Hakuna vitendo vya wizi Bandarini: TPA yatoa taarifa kwa umma

MIMI BABA YENU

JF-Expert Member
Mar 1, 2019
295
679
HAKUNA VITENDO VYA WIZI BANDARINI!

MAMLAKA YA USIMAMIZI WA BANDARI TANZANIA

TAARIFA KWA UMMA:

IJUMAA OKTOBA 11, 2019

DAR ES SALAAM.

Mapema leo katika Mitandao ya Kijamii hasa katika Instagram, kumesambaa habari kwa njia ya Video na picha za Mnato zikionyesha tukio la Wizi wa Vifaa vya Magari ukifanywa na Vijana katika eneo linalosadikiwa kuwa ni moja kati ya Bandari za Tanzania.

Taarifa hiyo iliambatishwa na maelezo yanayosomeka kuwa ‘Aina ya wizi mpya Bandarini, Magari yanapofika wahuni hawa wanabadilisha matairi na Rims…yanawekewa ya zamani its Pathetic ‘.

Taarifa hiyo imezua taharuki kubwa, kusambazwa na kupata Wachangiaji wengi katika Mitandao ya Kijamii wanaoilaumu TPA kutokana na vitendo hivyo.

Kupitia taarifa hii, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inapenda kuujulisha Umma kuwa, Taarifa hizi si sahihi hata kidogo na kwamba hazistahili kupewa umuhimu wowote, zipuuzwe. Sababu za Msingi za Kanusho hili ni hizi zifuatazo:

Kwanza:

Namba za Makasha(Kontena) zinazoonyeshwa kwenye picha hizo haziko katika mifumo ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wala ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TANCIS). Hii inamaanisha kwamba, Kontena hizo hazipo Tanzania.

Pili:

TPA haina miundombinu katika Bandari zake kama inavyoonekana katika Video na Picha za ,mnato zilizosambazwa.

Tatu:

Bandari zetu hazina geti linalotumika kuondoa Shehena ya makasha na gari kwa wakati mmoja kama ilivyoonekana kwenye taarifa hiyo. Pia na gati na yadi zinazotumika kushusha na kuhifadhi mizigo hiyo haziko pamoja.

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inapenda kuwasihi Wananchi wote na hasa Watumiaji wa Mitandao ya Kijamii kuepuka kutuma taarifa zenye kupotosha, kuchafua taswira ya Mamlaka na kuleta taharuki kwa Wateja, Wadau na Umma kwa ujumla.

Tunasisitiza kuwa, hakuna matukio wala Vitendo vya Wizi wa vifaa vya magari katika Bandari za Tanzania hasa baada ya TPA kufanya maboresho makubwa katika mifumo yake ya kiulinzi.

Tunawasihi Wateja wetu, Wadau na Umma kwa ujumla kuendelea kutumia Bandari zetu kwa uhakika kwa kuwa Sheria, Kanuni na taratibu za Uendeshaji wa Bandari zetu zinazingatiwa kikamilifu ambapo ulinzi na usalama wa mali za Wateja na Bandari unasimamiwa kikamilifu.

Imetolewa na:

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA)
 
Back
Top Bottom