Hali ya uwekezaji kwenye nyumba za kuhamishika katika mji wa Tukuyu, jijini Mbeya Tanzania

Aliko Musa

Member
Aug 25, 2018
97
143
Nyumba za kuhamishika zimekuwa zikitumika kwa ajili ya makazi na biashara. Lakini kwa mazingira ya kwetu Tanzania nitakushirikisha zaidi kuhusu fremu za biashara.

Hii ni kwa sababu karibu nyumba zote za kuhamishika hutumika kwa ajili ya biashara tofauti tofauti.

Sababu za kumiliki nyumba za kuhamishika badala ya nyumba zisizohamishika zinaweza kuwa kama ifuatavyo;-

✓ Kutokuwa na kiwanja. Unaweza kumiliki nyumba ya kuhamishika hata kama hauna kijwanja.

✓ Kuwa na kiasi kidogo cha mtaji fedha. Unaweza kutumia Tshs.500,000 hadi Tshs.1,500,000 au zaidi kumiliki fremu moja ya kupangisha kwa wafanyabishara.

✓ Uhitaji wa nyumba za kuhamishika. Sehemu ambapo nyumba za kuhamishika hulipa zaidi inakuwa inakushawishi kuwekeza.

✓ Kuegesha nyumba eneo lenye kukodishwa fremu za biashara kwa kiasi kikubwa cha kodi. Unaweza kuwa na kiwanja sehemu ambayo fremu zake zinakodishwa kwa bei nafuu.

Ili uweze kumiliki nyumba ya kuhamishika utakayoilpwa kiasi kikubwa cha kodi sio lazima uwe na kiwanja.

Gharama za Matengenezo.

Nyumba za kuhamishika hugharimu kuanzia Tshs.400,000 hadi tshs.1,500,000 kwa fremu moja ya kupangisha kwa wanafanyabiashara wadogowadogo.

Gharama inaweza kuwa pungufu ya tshs.400,000 kutegemeana na ukubwa wa fremu husika.

Gharama inaweza kupungua kufuatana na makubaliano yenu kati yako na fundi vyuma.

Kwa gharama hizi, nyumba za kuhamishika zinalipa faida nzuri. Makadirio ya jumla ya gharama za matengenezo yanatakiwa kufanywa kabla ya kutengeneza nyumba au banda lako.

Makadirio unatakiwa kufanya kwa kuzingatia kiasi cha kodi ya fremu moja ya mazingira yako. Kodi ya hapa Tukuyu ni kuanzia Tshs.20,000 hadi 70,000 kutegemeana na banda lilipo.

Pia, kodi inaweza kupungua au kuongezeka kutokana na makubaliano yenu kati yako na wapangaji kwa kuzingatia gharama za matengenezo.

Kiasi cha kodi ya egesho kwenye ardhi

Kwa hapa Tukuyu, kodi unaanzia tshs.5,000 hadi 15,000 kwa kila fremu moja ya nyumba au banda la kuhamishika.

Gharama hii unatakiwa kuzingatia wakati wa kupanga kiasi cha kodi ya kupangisha banda lako.

Unatakiwa kutafuta nafasi ambayo ni nzuri na wanaegesha nyumba za kuhamishika kwa kiasi kidogo cha kodi.

Lakini nyumba inaweza kuegeshwa sehemu ambayo mpangaji wako anaitaka. Mpangaji atakuwa huru kuhamisha nyumba yako ili hali unaendelea kutengeneza kodi nzuri.

Makisio ya kodi ya banda ya chumba kimoja


Kwa kawaida kodi ni kuanzia elfu 20 hadi 70,000 kutegemeana na ubora wa fremu yenyewe na sehemu ambapo umeegesha fremu yako.

Uwiano wa kutengeneza kipato endelevu ni 3% (au zaidi) ya jumla ya bei ya banda kwa hapa Tukuyu.

Kwa hapa Tukuyu ni rahisi kutengeneza kodi ya zaidi ya 3% ya jumla ya gharama za kutengeneza banda la chumba kimoja.

Kiwango kizuri cha kutengeneza kipato endelevu kinatakiwa kuwa 4% au zaidi ya bei ya banda husika. Kwa hapa Tukuyu, hili limewezekana bila shida yoyote.

Kwa kanuni hii ya 4%, fremu moja ya kupangisha tshs.30,000 kwa mwezi unatakiwa kutumia jumla ya tshs.750,000 kwa ajili ya matengenezo.

Asilimia hii 4% ni kipato ghafi cha kila mwezi kutoka kwenye nyumba yako ya kuhamishika.

Kama utamiliki nyumba ya kuhamishika kwa miaka miwili ikiwa na wapangaji mtaji wako utakuwa umekusanya kwa asilimia 100.

Msingi wa banda au nyumba

Uimara wa msingi wa nyumba hutegemea sana mambo yafuatayo:-

✓ Historia ya matukio uhalifu. Kwa hapa Tukuyu, kuna historia ya matukio machache sana ya kiuhalifu ukilinganisha na mikoa ya Tabora mjini. Viti vya plastiki huku vibaki nje na hakuna uharibifu unaotokea. Banda za mbao hutumika kuuza bidhaa za nyumbani na hakuna uharibifu unaotokea wakati wa usiku.

✓ Thamani ya bidhaa zinazouzwa kwenye banda husika. Banda linapotumika kwa ajili ya bidhaa za thamani kubwa msingi wake unatakiwa kuwa imara bila kujali historia ya uhalifu kwenye kata au halmshauri husika.

Pia, ni muhimu kujenga msingi wa banda ambao utakuwa rahisi kubomoa pale unapohitaji kuhamisha banda au nyumba yako.

Biashara Zinaweza Kufanyika Kwenye Nyumba Za Kuhamishika.

Kila aina ya biashara inaweza kufanyika kwenye nyumba za aina hii. Huduma za wateja wa hali ya juu haziwezi kufanyika kwenye banda hizo.

Huduma za benki, huduma za taasisi kubwa za uwekezaji na viwanda vikubwa ni moja ya biashara ambazo ni vigumu kufanyika kwenye nyumba za kuhamishika.

Biashara zinazoweza kufanyika kwenye nyumba za kuhamishika ni kama ifuatavyo;-

✓ Biashara ya kutoa huduma mbalimbali kama vile uwakala wa bima, uwakala wa viwanja na nyumba, ushauri wa kitaalamu, na kadhalika.

✓ Biashara ya chakula maarufu kama migahawa.

✓ Biashara za kuuza bidhaa za urembo, duka la vifaa na malighafi za ujenzi, duka la bidhaa muhimu za nyumbani, duka la vifaa na dawa za mifugo na kilimo, fremu ya kushonea nguo na viatu, fremu ya kuingiza nyimbo na kukodisha CD, DVD, na kadhalika.

✓ Biashara ya kuhamisha fedha kama vile M-pesa, Tigopesa, Airtel money, halopesa na TTCL pesa.

✓ Biashara ya vifaa vya shuleni na maofisini maarufu kama stationary.

✓ Biashara ya kuuza bidhaa za teknolojia na mawasiliano kama vile mifuniko ya simu, mabetri ya simu, chaja za simu na kadhalika.

✓ Biashara ya vinywaji baridi na vya moto.

Sheria za mamlaka ya Mipango Miji na Vijiji


Kama kweli una maono ya kupiga hatua kubwa sana za kujenga utajiri kupitia uwekezaji wa viwanja na nyumba ni muhimu sana kutii sheria, taratibu na kanuni za serikali za mitaa na serikali kuu.

Unatakiwa kuzingatia sheria za mamlaka ya halmshauri husika. Usiegeshe nyumba zako sehemu ambayo wanakataza. Fanya tathimini ya sheria za matumizi ya ardhi katika halmashauri husika kabla ya kuanza uwekezaji huu.

Karibu Tujadili Pamoja.

1. Kitu gani umejifunza kutoka kwenye makala ya leo kuhusu nyumba za kuhamishika?

2. Orodhesha mambo unayopendekeza niongeze kwenye somo hili kulingana na uzoefu kutoka kwenye halmshauri unayoishi?.

3. Naomba nishirikishe hali ya soko mahalia ya nyumba za kuhamishika kwenye halmshauri unayoishi.

4. Je, umependezwa na uwekezaji kwenye nyumba za kuhamishika?. Ni lini utaanza kuwekeza au kukuza uwekezaji wako kwenye nyumba za kuhamishika?

5. Naomba uwashirikishe watu watatu kuhusu maarifa haya endapo umeona yatakusaidia wewe na huyo rafiki yako.

6. Tafadhali jiunge na kundi la ARDHI NA NYUMBA CLUB ili usipitwe na maarifa sahihi kuhusu mbinu bora za kuwekeza kwenye viwanja na nyumba.

Rafiki yako,

Aliko Musa.

WhatsApp/calls; +255 752 413 711
 

Aliko Musa

Member
Aug 25, 2018
97
143
Picha tafadhali

Screenshot_20220603-145620.png
 
1 Reactions
Reply
Top Bottom