Hakielimu: Siasa zimeathiri matokeo kidato cha nne

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,011
Hakielimu: Siasa zimeathiri matokeo kidato cha nne

Saturday, 29 January 2011 08:55 0diggsdigg


missokiahakielim.jpg

Mkurugenzi wa Shirika la Haki Elimu, Elizabeth Missokia akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana juu ya hali halisi ya matokeo ya mtihani wa kidato cha Nne Kitaifa 2010 yaliyotangazwa hivi karibuni, jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mchambuzi wa Sera wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET) FlorenceFrancis.Picha na Zacharia Osanga

Fidelis Butahe
Mwananchi

KUSHUKA kwa kiwango cha ufaulu kidato cha nne mwaka 2010 kwa asilimia 22 ni matokeo ya serikali kuruhusu propaganda za kisiasa katika mipango ya elimu, imeelezwa.

Hayo yalielezwa na Taasisi ya HakiElimu ikishirikiana na Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) katika mkutano na waandishi wa habari, Jijini Dar es Salaam, jana.

Walieleza kwamba serikali imekuwa ikipanga mambo mengi ya elimu yakiongozwa na propaganda za kisiasa jambo ambalo halitekelezwi kikamilifu.Wakatoa mfano kuwa serikali iliwahi kutoa ahadi ya kujenga nyumba za walimu 21,000 lakini hadi unafika mwisho wa kipindi kilichokadiriwa ni 260 tu zilikuwa zimejengwa.

"Wanaweza kueleza kuwa wanajenga nyumba za walimu 21,000 lakini mpaka kipindi walichopanga kinamalizika wamejenga nyumba 260 tu," Alisema Ofisa Utetezi wa sera za elimu wa TEN/MET, Florence Francis.

Kutokana na hali hiyo, alishauri kwamba siasa isiingizwe katika sekta ya elimu kwa kuwa italiangamiza taifa.Francis alisema elimu ya Tanzania haitafika katika kiwango cha juu kama masuala ya siasa yataendelea kuchanganywa na elimu.
"Binafsi naona bora kuwa na sheria kuwa kila mtanzania, awe na fedha au asiwe nazo apeleke mtoto wake kusoma katika shule za serikali za Kata, kwa sababu vigogo hawaoni hasara ya shule hizi kwa kuwa watoto wao hawasomi huko," alisema Francis.

Alisema kuwa umefikiwa wakati kwa wananchi kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kufanya mikutano ya kamati za shule na kuwasilisha matatizo yao sambamba na kufuatilia maendeleo ya watoto wao."Umefikia wakati wa serikali kutimiza ahadi zake, mpango wa MMES na MMEM ni mzuri, lakini wanaweza kueleza kuwa wanajenga nyumba za walimu 21,000 lakini mpaka kipindi walichopanga kinamalizika wamejenga nyumba 260 tu," alisema Francis.

Januari 25 Baraza la mitihani (Necta) ilitangaza matokeo ya kidato cha nne uliofanyika Oktoba, 2010 yanayoonyesha kuwa kiwango cha ufaulu kimeshuka kwa asilimia 22 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2009 huku wasichana wakiwa wanaoongoza kwa kufanya vizuri.


Mkurugenzi wa Hakielimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Hakielimu, Elizabeth Missokia alisema licha ya kuwa idadi ya watahiniwa waliofanya mtihani huo kuongezeka kwa asilimia 43, bado mazingira yanawagandamiza watoto wa masikini na kwamba wengi wao ndio waliofeli mtihani huo."Maelfu ya wanafunzi walioshindwa mtihani wametokea katika shule za kata ambako ndiko kwenye wananchi masikini zaidi.

Kwa mwenendo huu tutawakomboaje watu masikini wa nchi hii ambao ni wengi," alisema Missokia.Alisema tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo shule za serikali zilikuwa zikiongoza, hivi sasa mambo yamebadilika ambapo shule hizo zimekuwa zikifanya vibaya.

Kwa sababu hiyo akahoji ni kwa nini serikali isijifunze kuendesha shule zake kama zinavyoendeshwa shule za binafsi."Shule binafsi hazipati ruzuku ya serikali. Kwa nini uwekezaji wa serikali katika elimu usiendane na matarajio ya wananchi, walipa kodi," alihoji Missokia.Alisema kuwa hatua za haraka zinatakiwa kuchukuliwa ili kuboresha sekta ya elimu kwa kuwa kila mwaka mikoa inayofanya vizuri ni ile ile.

"Tumesikia wasichana kuwa wamefanya vizuri, tujiulize ni wasichana wangapi waliofanya mtihani ule? Wavulana waliofaulu ni asilimia 56.28 na wasichana ni 43.47, waliopata daraja la I-III, wasichana ni asilimia 7.81 na wavulana ni 14.62.

Hii ni tofauti kubwa," alisema.Aliongeza " Haiwezekani kujifariji kwa kuangalia ufaulu wa wasichana wachache wakati huo huo fursa za walio wengi zikibinywa, malengo ni kuwaendeleza wote, wasichana kwa wavulana."Alizitaja sababu zilizochangia kushuka kwa ufaulu kuwa ni pamoja na uhaba wa walimu, mazingira duni ya kujifunzia, uhaba wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia pamoja na hamasa ndogo ya wanafunzi.

Alisema kuwa ili elimu haiwezi kuboreshwa kwa kuendelezwa kwa watu wachache wanaopata fursa za kipekee kwenye shule chache huku elimu ya jamii pana ikiwa mashakani."Hakuna haja ya kulumbana wala kuingiza siasa katika elimu, bali serikali itekeleza mipango na sera zilizopo na kuboresha mapungufu kwa kushirikiana na wadau," alisema Missokia.

Alisema kuwa ili kuboresha elimu kusiwe na njia za mkato bali ni kuwa na njia za kuwekeza kwa umakini katika elimu.Alisema ahadi zilizotolewa na rais Jakaya Kikwete katika Uchaguzi mkuu wa Oktoba 31 mwaka huu zifanyiwe kazi."Rais alitoa ahadi ya kuipa kipaumbele sekta ya elimu, kuboresha maslahi ya walimu, Wizara ya Tamisemi nayo iliahidi kuboresha mafunzo ya walimu, nyumba za walimu zitajengwa, maabara zitaongezwa, umeme utafika mashuleni ili kuboresha shule za serikali.

Ni matumani yetu kuwa ahadi hizi zitatekelezwa," alisema Missokia.Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Joyce Ndalichako, aliwaambia waandishi wa habari wakati akitangaza matokeo kuwa wasichana wamefanya vizuri zaidi kuliko wavulana.Kwa mujibu wa matokeo ya mtihani wa mwaka jana, kati ya shule kumi bora katika kundi la shule zenye watahiniwa chini ya 40, saba ni shule za seminari na huku Shule ya Seminari ya Uru inaongoza shule kumi bora katika kundi la shule zenye watahiniwa zaidi ya 40. Matokeo hayo yanaonyesha kuwa shule kumi za mwisho ni mchanganyiko wa shule za serikali na watu binafsi.

Joseph Mungai naye anena
Waziri wa zamani wa Elimu na Utamaduni, katika Serikali ya awamu ya tatu, Joseph Mungai amesema matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne yamesababishwa na Serikali ya awamu ya nne kuyatupa baadhi ya mambo mazuri yaliyokuwemo kwenye mpango MMES.

Mungai ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini Mkoani Iringa kwa nyakati tofautitofauti na Waziri katika awamu ya kwanza na ya pili kabla ya kuwa Waziri wa elimu mwaka 2000 hadi mwaka 2005, aliyataja baadhi ya mambo hayo ni kuwepo na mizania kati ya upanuzi wa elimu ya sekondari na upanuzi wa mafunzo ya walimu wa sekondari.

Alitaja sababu nyingine ambazo zilizochangia wanafunzi wengi waliohitimu kidato cha nne kushindwa mitihani kuwa ni upanuzi wa elimu ya sekondari bila kufuata mpango wa maendeleo ya elimu hiyo yaani MMES."Nafikiri kwa maoni yangu, haya matokeo ya sekondari yanatokana na kupanua elimu ya sekondari bila kufuata mpango wa elimu ya sekondari," alisema Mungai na kuongeza:"Kulikuwa na mpango wa MMES niliuacha pale (Wizara ya Elimu) tulikuwa tumepanga mambo mengi na ilikuwa yaende hatua kwa hatua.

Mojawapo ni kwamba ilikuwa baada ya miaka mitano, kuanzia 2005, idadi ya wanafunzi wanaokwenda elimu ya sekondari ndiyo wafikie asilimia 50.
Alisema baada ya mafanikio makubwa katika elimu ya msingi kutokana na utekelezaji wa MMEM na MMES ambao ulipaswa kuanzia mwaka 2005 na mwaka huo ndipo vilianzishwa Vyuo Vikuu vya Elimu vya Mkwawa na Chang'ombe kwa lengo la kusaidia upatikanaji wa walimu wa sekondari.

Alisema Mkwawa na Chang'ombe vilianzishwa kwa lengo la kuweka mizainia kati ya upanuzi wa elimu ya sekondari na upanuzi wa mafunzo ya walimu wa sekondari.
Mungai aliongeza kwamba walikuwa wameongea na Vyuo hivyo baada ya kuanzishwa, kwamba wanafunzi wa mwaka uliokuwa unaonza wafundishwe zaidi mbinu za ufundishaji ili baada ya mwaka huo waende kusaidia kufundisha sekondari kupunguza uhaba wa walimu.

"Tulitaka wanafunzi walioingia mwaka wa kwanza wakati Vyuo hivyo vinaanzishwa, mkazo uwekwe zaidi kwenye mbinu za ufundashaji," alisema Mungai.

Mungai alisema serikali iliharibu pale ilipoendeleza mpango huo kwa kujenga shule ya sekondari kila kata huku zikikabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu. "Sasa kuna baadhi ya shule katika kata zina mwalimu mmoja au wawili... Ilifika wakati Wizara walilazimika kuanza kupanga upya walimu, haikuwa mbaya lakini tatizo ni kwamba baadhi ya shule zilikuwa zinafanya vizuri lakini walimu wake walipoondolewa na kuhamishiwa sehemu nyingine, shule hizo ziliathirika pia," alifafanua.

Tatizo lingine ambalo Mungai alisema limechangia matokeo mabaya ni mlundikano wa masomo kwa ngazi hiyo ya sekondari huku baadhi ya masomo yakiwa yanafundishwa kwa kiwango hafifu kutokana na walimu kutoyamudu. "Tulitengeneza Programu ya kupunguza wingi wa masomo katika shule za sekondari tukaondoa masomo ya michepuo kama ufundi, kilimo na biashara na tukaweka mkazo kwenye hisabati ili hisabati liwe na hesabu za biashara.

Hilo nalo liliondolewa," alisema. Alisema ili kuboresha elimu hiyo ya sekondari kuna haja ya kufanya marejeo ya Mpango mzima wa MMES pamoja na kuweka mkazo kwamba shuleni ni mahali pa mwalimu kufundisha na mwanafunzi kusoma.

"Nilipoingia Wizara ya Elimu nilikuta Pass rate (Kiwango cha kufaulu) kilikuwa asilimia 19 lakini kwa kuweka mkazo kwamba shuleni ni mahali pa mwalimu kufundisha na mwanafunzi kusoma na kufuta Umtashumta na Umiseta ingawa nalaumiwa mpaka leo, kiwango cha kufaulu kilipanda hadi asilimia 62 mwaka 2005."Lakini hebu angalia leo kiwango cha kufaulu darasa la saba kimekuwa kikishuka kila mwaka," alisema.
 
Back
Top Bottom