao ulipambwa na vichwa vya kongoni na swala.

Mwalimu Thomas Plantan mtoto wa Affande Plantan mkuu wa Germany Constabulary alikuwa mwindaji.

Kaijua bunduki toka udogoni kwani baba yake Chief Mohosh kutoka Kijiji Cha Kwa Likunyi Imhambane aliingia Tanganyika akifuatana na Hermann von Wissman kuja kupigana na Abushiri bin Salim Al Harith na Mtwa Mkwawa waliokuwa wanapambana na utawala wa Wajerumani Pangani na Kalenga.

Nyuma yake Chief Mohosh wa Shangaan alikuwa na kikosi cha Wazulu mamluki 400.
Katika hawa Wazulu 400 kuna baadhi walifia vitani katika ardhi ya Tanganyika katika vita hivi.

Katika Vita Vya Kwanza Vya Dunia (1914 - 1918) sasa Wazulu hawa wakipigana dhidi ya Waingereza chini ya Von Lettow Vorbeck Wajerumani ilipowadhihirikia kuwa wanashindwa vita Von Lettow Vorbeck na jeshi lake walivuka mpaka na kuingia Mozambique kujinusuru kukamatwa mateka wa vita.

Historia ya vita hii Kleist Sykes kaiandika yote katika mswada wake wa kitabu kabla ya kufa kwake wakati ule yeye akiwa katika jeshi hilo na Schneider Plantan, Kleist akiwa Aide de Camp wa Von Lettow Vorbeck.

Baba zao walipigana vita dhidi ya wananchi wa Tanganyika chini ya Wissman na watoto wakapigana vita dhidi ya Waingereza chini ya Vorbeck.

Bunduki kwa Mwalimu Thomas na hawa nduguze ilikuwa sawa na bakora ya kutembelea.

Wakati mimi naanza kuingia nyumba ya Mwalimu Thomas Plantan katika miaka ya mwishoni 1960 Mzee Thomas Plantan alikuwa hai.

Mjukuu wa Mwalimu Thomas Plantan, Bi Jasmine siku moja katika mazungumzo alinifahamisha kuwa babu yake alifariki siku ile Apollo 11 inapaa kwenda mwezini.

Nyumba hii ilikuwa jirani na nyumba ya John Rupia ambayo kabla ya Mzee Rupia kuinunua nyumba hii ilikuwa nyumba ya Mwalimu Cecil Matola Rais Mwasisi wa African Association.

Katika nyumba hii ndipo ulipofanyika mkutano wa kuasisi African Association mwaka wa 1929.
Atakae kuijua historia ya TANU mahali pa kuanzia ni nyumba hii.

Cecil Matola alifariki mwaka wa 1933.

Jirani na Mtaa wa Masasi kwa upande wa Kitchwele ilikuwa nyumba ya Mwalimu Nicodemus Ubwe na nyumba yake nyingine ilikuwa Mtaa wa Likoma.

Mbele ya nyumba hii hivi sasa limejengwa kanisa.
(Clement MTAMILA alimuoa bint ya Mwalimu Nicodemus Ubwe lakini alifariki muda mfupi).

Sehemu hii ilikuwa wazi kwa miaka mingi sisi tukiwa wadogo.
Mtaa huo wa Likoma akiishi Mwalimu Subeti Salum akisomesha useremala Shule ya Kitchwele.

Mwalimu Subeti alikuwa mpiga violin bingwa akipiga kikundi cha taarab cha Egyptian.
Mwalimu Subeti kawasomesha baba zetu wote waliopita Shule ya Kipata katika miaka ya 1940.

Mwalimu Subeti amezaliwa mwaka wa 1903 na kafariki 1974.
Mwalimu Subeti ni mmoja katika picha mashuhuri ya mwaka wa 1957 ya Baraza la Wazee wa TANU.

Wazee hawa wote niliowatambulisha kama walimu walikuwa walimu Kitchwele Government Boys School isipokuwa Mwalimu Thomas Plantan aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Mchikichini.

Zama zile kazi ya ualimu ilikuwa kazi yenye heshimanya juu sana kupitia kiasi.

Hawa wote walikuwa walimu wa kuheshimika katika mji wa Dar es Salaam na hakuna ambae hakuwa mwanachama wa TANU hakushiriki katika harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika.

Lakini siku katika mkutano wa hadhara Jangwani Bi. Titi Mohamed katika hotuba yake alimpamba Julius Nyerere kwa sifa yake ya ualimu na kusema kuwa Nyerere anawasomesha Waingereza siasa.

Kutokea siku hiyo hawa wote wakaacha kuwa walimu na cheo Cha ualimu na lakabu hiyo wakamvisha na wakamuachia Nyerere awe Mwalimu pekee Tanganyika nzima.

Ikawa mtu akitaja Mwalimu hafikiriwi Mwalimu Adam Maki wa Al Jamiatul Islamiyya au Mwalimu Thomas Plantan wa Shule ya Mchikichini au Mwalimu Steven Mhando wa Shule ya Kitchwele.

Mwalimu alikuwa Julius Kambarage Nyerere.

Walimu hawa wote niliowataja hapa waliishi Mission Quarters sehemu maalum Waingereza walitenga kwa makazi ya Wakristo katika ghilba zao za kuwagawa wananchi ili wabaguane watawalike vyema.

Hapa Mission Quarter ndiyo sehemu pekee katika mji wa Dar es Salaam palipojengwa kanisa dogo.

Kanisa la pili ndilo hilo mkabala na nyumba ya Mzee Ubwe lililokuja kujengwa miaka mingi sana baada ya uhuru kupatikana mwaka wa 1961.

Sasa turejee pale tulipoanzia kwa Mwalimu Thomas Plantan na Clement Mtamila.
Siku hiyo Ally Sykes kanichukua Mlandizi kwa Dossa Aziz.

Tulikuwa watatu Ally Sykes, mama mmoja Mmarekani Mweusi Mwandishi wa Washington Post aliyekuwa mgeni wa Ally Sykes na mimi.

Tuko nyumbani kwa Dossa Aziz Mlandizi barazani kwake.
Mimi nikamuuliza Mzee Dossa vipi vijana waliingia katika uongozi wa TAA mwaka wa 1950.

Kwa utulivu mkubwa Mzee Dossa akanihadithia kuhusu mapinduzi waliyofanya Abdul Sykes na Hamza Mwapachu kwa kuvamia ofisi ya TAA New Street na kuwatoa Mwalimu Thomas Plantan na Clement Mtamila ofisini na kuidhibiti ofisi kwa mabavu kwa siku chache.

Serikali ya Kiingereza haikuweza kustahamili jambo waliloliona ni vurugu za siasa za Waafrika wakaitisha mkutano wa wanachama wote ili ufanyike uchaguzi kama ilivyo desturi.

Dr. Kyaruzi katika mswada wake, ''The Muhaya Doctor," kaeleza mvutano uliokuwapo katika mkutano ule ambao mwishowe utangamano ulipatika.

Judith Listowel kanakili kipande hiki na kukitia katika kitabu chake, "The Making of Tanganyika,'' na kumtaja Schneider Plantan kama mmoja wa wanachama wa African Association aliyesaidia kuleta mabadiliko ya uongozi ndani ya chama.

Hivi ndivyo TAA sasa ikaingia katika uongozi wa Dr. Vedasto Kyaruzi kama President na Abdul Sykes Secretary.

Laiti kama Mzee Dossa asingenihadithia historia hii naamini ingelipotea na tusingeijua.

Kitu cha kustaajabisha kidogo ni kuwa katika wazee waliokuwa katika TAA ile ya viongozi wazee wa enzi ya Wajerumani na wengine walipigana ndani ya jeshi la Wajerumani dhidi ya Waingereza Vita Vya Pili Vya Dunia (1939 - 1945) kama Schneider Abdillah Plantan yeye alikuwa anaunga mkono vijana akishinikiza kaka yake Mwalimu Thomas Plantan atolewe katika uongozi waachiwe vijana.

Schneider Plantan alikuwa na azma vijana wachukue uongozi zianze harakati za kuidai Tanganyika irudishwe kwa Waafrika wenye nchi yao.

Hizi ndizo zilikuwa siasa za nyakati zile na inasikitisha unaposikia wanasiasa wanapoipa TAA sifa isiyokuwa yake ya kuwa ati TAA haikuwa na mwelekeo wa siasa.

Wazee hawa wa enzi ya Wajerumani kama Mzee bin Sudi, Mwalimu Subeti Salum, Mwalimu Thomas Plantan na Schneider Plantan na wengine wengi waliiona TANU ikiasisiwa mwaka wa 1954 na wakashuhudia bendera ya Tanganyika huru ikipandishwa juu mlingotini.

Mzee bin Sudi alifariki mwaka wa 1972 na Jaffar Nimieri Rais wa Sudan alipotembelea Tanzania mwaka 1972 alifika ofisi ya TANU akiwa na Nyerere na hotuba ya kumkaribisha Makao Makuu ya TANU ilisomwa na Mzee bin Sudi na picha yake akiwa na Nyerere na Nimieri ilitoka katika Daily News ukurasa wa mbele.

Jambo la kushukuru kuwa Mwalimu Nyerere alibahatika kukutana na kufahamiana na Mzee bin Sudi mmoja wa waasisi wa African Association mwaka wa 1928 na Al Jamiatul Islamiyya Fi Tanganyika mwaka wa 1933.

Viongozi hawa ndiyo waliojenga ofisi ya African Association aliyoikuta Nyerere alipokuja kuwa kiongozi wa TAA 1953.

Siku moja Abbas Sykes tukiwa tumebarizi katika majlis yetu nyumbani kwake Sea View akinieleza yale yaliyopitika hadi kufikia Nyerere kujiuzulu kazi ya ualimu aliniambia kuwa Clement Mtamila ndiye alikuwa Mwenyekiti wa TANU pale TANU HQ.

Barua ya Nyerere kutakiwa achague kati ya siasa au kazi ya ualimu Nyerere aliifikisha kwanza kwa Abdul Sykes na msimamo wa Abdul ulikuwa Nyerere aache kazi.

Kikao cha dharura cha Halmashauri Kuu ya TANU kiliitishwa nyumbani kwa Mzee Mtamila kama Mwenyekiti wa TANU na kikao kile kilimuunga mkono Mwalimu kuacha kazi ya ualimu na kuongoza harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.

Katika waliohudhuria kikao kile walikuwa Bi. Titi Mohamed na Bi. Tatu bint Mzee.

Huyu ndiye yule Clement Mtamila ambae vijana Abdul Sykes na Hamza Mwapachu walimtoa madarakani kwa mapinduzi.

Clement Mtamila juu ya msukosuko ule wa 1950 hakujiweka pembeni aliendelea kuwa katika siasa akachaguliwa kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya TANU na akawa Mwenyekiti wa TANU.

Ukitazama picha za ikutano ya mwanzo ya TANU Mnazi Mmoja utamuona Mzee Mtamila ni katika waheshimiwa waliokaa jukwaani na Nyerere pamoja na Bi. Titi Mohamed, Sheikh Suleiman Takadiri, John Rupia, Zuberi Mtemvu, Rajab Diwani na Mama Maria Nyerere.

Abbas Sykes anasema kuwa Mwalimu Thomas Plantan alikuwa akipenda sana kuwinda muda mwingi alikuwa porini na bunduki yake hakuwa na muda na TAA.

Hii ndiyo ikawa sababu kubwa ya kuzorota kwa TAA katika kipindi chake na Clement Mtamila.

Ikawa hapa kanikumbusha vile vichwa vya kongoni na swala kwenye kuta za nyumba ya Mwalimu Thomas Plantan Mtaa wa Masasi, Misheni Kota.

Kila watafiti wakija kunihoji hutaka kuona nyumba ya Abdul Sykes aliyoishi na Mwalimu Nyerere 1955 na kuona nyumba ya Clement Mtamila Mtaa wa Kipata na Sikukuu.

Hizi nyumba haziko mbali ziko jirani sana Mtaa wa Kipata na Stanley.
Nyumba zile zote sasa hazipo badala yake kuna magorofa marefu.

Nyumba ya Mzee Mtamila ilinunuliwa na Mzee Bahashuwan na akavunja akajenga gorofa.

Nilibahatika siku moja kuingia nyumba hii katika miaka ya tisini kabla ya kuvunjwa nikawa najiambia mwenyewe ni lini watu watakuja kujua yaliyopitika nyumba hii katika harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika?

Naendelea kuwaonyesha watafiti nyumba hizi lau kama hazipo na hawa watapiga picha na kisha nitawapitisha Kariakoo ilipokuwa ofisi ya Market Master Abdul Sykes wakati wa kuunda TANU na kupigania uhuru.

Wote huwa wanashangaa kuwa hadi leo hapajawekwa kibao kinachoeleza historia ya sehemu zote hizi muhimu kwa historia ya Julius Nyerere na pia muhimu katika histora ya ukombozi wa Tanganyika.

PICHA:
1. Thomas Plantan
2. Clement Mtamila
3. Subeti Salum
4. Mzee bin Sudi
5. Julius Nyerere
6. Dossa Aziz na Bi. Titi Mohamed

Screenshot_20220517-070612_Facebook.jpg
 
Hivi hakukuwa na uwezekano wa hizo nyumba za waasisi wa TANU kutuzwa kama Museums for our national development, for this wonderful historical impacts,,,
 
Ahsante kwa historia...
Smart...
Karibu.
Hivi hakukuwa na uwezekano wa hizo nyumba za waasisi wa TANU kutuzwa kama Museums for our national development, for this wonderful historical impacts,,,
Yuri...
Waliokuwa madarakani baada ya uhuru hawakuitaka historia ya uhuru wa Tanganyika kwa kuwa wao hawako katika historia hii na waliowakaribisha katika harakati walikuwa wamefanya makubwa.

Baada ya uhuru kupatikana wakawa wanashughulika na kuihujumu historia ya kweli ya TANU.
Hii ndiyo iliyo nifanya mimi kuandika litabu cha Abdul Sykes kueleza historia ya African Association kuanzia 1929.

Nikaandika kufika kwa Nyerere Dar es Salaam 1952 na kupokelewa na Sykes.
Nikaendelea kuanzia 1953 Nyerere alipochaguliwa kuwa rais wa TAA makamo wake Abdul Sykes.

Kuna historia ya kusisimua hapa.
Nikaenda majimboni vipi waliunda TAA na kufungua matawi ya TANU.

Hapa pia utawakuta wazalendo watu wa kawaida na makubwa waliyofanya.
Tatizo la historia ya uhuru ni kuwa imetawaliwa na Waislam.

Hili ndilo lililowatisha walioshika madaraka.
Ingekuwa kutunzwa nyumba za wapigania uhuru Dar es Salaam ingebidi wahifadhi nyumba ya Abdul Sykes ya Mtaa wa Stanley.

Nyumba hii Mwalimu Nyerere aliishi hapo.
Nyumba ya Ally Sykes Mtaa wa Kipata hapo ndipo ilipofichwa machine ya kuchapa makaratasi ya uchochezi.

Bukoba nyumba ya Sued Kagasheki, Tabora nyumba ya Nyange bint Chande, Zarula bint Abdulrahman, Moshi nyumba ya Halima Selengia, Mikindani nyumba ya Ahmed Adam kwa uchache.

Hapo chini ni nyumba ya Ahmed Adam Mikindani aliyofikia Mwalimu Nyerere 1956 kama ilivyo hivi sasa.

1652845670453.jpeg
 
2 Reactions
Reply
Back
Top Bottom