Hakuna mambo matakatifu yasiogusika kujadiliwa katika katiba

Kakke

JF-Expert Member
Dec 4, 2010
1,883
1,482
[h=1][/h]Written by amini // 03/12/2011 // Habari // No comments

Hakuna mambo matakatifu yasiogusika kujadiliwa katika katiba

Posted on December 3, 2011 by zanzibaryetu
—
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) ambaye ni makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akihutubia katika mkutano wa wananchi wa Donge katika ziara zake katika majimbo mbali mbali Unguja na Pemba
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema hakuna mambo yaliyoainishwa kuwa ni matakatifu ambayo hayatakiwi kuguswa wakati wa kujadili Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano, hivyo Wazanzibari wajiandae kutoa maoni yao juu ya Katiba wanayoitaka, ikiwemo mfumo wa Muungano wenye maslahi kwao.
Maalim Seif amesema hayo huko Ole, Kaskazini Pemba alipokuwa akihutubia kwenye mkutano wa hadhara, akiwa katika ziara ya siku nne kisiwani humo. Alisema baada ya hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano kutia saini mswada uliopitishwa na wabunge kuhusu katiba mpya, hatua inayofuata ni kuundwa Tume ya kuratibu maoni ya wananchi juu ya katiba hiyo, na wananchi wanapaswa kujiandaa kutoa maoni bila ya uoga, na jambo muhimu ni kuhakikisha katika maoni yao hawamtukani mtu.
Makamu wa Kwanza wa Rais alisema tume hiyo itakayokuwa na wajumbe sawa kati wale wanaotoka Zanziba na Tanzania Bara, itatoa fursa ya kipekee kwa wananchi wa Tanzania, na Wazanzibari hiyo itakuwa nafasi yao muhimu kueleza nini wanataka, ikiwemo suala la mfumo au muundo wa Muungano.
“Nyinyi Wazanzibari na ndugu zetu wa Tanzania Bara ndio tuliovaa kiyatu (Muungano) na aliyevaa kiyatu ndiye anayejua msumari unachomea wapi, au anayelala kwenye kitanda ndiye anayejua kunguni wake”, alisema Maalim Seif.
Hata hivyo, alisema kwamba itakuwa ni jambo la maana zaidi Wazanzibari wakiwa na msimamo mmoja juu ya mambo wanayotaka katika katiba mpya na waweke kando itikadi zao za kisiasa katika jambo hilo.
Alieleza kwamba ni vyema wakaendelea na na msimamo kama ule waliouonesha wakati wa kutoa maoni juu ya rasimu ya mswada wa katiba mpya ulioandaliwa mara ya kwanza, kabla ya kuwasilishwa Bungeni, ambapo Wazanzibari kwa kauli moja waliupinga na ukarekebishwa.
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alisema hilo linawezekana kabisa kwasababu kuna Wazanzibari wengi ambao ni wanachama wa CCM wamekuwa wakiwasiliana naye wakitaka kuwe na msimamo mmoja wa Wazanzibari juu ya Katiba mpya, mambo ambayo yatakuwa na maslahi kwa Wazanzibari waliopo sasa na vizazi vijavyo.
“Mtasema wenyewe Wazanzibari mnataka nini katika Muungano, kama mlivyoamua wakati wa kuandaa mswada wa katiba mpya na mkasikilizwa, kama tungekumbatia itikadi za vyama vyetu mswada ungepita ule ule tulioletewa awali”, alisema Makamu wa Kwanza wa Rais.
Alionya kuwa katika kuzingatia mambo yenye maslahi kwa Zanzibar wasitokee watu wakaweka maslahi binafsi mbele, alisema haitakuwa jambo la manufaa kwa Zanzibar iwapo watajitokeza baadhi ya viongozi wakaanza kujadili nafasi zao za Ubunge na uongozi, iwapo muundo Fulani wa Muungano utapita.
Alisema kwa mfano baadhi ya watu wanaweza wakaweka maslahi binafsi wakaanza kuwaza nafasi zao za Ubunge zitakuwa zipi iwapo mfumo Fulani utapita hata kama ndio wenye maslahi kwa Zanzibar, bali wajadili maslahi ya Wazanzibari wote.
Maalim Seif alisema kutoa maoni juu ya katiba mpya ni fursa muhimu na adhimu kwa Wazanzibari ambao kwa muda mrefu wamekuwa na malalamiko ndani ya Muungano.
Aidha amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kuonesha hadharani kukwera na hatua ya Wazanzibari kupewa nafasi na fursa sawa na wenzao wa Tanzania Bara katika kujadili na kutoa maoni katika katiba mpya ya nchi yao, kwa madai Zanzibar ni ndogo na ina watu wachache, ikilinganishwa na Tanzania Bara.
Habari na Khamis Haji, (OMKR)
 
Back
Top Bottom