Hapa Yanga hamtoki wala kutoboa, Kocha Pablo atoa neno

Job Richard

JF-Expert Member
Feb 8, 2013
3,865
2,168
Hapa Yanga Hamtoki Wala Kutoboa, Kocha Pablo Atoa Neno

[https://lh3]

KWA ‘mziki’ huu hamtoki, ndio tambo za mashabiki kwenye mitandao ya kijamii pamoja na vijiwe mbalimbali vya soka nchini kila moja akivutia upande wake kuhusu mechi kubwa ya kitaifa yenye historia ya kipekee kati ya Simba na Yanga itakayopigwa keshokutwa Jumamosi pale Estadio De Benjamin Mkapa.

Simba, wenyeji wa mchezo wanaamini kama si Meddie Kagere basi Bernard Morrison walio kwenye ubora msimu huu watawapa furaha hivyo hivyo kwa Yanga kama si Fiston Mayele basi atakuwa Feisal Salum ambao si rahisi kukabika.

Ukiondoa wachezaji hao wanaotazamwa kwenda kuzipa furaha timu zao kuna maeneo mengine yanaweza kuamua mshindi wa pambano hilo kutokana na viwango vyao walivyoonyesha katika Ligi Kuu Bara na mashindano mengine.

MAKIPA

Eneo la kwanza linaloweza kuamua mshindi wa derby hii ni kipa Aishi Manula wa Simba na Djugui Diarra wa Yanga ambao kila mmoja amecheza mechi zote ya vikosi hivyo.

Manula katika mechi saba ameruhusu mabao mawili na kamaliza michezo mingine mitano bila kufungwa bao wakati huo huo alihusika katika bao muhimu la ushindi dhidi ya Dodoma Jiji.

Kwenye mechi ya Dodoma Jiji, Simba walishinda bao 1-0, ambalo lilifungwa na Kagere aliyemalizia pasi ya kichwa iliyotoka kwa Chriss Mugalu ambaye alipokea mpira mrefu wa juu kutoka kwa Manula.

Diarra aliyesajiliwa na Yanga msimu huu akitokea Stade Malien ya nchini Mali, amekuwa katika kiwango bora.

Mpaka sasa katika ligi, Diarra ameruhusu mabao mawili kama Manula na kwenye mechi ya ufunguzi wa msimu dhidi ya Simba alipiga pasi ya maana kwenda kwa Farid Mussa ambaye alipiga pasi kwa Mayele aliyefunga bao pekee la ushindi.

Kutokana na ubora Manula na Diarra katika kuokoa na kusambaza mipira na mambo mengine ya kiufundi yanayofanana, Jumamosi wanaweza kuwa sababu ya ushindi.

KIUNGO
Kati ya silaha za Yanga msimu huu ni ubora wa safu yao ya kiungo ambayo inaongozwa na watu watatu kutoka katika mataifa tofauti, Khalid Aucho (Uganda), Yannick Bangala (DR Congo) na Mtanzania Fei Toto.

Aucho na Bangala wamekuwa wakicheza kwa kuelewana haswa kwenye kuzuia mashambulizi ya timu pinzani pamoja na kufanya kazi ya kuanzisha mashambulizi kwenda kwa Feisal aliye na ubora wa kupiga pasi za mwisho pamoja na kufunga mwenyewe.

Uwepo wa wachezaji hao watatu katika eneo la kiungo la Yanga ulitosha kuwapoteza Simba kwenye mechi ya Ngao ya Jamii na kuwalaza kwa bao 1-0 na kama haitoshi, utatu huo umejenga pacha ya hatari inayotawala eneo la kiungo kwa kupiga pasi nyingi ambazo zinaweza kumpasua kifua mpinzani kwa kuusaka mpira kwa tochi asipojipanga vyema.

Kwenye eneo la kiungo Simba msimu huu tangu kuondoka kwa Clatous Chama na Luis Miquissone wamekuwa na shida ya kupata viwango bora vya wachezaji wanaocheza kwenye eneo hilo.

Katika eneo la kiungo la Simba kumekuwa na mabadiliko ya mara kwa mara anaweza kuwepo Jonas Mkude, Mzamiru Yassin na Dilunga, muda mwingine wanabadilika anaingia Sadio Kanoute, Rally Bwalya au wengine.

Kukosekana kwa Taddeo Lwanga aliye majeruhi na mabadiliko ya mara kwa mara Simba wanatakiwa kuanza na wachezaji walio kwenye ubora ili kwenda kuwakabili wapinzani Yanga kwenye eneo hili la kiungo ikiwa tofauti wanaweza kwenda kupata shida na mechi kuwa ngumu kwao kama ile ya Ngao ya Jamii.

HUKU KAGERE, KULE MAYELE
Kwenye ligi Simba wamefunga mabao nane katika michezo saba wakati huo huo straika wao chaguo la kwanza kwa sasa, Meddie Kagere amefunga nusu yake, manne licha ya kupata muda mchache wa kucheza mwanzoni mwa msimu.

Simba wanapokwenda kufanya mashambulizi muda mwingi Kagere anakuwa katika nafasi sahihi ya kufunga kutokana na uwezo wake wa kulitimiza hilo na rekodi zinambeba.

Kagere kwa muda wa misimu minne ameifunga Yanga mara mbili kwenye ligi na msimu huu ndio silaha ya Simba katika kufunga mabao na kama atakuwa katika kiwango bora ni wazi atakwenda kusuambuana na mabeki wa Yanga, Bakari Mwamnyeto na Dickson Job.

Kule Yanga huenda wakawa wanatembea kifua mbele kwa safu yao ya ushambuliaji kwani mbali ya ubora wa Fei Toto, Jesus Moloko na wengineo kuna balaa linaitwa Mayele.

Mayele amekuwa na mwanzo mzuri katika kikosi cha Yanga kwenye msimu wake huu wa kwanza nchini na alifunga bao dhidi ya Simba ambalo liliipa timu yake taji la kwanza msimu huu (Ngao ya Jamii). Ubora wa Mayele umewafanya Yanga hata kumsahau shujaa wao wa zamani, Heritier Makambo ambaye huanzia benchini.

Ubora wa Mayele huenda ukawapa shughuli pevu ya kufanya Joash Onyango na Pascal Wawa, au Henock Inonga, Kennedy Juma au Erasto Nyoni.

MABENCHI
Benchi bora la ufundi litakalokuwa na mbinu bora za kumkabili mpinzani ndilo lenye nafasi kubwa ya kumaliza mechi mapema.

Benchi la ufundi la Yanga lipo chini ya Profesa, Nesreddine Nabi ambaye atakuwa anapata ushauri wa kutosha kutoka wasaidizi wake akiwemo, Cedrick Kaze pamoja na mkurugenzi wa soka la vijana, Mwinyi Zahera.

Upana wa benchi hilo la ufundi la uelewa wao wa soka bila kuwasahau wale wengine kama kocha wa makipa, Razack Siwa na wengineo ni kati ya vitu vinavyoweza kuwabeba.

Vivyo hivyo, kwa upande wa Simba wakati wanapoteza mechi dhidi ya Yanga msimu huu makocha wawili, Pablo Franco na Hitimana Thierry hawakuwa sehemu ya timu hiyo ila alikuwepo, Selemani Matola.

Tangu ameingia Pablo, morali na ufundi katika kikosi cha Simba vimezidi kuimarika na kuwa juu zaidi kutokana na kupata matokeo mazuri katika ligi pamoja na kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Pablo na Hitimana wakiunganisha nguvu na Matola aliyekuwa kwenye kikosi tangu msimu uliopita watakuwa na uwanja wa mpana kuandaa timu katika mazingira sahihi ya kiufundi ili kwenda kupata ushindi.

HAWATEGEMEWI
Kwenye pambano hili mbali ya maandalizi ya kutosha kwa wachezaji, makocha na viongozi huwa yanatokea mambo ambayo hayakutarajiwa na hasa wafungaji mabao.

Katika kipindi cha karibuni hakuna ambaye alitegemea kama Zawadi Mauya angekwenda kuwalaza Simba na viatu katika mechi ya mzunguko wa pili kwenye ligi msimu uliopita.

Jambo kama hilo halikutegewa Simba yenye Chama, Miquissone, Mugalu, John Bocco na wengineo wengi katika mechi ya fainali Kombe la Shirikisho (ASFC), bao pekee la ushindi lingekwenda kufungwa na Lwanga.


NAMBA
Namba wala hazidanganyi, Yanga wataingia katika mchezo huo wakiwa na hali fulani ya kujiamini kutokana na matokeo mazuri waliyonayo msimu huu ikiwemo ubora wa kikosi chao.

Yanga wapo nafasi ya kwanza kwenye ligi, katika mechi saba wameshinda sita, wametoka sare moja, hawajapoteza mchezo, wamefunga mabao 12, wamefungwa mawili na wamekusanya pointi 19.

Wapinzani wao Simba licha ya kuwa nafasi ya pili kwenye ligi kuna baadhi ya mechi mashabiki wao hawakuridhishwa na kiwango cha timu kama ushindi ule wa 2-1 dhidi ya Geita Gold.

Simba wapo nafasi ya pili wamecheza mechi saba, wameshinda tano, wametoka sare mbili, hawajapoteza mechi, wamefunga mabao nane, wamefungwa mawili wamekusanya pointi 17 na kama watamfunga Yanga wao ndio watakaa kileleni.

MKUDE MECHI 21
Kiungo wa Simba, Jonas Mkude huenda akawa mchezaji wa kuangaliwa zaidi katika eneo la kiungo la Simba kutokana na uzoefu wake akiwa kinara wa derby nyingi (20).

Kama Mkude atakuwa sehemu ya kikosi atatimiza derby yake ya 21 na atakuwa silaha kwa kuwaongoza wenzake kutokana na uzoefu.

WASIKIE HAWA
Mchezaji wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema kiufundi ukiangalia maeneo ya msingi mengi yanaipa nafasi Yanga kushinda mechi hiyo, “lakini mechi hii muda mwingine inakuwa na matokeo ya kushangaza, timu ambayo inapewa nafasi ya kufanya vizuri huwa inashindwa na mifano hiyo ipo mingi.”

Kocha wa zamani wa Simba, Masoud Djuma alisema: “Mechi hii si ya kuangalia rekodi au timu gani ipo vizuri bali ile ambayo itakuwa na maandalizi bora ndio inafanikiwa.”

PABLO ATOA NENO
Kocha wa Simba, Pablo ameweka wazi kuwa hajapata muda mwingi wa kuwasoma wapinzani wao Yanga kutokana na kupata muda mchache tangu aingie nchini.

“Mechi hii hauwezi kuiandaa kwa siku tatu au wiki tatu ambazo ninazo tangu nifike hapa, lakini niliwasoma wachezaji wangu na tunajipanga vyema,” alisema.
 

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom