Hapendwi mtu, maslahi ya Taifa mbele ......... Mswada wa Umeme wakataliwa tena!

Keil

JF-Expert Member
Jul 2, 2007
2,214
802
Kivuli cha Karamagi: Wabunge waukataa muswada wa umeme, mafuta

*Wakataa muswada wa sheria ya umeme
*Wasema hauna maslahi kwa taifa

Na Waandishi Wetu

WABUNGE wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wameukataa kwa mara nyingine muswada wa sheria ya umeme, wenye lengo la kufungua milango kwa wawekezaji wa nje kuwekeza katika sekta hiyo badala ya huduma hiyo kutolewa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) pekee.

Wakizungumza katika semina ya siku mbili iliyofanyika jijini Dar es Salam jana, wabunge hao walionyesha kukerwa na muswada huo, wakidai kuwa bado una harufu ya aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi.

Akizungumza mara baada ya kuwasilishwa kwa mada mbalimbali zinazohusu muswada huo, Mbunge wa Karatu, Dk Willibroad Slaa ( Chadema) alisema hajaona tofauti yoyote katika muswada huo na uliowasilishwa mara ya kwanza, ambao ulipitiwa na kutoa mapendekezo ya mabadiliko katika baadhi ya vipengele.

Aliongeza kuwa mswada huo pia hauonyeshi mpango wowote wa kuweka umeme maeneo ya vijijini ambako ndiko kuna wananchi wengi.

"Mswada ni ule ule na umesainiwa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, sijaona mabadiliko licha ya tulipoupitia Dodoma kutoa mapendekezo ya sehemu za kuufanyia mabadiliko. Pia umeshindwa kutoa dhamana ya mpango wa kuendeleza umeme vijijini,"alisema Dk Slaa.

Aliangaliza kuwa hakuna kwa sasa kampuni yoyote ya uwekezaji inayoweza kupeleka umeme vijijini, hivyo aliitaka serikali kuhakikisha kuwa inatekeleza jukumu hilo yenyewe na kuongeza kuwa kuukubali mswada huo ni sawa na kuiweka nchi mikononi mwa wawekezaji.

"Sijawahi kuona nchi yoyote duniani inayobinafsisha sekta ya umeme, Tanzania tumeamua kutoa mali zetu kiholela. Hii ni aibu tunawanyenyekea wawekezaji na hatima yake tunajikuta tunaingia kwenye mikataba mibovu. Naomba tuisaidieTanesco ili iweze kujiendesha...," alisema Dk Slaa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Anne Kilango alisisitiza kuwa hawezi kuukubali muswada huo kwa sababu una mapungufu mengi na kwamba hauna maslahi kwa wananchi.

"Mwenyekiti naomba niukatae muswada huu kwa mara ya pili, awali mjini Dodoma niliukataa bila kutoa sababu, sasa nimefanya utafiti nimeandika mada nikilinganisha na mataifa mengine, ambayo nitaiwasilisha kwenye Kamati za Kudumu za Bunge," alisema na kuongeza:

"Tuionee huruma Tanesco, sisi ndio tumeifikisha hapo ilipo, "halafu tunataka kumletea Tyson apigane na mtoto wetu wa miaka 10 ambaye ni mgonjwa mahututi akiwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi'. Hii ni sawa na kukubali mtoto wako auawe, sisi ni wazazi gani tusio na huruma".

Alimtaka Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kutoyakanyaga maneno yake aliyotoa mara baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo ili kuinusuru Tanesco.

Alisema Waziri Ngeleja aliahidi jambo la kwanza kulishughulikia atakapo ripoti kazini ni suala la Tanesco, hivyo ni wakati muafaka wa kushughulikia suala hilo badala ya kuwashawishi wabunge wapitishe muswada huo ambapo hauna maslahi kwa wananchi.

"Tunataka ushindani lakini si sasa muda haujafika kuruhusu utokee katika sekta ya umeme," alisisitiza Kilango.

Awali Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Halima Mamuya alieleza kusikitishwa kwake kwa serikali kuwatumia wabunge kuwapa posho kwa kuandaa semina zenye lengo la kuwashawishi kupitisha vitu ambavyo havina maslahi kwa wananchi.

Alisema serikali imekuwa na kawaida ya kuandaa semina na kuwapa wabunge posho ya Sh 80,000 kisha kuwaletea vitu mbalimbali ikiwamo miswada muhimu inayogusa maslahi ya wananchi, ili wabunge hao wayapitishe na kutoa mfano wa semina kama hiyo iliyowahi kususiwa mjini Dodoma ambapo alisema siku hiyo walipewa posho hiyo, lakini baada ya kususia semina hiyo, aliyekuwa waziri wa nishati na madini alitamka wazi na kuhoji kwanini walichukua posho zao wakati waliisusia semina hiyo.

"Muheshimiwa mwenyekiti, mimi nilinyanyasika sana, maneno haya yananikera siku ile wabunge tuliandaliwa semina kama hii, wakati tunaingia tu mlangoni waandaaji walitusainisha posho na kutuletea miswada hiyo siku hiyo hiyo, hatukuwa na muda wa kuisoma hivyo walifikiri tungepitisha hivi hivi,"alisema.

"Lakini baada ya mambo kubadilika, waziri alisema kwanini tumechukua posho zao wakati tumeisusia semina yao, niliirudisha pesa ile, lakini walikataa kupokea na badala yake walisema niipeleke kwa watoto yatima, huu ni unyanyasaji mkubwa."

Mamuya alisema muda wa wabunge kutumiwa kwa posho za vikao umepitwa na wakati, badala yake serikali ibadilike kwani sasa ni enzi ya Watanzania kujua mambo na si enzi ya kupitisha mambo kwa maslahi ya wachache.

Naye Mbunge wa Nkasi CCM, Ponsiano Nyami alisema kuwa suala la umeme kufika maeneo ya vijijini mara baada ya wawekezaji kuingia katika sekta hiyo, ni kiini macho na ni sawa na kuwadanganya wananchi ambao wamekuwa wakiteseka kwa miaka mingi kusubiri huduma hiyo.

Aliishauri serikali kuacha kutegemea umeme unaotokana na maji kwa kuwa sasa hauna uhakika kutokana na hali ya hewa kutoeleweka.

Semina hiyo ilihudhuriwa na wabunge wote pamoja na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye alifungua semina hiyo, Mkurugenzi Mkuu Tanesco, Dk Idrisa Rashid, Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Balozi Fulgence Kazaura, maafisa mbalimbali kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Maji (Ewura), pamoja na maafisa mbalimbali wa serikali.

Source: Mwananchi

Maswali ya ziada:
Kwanini bado wanarudisha mswada ule ule ambao ulisainiwa na Waziri Karamagi? Kuna watu wana kampuni zao wanataka kuja kuinunua TANESCO? Au kuna watu serikalini walishakula mshiko (10%) ili kuhakikisha kwamba kampuni fulani zinapata upenyo wa kuingia Tanzania kuja kuwekeza kwenye umeme? Maswali ni mengi kuliko majibu.

Waziri Ngereja asipokuwa makini anaweza kujikuta anamfuata Karamaji kwa kuwa hiyo wizara ni bomu kwa sasa na inagusa sekta ambazo ziko sensitive kwa wananchi. Kazi kwake na ninamtakia kila la heri!

Mama Kilango mfano wa kuigwa na ndiyo tunataka wabunge wanaokwenda na dataz ili kuiumbua serikali inapokurupuka halafu baadaye inakuja kusukumia mzigo kwa washauri/wasaidizi kwamba hawakutoa ushauri unaofaa. Nina uhakika mikataba mibovu tuyoiona leo hii isingeweza kupitishwa kama ingekuwa inapitia Bungeni na wala akina Lowassa wasingepata nafasi ya kujitetea kwamba hawakushauriwa vizuri!
 
Na kwa nini watuhumiwa wa ufisadi akina Lowassa na Msabaha kuhusiana na kashfa za Richmond bado wako Bungeni? Hivi CCM haina utaratibu wa kuwafukuza uanachama wanachama wao waliogubikwa na kashfa nzito kama Richmonduli? Itaendelea kuwakumbatia wanachama wenye tuhuma nzito mpaka lini?:confused:
 
"Sijawahi kuona nchi yoyote duniani inayobinafsisha sekta ya umeme, Tanzania tumeamua kutoa mali zetu kiholela. Hii ni aibu tunawanyenyekea wawekezaji na hatima yake tunajikuta tunaingia kwenye mikataba mibovu. Naomba tuisaidieTanesco ili iweze kujiendesha...," alisema Dk Slaa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Anne Kilango alisisitiza kuwa hawezi kuukubali muswada huo kwa sababu una mapungufu mengi na kwamba hauna maslahi kwa wananchi.

"Mwenyekiti naomba niukatae muswada huu kwa mara ya pili, awali mjini Dodoma niliukataa bila kutoa sababu, sasa nimefanya utafiti nimeandika mada nikilinganisha na mataifa mengine, ambayo nitaiwasilisha kwenye Kamati za Kudumu za Bunge," alisema na kuongeza: "Tuionee huruma Tanesco, sisi ndio tumeifikisha hapo ilipo, "halafu tunataka kumletea Tyson apigane na mtoto wetu wa miaka 10 ambaye ni mgonjwa mahututi akiwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi'. Hii ni sawa na kukubali mtoto wako auawe, sisi ni wazazi gani tusio na huruma".

Alimtaka Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kutoyakanyaga maneno yake aliyotoa mara baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo ili kuinusuru Tanesco.
Alisema Waziri Ngeleja aliahidi jambo la kwanza kulishughulikia atakapo ripoti kazini ni suala la Tanesco, hivyo ni wakati muafaka wa kushughulikia suala hilo badala ya kuwashawishi wabunge wapitishe muswada huo ambapo hauna maslahi kwa wananchi.
"Tunataka ushindani lakini si sasa muda haujafika kuruhusu utokee katika sekta ya umeme," alisisitiza Kilango.

Bunge la safari hiii litakuwa na maneno sana, I mean inaonekana kuwa sasa tembo ameanza kuamka, baada ya kulala for the past 45 years.
 
Bunge la safari hiii litakuwa na maneno sana, I mean inaonekana kuwa sasa tembo ameanza kuamka, baada ya kulala for the past 45 years.

FMES,

Nyerere si alisema ukishaonja nyama ya binadamu, utaendelea kuila tu.

Wabunge wetu wameshaonja raha ya kuwa huru kwenye nchi yao na bunge lao, sidhani kama kuna kurudi nyuma tena. Mawaziri wengi wataenda na maji kabla ya 2010.

Sisi wengine tuendelea kushangilia pembeni.
 
Mkuu Wangu Mtanzania,

Unajua nilitabiri tena jana kuwa, this time bungeni kutakuwa na moto,

1. Lowassa, lazima ana machungu ambayo angependa kuyatoa kwa Six, na wabunge waliomtosa, na wao pia sasa hivi wako macho kumsubiri aupande mkenge tu.

2. Wabunge baada ya kumtosa Lowassa, sasa wako confident kuwa wanaweza kum'goa hata rais, na ndani ya bunge sasa hakuna wa kuwatisha tena kaa zamani, maana nasikia Lowassa alikuwa akiwaendesha wabunge kama watoto na ndio hasa chanzo cha resentment yao kwake.

3. Sio siri kuwa Lowassa ana wafuasi wengi sana ndani ya bunge, sasa ili kuwapunguza nguvu yeye na watu wake, dawa ni kufukua more uozo against mawaziri wake, hilo tayari liko in the works.

4. The loser wa hili saga ni muungwana, the beneficiary tutakuwa ni sisi wananchi, lakini all and all, this is good stuff kwetu wananchi.
 
Jamani mimi binafsi nataka sana muswada huu upitishwe ili kuruhusu makampuni ya kigeni yaingie kwenye power sector TZ BUT UNDER ONE CONDITION:::::

Tanesco isiwe responsible kabisa na mikataba ifuatayo iende serikalini na wao wawape hao wawekezaji hiyo mikataba:::

IPTL
SONGAS
KIWIRA
Alstom
DOWANS


Ukiondoa hiyo mikataba kwenye responsibility ya TANESCO nina imani kubwa kuwa wataweza kupambana na mwekezaji yeyote.

SO since serikali ndio ilisign hiyo mikataba kimabavu basi tuwape wawape hao investors wao since serikali seems to act like they know so much and have faith kwa hao wawekezaji.

Naomba niwasilishe hoja!!!!!
 
moelex23
i Gave U Thanx For Taking Ur Time To Write N Shame Upon U
ushindi--- Lazima
usiku-asubuhi Njema
 
moelex23
i Gave U Thanx For Taking Ur Time To Write N Shame Upon U
ushindi--- Lazima
usiku-asubuhi Njema


mkuu pdidy sijakuelewa kidogo hapo::

i Gave U Thanx For Taking Ur Time To Write N Shame Upon U

Pse clarify for me!!!
 
Nashangaa kitendo cha serikali kutaka ikaba Roho Tanesco ili kuongeza uwezo wa Maharamia kuzarisha umeme Tanzania.

Tanesco mpaka sasa hivi ina uwezo wa kuzarisha 947MW wakati peak Demand Tanzania ni 562MW.
60% ya umeme huu ni hyro na 40% Thermal.

Utetezi wa serikali unao ruhusu wawekezaji Binafsi kuruhusiwa kuikaba koo Tanesco unatoka na uchambuzi mbaya wa makusudi unao engua miradi mizito ya kuzarisha umeme kama ya STIGLER GORGE ambayo serikali inaizima kwa kutumia nguvu zake zote kila siku.

Ukichambua tatizo la umeme Tanzania kwa kuzingatia uzarishaji wa Mtera na Kidato jawabu ulipatalo ni la kuwaruhusu Maharamia kuendelea kuwanyonya wananchi wa Tanzania kwa kuwekeza katika sekta ambayo inaweza kujitosheleza.

Kwa mijibu wa Taarifa ya 2006 iliyopo kwenye Website hii;
[media]http://tc.iaea.org/tcweb/abouttc/strategy/Thematic/pdf/presentations/energysystemplanning/Nat_Needs_thru_Integrated_Reg_App.pdf[/media]

Tanesco inaweza kuzarisha zaidi ya 2400MW za umeme iwapo Bunge litapitisha ujenzi wa Hydro leletric power ya STIGLER GORGE.

Wazungu walio tutawala tangu miaka 1880 wanatushangaa sana kwa nini tunakimbilia kujiingiza kwenye matatizo ya vijikampuni uchwara kama IPTL ya Kikwete na RDC ya Lowassa wakati tunaweza anzisha mradi kabambe wa kuzarisha Megawati hadi kufikia 4000MW huko STIGLER GORGE kama ni kweli tuna nia na hamu ya kujikwamua katika sekta ya nishati????

Mswada ulio pelekwa na serikali Bungeni una nia moja kuua uwezo wa wa Tanzania kujitafutia maeendeleo yao na kukuza uchumi wa nchi yao. Kuiweka Sekta ya umeme mikononi mwa Wageni ambao hujali maslahi yao kuliko yetu.
Wawekezaji wote wa maana hawawezi kuja Tanzania kuwekeza kwa sabau umeme wetu ni aghali sana ukilinganisha na umeme wa nchi nyingi zenye viwanda za Asia na South Amerika.
Wakiimbie Gharama za umeme kwao ksiha waje wakutane na gharama za umeme zinazo wafaidisha akina Lowassa na kikwete?

kampuni karibu zote zilizopo Tanzania katika sekata nyingi ni zile za matapeli wa kimataifa au zilizo undwa kwa mikono ya viongzoi wa Tanzania kwa kutumia Watu wa nje wenye nia ya kutengeza fedha haraka.
Huwa nashangaa na kuishiwa nguvu pale nionapo MH Kikwet akijifanya kupiga Debe la kuita wawekezaji waje Tanzania kuwekeza wakati yeye Binafsi kama Rais wa nchi anashiriki kikamilifu kuhujumu sekta ya Nishati.

Hivi Rais anadhani wawekezaji wakija watatumia Nishati ya Mkaa kutoka Misitu ya Bagamoyo au Mboga ya Mchunga??

Ili tuvutie wawekezaji wa viwanda na biashara nyingine ni lazima kwanza Tuimarishe nguvu za umeme Simu na Internet na kuzifanya ziwe za bei nafuu ukilinganisha na zile za nchi zinazoendelea kama sisi.

Bunge ni lazima lianzishe kwa nguvu Muswada utakao pelekea Serikali kuanza kujenga mitambo ya kuzarisha umeme mkubwa wa STIGLER GORGE ambao una uwezo wa kuzarisha zaidi ya 2400 MW.

Umeme wa Stigler Gorge ukijumrishwa na ule wa Mtera na Kidato utatuwezesha kuaxcha kabisa kutegemea hivi vijenereta uchwara vya akina Lowassa RDC na MH Kikwete IPTL.

N Bahati mabay kwamba Viongozi wetu wote wamekosa Uzalendo na mwelekeo wa kuikwamua Tanzania katika makucha ya Umasikini. Viongozi wetu wana nia ya kujenga himaya ya watu wachahche watakao jilimbikizia mali za mabilioni na kutwaa nguvu za kufanya chochote watakacho Tanzania wao na Vizazi vyao.


Nimewahi kuwasikia viongozi wengi wakilaani Ufisadi ulioko ndani ya Serikali ya Nigeria hata kufikia mahali kuwaasa Watanzania wasiolewe na au kuoa Wanaigeria. Wito huo unaoneka kukosa nguvu kabisa ukiyaweka wazi matukio ya Wizi wa kutumia madaraka na kiburi unaoendelea Tanzania.

Viongozi wa Tanzania wana Tofauti gani na kina Sani Abacha walioiba mabilioni kwenye benki kuu yao??

Nimefurahishwa na kitendo cha wabunge wa bunge la Jamhuri kuacha ushabiki wa Kichama na kushupalia Mswada mmbovu unaliweka taifa pabaya.
Mpaka dakika hii tegemeo pekee la maendeleo ya wananchi wa Tanzania ni Ubora wa utendaji wa Bunge letu.
Hatuna mategemeo ya maana kutoka Ikulu kwa sababu ikulu imeingiliwa.
Wengine wote waliobaki wameteuliwa na ikuli kwa hiyo wana udhaifu ulio sawa na aliye wateua.
 
Lakini mpaka unpopular muswada unarudishwa mara mbili bungeni, JK anakuwa hana habari kweli? Je, rais huwa anatoa baraka kabla ya miswada mipya na nyeti/muhimu kupelekwa bungeni?
 
Baada ya kusoma maelezo ya habari ile ile kwenye gazeti la Mtanzania, ninaanza kupata mashaka kwamba huyu Mheshimiwa sana Pinda pamoja Waziri Kijana (Ngeleja) hawako serious ama walidhani kwamba yaliyotokea Dodoma yalikuwa yamemlenga Bwana Karamaji, na kwamba baada ya Karamaji na EL kuondoka mambo yangeenda mswano.

Hao wabunge ikifika 2010 wakija kuomba kura tutawasuta kwa kuwauliza wanafanya nini huko ilhali mambo kila siku yanazidi kuwa mabaya na wao ndo watunga sheria na wasimamizi wa serikali na ndiyo watetezi wetu.

Mh. Pinda anatakiwa kufungua macho na speech kama hii sidhani kama inahitajika kipindi hiki. Kinachotakiwa ni kuwa wakweli na wawazi zaidi ili tuone kilicho katikati ya maneno yaliyo kwenye hiyo miswada ya umeme na biashara ya mafuta.

Title ya gazeti imekaa ki-Agenda 21 sana na hata maneno ya speech ya Mh. Pinda yamewekwa mengi ili kujaribu kum-discredit wakimlinganisha na EL na hivyo watu tuweze kuona kwamba EL was better than Pinda. Pamoja na hayo it is too early kusema chochote na pia Pinda anatakiwa ajue kwamba kuna watu wako nyuma ili kujaribu kum-discredit kwa lengo la kuonyesha kwamba his former boss was better! Pinda kaa macho .....
------------------------------------------

Wabunge wamtosa Waziri Mkuu Pinda

  • Waukataa tena muswada wa kurekebisha TANESCO
  • Wasema utalipeleka shirika hilo kongwe kaburini
  • Waziri Ngeleja alaumiwa kwa kutafuna maneno yake

na khamis mkotya

WABUNGE wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jana waliukataa Muswada wa Sheria ya Umeme nchini kwa mara ya pili, wakisema ni muswada uliojaa ubabaishaji na unaolenga kuwanufaisha zaidi wawekezaji.

Uamuzi huo wa wabunge unapeleka pigo la kwanza kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye alikuwa amewashawishi waukubali muswada huo baada ya kufafanuliwa uzuri wake na watalaamu katika semina iliyoandaliwa kwao jijini Dar es Salaam kwa ajili hiyo.

Wakizungumza katika semina hiyo, iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini, wabunge hao walisema kuidhinisha muswada huo ni sawa na kuidhinisha hati ya kifo kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Semina hiyo iliyofanyika Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam, ililenga kuwapa fursa wabunge kuijadili miswada ya sheria mpya za umeme na biashara za mafuta ya petroli, ikiwa ni mwendelezo wa semina kama hiyo iliyovunjika mjini Dodoma mwezi uliopita.

Katika semina hiyo iliyohudhuriwa pia na Pinda pamoja na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, wabunge hao waliendelea kusisitiza kwamba lazima TANESCO ijengewe uwezo kwanza ndipo wawekezaji binafsi waruhusiwe.

Pamoja na mambo mengine, muswada huo wa umeme unapendekeza kuruhusiwa kwa wawekezaji binafsi kuzalisha umeme na kuuza moja kwa moja kwa walaji, kama hatua ya kumaliza ukiritimba wa TANESCO.

Mapema akitoa hotuba yake kabla ya kuwasilishwa kwa mada mbalimbali zinazohusu TANESCO na huduma ya nishati, Waziri Mkuu aliwataka wabunge kusahau yaliyopita na badala yake wapitishe muswada huo ili harakati za maendeleo ziendelee kusonga mbele.

Pinda alisema, hakuna haja ya kuendelea kubakia na mawazo ya mkutano wa Dodoma uliovunjika, kwani matokeo ya kuvunjika kwa semina ile tayari yamekwishaonekana kwa baadhi ya viongozi serikalini kuwajibika.

"Semina hii ni matokeo ya kilichojitokeza katika semina iliyofanyika kabla ya mkutano wa kumi wa Bunge kule Dodoma ambapo waheshimiwa wabunge walishiriki kujadili Muswada wa Sheria ya Umeme na Muswada wa Biashara ya Mafuta ya Petroli.

"Semina ile haikuweza kumalizika vizuri na hivyo kutokidhi malengo yaliyotarajiwa. Yaliyojitokeza katika semina ile ni historia. Lengo la semina hii ya leo (jana), ni kuwawezesha wabunge kuipitia na kujadili miswada ile tena kwa manufaa ya Taifa letu
," alisema.

Katika semina hiyo iliyofanyika chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Mbunge wa Bumbuli, William Shelukindo (CCM), baadhi ya wabunge waliopata fursa kuchangia, walionekana kuziba masikio dhidi ya hotuba ya Waziri Mkuu na kuamua kuijia juu serikali kwa kuuleta tena muswada huo.

Mbunge wa viti maalum, Halima Mamuya (CCM), alikuwa wa kwanza kuchangia, na kuituhumu serikali kwamba imekuwa haiwapi fursa pana wabunge katika kuisoma miswada mbalimbali inayofikishwa ili waweze kuilewa vizuri.

Mbali na hilo, mbunge huyo alisema serikali imekuwa ikifanya mambo kwa kuangalia maslahi ya wawekezaji zaidi kuliko maslahi ya wananchi, kitendo alichosema kinatoa sura mbaya katika kueleza dhamira ya serikali kuhusu maendeleo ya wananchi.

"Mara nyingi tumekuwa tukipewa miswada hii mlangoni tunapoingia. Wanataka tupitishe miswada bila kusoma na kuijadili kwa upana wake. Katika maelezo ya Waziri (William Ngeleja), anasema sheria hii ipitishwe ili kuwapa imani wawekezaji," alisema nakuongeza.

"Hivi serikali inaleta miswada mbele yetu kwa ajili ya kutafuta maslahi ya wawekzaji? Muda wa kuwaenzi wawekezaji na kuwadhalilisha wananchi umepiptwa na wakati. Tuache kuona wawekezaji wana umuhimu sana kuliko wananchi," alisema.

Kwa upande wake mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela (CCM), aliweka msimamo wake wazi katika kuupinga muswada huo, akisema kupitisha muswada huo ni sawa na kuruhusu kifo cha TANESCO.

"Katika semina iliyovunjika kule Dodoma sikuwahi kueleza sababu za kuukataa muswada huu. Leo tena naukataa muswada huu kwa mara ya pili. Muswada huu siyo wakati wake, siyo kipindi muafaka cha kuuleta. Tuwaonee huruma TANESCO wenzetu wana hali mbaya," alisema nakuongeza;

"Mwenyekiti, kuruhusu muswada huu ni sawa na kuruhusu Tyson (bondia Marekani) apigane na mtoto wa miaka kumi. Kufanya hivyo ina maana wewe mzazi umeruhusu kifo cha mtoto wako. Hatukatai wawekezaji, lakini tunataka Tanesco ijengewe uwezo kwanza," alisema.

Kilango aliendelea kusema. "wakati mheshimiwa Waziri Ngeleja alipoteuliwa kuwa Naibu Waziri mwaka jana, alisema kazi yake ya kwanza ni kuhakikisha kuwa TANESCO inajengewa uwezo ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi. Ngeleja asikanyage maneno yake, atimize ahadi yake kabla ya kuruhusu wawekezaji," alisema.

Naye mbunge wa Karatu, Dk. Wilbroad Slaa (CHADEMA), alisema muswada huo ni hatari kwa uhai wa Taifa na kueleza kwamba bila kufanyiwa marekebisho ya kutosha, Taifa linaweza kuingia katika wakati mgumu kutokana na kubinafsisha huduma hiyo nyeti.

Dk. Slaa alisema, serikali haijafanya marekebisho yoyote katika muswada huo kama ilivyokuwa imependekezwa na wabunge, wakati wa semina ya kwanza kama hiyo iliyovunjika mjini Dodoma.

"Tulipendekeza mambo kadhaa yarekebishwe katika muswada huu kabla haujaletwa tena kwa mara nyingine. Lakini ukiangalia muswada huu uko vile vile kama ulivyoletwa, tarehe ni ileile. Nashangaa kuona jina Nazir Karamagi. Hii ni 2008 siyo 2007," alisema nakuongeza;

"Kimsingi muswada huu nauona umejaa ubabaishaji mwingi, wabunge tulipendekeza mambo ya msingi lakini yamepuuzwa.

Kucheza na umeme ni sawa na kucheza na damu katika mwili wa binadamu. Huwezi kuruhusu wawekezaji binafsi wakati wewe mwenyewe uko taabani," alisema.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Dk. Idris Rashid, alisema Shirika lake linashindwa kufanya kazi kutoka na kuelemewa na mzigo mkubwa wa madeni, kwani asilimia 96 ya mapato yanayokusanywa inatumika kulipa madeni.

Katika hali iliyowashangaza wabunge, Dk. Rashid alisema ni asilimia kumi tu kati ya watu zaidi ya milioni 36 waliopo nchini ndiyo wanaopata huduma ya umeme. Hata hivyo wateja waliopo ni 670,000 tu kati ya idadi hiyo ya watu nchini.

Kwa upande wa Zanzibar Dk. Idris alisema kasi ya wateja ni nzuri ikilinganishwa na upande wa bara, kwani hadi sasa watu wanaotumia nishati hiyo ni asilimia 96 kati ya wananchi wote wa visiwa hivyo.

Semina ya kujadili miswada hiyo ilivunjika mjini Dodoma, baada ya wabunge kudai kwanza wasomewe ripoti ya kashfa ya Richmond kabla ya miswada hiyo kuwasilishwa bungeni.

Baada ya kusomwa kwa ripoti hiyo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge, Dk. Harrison Mwakyembe, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, na mawaziri Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi walilazimika kujiuzulu.

Source: Mtanzania
 
Mapema akitoa hotuba yake kabla ya kuwasilishwa kwa mada mbalimbali zinazohusu TANESCO na huduma ya nishati, Waziri Mkuu aliwataka wabunge kusahau yaliyopita na badala yake wapitishe muswada huo ili harakati za maendeleo ziendelee kusonga mbele.

Pinda alisema, hakuna haja ya kuendelea kubakia na mawazo ya mkutano wa Dodoma uliovunjika, kwani matokeo ya kuvunjika kwa semina ile tayari yamekwishaonekana kwa baadhi ya viongozi serikalini kuwajibika.

"Semina ile haikuweza kumalizika vizuri na hivyo kutokidhi malengo yaliyotarajiwa. Yaliyojitokeza katika semina ile ni historia. Lengo la semina hii ya leo (jana), ni kuwawezesha wabunge kuipitia na kujadili miswada ile tena kwa manufaa ya Taifa letu," alisema.

Nilikuwa ninampa Waziri Mkuu mpya the benefit of the doubt, lakini ninaanza kuwa na wasi wasi na hizi kauli, kama kweli mkulu ni kichwa kama tulivyoambiwa, mhhhhhhh! yaaani wabunge wapitishe tu muswaada, bila ya kuujadili kwa sababu ulipojadiliwa mara ya mwisho ulisababisha mwawaziri kujiuzulu, yaaani hiyo tu inatosha kuwa sababu ya kuupitisha muswaada?


"Mara nyingi tumekuwa tukipewa miswada hii mlangoni tunapoingia. Wanataka tupitishe miswada bila kusoma na kuijadili kwa upana wake. Katika maelezo ya Waziri (William Ngeleja), anasema sheria hii ipitishwe ili kuwapa imani wawekezaji," alisema nakuongeza.
"Hivi serikali inaleta miswada mbele yetu kwa ajili ya kutafuta maslahi ya wawekzaji? Muda wa kuwaenzi wawekezaji na

Hivi huyu Ngeleja naye vipi mnaojua uwezo wake tupeni dataz, maana this do not sound good kuhusiana na uwezo wake wa kufikiri mpaka kikazi? Hivi si kuna watu walisema ni kichwa huyu?
 
What we lack in our country ni political will hususani kutoka kwa viongozi wetu, binafsi nafikiri shirika kama la umeme na mafuta[TPDC] yasibinafsishe kwa namna yoyte ile na kama ni kubinafisshwa basi serikali iendelee kuwa na shares nyingi zaidi dhidi ya mwekezaji, kama kweli serikali ikiamua kwa dhati kabisa na kufanya jitihada za maksudi kuyasimamia mashirika haya sidhani kama yatashindwa kujiendesha yenyewe tena kuwa FAIDA.
 
Hivi serikali inashindwa nini kuruhusu Tanesco ijiendeshe kibiashara?

Tanesco ikiruhusiwa kujiendesha yenyewe serikali pia itatakiwa ishirikishe wananchi ili wataalam wa nishati nao wapewe nafasi ya kuanzisha kampuni au kuzinunua hizo zilizopo ili zimilikiwe na waTZ.

Siku zote serikali yoyote ile ina jukumu la kuwapa wananchi wake fursa ya kushiriki shughuli mbalimbali za kuzalisha mali na kuleta tija kwa taifa kupitia ajira.

Mheshimiwa raisi lazima afahamu kuwa sasa hivi hatuhitaji makampuni ya kuja kunyonya watanzania fwedha ambazo zinatakiwa zibaki Tanzania.

Kama kweli hao wahisani wana lengo la kutusaidia kupata maendeleo basi ni budi watupe wataalam wao wa nishati ambao watatusaidia kubuni,kujenga mabwawa na viwanda vya kuzalisha umeme kwa kila mkoa na wilaya na watanzania kuachiwa kazi ya kusimamia makampuni hayo hapo tunashindwa nini?

Kwa mtazamo wangu, naona kama bado tuna dhana ya kwamba kama watu walishindwa kusimamia mashirika ya umma basi hatuwezi sisi tutabakia kuwa wajinga.

Lakini kama wabunge wote wana lengo la kuleta maendeleo kwa watanzania kupitia mambo madogo kama ya kusimamia nishati, basi hatutachukua muda kusimama kiuchumi.

Kheri ya Pasaka!
 
Nilikuwa ninampa Waziri Mkuu mpya the benefit of the doubt, lakini ninaanza kuwa na wasi wasi na hizi kauli, kama kweli mkulu ni kichwa kama tulivyoambiwa, mhhhhhhh! yaaani wabunge wapitishe tu muswaada, bila ya kuujadili kwa sababu ulipojadiliwa mara ya mwisho ulisababisha mwawaziri kujiuzulu, yaaani hiyo tu inatosha kuwa sababu ya kuupitisha muswaada?




Hivi huyu Ngeleja naye vipi mnaojua uwezo wake tupeni dataz, maana this do not sound good kuhusiana na uwezo wake wa kufikiri mpaka kikazi? Hivi si kuna watu walisema ni kichwa huyu?

Tatizo sio Ngeleja,Tatizo ni mfumo wa serikali nzima ya CCM,Yeye anatetea yale ambayo Serikali na IMF wanayoyata,hii itakuwa ni sera ya mataifa ya nje tu
 
Hivi Ngereja umelogwa au umedanganywa,au ni dharau,huo mswaada siulikataliwa Dom hadi walalahoi tukajulishwa leo unarudisha the same mswaada kwa MH.Kilango ambae you know that yuko serious na TZ leo unataka kumpima Kilango hivi uko kamili.Au umedanganywa na waganga wa Bagamoyo kwamba wabunge wamesahau peleka hivyohivyo,mimi siamini.Cha kushangaza umepeleka hiyo proposal ikiwa imesainiwa na Karamagi,hivi wewe ni kibaraka wa Karamagi.
Tukisema wewe ni fisadi utakataa?

Wanaume na wanawake wenye akili zao timam,waliojaa maadili ya uongozi tena wanaofanya tafiti za uhakika bila kukurupuka wamekwishasema mswaada huo haufai,wewe leo unaona unafaa,wewe ni nani ktk nchi hii.JAMANI JAMANI,HII JF MTAKUJA KUILILIA.Nyie viongozi wetu mlioko madarakani kama mnafalsafa ya kutesa kwa zamu then tutaingia wenye nchi na kutesa mfululizo,hapo moto utawaka.

Adhabu ya kunyongwa hadharani itafuata mkondo wake kwa viongozi wasiokua waadilifu
 
Tatizo sio Ngeleja,Tatizo ni mfumo wa serikali nzima ya CCM,Yeye anatetea yale ambayo Serikali na IMF wanayoyata,hii itakuwa ni sera ya mataifa ya nje tu

Swadakta,

Mkuu Gembe,

Mimi nimesoma hoja za Dr Rashid kwamba hali ya kifwedha ni ngumu pale Tanesco na kwamba NetGroup Solutions walisaidia kwa kiasi kikubwa kurudisha hali ya fwedha hizo.

Sasa tusisahau kwamba Dr Rashid ni msomi tena wa PHD ya uchumi kwa hio katika masuala ya "adjustments" na "restructuring" ya "firm" yoyote ile, yeye labda ana mtizamo wa kuwa na suluhisho ni kuua kabisa kampuni halafu kuwaleta foregn companies wawe ndio wachezaji.

Mimi nina wasiwasi kwamba Dr Idris Rashid ndie playmaker hapa na amepelekwa Tanesco kwa minajili ya kfnza hicho anachopendekeza- kuiua Tanesco.

Unajua huyu Dr Rashid alipokuwa pale BOT, ni yeye
ndie alikuja na mawazo ya IFM na WB ya kupunguza wafanyakazi na akafanikiwa kwa hilo.

Halafu akaenda NBC napo anafanikiwa kutekeleza hizo sera za IFM na WB.

Sasa kwa mtazamo wangu mhhh..., naona huyu Dr Rashid nae ni sehemu ya timu nzima ya wale ambao wapo kuhakikisha kila kitu kinakuwa mali ya wageni.
 
Wakuu najitahidi kutokuwa optimist, alkini nashindwa. Jamani iweje hata yule uliyejua ni msafi akishapewa hiyo dhamana ya kutuongoza anageuka monster? sasa tutapata wapi viongozi wa kutuongoza?

Maana hapa nikiona kauli za Pinda na Ngeleja kwa maswala muhimu ya kitaifa kama umeme na nishati naishiwa nguvu kabisa!
Perhaps lets evaluate tuna tatizo gani! Iam getting worried day after day, kama akina Ngeleja na Pinda wanaelekea huko huko kwa akina EL! Juzi mlisikia kauli ya Masha kuhusu Richomnd..ehh aise hali inatisha nchi yetu inakokwenda.

Mi nadhani Rashid ni kiongozi mzuri tatizo ni bureacracy za serikali inataka ifanye mambo kienyeji bila accountability. Huwezi kuendesha economics za leo kwa kutumia sera za akina Makamba jukwaani! We ought to get real!

"THE GREATEST LESSON IN HISTORY IS THAT MEN NEVER LEARN FROM HISTORY"
 
Lakini mpaka unpopular muswada unarudishwa mara mbili bungeni, JK anakuwa hana habari kweli? Je, rais huwa anatoa baraka kabla ya miswada mipya na nyeti/muhimu kupelekwa bungeni?

JK yuko busy na mambo ya Comoro maana kamaliza ya Kenya .
 
Swadakta,

Mkuu Gembe,

Mimi nimesoma hoja za Dr Rashid kwamba hali ya kifwedha ni ngumu pale Tanesco na kwamba NetGroup Solutions walisaidia kwa kiasi kikubwa kurudisha hali ya fwedha hizo.

Sasa tusisahau kwamba Dr Rashid ni msomi tena wa PHD ya uchumi kwa hio katika masuala ya "adjustments" na "restructuring" ya "firm" yoyote ile, yeye labda ana mtizamo wa kuwa na suluhisho ni kuua kabisa kampuni halafu kuwaleta foregn companies wawe ndio wachezaji.

Mimi nina wasiwasi kwamba Dr Idris Rashid ndie playmaker hapa na amepelekwa Tanesco kwa minajili ya kfnza hicho anachopendekeza- kuiua Tanesco.

Unajua huyu Dr Rashid alipokuwa pale BOT, ni yeye
ndie alikuja na mawazo ya IFM na WB ya kupunguza wafanyakazi na akafanikiwa kwa hilo.

Halafu akaenda NBC napo anafanikiwa kutekeleza hizo sera za IFM na WB.

Sasa kwa mtazamo wangu mhhh..., naona huyu Dr Rashid nae ni sehemu ya timu nzima ya wale ambao wapo kuhakikisha kila kitu kinakuwa mali ya wageni.

Right on Richard,

watu wengi wameuliza sana utendaji kazi wa Dr Rashid lakini ikaonekana kuwa ana watetezi wengi sana hapa JF. Inaelekea kuna mengi yatajulikana karibu hasa katika suala hili la uzalishaji wa umeme....

nashikilia maoni yangu kwa sasa!
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom