Shayu
Platinum Member
- May 24, 2011
- 608
- 1,655
Dunia ni chuo kama tunaishi kila siku tunajifunza. Toka tunazaliwa tunajifunza. Kwanza tunajifunza kutambaa, kisha kutembea, kusimama na kuongea, alafu tunajifunza mahusiano yetu na wengine. Mahusiano yetu na wazazi, marafiki na majirani.
Tunajifunza kutafuta ili kuendeleza maisha yetu ya kila siku na kujenga miji yetu. MAISHA ni kujifunza bila kujifunza binadamu hawezi kukua. Binadamu hawezi kuendelea pasipo kujifunza. Maisha ya binadamu yanasonga mbele pale tu atakapofanya kujifunza kuwa tabia yake ya kila siku.
Kwahiyo isipite hata siku moja katika maisha yako bila kujifunza kitu. Ni muhimu kujua angalau kitu kimoja kila siku kitakacho kuongezea uelewa wako. Kitakacho fungua milango yako ya ufahamu. Bila maarifa maisha ya binadamu yana dumaa na maendeleo yake yanakuwa finyu.
Tunajifunza katika maisha yetu wenyewe lakini tunajifunza katika maisha ya watu wengine , na kurekebisha maisha yetu kutokana na makosa ya maisha ya watu wengine.
Tunaona mifano katika maisha ya watu wengine. Mifano hiyo inatuongoza katika maisha yetu ili tusifanye makosa. Kama tunaendelea kuishi ni muhimu sana kuendelea kujifunza. Na tunapofanya makosa tusikubali kurudia makosa na kufanya makosa kuwa tabia yetu.
Binadamu anakuwa mwenye afya bora ya kimwili na kiakili pamoja na ya kiroho pale tu anapoendesha maisha yake vyema na kuwa na makosa machache. Makosa haya mara nyingi hutupelekea kukosa furaha.
Mara kibao tumezikosea familia zetu, ndoa zetu na majirani zetu na kupelekea mahusiano yetu kuwa hafifu. Kujenga chuki na visasi. Haya mambo sisi kama binadamu hatuyahitaji. Tunahitaji kupendana. Kwasababu sisi wote ni binadamu.
Kwahiyo wakati tunahishi kwenye hii dunia ambayo tuko kwa kipindi kifupi mno tunahitajika kuishi kwa busara sana. Sisemi kwamba mimi ni mtu bora zaidi hapana. Mimi nafanya makosa kama wengine lakini kila wakati najirudi na mara nyingi natafuta njia iliyo sahihi kupita. Kwasababu najua uwepo wangu duniani niko kujifunza na kukua, Na pasipo kujifunza siwezi kukua. Siwezi kuwa na nguvu pasipo kutafuta maarifa.
Kwahiyo tunapokosea ni muhimu kukubali makosa yetu na kama tumekosea wengine kuwaomba msamaha na kama tumejikosea wenyewe kujirudi. Kwasababu kuna makosa ambayo tunafanya yenye madhara kwa roho zetu wenyewe.
Kuna ukweli ambao siwezi kuupinga kwa kusoma kwangu falfasa na dini na kutafakari karibu kila siku. Ukweli ni kwamba upendo huongoza kila kitu. Hatuwezi kuwa wakamilifu pasipo kuwa na upendo. Pasipo kuangalia binadamu wengine kwa jicho la upendo. Na hakutakuwa na amani duniani kama hatutajifunza kupenda.