Haki si tu itendeke lazima idhihirike kweli imetendeka

MULANGIRA

Member
Oct 10, 2010
74
0
Haitoshi haki itendeke, lazima idhihirike kweli imetendeka

lC.gif
Hidaya​
Novemba 17, 2010
rC.jpg

Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.​
Mpenzi Frank,
POLE sana mpenzi wangu. Yaani watu wengine sijui akili zao zikoje! Au kama anavyosema yule fyatu wako Makengeza, kama akili yako iko katika kulamba miguu ya watu, si inabidi uiname fulutaimu hivyo unachoona ni buti za mabosi tu badala ya hali halisi za watu.
Yaani bado siamini kwamba mtendaji kata ambaye ni mtu wa serikali anaweza kuwanyima kituo chenu cha vijana eti kwa kuwa mlifanyia kampeni upinzani. Inamhusu nini? Kituo kile ni cha chama? Namkumbuka yule mwalimu aliyetuadhibu sisi sote eti kwa kuwa tulisema hajui kufundisha tunamtaka mwingine.
Akatembeza bakora kutufunza adabu! Adabu gani? Si tulimchukia zaidi. Badala ya kutafuta kufundisha vizuri zaidi akatuadhibu kwa uzembe wake mwenyewe. Kama ni hivyo sijui tutafika wapi.
Upande wangu, mimi mzima mpenzi kama si wazimu ya mambo hayo yanayotokea. Binti Bosi alirudi jana kutoka shule na mambo mapya. Nilijua kabisa kwamba alitaka kumchokoza baba maana alikuwa hatulii. Kila akisikia mlio wa gari, anachungulia dirishani.
Lakini hebu nianze mwanzo. Unajua BB ameanza kuwa pinzani ndani ya tawala ha ha! Maana tangu harakati za kampeni hakubaliani na bosi na kila wakati anaonyesha vidole viwili. Yaani bosi anavyokasirika sisemi hadi mama bosi anambembeleza nusura ya kufa eti hii ni nyumba ya amani na upendo lakini BB hataki kunyamaza. Hata bosi alipomnyima auti zake za kila wikiendi hakujali bali aliendelea kupiga kelele.
‘Unaona sasa? Badala ya kujadili katika kutafuta ukweli, unatumia nguvu uliyo nayo kulazimisha. Hayohayo ninayosema!!’
‘Toka hapa mpumbavu. Kinda wa jana unataka kujipanuuua kama yule chura aliyepasuka katika kujifananisha na ng’ombe.’
‘Lakini wewe baba si unasema unapenda demokrasi.’
‘Napenda sana lakini siyo democrazy’
‘Sasa kwa nini mnaweka sheria zinazopingana na demokrasi kabisa. Iweje mitume wa tume ya Uchaguzi wasihojiwe hata kidogo kisheria. Hasa kama tunajua nani kawatuma mitume hiyo.’
Ghafla bosi akanigeukia mimi. Nilikuwa nimejisahau na kuanza kusikiliza bila kujifanya niko bize. Ikabidi nianze kusafisha dirisha kwa nguvu sana bila hata kitambaa. Lakini bahati nzuri bosi hakuona.
‘Hidaya. Hebu leta sabuni hapa haraka sana.’
Nilishangaa lakini ikabidi nilete. Nikakuta BB na baba yake bado wanatumbuliana macho utadhani wanandondi kabla ya mapigano. Bosi akachukua sabuni harakaharaka na kumshika mwanaye na kutaka kumwekea sabuni mdomoni.
‘Wewe kisaliti kidogo nimechoka kuvumilia uchafu wa mdomo wako. Hebu kula hiyo sabuni kuondoa uchafu wote.’
Akaanza kumlazimisha lakini BB akamkwepakwepa na kupiga kelele kubwa sana.
‘Unaniua! Unaniua!’
Mimi nilikuwa sijui nifanye nini mpenzi lakini bahati nzuri MB akaja mbiombio na kuingilia kati.
‘Unafanya nini mume wangu ! Hebu tulia.’
‘Hapana! Lazima nimfundishe huyu maaluni adabu. Akitaka kubwata mambo ya kijinga, afanye nje ya nyumba hii siyo hapa mbele yangu. Mtoto gani ambaye hamheshimu baba yake.’
‘Lakini mume wangu, kumlazimisha hivyo hakusaidii.’
Wakati wanasemana hivyo BB akamponyoka baba yake na kwenda kusimama mbali.
‘Baba, baba, kweli unanifanyia hivyo?’
‘Lazima unifundishe adabu.’
‘Siyo hivyo. Nakuheshimu sana lakini siyo unapopingana na ukweli. Hata ukikata ulimi wangu kabisa, siwezi kuacha kufikiri. Bora unikate kichwa kabisa.’
Na kabla bosi hajaweza kujibua akaangua kilio ya nguvu kabisa. Mpenzi, sipaswi kukuambia hivyo maana hata mimi naweza kuitumia siku nyingine kwako teh teh, lakini machozi ni silaha nzuri kweli. Bosi alishindwa kuendelea na hasira zake akatoka na kumwacha MB ajitahidi kumtuliza mwanaye.
Lakini ilikuwa wazi BB bado alikuwa anamsubiri baba yake waendelee na mapambano maana naona yeye na wenzie walikuwa wameudhika sana na mambo yote ya safari hii. Ndiyo maana alikuwa hatulii wakati wa kumsubiri baba yake. Mwisho wake baba akaja. BB akamsalimia vizuri na kusubiri apate wiski yake kwanza, maana alijua mwisho bosi atamwuliza shule ilikuwaje.
Na kweli swali likaja. BB akatabasamu tabasamu la kifedhuli kama wanavyosema katika riwaya zetu kisha akasema.
‘Unajua baba leo tulipewa msemo mzuri kweli. Katika maisha si tu ni lazima haki itendeke bali ni lazima idhihirike imetendeka.’
Naona bosi alikuwa bado hajamtegea sikio vizuri mwanaye maana alikuwa anasikilizia kwanza wiski inavyoshuka.
‘Eti nini mwanangu?’
‘Haitoshi haki itendeke. Ni lazima idhihirike kwamba imetendeka. Ni lazima watu wote waone waziwazi kwamba imetendeka.’
‘Kwa hiyo?’
‘Baba unanisikiliza kweli? Katika huu uchaguzi uliopita imedhihirika hivyo? Wakati kuna mambo mengi yalienda kinyume, utadhihirishaje kwamba haki imetendeka.’
‘Kama watu hawajaridhika si waende mahakamani!’
‘Waende kwa misingi gani baba wakati sheria hairuhusu hata kuhoji kazi ya Tume ya Uchaguzi upande wa kura za Rais. Watu walianza kusema kwamba kesi ya ngedere huwezi kupelekea nyani lakini kumbe kesi haiwezekani kabisa hata ungetaka kupeleka. Mahakama imefungwa. Kweli haki imedhihirika hapa?’
Baba akaanza kukasirika tena lakini safari hii BB alikaa mbali naye kisha alionekana kutaka kuwa mlaini safari hii.
‘Siyo kwamba nataka kupinga kila kitu baba. Lakini wewe hujui matatizo yanayonipata shuleni. Watu wote wanabeza matokeo, wanabeza washindi, wanatubeza sisi tulio watoto au ndugu wa washindi.’
‘Wewe unapaswa kuwa imara katika msimamo na kuwadharau hao wasiojua kitu.’
‘Nataka kufanya hivyo baba lakini nitawezaje kutetea wakati bado kuna maswali kibao ambayo hayajibiwi. Ndiyo maana ninafurahia huo msemo kwamba lazima haki idhihirike. Unajua wanaita nini chama chako siku hizi? Chakachua Matokeo.’
‘Na wewe mwanangu mbona unataka kuleta kila takataka hapa kana kwamba unataka kunichokoza tu.’
‘Siyo hivyo baba. Nakupenda baba yangu, nimejivunia kuwa na baba kama wewe maisha yangu yote lakini sasa watu wote wanakudharau wewe na wenzako.’
‘Usitie chumvi. Bado tunapendwa na wengi …’
‘Lakini siyo vijana wenzangu. Na sina jibu la kuwapa maana hata mimi naona kinachotumika ni ubabe sasa siyo ubaba.’
Baba alionekana kutaka kuchukua hatua tena hivyo mimi nilikaa mbali kabisa na BB akaangua kilio tena hadi MB akaja.
‘Sijamgusa. Yeye tu ananichokoza …’
BB aliendelea kulia.
‘Babaaa …. Babaaa onyesha haki jamani …. Babaaaaa’
Ndiyo hivyo mpenzi. Hata ndani ya nyumba ya bosi, bado madonda ya uchaguzi ni mabichibichi sembuse kwa watu wengine. Sasa kwa kulindana huko, na matumizi ya mabavu, na kutowasikiliza watu madonda yatapona kweli?
Na wanapoanza kuwafanyia visasi kama kwako mpenzi wangu, huku watu wamechukia namna hii, wanataka tuwe na amani au …. Haki idhihirike … kulindana kukome … kisha waonyeshe kweli walistahili kuchaguliwa siyo kuchakachuliwa. Lakini wakati wanalamba miguu tu, wataona hilo?
Akupendaye daima
Hidaya
hs3.gif
Chanzo: Raia Mwema

Barua-pepe:
mabala@gmail.com
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom