Haki ya Mwanamke kabla ya Uislamu: Sheria Mbalimbali zinazolinda Haki za Mwanawake

Influenza

JF-Expert Member
Jul 1, 2018
1,445
3,403
Ulinzi wa haki za binadamu ni haki ya msingi kwa kila mwanadamu ambapo mwanamke na mwanamme wana haki sawa katika kufaidi haki hizo. Kukosekana kwa haki hizo kunapelekea kudharaulika, kuongezeka umasikini na kukosekana kwa amani ya wanawake.

Mikataba mbalimbali imepitishwa ili kuhakikisha kuwa wanawake wanafaidi haki hizo. Pia kuna Sera, Sheria na miongozo mbalimbali inayoelekeza haki za mwanamke

Lengo kuu la mikataba ya haki za binadamu ni kuondoa ubaguzi katika kunufaika na haki za binadamu kwa msingi wa jinsi, dini, kabila, rangi, umri, utaifa na kadhalika. Baadhi ya mikataba hiyo ni:-

1. Mikataba ya Kimataifa inayolinda haki za wanawake; Mkataba wa kimataifa wa kuondoa aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake wa mwaka 1979:

Mkataba huu kwa jina jingine unajulikana kama ‘Mkataba wa Wanawake’. Huu ndio mkataba mkuu unaolinda haki za wanawake duniani.

Ulikubaliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mwaka 1979 na utekelezaji wake ulianza tarehe 3 Septemba, 1981. Tanzania iliridhia mkabata huu na kusaini makubaliano tarehe 19/09/1985. Mkataba huu unalenga kuhakikisha kuwa wanaume na wanawake wanafaidika kwa usawa na fursa za kiuchumi, kijamii, kitamaduni, kiraia na kisiasa kwa kuondoa aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake.

2. Mkataba nyongeza wa Haki za Wanawake Barani Afrika wa mwaka2003:

Mkataba huu ulipitishwa na wakuu wa nchi na serikali za Afrika mwaka 2003 huko Maputo, Msumbiji. Hadi Agosti 2004, ni nchi nne (4) tu za Umoja wa Afrika zilizoridhia mkataba huu.

Tanzania ilisaini mkataba huu tarehe 5 Novemba 2003. Kwa ujumla,mkataba huu ambao pia unajulikana kama “Mkataba wa Maputo” unalinda haki za wanawake wa bara la Afrika.

3. Azimio la Beijing la mwaka 1995

4. Mkataba wa SADC unaozungumzia ukuzaji wa kijinsia wa mwaka 1997

Makubaliano ya ILO juu ya haki sawa Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 na ya Zanzibar ya mwaka 1984:

Katiba zote mbili (pamoja na marekebisho yake ya mara kwa mara) zinatamka kuwa “binadamu wote ni huru na sawa”.

Pia “watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki bila ya ubaguzi wowote kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria”. Katiba zote mbili zinakataza sheria kuweka sharti lolote ambalo ni la kibaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake.

Ubaguzi unaokatazwa na Katiba unaweza kuwa dhidi ya rangi, kabila, jinsi, utaifa, mahali mtu alipozaliwa au hali ya maisha ya mtu. Kwa maana nyingine, katiba ya nchi inatoa haki sawa kwa wanaume na wanawake nchini Tanzania katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Sheria na Sera za nchi zinazolinda haki za wanawake Sera ya Jinsia ya Zanzibar:

Ni sera inayotambua na kuainisha mahitaji mbalimbali ya kijinsia baina ya mwanamke na mwanamme. Lengo kuu la sera hii ni kuweka mazingira mwafaka yatakayowezesha wanawake na wanaume kutekeleza majukumu yao katika jamii kwa kuzingatia usawa na mahitaji yao kijinsia.

Sera nyingine zinazozingatia haki za wanawake ni:
1. Sera ya Elimu ya mwaka 2006. Moja ya malengo ya sera hii ni kutoa fursa sawa ya elimu kwa watoto wa kike na wa kiume bila ya ubaguzi kwa kuzingatia kuwa elimu ni haki ya msingi ya binadamu. Sera hii imetoa mwongozo kuwa watoto wote bila kujali jinsia wakifika umri wa miaka 4 waanzishwe elimu ya maandalizi kwa muda wa miaka 2 na wakifika miaka 6 wote waanze elimu ya msingi.

2. Sera ya Ajira
Baadhi ya Sheria zinazolinda haki za wanawake Zanzibar:
Serikali imepitisha sheria mbalimbali zinazolinda haki za wanawake. Miongoni mwake zipo sheria muhimu ambazo ni pamoja na:-

(a) Sheria ya Mahakama ya kadhi Na. 9 ya mwaka 2017. Hii ni sheria mpya baada ya Sheria ya awali ya mwaka 1985 kufanyiwa marekebisho.

Sheria hii inasimamia mambo makuu 7 ikiwemo masuala yote ya ndoa na talaka, masuala binafsi (Personal Status), matunzo na uhifadhi wa mtoto, usia na masuala ya mirathi, kuachana na mgawanyo wa mali kwa wanandoa waislam. Hii ni sheria muhimu sana katika upatikanaji wa haki za wanawake wa kiislamu.

(b) Sheria ya Elimu Na. 6 ya mwaka 1982, inatoa fursa kwa watoto wa kike kupatiwa elimu bila ya ubaguzi. Aidha sheria hii imetoa fursa kwa watoto wa kike watakaopata ujauzito wakiwa wanafunzi kuweza kuendelea na masomo mara tu baada ya kujifungua.

(c) Sheria ya Ajira/kazi; Wanawake wanapewa haki ya kuwa na fursa ya kufanya kazi na kulipwa ujira unaostahili. Pia sheria za kazi zinatoa haki ya mwanamke kufaidi mafao ya uzazi ikiwemo likizo ya miezi 3 na masaa 2 ya kunyonyesha kwa kila siku.

(d) Sheria ya adhabu: Sheria hii imekuwepo ili kulinda na kurudisha utu na heshima ya wanawake na watoto. Sheria hii inatoa adhabu kali kwa makosa ya kujamiiana kama vile ubakaji na udhalilishwaji wa wanawake na watoto wa kike.

(e) Sheria ya ndoa na talaka kwa waislam ibara ya 91. Ingawa Sheria hii inasomeka kama sheria ya ndoa na talaka, bado haijakidhi haja kwani inatoa mwongozo tu wa namna ya kusajili vyeti vya ndoa na vya talaka pamoja na umuhimu wake.

Haijatoa fursa wala haki kwa wanandoa ambao wanastahiki kuzipata wakiwa au baada ya kuvunjika kwa ndoa zao.

(f) Sheria za Ardhi: Zanzibar kuna sheria nyingi zinazohusiana na umiliki wa ardhi lakini sheria zote hizo zipo kimya juu ya haki ya umiliki wa ardhi kwa mwanamke kwani hazitoi fursa maalum lakini pia hazijamnyima fursa mwanamke kumiliki ardhi.

Imeandaliwa na
Shirika la Konrad Adenaure Stiftung kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA)
 
Back
Top Bottom