9 Julai 2020
Haki msingi wa amani, na haki ni kwa wote, kokote, bila ubaguzi - Jenerali Ulimwengu
Source : Jenerali Online
Dhana ya Msamaria Mwema niliyoitumia kuhitimisha makala yangu ya mwisho ni muhimu sana katika falsafa ya kisasa kwa maana kwamba inaelezea wema unaotendwa na mtu ambaye ndani ya jamii husika hatarajiwi kutenda wema. Msamaria Mwema aliyetolewa mfano na Bwana Yesu alikuwa mpita njia tu, kama walivyokuwa wapita njia wengine waliomkuta msafiri kapigwa, kaporwa na yu mahututi, mlangoni mwa kifo.
Walikwisha kupita watu wenye sifa za kutenda wema, wakiwemo makuhani, lakini wote walimuona mtu huyo kama mtu asiye na thamani, na wala hawakuona sababu ya kumsaidia. Hali yake ilikuwa haiwahusu, na ilibidi yeye mwenyewe apambane na hali yake, kama msemo wa siku hizi ulivyo. Msamaria akamuonea huruma mhanga yule, akamchukua, akampeleka hadi hospitalli, akamkabidhi kwa wauguzi na akalipia matunzo yake.
Ipo tofauti kubwa baina ya binadamu na mtu. Binadamu maana yake ni mwana wa Adamu na Hawa, kama ambavyo vitabu vya hekaya za Wayahudi zinavyoeleza. Sote tunachukuliwa kama watoto wa hao wawili waliokula lile tunda na, kutokana na kula lile tunda, wakatuachia changamoto za kila aina hadi leo hii. Mtu ni tofauti, kwa sababu pamoja na kuwa binadamu kwa maana niliyoeleza hapo juu, ana sifa ya nyongeza, kwa sababu yeye ana utu ndani yake.
Nakumbuka wimbo mmoja wa marehemu Marijani Rajabu ambamo anasema. ‘kwenye watu kumi, binadamu mmoja’. Niliwahi kumwambia mwanaziki huyo kuhusu kosa lake, lakini nilikubaliana naye kwamba ilikuwa haiwezekani kurekebisha kosa hilo, hasa kwa sababu halaiki ya wapenzi wa muziki walikwisha kulikubali kosa hilo kama sahihi.
Lakini uhalisia wa maneno hayo unatuambia kwamba ingawa wote waliopita na kumuona bwana yule amepigwa na kaumia walikuwa wote ni binadamu, aliyekuwa na UTU alikuwa ni mmoja peke yake, yule Msamaria, mtu wa kabila lisilo na thamani lakini yeye mwenyewe akawa na roho ya utu. Huko ndiko inakotokea dhana ya kisasa ya UBUNTU iliyoibuliwa na ndugu zetu wa Afrika Kusini, hata kama wao wenyewe kwa kiasi kikubwa dhana hiyo inawashinda.
Na tuwe watu, basi, badala ya kuwa binadamu tu, kwa sababu ni utu peke yake unaotutofautisha na hayawani. Utu unatutaka tuwatendee wenzetu, hata tusiowajua, kama vile ambavyo tungependa sisi wenye tutendewe na wenzetu, hata kama hawatujui. Kumtendea wema mtu unayemjua ni jambo jema, lakini inawezekana wema huo umetokana na jinsi unavyomjua huyo unayemtendea wema.
Inawezekana huyo unayemtendea wema ni ndugu yako au rafiki yako, la sivyo usingetenda wema uliotenda. Huo ni wema wa bei kidogo, kwa sababu kwa maana moja, huo ni wema unaojitendea wewe mwenyewe. Wema unayemtendea mtu usiyemjua unayo thamani kubwa zaidi, kwa sababu hapo unatenda wema kwa ajili ya kutenda wema, na si kwa sababu ndugu yako au rafiki yako anahusika.
Hii inatufundisha tuwe na roho ya kuwapenda watu wote na kuwasaidia. Bila shaka kama falsafa hii ingetamalaki katika jamii iliyo pana tungekuwa na watenda wema kila kona ya jamii, na wala tusingekuwa na haja ya mahubiri ya kila wikiendi ya kuhamasishana kutenda wema.
Unapita mtaani, na unashuhudia uovu ukitendeka lakini anayetendewa uovu huo ni mtu usiyemjua, na kwa sababu humjui, unajipitia na kuendelea na hamsini zako. Umeshindwa kutenda wema. Unamkuta mtu anatenda kosa kwa makusudi, lakini kwa sababu kosa hili hakikuumizi wewe mwenyewe kwa namna yo yote ile, unaona ni jambo lisilokuhusu na unaendelea na safari yako kana kwamba hukuona jambo lo lote.
Kosa la kuwa na mitazamo kama hii ni kwamba si wewe pekee utakayefanya hivyo. Wenzako pia, katika pita-pita zao watashuhudia maovu kama lile uliloshihudia na watakaa kimya kwa sababu hayawahusu, lakini kumbe linakuhusu wewe, lakini kwa sababu jamii yenu ilikwisha kujizoeza kutokuingilia mambo yasiyowahusu, utaumia na hakuna atakayekusikia.
Watanzania tumekwisha kufikia kiasi hiki cha kutokujali. Tunawaona watu wanaumizwa kila siku, lakini kwa sababu hao wanaoumia si ndugu zetu au marafiki zetu, tunaendelea na hamsini zetu kama vile hatujaona kitu. Tunasahau kwamba na sisi tutakapokuja kupatwa na hayo, wenzetu nao hawataona tunavyoteseka. Hakuna utu unaotendeka kwa kubaguana baina ya wale wanaostahili kutendewa haki na wale wasiostahili kutendewa haki. Bima ya kweli ya w ewe kutendewa haki na watu wasiokujua ni wewe kutenda haki kwa wale usiowajua.
Tumewaona wakuu wa polisi wakiangalia watu wanapigwa na kuumizwa, halafu wakuu hao wanatoa visingizio vya kutia kichefuchefu, mara nyingi wakiwalaumu wahenga kwamba ndio walioanzisha fujo. Mkuu kama huyo wa polisi akija kumkuta mwanaye kapigwa na kutobolewa jicho na askari polisi asiyemjua, atakuwa na ujasiri wa kumlaumu mwanaye kwa kuwa sababu au chanzo cha kujeruhiwa kwake?
Tunashuhudia watu wakikamatwa na kufunguliwa mashitaka mbali mbali ambamo vinaingizwa vipengele vya money laundering , hata katika mazingira yasiyofanana kabisa na kosa hilo. Kisa ni kwamba waendesha mashitaka wanatafuta njia ya kuhakikisha kwamba mshitakiwa hatoki nje kwa dhamana.
Halafu, kwa muda mrefu tumekuwa na utaratibu ambao sielewi ulitoka wapi, eti ofisa huyo huyo anayekushitaki ndiye pia amwambie hakimu iwapo unafaa kupewa dhamana au la! Mambo yale yale, ya riwaya za George Orwell. Huyu ndiye anashitaki, na anataka mshitakiwa afungwe, halafu ndiye anaulizwa iwapo anadhani ni sawa kwa mshitakiwa kuachiwa kwa dhamana! Tusije kuwasingizia Wazungu kwamba ndio waliotufundisha mantiki hii. Hii ni yetu na tuliipata kule kule katika ‘collective imbecilization’ ya Seithy Chachage.
Wakati naandika makala hii tumepata habari kwamba katika jimbo fulani la ubunge, mgombea wa chama cha upinzani ameshindwa kukabidhi fomu za kumfanya mgonbea, halafu anatangazwa mgombea wa chama tawala kwamba amepita bila kupingwa! Hivi huu si utaratbu wa kuwafanya watu wapate kichaa na hatimaye waseme, ‘liwalo na liwe!’?
Najiuliza ni kwa nini tunadhani kwamba vurugu zinazozuka katika nchi nyingine za bara la Afrika haziwezi kutokea kwetu. Wale waliokumbwa na vurugu tunazozifuatilia ni watu wenye akili kama sisi, na hawajamkosea Mungu kwa kiasi kinachozidi makosa yetu kwa Bwana Mkubwa huyo. Ni kwa nini tunadhani kwamba sisi tunayo kinga inayotufanya tuenende bila kujali mantiki, halafu tuepukane na hayo yaliyowapata wenzetu?
Msingi wa amani ni haki, bila haki hatuwezi kuwa na amani. Aidha, haki haina tabia ya kuangalia sura ya mtu, wala kabila lake, wala dini yake. Ndiyo maana alama ya haki duniani kote ni yule mawanamama aliyefungwa kitambaa usoni; haoni. Tunapokuwa na mifumo ya kutoa haki kwa upendeleo unaotokana na kuwaangalia watu usoni hatutakuwa na haki hata chembe.
Nasema kwamba msingi wa haki zote ambazo tunadai leo ni haki ya ushiriki wa kisiasa. Bila kuwa na haki katika ushiriki katika siasa hatuwezi kubuni haki nyingine zo zote na zikawa na mashiko. Ushiriki wa kisiasa kwa raia wote unapokuwa umetengenezewa mifumo inayokubalika na watu wakairidhia, ndiyo bima ya juu kabisa ya kuondoa uwezekano wa chokochoko ndani ya jamii.
Mtawala mwenye busara ataiona hii mantiki, na kila siku atapanuwa wigo wa ushiriki huo ili asiachwe ye yote nje ya wigo wa ushiriki wa kisiasa. Mtawala asiye na busara hii atazidi kila siku kubinya hata ule wigo uliopo, huku akiongeza asilimia ya wale wanaoachwa nje ya wigo wa ushiriki. Huyo anaitakia majanga jamii yake.
Source: Haki msingi wa amani, na haki ni kwa wote, kokote, bila ubaguzi