Haki vs Amani vs Utulivu

Wamkopeka

Senior Member
Apr 2, 2012
136
308
Tukielekea kwenye uchaguzi siku 24 kuanzia leo kumekuwepo na mkanganyiko mkubwa wa hayo maneno hapo juu.

Ukisikiliza sera na ilani hasa za vyama vikuu 2 shindani unabaki unachanganyikiwa kujua ni chama kipi hasa kiko sahihi.

Wakati upande wa ccm na wagombea wao wako msitari wa mbele kusisitiza amani kwenye uchaguzi huu, na wanakwenda mbele zaidi kwa kusema ili tudumishe amani iliyopo basi hatuna budi kuichague ccm na wagombea wao. Kwamba kutoichagua ccm ni kukaribisha machafuko, wakitolea mfano wa Libya na Iraq ingawa kiukweli nchi hizo hazikubadilisha viongozi kwa njia ya uchaguzi bali vita.

CCM pia wamekuwa mstari wa mbele kutuasa sisi wapiga kura kuwa mgombea wa chadema ametumwa na mataifa ya kigeni kuja kugombea ili akifanikiwa aiuze nchi yetu.(na hapa ndipo msingi mkuu wa beno mabeberu ulipo)

Kwangu mimi naona hizi ni tuhuma kubwa sana ambazo hazitakiwi kuchukuliwa kirahisi. Lakini natatizwa na jambo moja tu kwamba kama hizi tuhuma zina ukweli ilikuweje mtu huyu akaruhusiwa kugombea nafasi nyeti kama hii? Na je wananchi wakimchagua kwa kuupuza hizi tuhuma itakuwaje?

Kwakuwa jukwaa letu ni la great thinkers nadhani mtanisaidia kupata ufumbuzi wa hayo maswali yangu.

Kabla sijazungumzia mtazamo wa CHADEMA na wagombea wao naomba nimalizie kwa kusema, ccm wanasema nchi yetu amani imetamalaki, wakitolea mfano kwamba mtanzania unaweza kutoka sehemu moja ya nchi kwenda sehemu nyingine kuishi au kufanya shughuli zako bila bughudha, wanasema pia kumekuwepo na uhuru wa kuabudu ndio maana tuna madhehebu na misikiti mingi tu,na upatikanaji wa elimu kwa wote.

Sasa ukija upande wa CHADEMA wao msisitizo wao mkubwa kwenye uchaguzi huu umejikita kwenye suala zima la haki.

Wanasema ili tuwe na amani ya kweli basi ni lazima watanzania tuhakikishe uchaguzi huu unaendeshwa kwa haki maana haki ndio msingi wa amani. Amani haiwezi kujengwa hewani tu bila msingi ambao ni haki.

Wanasema kwa sasa Tanzania kuna utulivu tu lakini amani ya kweli haipo hii ni kutokana na kutikiswa kwa msingi mkuu ambao ni haki.

Hoja yao wanaijenga kwa kuhusianisha na matukio kadhaa yanayopoka haki za kiraia. Kama utekaji nyara unaopelekea watu kupotea au kuumizwa nk. Watu kupigwa risasi mchana kweupe kama Aquilina, Shekh Ponda na Lissu na wahusika kutokukamatwa, watu kuuawa kama Alphonce Mawazo, Aliyekuwa diwani wa Ananasifu Kinondoni,Luena kule Morogoro, Kanguye nk.

Watu kufunguliwa kesi zisizokuwa na dhamana kwasababu tu ya kuwa kinyume na matendo ya serikali, watu kufirisiwa nk. Wanadai kwasasa kumeibuka mtindo wa polisi kukamata watu hasa wenye itikadi tofauti na ccm kwa mtindo wa kuteka, kutesa na kufichwa kusikojulikana ili kuleta taharuki kwa ndugu jamaa na marafiki wa mtuhumiwa..

Wapinzani kutokutendewa haki katika mchakato mzima wa chaguzi zetu, ikiwemo kuenguliwa bila sababu za msingi jambo ambalo halitokei kwa wagombea wa ccm, kunyimwa form za ugombea au kuporwa, kuzuiwa kuapishwa kwa mawakala wa upinzani, kupigwa mabomu misafara yao bila sababu za msingi na huku misafara ya ccm ikilindwa bila kubughudhiwa.

Wanasema mambo hayo ni kupoka haki hivyo kuvuruga msingi mzima wa amani.

Wao kwenye uchaguzi huu wanasisitiza haki itendeke ili mshindi wa kweli apatikane. Kinyume cha hapo wanasema hawako tayari na hakitaeleweka.

Je tunafanyaje ili tutoke salama? Kipi kiwe kipaumbele chetu kwenye uchaguzi huu?

1.AMANI
2.HAKI
3.UTULIVU
 
Back
Top Bottom