Hakuna biashara inafilisi kama uchimbaji wa madini

ulimi waupanga

JF-Expert Member
Aug 31, 2014
470
1,161
Niko hapa najililia nakujigalagaza, sina pa kuanzia wala pakuishia. Kwa ufupi ndugu zangu ukipata kimtaji chako hata kiwe million 200 nenda kafanye kazi zingine achana na mambo ya uchimbaji Madini bora kubet kuliko iyo kazi.

Mwaka 2015 baada ya kumaliza kielimu changu cha Uhandisi wa Migodi( Mining Engineering) niliamua kupambana kutafuta ajira siyo serikalini wala Migodini hali ikawa ngumu maana miaka hiyo ndio secta hii imeanza kuharibiwa kwa kufunga Migodi. Nikaona isiwe shida ngoja niende Machimbo ya kienyeji nipambane maana Nyumbani mama ilikuwa kila akiniona nipo tu bila kazi anaumia na kunambia " Mwanangu sikupambana kupika gongo usome halafu uwe hivi ulivyo" sisi wazazi wetu wanajua aliyesoma ni Yule mwenye kazi Serikalini. Ili kupunguza shida ikabidi niende mbali na macho ya maza.

Basi hapo nikaelekea Majita Musoma kuna eneo linaitwa Nyarufu nikapambana weee mpaka suruali zikaisha, kila siku unaona bora Jana yake. Nikazunguka mkoa mzima wa Mara kila nikisikia kuna sehemu inatoa nakimbilia huko, yaani kwenye kibegi(bob) nimebeba MOKO, PONCHI na NYUNDO. Toka mwaka 2016 mpaka 2019 sikufanikisha chochote mpaka nikasahau nimesoma fani gani hakika nikajiona labda kuna dhambi haijaandikwa ndiyo kubwa kuliko zote na Mimi ndiyo nimemtendea Muumba.

Mwezi wa 4 mwaka 2019 wakati wa makinikia Serikali iliruhusu wananchi Kuvamia eneo la Barick Mgodi wa Bulyanghulu, ikabidi wachimbaji tufunge safari kwenda kufanya Kazi pale. Jamaa yangu akinishauri kwamba tatizo langu naleta usomi kwenye Madini akanambia twende Bariadi kwanza tuagwe ndio tuingie Mgodini Kakola. Sikujiuliza mara 2 maana lengo langu nifanikiwe ili nimfurahishe mama yangu apunguze majuto ajione kweli alipambana ili mwanae nisome. Tulienda kule kuna Kijiji kinaitwa Sengerema unapita kisenta fulani kinaitwa Dutwa kuna babu anaitwa Matugandama, tukafanya ya kufanya na kuagwa( ili nalifupisha maana siyo lengo la stori).

Tukafika Kakola Kahama hapo mgodini Bulyanghulu, watu wamejaa utafikiri Sokoni Kariakoo, mie toka mwanzoni nilitamani kumiliki shimo(Duara) langu mwenyewe kwahiyo sikupendelea kufanya Kazi kwa watu, jamaa akanishauri kwavile mtaji hatuna basi tuombe shift kwenye mashimo yenye kuzalisha kukipata nguvu ndiyo tuanzishe letu. Ndani ya siku 5 tukapata shift sehemu tukapambana shift yetu ilipotoka tukapata mgao Kama laki 8 kila mtu, jamaa yangu akanambia umeona kwamba ukitumia njia ya kienyeji unapiga hela fasta? Kweli kwa vile na mimi nilikuwa sijapata hiyo pesa long time nikajiona nilichelewa kweli. Kwa mara ya kwanza nikamtumia mama laki 3, hakika maombi aliyoyapiga siku ile nilifikiri mbingu zinafunguka.

Kwa miezi 2- 4 ya mwanzo hali ilikuwa siyo mbaya sana tukawa tumepanga chumba sehemu moja inaitwa Bugarama tukawa tunakibubu chetu, mwezi wa 9 mwaka huo 2019 tukavunja kibubu ili tuanze kuzamisha Mgodi wetu. Tukakuta tuna kiasi cha million 7 na usheee! Jamaa akanambia kabla ya lolote turudi Bariadi kwanza kwa babu tunyooshe njia na Mimi nikwambia pamoja na hayo tupite Mwanza kuna jamaa namfahamu anayo mashine ya kudetect miamba ya Madini atukodishie tuituimie na yenyewe, jamaa akanambia babu akikubali tutafanya hivyo. Tulivyofika kwa babu akatuaga tena na ile ishu yangu ya kutumia mashine akanambia wewe tumia tu.

Tukarudi Mgodini nikatumia ile Gold detector kutafuta sehemu yenye anomalies nyingi, huku Sayansi kule dawa za babu zinachomwa ilimradi tu tupate dhahabu. Kipindi hicho mvua zilikuwa siyo za kitoto kila mkichimba mita 1.5 lazima shimo lifungwe na timba, mpaka tunafikisha mita 17 mtaji ukakata, bahati nzuri au mbaya zaidi pembeni ya ule Mgodi tuozamisha kulikuwa na shimo la zamani lishafukiwa kwahiyo kuna wazee wakawa wanatutia moyo kwamba tukifisha ule ule tunapiga kwenye mshono.

Ikabidi tumtafute mdhamini, nikafunge safari mpaka Nzega maana nimekulia pale kuna jamaa alikuwa anatinga Mgodini Resolute Nzega ndiye alinifanya nisome kozi ya Mining kwa life style alokuwa anaishi. Kwa muda huo alikuwa ameacha kazi pale Nyamongo so alikuwa na kimtaji bado nikamuimbisha na kwa vile aliniona nimesomea ile kitu akanielewa nikaondoka naye mpaka Bulyanghulu.

Jamaa akajitoa kwa kila njia, akanunua mashine za kupulizia upepo, mashine za kuvuta maji, akafunga na winchi,basi kwa vile sasa tuna jeuri ya mataji ikapedi tupige funka (maana yake unafungua njia ya horizontal huko huko underground kuelekea upande unaotaka) kuelekea kwenye lile shimo la zamani. Kazi ikawa nyepesi ni kufukua na kufunga timba.

Tumepambana mpaka mizamo 62 Kama mita 94 underground tukaanza kuona mwangaza kwamba sasa tunakaribia kufika mwisho ili tuanze kuvunja mwamba mara paaa Serikali ya Tanzania wamekubaliana na kampuni ya Barrick kuunda ubia hivyo mgogoro umeisha. Ndani ya siku mbili gari za polisi zinapita zikitangaza kwamba ndani ya wiki moja ibaki miti na ndege. Siku hiyo nilimwona Yule jamaa yangu mdhamini akichanganyikiwa presha ikapanda mpaka tukaanza kumpepea.

Ule muda wa wiki moja tuliopewa hatukuokoa chochote, tukashuhudia Mapolisi wakifukia Mgodi wetu pendwa tuliopambana kwa jasho na damu kuufikisha pale, mbaya zaidi ndio tumeanza kuyaona matunda ya kazi yetu tunaambiwa tuondoke hakika iliuma.

Jamaa yetu mdhamini akaondoka kuelekea kwake Nzega akiwa amefilisika, sisi tukabaki Kakola hatuna nyuma wala mbele. Kwa vile pale alikuwa amenunua mashine tofauti tofauti za gharama ikabidi tushauriane naye tuziuze angalau achukue hiyo hela afanye kutuliza familia yake iliyokuwa imeparanganyuka. Jamaa akasema japo pesa alitoa yeye lakini zile ni mali za ushirika maana Kama tungefanikiwa kupata dhahabu zile gharama tungezikata kabla ya kugawana faida. Akashauri tutafute mteja tuziuze tukipata hela tufanye biashara ya makinikia ambayo ilionekana ina risk ndogo.

Tukapambana akapatia mtu wa kutupatia milioni 15. Baada ya kufuka happo wachimbaji walielekea upande wa mashariki mwa Mgodi wa Bulyanghulu wilaya ya Msalala kuna milima watu walikuwa wanachimba mawe wanawauzia matajiri kwa ajili ya kutengeneza masenga (makinikia), ikabidi tufanye research kule kujua yana ppm ngapi ili tuwekeze kule.

Ikaonekana ni mazuri sana nikachukua sample nikaenda maabara Geita nikakuta yanasoma 10 ppm AU na 45 ppm Cu. Nikashauri tupige kazi pale, jamaa akarudi pori tukaingia kule milimani, kule mawe yanauzwa kwa mnada kwahiyo ukibahatika ukanunua yaliyopigwa vizuri unapata yanayosoma vizuri Kama walipiga sakayonsa unabeba uchafu tu.

Tukapambana kwa miezi miwili tukinunua mzigo wa kuurundika tu sehemu maana hatukuwa na mtaji wa kununua Ball Mill (crusher) na kujengea mwalo (plant). Baada ya kuona mzigo umekuwa mkubwa tukawaza tufanye nini tupate crusha, ikaonekana tunaweza kupata la kukodi, so gharama zote na kuendesha na kujengea mwalo kama million 7 ili tusage mzigo wote uliokuwa unakadiriwa Kama tani 170 mpaka 190.

Jamaa akajitoa kivingine akasema kuna kishamba chake huko kwao kijijini Bukoba ngoja akiuze liwalo na liwe ili tumalizie kazi yetu. Akakiuza na kupata iyo pesa, tukaanza kusaga mizigo yetu! Ile kuopoa round ya kwanza nikachukua sample nikatuma mahabara mbili tofauti moja ikasoma 6.5 nyingine 12. Tukashangaa mbona tofauti ni kubwa sana? Ikabidi nichukue tena nipeleke Mwanza, ikasoma 8ppm tukaona siyo mbaya inamaana averagi itakuwa ni 7 na usheee.

Tukaanza kuyasaga kwa fujo ili kukimbizana na muda maana crusha tulikodi kwa miezi miwili. Ile tumebakiza Kama tani 6 yaishe yote nikachukua sample kwenda maabara nakuta inasoma 2.1ppm. Ikabidi nisiwapatie majibu nichukue tena sample niagize Mwanza, Mwanza ikasoma 1.3ppm. Bahati mbaya majibu yalituma kwa njia ya whatsup na aliyekuwa na smartphone ni jamaa yetu. Duuu, jamani sijieni tu inatokea kwa mwingine, jamaa kwa sababu ya mshutuko presha ilipanda mpaka sasa amepooza, tukaone yale maudongo tuyapeleke wapi tukaanza kupambana kutafuta angalau mnunuzi kila mtu akija akichukua sample harudi tena.

Mwishowe ikabidi tuyauze kwa hasara ya Milioni 2 angalau tupate nauli ya kumsafirisha jamaa kwenda kwao kijini maana familia yake imevunjika vipande vipande.

Kila mtu kasambaa kivyake Mimi nimeamua kuja Kibaha niko nauza matunda barabarani, najuta kwanini nilienda kutafuta Elimu, najuta mzazi kupoteza vijisenti vyake kunipeleka shule, najuta kujiingiza kwenye uchimbaji Madini.
 
Back
Top Bottom