HakiElimu yawaunga mkono walimu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

HakiElimu yawaunga mkono walimu

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Makoba, Nov 5, 2009.

 1. M

  Makoba Member

  #1
  Nov 5, 2009
  Joined: May 25, 2009
  Messages: 10
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Lipeni Walimu Malimbikizo ya Stahili Zao Ili Kuepuka Mgomo Mkubwa wa Walimu Unaolinyemelea Taifa!
  Elimu ndiyo msingi muhimu kwa maendeleo ya taifa. Kama nchi, tunaweza tu kusonga mbele kimaendeleo endapo sisi raia tutakuwa tumeelimika, tunao ufahamu na ujuzi wa kutosha utakaotuwezesha kuwa wakulima tunaozalisha kwa tija zaidi, wafanyabiashara wazuri na viongozi werevu, wenye busara na hekima.

  Hii ina maana kwamba hatuna budi kuwa na walimu wa kutosha wenye uwezo wa kuwajengea watoto wetu ufahamu sambamba na kuhakikisha kwamba elimu bora inapewa umuhimu wa kipekee. Hii pia ni pamoja na kufuatilia maendeleo ya mtoto mmoja mmoja anapokuwa katika mchakato wa kujifunza. Aidha, tunahitaji kuongeza idadi ya walimu na sisi wenyewe kujiwekea viwango vya utoaji wa elimu bora kama vile uwiano wa mwalimu na wanafunzi, n.k.. Mwalimu ni mtu muhimu sana kwa mstakabali wa taifa hili.

  Lakini kwa bahati mbaya sana, siku hizi katika nchi hii, walimu hawathaminiwi kama kiungo muhimu katika kuhakikisha kuwa nchi inaingia katika ushindani wa kielimu na kimaarifa hapo baadaye. Hii ni tofauti sana na miaka ya nyuma ambapo mwalimu aliheshimika na kujaliwa sana katika nchi yetu. Walimu wengi wanapangiwa shule huku kukiwa na nyumba chache za kuishi, au kukiwa hakuna nyumba kabisa za walimu! Aidha, walimu hawa hukosa hata mahitaji yao ya muhimu. Licha ya hali mbaya ya maisha ambayo baadhi yao hulazimika kuishi, walimu hao hao hulipwa mishahara ambayo siyo tu ni midogo sana isiyoweza kukidhi mahitaji yao ya kila siku, bali pia hulipwa kwa kuchelewa sana.

  Hali hii inatupa taswira mbaya na mwelekeo wa hatari kitaifa ambao dalili zake zimeanza kuonekana. Wakati tayari kuna upungufu mkubwa wa walimu, upo ushahidi kuwa walimu waliopo wanaacha kazi yao ya ualimu na kukimbilia kazi nyingine ambazo zina maslahi mazuri zaidi. Si hivyo tu, bali pia wanafunzi wanaohitimu katika shule za sekondari na vyuo vikuu wengi wao hawataki kujiunga na fani ya ualimu kwa sababu ya mazingira duni ya kufanyia kazi na mishahara isiyoridhisha. Tunaelewa sana kuna ufinyu wa bajeti, lakini licha ya ufinyu huo ni muhimu sana kuweka vipaumbele katika mipango yetu, mojawapo ni maslahi ya walimu wetu.

  Hoja ya kuwa walimu wetu wapatiwe mahitaji yao ya muhimu si tu inastahili kupewa kipaumbele kadri siku zinavyokwenda bali pia ni suala linalopaswa kutatuliwa haraka. Wakati Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilitoa shilingi bilioni 7.6 katika mwaka wa fedha 2008/09 kwa ajili ya kulipa malimbikizo ya mishahara ya walimu, posho na maslahi mbalimbali kwa walimu 3,202 ni shilingi 1.2 bilioni tu ndizo zilitumika kwa malipo hayo. Kwa mujibu wa taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kuna shilingi bilioni 22.8 za malimbikizo hayo bado hazijalipwa. Hivyo bado kuna takribani mara 2½ zaidi ya kiasi ambacho bado hakijalipwa.

  Hakuna mtu anayefahamu uzito wa tatizo hili kwa undani zaidi kuliko walimu wenyewe. Wamesubiri malipo yao kwa miaka kadhaa sasa bila mafanikio, na inavyoelekea hawataweza kuendelea kusubiri zaidi. Yote haya sasa yanaelekea kuzua tafrani inayoambatana na vitisho, migomo baridi, n.k.; mambo yanayoenea takribani nchi nzima sasa:


  • Mathalani, huko mkoani Tanga, wiki mbili zilizopita, kwa mujibu wa gazeti Tanzania Daima, 16/10/09 (uk. 6), walimu 300 katika wilaya ya Muheza walivamia ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya kwa zaidi ya wiki moja wakijaribu kufuatilia stahiki zao hadi Mkuu wa Mkoa alipoingilia kati suala hilo.

  • Nayo magazeti ya The Citizen la tarehe 27/10/09 (uk. 7) na Daily News la tarehe 24/10/09 yalibainisha kuwa huko mkoani Kagera, walimu wanadai shilingi milioni 917, na kuwa bado kuna madai zaidi ya walimu wa sekondari wakati mara baada ya kufanyia uhakiki, walimu wengi wa shule za msingi tayari wamekwisha kulipwa madai yao. Maelezo haya ni sahihi isipokuwa tu kwa walimu wa shule za msingi ambazo zimeanzishwa hivi karibuni hususan wilaya ya Chato ambayo rekodi yake ya malimbikizo inafikia shilingi milioni 311, hazina ilitoa shilingi milioni 31 tu kutokana na makosa ya kiuandishi.

  • Huko Mbeya vyombo vya habari vimeripoti kuwa walimu wa sekondari na wakufunzi wa vyuo waliipa serikali hadi tarehe 31 Oktoba 2009 kuwalipa malimbikizo ya madai yao yote, kinyume na hivyo wangeitisha mgomo. Hali kadhalika walimu wa shule za msingi ambao hawajalipwa madai yao wako tayari kuungana na wenzao katika mgomo huo.

  Kwa kuwa sasa tarehe ya mwisho iliyowekwa imeshapita, Chama cha Walimu Tanzania kimetangaza mgomo nchi nzima utakaoanza tarehe 7 Novemba. Wakati hakuna mtu anayetaka kuona mfumo wetu wa elimu ukiathirika na kusambaratika, HakiElimu inasimama nyuma ya walimu hawa na inatangaza kuunga mkono jitihada zao za kujiunga pamoja na kuishinikiza serikali ili itekeleze madai yao. Wamekuwa wavumilivu kwa muda mrefu, lakini tusichukulie uvumilivu huo kama kigezo cha kuendelea kulinyamazia tatizo hilo na hivyo kuendelea kuwanyima haki yao. Matokeo haya ya kulinyamazia jambo hili ndiyo tunayaona sasa yamefikia kilele cha uvumilivu wao; walimu hawa wanajiunga pamoja na kujiandaa kugoma.

  Ingawa tunaelewa matatizo mengi ya walimu na kuunga mkono kilio chao, lakini HakiElimu inaamini vilevile kwamba haki ya watoto wetu kupata elimu, na maendeleo ya taifa letu kwa baadaye ni lazima yawe ya thamani ya juu zaidi. Hivyo basi wakati tunaunga mkono hatua ambazo walimu hawa wanazichukua na kwa kuelewa umuhimu wa kuchukua hatua za haraka pale ambapo njia za kudai malipo yao kwa kuomba zinaposhindwa kufanikiwa, ni vema basi pia walimu mtambue kuwa si jambo la busara nchi yetu ikaingia katika mgomo wa namna hii, na watakaoathirika ni watoto wetu wenyewe.

  Wizara imetangaza kwamba walimu sasa watalipwa madai yao; hivyo tunaiomba serikali isimamie hili ili ahadi hii itimizwe kweli na tatizo hili kutokomezwa kabisa. Kwa hiyo inashauriwa kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na TAMISEMI zihakikishe kuwa watumishi hawa wa umma wanalipwa mara moja madai yao, kwa lengo la kuboresha elimu na kuhakikisha kuwa nchi yetu inabaki katika hali ya utulivu na amani.

  Hatuamini kuwa hili ni tatizo la kifedha, bali ni suala la kuwa na nia ya dhati/utashi wa kisiasa na kulipa kipaumbele suala hili. Hii ni gharama ndogo kwa serikali kulipa, na walimu ni watumishi muhimu sana wa umma wanaoweza kulihakikishia taifa uzalishaji wenye tija hapo baadaye. Hivyo tuwafanye walimu pamoja na mahitaji yao kuwa ndivyo vipaumbele vyetu vya kwanza.

  Mchakato wa kupeleka madaraka ya utawala, usimamizi na maamuzi kwa wananchi kupitia serikali zao za mitaa ndiyo njia sahihi kabisa kwa serikali kushughulikia kero za walimu kama vile mishahara na malimbikizo mengine. Maafisa wa wilaya lazima wapewe majukumu haya, kwa kuwa njia hiyo ni rahisi na nafuu. Katika kipindi hiki cha mpito, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inahitaji kufanya kazi kwa karibu zaidi na TAMISEMI ili kuhakikisha kuwa kuna ufuatiliaji wa kutosha unaofanywa na maafisa wilaya ili kuhakikisha kuwa watumishi wote wa umma wanalipwa stahiki zao.

  Uchunguzi juu ya madai ambayo bado hayajalipwa umekwisha kufanyika; kiasi cha fedha zinazodaiwa tayari kimejulikana. Serikali inahitaji kuwaonesha watumishi wa umma kwamba inawajali na kwamba inazingatia utoaji wa elimu bora nchini kwa kuwalipa iliyo stahiki yao.
   
Loading...