Haki Huinua Taifa

George Kahangwa

JF-Expert Member
Oct 18, 2007
547
147
Siku moja, nikiwa Mkuu wa Idara ya Itikadi na mafunzo katika chama cha siasa(naomba nisikitaje),nilirushiwa swali na mtu mmoja akitaka nimweleze ni nini itikadi ya chama chetu na inatofautianaje na ya vyama vingine. Sehemu ya kwanza ya swali lake ilikuwa nyepesi kujibu,maswali zaidi yaliibuka katika kujitofautisha na wengine. Swali lake liligeuka kuwa mjadala mrefu ambao uliambatana na nukuu kama vile, wewe wasema unamwamini Mungu,mashetani nao wanaamini na kutetemeka,ni nini basi tofauti ya uumini wako na ibilisi

Yamkini tofauti ya kiitikadi baina ya vyama vya siasa nchini Tanzania, si dhahiri sana.Matharani, kwa vyama vya mageuzi ambavyo vimejitambulisha kama wafuasi wa itikadi ya Demokrasia ya Jamii haviko mbali na utambulisho wa chama tawala kiitikadi (hapa nidokeze kuwa TANU iliwahi kutaja kwamba inaamini katika Social Democracy)
Taifa letu lina vyama vya siasa vipatavyo kumi na vinane(1, kwa maana hiyo kama kila chama kina itikadi yake, basi vyama hivi vinaamini katika masuala 18 yaliyo tofauti. Binafsi siamini kwamba hivyo ndivyo ilivyo.

Yamkini pia baadhi ya vyama imani zao zinafanana, tofauti iko katika nani ana msimamo mkali,msimamo wa wastani au vinginevyo katika itikadi husika.

Kimsingi bado linabaki ni jukumu la chama husika kubainisha mrengo wake ili kieleweke mbele ya umma ni mambo gani kunasimamia. Kutokana na msimamo huo wa kiitikadi ndipo chama utunga sera zake ili ziendane na kile kinachoaminiwa miongoni mwa wanachama. Hakika itikadi(na sera) ndio ilipaswa kuwa sababu ya mtu kujiunga na chama fulani au kukiunga mkono,matharani wakati wa uchaguizi.

Muuliza swali la awali,aliendelea kunihoji, ati tuseme leo hii chama chenu(changu) kingepewa dhamana ya kuongoza nchi,tutegemee kwamba mtatumia sera za kijamaa au kibepari?
Nilimjibu kichama, nikisisitiza msimamo wa chama kuhusu itikadi.

Nikusudialo kumshirikisha msomaji hapa, ni kile ambacho mimi ninaamini ndicho kinapaswa kuwa itikadi/imani sahihi ya taifa liwalo lolote. Ufafanuzi zaidi wa imani yangu, ni kama ifuatavyo:

ITIKADI YA HAKI (JUSTICISM)

YALIYOMO

Utangulizi
Falsafa ya Haki
Dhana ya Haki
Mafundisho ya kidini kuhusu haki
Haki kama Itikadi
Mfumo Haki wa Uchumi
Mfumo Haki wa Kisiasa
Mfumo Haki wa Kijamii
Mfumo wa Sheria zitendazo Haki

SEHEMU YA KWANZA

UTANGULIZI
Historia nzima ya kuwepo kwa mwanadamu hapa duniani inathibitisha wajibu alionao mwanadamu wa kufanya shughuli mbalimbali ili kujipatia riziki na au kuyaendesha maisha yake. Shughuli hizo zinamlazimu mwanadamu kuwa na mahusiano mazuri na mazingira yanayomzunguka ili kutoka katika mazingira hayo apate anachokihitaji. Kadiri mazingira yanavyokuwa bora ndivyo maisha ya mwanadamu yanavyostawi vyema. Ila kwa kadri mazingira yanavyoharibiwa ndivyo maisha ya mwanadamu yanavyokuwa hatarini. Kwa ufupi maisha ya mwanadamu huyategemea mazingira karibu kwa kila kitu.

Matharani, mwanadamu wa kale aliyeishi kwa kuwinda, kukusanya mizizi na matunda aliitegemea mimea na wanyama waliomo katika mazingira ili kupata mahitaji yake hayo. Alifika mahali uwindaji na ukusanyaji wake ukamtaka awe na zana za kufanyia shughuli hizo. Hata katika hili la kupata zana aliyategemea mazingira hayo hayo. Kutoka katika mazingira akaweza kupata mawe akatengeneza zana za mawe, kisha akagundua chuma na teknolojia yake, hatimaye akawa kiumbe anayeboresha zana zake kwa kugundua tekinolojia bora zaidi mara kwa mara.

Mwanadamu vilevile akawa kiumbe asiyeweza kufanya kazi peke yake bila kushirikiana na wanadamu wenzake. Wanadamu wa kale walishirikiana kuwinda na kukusanya kisha kugawana sawa kilichopatikana. Haki ilitendeka na ilipaswa kuendelea kutendeka. Kadri siku zilivyokwenda ukaibuka mgawanyo wa kazi ukichochewa zaidi na ugunduzi wa tekinolojia zilizoboresha zana za kazi pamoja na ugunduzi wa mambo mengine mbalimbali kama vile dawa za matibabu na kadhalika. Wale waliokuwa vinara wa ugunduzi fulani ukafika wakati wakawa wanatumia muda mwingi kuzalisha teknolojia yao na kutoa huduma kwa waliohitaji kutumia teknolojia yao, ilihali watu wengine waliendelea na shughuli za kawaida. Shughuli hizo za kawaida zilihitaji zana zilizotengenezwa na wale wachache wagunduzi. Hali imekuwa ndio hiyo hadi leo.

Wakati huo huo kadri wanadamu walivyozaliana na kuongezeka, tabia mbali mbali tofauti zilijitokeza miongoni mwao. Pakajitokeza haja ya uongozi ili uweze kusimamia utaratibu unaokubalika na unaolinda maslahi ya kila mmoja. Lakini kwa hulka ya mwanadamu ubinafsi ukajitokeza, wengine wakawa na tabia ya kujipendelea kiasi cha kuwadhulumu wengine, baadhi ya waliopewa dhamana ya kuongoza wenzao wakatumia nafasi hizo vibaya kujinufaisha na kuwakandamiza wengine. Yakajitokeza mambo mengi yanayofanana na hayo, usawa ukatoweka madaraja na tofauti za watu zikajitokeza wengi wakapata zaidi ya haki yao, wengine wakakosa kilicho haki yao. Wakati huo huo mwanadamu akaendela kutumia kilichomo katika mazingira kwa kasi iliyohatarisha kutoweka kwa baadhi ya vitu vilivyomo katika mazingira hayo. Viumbe wengine wakawa hawana cha kuwatetea dhidi ya uhitaji wa mwanadamu unaoongezeka siku kwa siku.

Miongoni mwa wanadamu, wapo walioiona hatari ya hali hiyo ya kutotendeana haki tena miongoni mwa wanadamu wenyewe kwa wenyewe, na hatari ya matumizi ya mazingira yasiyo na utaratibu mzuri. Wenye fikra hawa waliweza kujenga hata nadharia za mahusiano ya watu wenyewe kwa wenyewe na mazingira yao yakoje, yamepitia hatua gani na yanastahili kuwaje. Wenye fikra wakaibua mawazo ya kwamba mahusiano haya yamepitia katika mifumo ya ujima, utumwa, ukabaila, ubepari na ujamaa. Wanabainisha zaidi kwamba kati ya mifumo hiyo mitano ni miwili tu ambayo ilionekana kuwa na kiwango kikubwa cha kujali maslahi ya kila mmoja, nayo ni ujima na ujamaa. Matharani katika ujima, watu waliwinda na kukusanya pamoja, mwisho wa siku wakagawana sawa haki ikatendaka. Lakini ulipojitokeza mfumo wa utumwa haki (ya mtumwa ikatoweka) mmiliki wa mtumwa akapata zaidi ya haki yake akawa yeye ndio binadamu na aliye mtumwa hadhi yake sawa na mnyama wa kazi. Katika mfumo wa ukabaila nako haki ilitoweka, ikawekwa tu mkononi mwa mwenye kumiliki ardhi. Hali kadhalika katika mfumo wa ubepari, mwenye haki akawa ni mmiliki wa mtaji na mfanya kazi haki yake ikanyongwa. Katika ujamaa kukajitokeza dhana ambayo ililenga kurejesha haki, kwamba umiliki wa mali uwe wa umma/ watu wote kwa pamoja. Lakini mfumo huu nao ukawa na madhaifu yake haki ya wote haikupatikana.

Katika miongo ya hivi karibuni, dunia ilishuhudia ushindani kati ya kambi mbili zinazoamini katika mifumo tofauti ubepari (uliokomaa ukawa ubeberu) kwa upande mmoja na ujamaa (ulioelekezwa kwenye ukomunist) kwa upande mwingine. Mifumo hii ikachukuliwa kuwa ndio imani (itikadi) za watu kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. Wengine huzitambua itikadi hizi kama mirengo, mmoja mrengo wa kulia na wa pili mrengo wa kushoto. Katikati ya mirengo hii miwili wakaibuka wenye kuchukia maovu ya ubepari lakini hawapendi mwelekeo wa kupita kiasi wa ujamaa. Wakaitwa hawa mrengo wa kati, miongoni mwao wakawa wale wanaoshikira itikadi ya Demokrasia ya Kijamii.

Miaka ya karibuni zaidi, imeshuhudua vile vile ubepari/ ubeberu ukishamiri na kuzizidi nguvu itikadi nyinginezo. Ukatanua makucha yake hasa baada ya kusambaratika kwa shirikisho la nchi za kisovieti za urusi (USSR) miaka ya 1990. Ubeberu umejitanua zaidi siku hizi kupitia dhana za utandawazi, soko huria na uwekezaji wa kimataifa. Haki ya waliowengi/ haki ya wote iliyotakiwa kuwepo tokea enzi za ujima haijapatikana. Laiti mifumo hii yote ingeamini katika kulinda haki ya kila mmoja bila suluhu.

SEHEMU YA PILI
FALSAFA YA HAKI
Kimsingi shughuli zote za mwanadamu na mahusiano ya watu hapa duniani yalipaswa kuwa ni kwa ajili ya kuboresha hali yake kimwili, kiakili, kiroho na kuongeza ubora wa mahusiano yake na viumbe wengine. Hivyo, mchakato wa kila shughuli afanyayo ulipaswa kuwa katika namna ambayo haina dhuluma, uonevu, madhalilisho, taabu, ubaguzi, wala vikwazo kwa mwanadamu awaye yeyote na kwa kiumbe hai kingine chochote.

Hali hiyo ya mchakato ulio mwema inawezekana pale tu mifumo iliyopo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii imeelekezwa katika kiwango cha juu kabisa cha kuzingatia haki ya kila mtu. Dunia itakuwa mahali bora pa kuishi endapo tu kutakuwa na HAKI KILA SIKU, HAKI KILA MAHALI, HAKI KWA KILA MMOJA. Palipo na haki pana utunzaji na utumiaji mzuri sana wa mazingira, pana mahusiano mazuri ya kiwango cha juu cha ustarabu na pana amani, maana amani ni tunda la haki.

SEHEMU YA TATU

DHANA YA HAKI
Zipo nadharia na maelezo mengi kuhusu dhana ya haki na umuhimu wake. Hapa nitatolea mfano wa mitazamo ya wanafalsafa japo wawili kuhusu haki.

Mwanafalsafa aitwaye Aristotle (katika karne ya 4 K.K), alibainisha manufaa ya uwepo wa haki kwa watu aliposema maeneno yafuatayo.

‘Kilele cha uwepo wa haki ni kuzalishwa na kutunzwa kwa furaha ya jamii na ya dola’
Kwa maana hiyo, jamii kamwe haiwezi kuwa na furaha ya kweli kama haki haitawali na wala dola haliwezi kusimama imara pasina kutunzwa kwa kiwango kikubwa haki ndani ya mipaka ya dola husika.

Aristotle alifafanua zaidi kwamba kwamba, kimsingi kuna aina mbili za haki ambazo ni kama ifuatavyo
(i) Haki katika sheria
(ii) Haki katika gawio stahili

Haki inapotambuliwa katika sheria kunakuwa hakuna upendeleo wala ubabaishaji (arbitrariness)

Ili haki iwepo katika gawio, hapana budi kuwa na usawa. Watu sawa hupokea gawio sawa, watu wasio sawa hupokea gawio lisilo sawa. Usawa ni sehemu ya haki. Usawa unakuwepo pale tu ambapo hakuna anayejisikia kunyonywa au kunyimwa stahili yake (Jown Rawls, 1957). Watu huhisi kutendewa visivyo haki pale matarajio yao yasipotimilizwa au pale wenye mamlaka wanapowanyima stahili zao.

Kanuni za haki katika jamii huwezesha kufafanuliwa vema kwa haki na wajibu wa kila mtu na wa taasisi za jamii. Kanuni hizo pia, hueleza ni nani anayestahili kunufaika na raslimali na matunda ya kazi ya jamii husika.

Mwanafalsafa huyu wa masuala ya kisiasa John Rawls (1921-2002) alijenga hoja zake k akitohoa katika mtizamo wa kiutopia wa Bentham na Mill, mawazo ya mkataba wa kijamiii ya Locke na mawazo ya Kant kuhusu haki. Rawls aliuelezea mtizamo wake wa kwanza na wa kimsingi kuhusu haki kama aliyoandika katika kitabu chake kiitwacho A Theory of Justice (1971) ambamo alipendekeza kwamba kila mtu anayo heshima ya kipekee ambayo msingi wake ni haki ambayo hata haki za pamoja za jamii haziwezi kuizidi hiyo haki ya mtu mmoja mmoja.

Kwa maana hiyo kanuni za haki zinakataa kwamba kumnyang’anya mtu uhuru wake kunahalalishwa na maslahi ya wengi. Mawazo ya Rawls yameainishwa tena katika kitabu kiitwacho Political Liberalism (1993),ambamo anaitazama jamii kama "mfumo mwema wa ushirikiano miongoni mwa watu uliodumu kwa muda fulani kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Jamii zote za wanadamu zina mfumo wa kimsingi wa kijamii, kiuchumi, na taasisi za kisiasa zilizo rasmi na zisizo rasmi. Katika kutibitisha ni jinsi gani vipengere hivyo vya mfumo hufanya kazi kwa pamoja, mtaalamu huyo Rawls alifanya jaribio kuhusu nadharia za uhalali wa mikataba ya kimfumo iliyomo katika kijamii. ili kutambua kama mfumo fulani unaoathiri mipangilio ya kijamii una uhalali, alisisitiza kwamba mtu hana budi kutazama kukubalika kwa mfumo huo miongoni mwa watu wanaoongozwa na mfumo husika. Yamkini si rahisi kumshirikisha kila mwana jamii katika kura ya maoni ili kubaini kiwango cha kukubalika kwa mfumo fulani miongoni mwa wanajamii, ila kila mwana jamii ana uelewa na mara nyingi anafanya maamuzi ya busara kwa kiwango cha kulidhisha, yahusuyo mfumo wa jamii yake. Kwa kuzingatia hayo, Rawls alitengeneza hoja ya hatua mbili za kuzingatia katika mchakato wa kutabua kinadharia jinsi gani wanajamii wanaweza kuukubali mfumo fulani :

Hatua ya kwanza;
Mwanajamii ukubali kuwakilishwa na mtu X kwa madhumuni fulani; kwa kiwango hicho, mtu X anakuwa amepewa mamlaka au nguvu, kama mdhamini wa haki za mwanajamii anayewakilishwa;

Hatua ya pili;

Mtu X hukubali kwamba matumizi ya kani fulani (sheria, kanuni, maagizo na amri) katika mtazamo wa kijamii ni halali kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa. kwahiyo wanajamii wanabanwa na uamuzi wao wenyewe wa kukubali wawakilishwe maadamu uwakilishi ni tendo la udhamini.

Ukweli uliomo ndani ya hatua hizi, unakubalika kila panapotokea mtu mmoja anawakilisha kundi la watu liwe dogo au kubwa. ( matharani, mtu anapopewa dhamana ya kuratibu tafrija ndogo anapoamua ni vazi gani litumike katika tafrija hiyo ni kwa sababu kakubalika na kupewa mamlaka ambayo sasa anayatumia kuamua kwa niaba ya wote)

Hatua hizi vilevile, zinakubalika katika ngazi ya kitaifa ambapo serikali kama chombo kilichopewa dhamana kuu, hubeba nguvu za uwakilishi kwa manufaa ya raia wote walio ndani ya mipaka ya nchi husika. Endapo serikali itashindwa kutekeleza majukumu yake na kuhifadhi maslahi ya wananchi kwa mujibu wa kanuni za haki, serikali hiyo si halali maana inakuwa imevunja mkataba wa dhamana iliyopewa.

Hata hivyo licha ya kwamba mwakilishi anakuwa amepewa mamlaka ya matumizi ya kani, kanuni kuu inayomwongoza inabaki kuwa kwamba, haki huchipuka au hutokana na watu na si shuruti toka kwa watunga sheria wenye mamlaka ya kiserikali. Ni lazima wenye mamlaka wazingatie uhuru walionao wanajamii. Rawls alidokeza pia kwamba, haki humpa mwanajamii uhuru kwa namna zifuatazo;

Uhuru wa kifikra / uhuru wa kufikiri
Uhuru wa utashi wa nafsi katika mahusiano ya mtu kijamii kwa mujibu wa imani yake ya kidini, falsafa na maadili yanayomwongoza mtu.

uhuru wa kisiasa (mfano kuwepo kwa taasisi za demokrasia ya uwakilishi,
uhuru wa kujieleza, wa vyombo vya habari na wa kukusanyika)
uhuru wa kujumuika na kushirikiana na wanajamii
uhuru wa mtu kwenda atakako na kuchagua kazi aitakayo bila kukinzana na misingi ya uadilifu
uhuru wa kupata haki binafsi zinazolindwa na utawala wa sheria.

SEHEMU YA NNE

MAFUNDISHO YA KIDINI KUHUSU HAKI
Dini nyingi zinapoeleza kuhusu uendeshaji wa nchi hapa duniani zinasema; HAKI HUINUA TAIFA.

Mafundisho ya kikristo yanajumuisha suala zima la utu. Mojawapo ya mambo ya kipekee katika mafundisho hayo ni suala la kuwajali maskini zaidi katika jamii. Mawili kati ya maeneo saba ya mafunzo ya kikristo yanagusia suala la haki ya kijamii ni haya yafuatayo:

Thamani ya maisha na utu wa mtu (Life and dignity of the human person): msingi wa mafundisho yote ya kikristo ni utakatifu wa maisha ya mtu na hadhi ya utu. Maisha ya mtu yana thamani kuliko chochote kile iwe umiliki wa mali au kitu kingine.

Fursa kwa maskini na walioko katika mazingira magumu: Mhasisi wa imani ya kikiristo,Yesu Kristo mwenyewe alifundisha kwamba, siku ya kiama Mungu atamhoji kila mmoja wetu ni kitu gani alifanya kuwasaidia maskini na wahitaji: " Amini,nawaambia, lolote mlilowafanyia hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinifanyia mimi”

Kanisa huzidi kufundisha kwamba, kwa maneno, maombi na matendo mtu sharti aoneshe mshikamano na upendo wake kwa maskini. Zinapotengenezwa sera za umma hapana budi fursa za maskini zipewe kipaumbele.

Ama kwa hakika kipimo cha uadilifu wa jamii yoyote ile ni jinsi jamii husika inavyowachukulia wanajamii hiyo walio katika mazingira magumu.

Hata kabla ya kusisistizwa katika rasmi mafundisho ya kikristo (hususan kanisa la kikatoliki), haki ya kijamii ilijitokeza sana katika masuala ya historia ya kanisa hilo.

Matharani,
Neno haki ya kijamii liliasisiwa na mkatoliki, Bwana Jesuit Luigi Taparelli mnamo miaka ya 1840, msingi wake ukiwa ni mafundisho ya Thomas Aquinas. Taparelli aliandika kwa mapana sana juu ya jambo hili katika jarida liitwalo Civiltà Cattolica, makala zake zilichambua nadharia za ubepari na ujamaa kama zinavyotazamwa katika mtazamo wa kikatoliki wa kanuni za asili. Msingi wa hoja zake ni kwamba nadharia hizi mbili za kiuchumi zinazohasimiana zinauhujumu umoja wa jamii. Si ubepari wa kiliberali wala ukomunisti ambao ulijali au ulijihusisha na falsafa ya maadili ya umma.

Naye Papa Leo wa 13 ambaye alifunzwa chini ya Taparelli, aliandika andiko liitwalo Rerum Novarum mnamo mwaka 1891 (kuhusu hali ya tabaka la wafanyakazi). Katika andiko hilo, Papa aliukataa mifumo yote miwili ya kijamaa na kibepari, bali akautetea utaratibu wa kuwepo kwa vyama vya wafanyakazi na umiliki wa mali binafsi kwa mtu mmoja mmoja. Alifafanua kwamba, jamii haina budi kujengwa katika misingi ya ushirikiano na si kwenye migogoro baina ya madaraja ya watu, wala kwenye ushindani. Katika andiko hilo Papa Leo alitoa kauli ya kanisa Katoliki kuhusiana na na kuyumba kwa jamii wakati ule na migogoro ya kazi iliyoshamiri wakati wa mapinduzi ya viwanda, mitafaruku iliyopelekea kuibuka kwa ujamaa (the rise of socialism). Papa alisistiza kwamba wajibu wa dola ( serikali, mahakama na bunge) uwe ni kulinda na kukuza haki ya kijamii (na si vinginevyo), kanisa kwa upande wake lifanye kazi ya kuongelea masuala ya jamii kwa lengo la kufundisha misingi sahihi ya kiutu na maelewano katika jamii.

Kwa upande wake Papa Pius wa 11 kwenye andiko liitwalo Quadragesimo Anno, la mwaka 1931 (kuhusu kuujenga upya utaratibu wa jamii) yeye anafundisha kwamba haki ya kijamii ni suala la sifa ya utu wa mtu mmoja mmoja ( personal virtue), na kwamba jamii inaweza kuwa yenye haki pale tu mwanajamii hiyo mmoja mmoja ni mwenye haki.

Papa wa sasa, Papa Benedict wa 16, katika andiko liitwalo Deus Caritas Est (Mungu ni pendo) anafundisha kwamba haki ya kijamii ndilo suala la kimsingi ambalo siasa zimepaswa kuhusika nalo, wakati suala kuu la kijamii linalolihusu kanisa ni usamaria mwema (usaidizi kwa wanajamii wahitaji)

Aidha, msimamo rasmi wa kanisa katoliki kuhusu haki ya kijamii umeelezwa katika kitabu kiitwacho Compendium of the Social Doctrine of the Church, cha mwaka 2004 kilichohaririwa mwaka 2006.

SEHEMU YA TANO

HAKI KAMA ITIKADI
Kwa kuwa haki ndio pekee iwezayo kumwakikishia kila mtu maisha mema binafsi na utengemano katika jamii, ni jambo jema jamii zikaiamini haki kama jambo la kipekee liwezalo kumwinua mwanadamu mmoja mmoja, jamii kwa ujumla na mataifa yote. Kwa maana hiyo ulimwengu unahitaji haki si tu kama itikadi ya kisiasa bali mwongozo wa kila mchakato wa shughuli za mwanadamu.

Haki ndio itikadi mbadala ya usoshalisti, ubepari na michepuo yake ambazo ni itikadi zilizothibitika kuwa na mapungufu mengi na zimeshindwa kuwapatia watu wote kile wanachokihitaji. Tunahitaji kufikiri sasa, na kuona haja ya kuwa na itikadi ya haki ambayo hakika vizazi na vizazi vitaiamini na kuifuata kwa kuwa ndio pekee inayomhakikishia kila mtu mustakabari mwema.

Itikadi katika ainisho rahisi ni imani kuhusu mahusiano kati ya watu na mfumo wa maisha katika jamii; kuna Itikadi zinazotetea mtu kumnyonya mwingine; pia zipo itikadi zinazokataa unyonyaji lakini hazidhibiti utegaji katika uwajibikaji na wakati mwingine hazina wepesi wa kutambua juhudi za mtu mmojammoja.

Ni ukweli ulio bayana kwamba kitu ambacho mwanadamu mahali popote awapo anakihitaji ni HAKI. Wanadamu kwa ujumla wetu, ili tuweze kuishi kwa mahusiano mema ya hali ya juu, kila mmoja wetu anapaswa kuamini katika HAKI yake mwenyewe, ya kila aitwaye mwanadamu na ya kila kiitwacho kiumbe hai.

Hakika itikadi stahili na ya kipekee kabisa kwa ajili ya mstakabali mwema wa maisha duniani ni HAKI (JUSTICISM).
Kutokana na itikadi hii, tutakuwa na mfumo haki wa uchumi (justifiable economy); mfumo haki wa kisiasa (justifiable political system); mfumo haki wa jamii (justice driven social system) na sheria zitendazo haki (just laws). Kwa maana hiyo, waamini wa itikadi ya HAKI, lolote lisilo haki si tu kwamba watalipinga bali watajiepusha nalo milele hata ukamilifu wa nyakati. Hakika itikadi hii itayainua mataifa, italiendeleza Taifa liwalo lolote.

Itikadi ya HAKI haiko mbali sana na yale ambayo baadhi ya wanamageuzi katika nchi mbalimbali duniani, kwa muda mrefu wamekuwa wakiyaamini kisiasa. Pengine ni suala la muda tu vyama vya siasa katika nchi mbali mbali vitaona haja ya kutamka rasmi na wazi kabisa kwamba itikadi yao ni HAKI.

SEHEMU YA SITA

MFUMO HAKI WA UCHUMI (JUSTIFIABLE ECONOMY)

Mfumo wa uchumi unaoheshimu haki unatambua uwepo wa haki ya raslimali asili, haki ya mwenye mtaji na haki ya mwenye nguvukazi. Mfumo huu unasisitiza kwamba sharti kuwepo maridhiasawa (amicability) kati ya pande tatu; raslimali asili, mtaji na nguvukazi au kati ya pande mbili; mtaji na nguvukazi/ raslimali asili na nguvukazi; kuhusu gawio (dividend) la uzalishaji. Maridhiasawa yanaweza kufahamika kimahesabu kwa kutambua thamani ya mtaji = (kizio chake ni HISA) na thamani ya nguvu kazi = ustadi wa nguvukazi x masaa ya kazi x 1% ya mtaji (kizio chake ni HISA-SHIRIKI)

Itikadi ya haki inasisitiza kuwa, daima rasilimali za nchi fulani ni mali ya wananchi husika na kamwe haimilikishwi kwa watu wasiokuwa raia wa nchi hiyo. Chini ya itikadi hii sharti mwenye mtaji aumiliki kihalali na si vinginevyo. Vile vile mfumo haki hauruhusu mtu awaye yeyote kupata gawio lisitahililo nguvukazi kama mtu huyo hakuitumia nguvukazi yake katika uzalishaji husika. Aidha mwenye nguvukazi sharti aitumie kujipatia ridhiki na kuiendeleza jamii yake.

SEHEMU YA SABA
MFUMO HAKI WA KISIASA (JUSTIFIABLE POLITICAL SYSTEM)

Mfumo wa siasa unaoheshimu haki unazingatia utashi na uamuzi wa kila mtu, unatambua haki ya mtu kuwa mfuasi wa chama cha siasa na hiyo unaruhusu uwepo wa mfumo wa vyama vingi vya siasa na demokrasia huru katika dola moja (Multi party system and free democracy) chini ya mfumo huu, itikadi ya mtu kisiasa au kutokuwa mfuasi wa itikadi yoyote haiwi sababu ya yeye kubughudhiwa katika nchi yake, kunyimwa ajira ya utumishi wa umma au kupewa dhamana ya uongozi wa umma uwe wa kuchaguliwa au kuteuliwa.

SEHEMU YA NANE
MFUMO HAKI WA KIJAMII (SOCIAL JUSTICE)
Mfumo wa jamii unaoheshimu haki unazingatia usawa wa watu wote bila kutazama tofauti za rangi ya mtu, asili yake, jinsia yake, umri au daraja lake kimapato. Mahali ambapo mfumo haki umesitawi hkuwezi kujitokeza tena hali ya kukandamizwa kwa baadhi ya jamii za watu kama ilivyowahi kutokea na inavyoendelea kujitokeza katika historia ya dunia yetu. Dunia imeshuhudia kukandamizwa kwa haki ya jamii za watu weusi wenye asili ya Afrika popote ulimwenguni tangia enzi ya kuchukuliwa utumwani, ukoloni, ubaguzi wa rangi hadi kuibiwa kwa maliasili za mtu mweusi. Dunia pia ina rekodi ya kutengwa kwa wahindi wekundu huko bara la Amerika kulikofanywa na jamii za watu wasio wa asili ya bara hilo. Kadhalika mambo makubwa ya kuvunjwa kwa haki ya jamii yalifanywa dhidi ya watu asilia wa Australia waitwao waaboligini. Chini ya mfumo wa haki ya jamii, hayo yote hayatasikika tena, kamwe.

Mfumo haki huifanya jamii iwe huru dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia, udhalilishaji wa watoto na uonevu wa namna yoyote ile. Habari ya huyu ni mwanaume na huyu ni mwanamke na hiyo stahili yake si sawa na ya mwingine, hufikia ukomo chini ya mfumo haki. Mfumo huu unatambua kuwa mfumo wa kibaolojia kwa ajili ya kuendeleza kizazi cha viumbe katu si sababu ya kufanya kuwepo kwa utofauti baina ya jinsia mbele ya haki na wajibu. Chini ya mfumo huu jamii itawajali kwa kiwango cha juu sana wasiojiweza, wazee, yatima na wote ambao kwa sababu zilizoko nje ya uwezo wao hawawezi kujisaidia.

Aidha mfumo huu huimiza ustarabu wa hali ya juu na huondoa kabisa tamaduni na mila zilizo kinyume na haki za binadamu. Ni mfumo unaoheshimu uhuru wa kuabudu, wa kujumuika na kushirikiana miongoni mwa wanajamii.

Haki ya kijamii maana yake ni kuwa na jamii yenye taratibu za haki. Yaani kuwa na jamii ambayo inampa mtu mmoja mmoja na/au vikundi vya watu fursa na stahili sawa. Hakika kila mtu angependa kuishi katika jamii yenye haki ingawa mirengo tofauti huitazama haki kitofautitofauti. Dhana hii ya haki ya kijamii hutumiwa sana na mirengo inayoamini kwamba katika jamii zetu leo hakuna haki, matharani mrengo wa kushoto ambao unatetea kugawana sawa mapato na ushirika . mrengo wa kushoto katika mtazamo wake hutoa hoja kwamba haki ya kijamii kwa njia ya soko huria na hisani . kimsingi mirengo hii miwili hukubaliana juu ya umuhimu wa utawala wa sheria, haki za binadamu an welfare safety net.

Haki ya kijamii wakati mwingine ina mwonekano usio wa kisiasa bali wa kifalsafa zaidi. Haki ya kijamii imekuwa katika mafundisho ya kikatoliki na ni miongoni mwa misingi minne ya vyama vya kijani. Haki ya kijamii pia ni dhana inayotumiwa na wanaharakati wa ujenzi wa dunia yenye haki. Kwa wao haki ya kijamii misingi yake ni haki za binadamu na usawa.

Haki ya kijamii ni moja ya nguzo kuu za vyama vya kijani. Haki ya kijamii ambayo wakati mwingine hutazamwa kama suala la usawa katika dunia nzima na haki katika uchumi, popote inapotajwa inaashiria msimamo wa jumla wa kuukataa ubaguzi wa watu kwa misingi ya madaraja, jinsia ya mtu, kabila lake au utamaduni wake. Katika mtazamo wa vyama vya kijani, tofauti za watu kwa kile walichonacho zinasababishwa na kutokuwepo kwa taasisi za kijamii zenye kudhibiti dhuluma ya wenye nguvu dhidi ya walio wanyonge.

Kwa ujumla vyama vya kijani vinaitafsiri haki ya kijamii kuwa ni kanuni inayosisitiza kwamba watu wote wanastahili mahitaji ya kimsingi ya mwanadamu bila kujali tofauti zinazoendekezwa, yaani kutofautiana kiuchumi, madaraja ya watu, jinsia, rangi, asili, uraia, dini, ulemavu au uzima wa maungo ya mwili. Haki ya kijamii ni pamoja na kufuta umaskini na ujinga, na kuwa na huduma bora za jamii kwa kila mmoja.

Haki ya kijamii ni ainisho la kifalsafa la haki, yaani kuwapa mtu mmoja mmoja au kikundi cha watu kile wanachokistahili ndani ya jamii walimo.

Dhana ya haki ya jamii imewavutia wanafalsafa tangu mwanafalsafa mkongwe Plato alipowakemea wanafalsafa chipukizi kutokana na madai yao kwamba haki maana yake ni chochote kile ambacho mwenye nguvu angeamua kiwe.

Mdahalo wa kifikra umedumu hata leo kuhusu kutumia vigezo vya jumla au la vya kutambua kama kuna haki ya kijamii au kigezo cha nani mwenye nguvu na nani hana.

Katika kitabu chake cha Republic Plato aliweka rasmi hoja yake kwamba jamii/dola iliyo barabara kabisa inaegemea kwenye nguzo nne za thamani, yaani;
i/ Hekima
ii/ Ujasiri
iii/ Udhibiti
iv/ Haki

Vilevile, dhana ya haki ya jamii inatazamwa katika namna mbili:
(a) Haki ya jamii inayomaanisha usawa katika jamii hususan linapokuja suala la kugawana mavuno na majukumu na hivyo hoja hii hutumiwa katika siasa kuzungumzia hoja ya gawio na haki sawa
(b) Haki ya jamii ni hoja inayoonekana kutumiwa zaidi katika siasa za mrengo wa kushoto ikilinganishwa na inavyotazamwa katika mrengo wa kulia.

Haki ya jamii inapata mamlaka yake kutoka katika vigezo vya maadili yanayoheshimiwa katika jamii husika.

Hakika haki ya jamii ni dhana pana, lakini katika lugha rahisi haki ya jamii inaakisi namna ambavyo haki za binadamu zinadhihirika na kutekelezwa katika maisha ya kila siku ya watu na katika viwango vyote vya maisha ndani ya jamii.

Haki ya ni chimbuko la changamoto ya hoja ya kuwapa watu wote fursa sawa na haki katika namna ambayo ni ya kweli na dhahiri. Hakika watu wote wana haki ya kushiriki kikamilifu ndani ya jamii.

Jamii yenye haki itachukua hatua dhahiri za kuwalinda wanyonge na itanuia kwa dhati kuondoa visababishi vya umaskini na masaibu mengine yanayowakwaza watu wengi wasifurahie maisha na wasitumie uwezo waliojaaliwa kikamilifu.

SEHEMU YA TISA
HAKI YA JAMII NA HUDUMA ZA JAMII

Haki ya jamii na Elimu
Haki ya jamii ni jambo la msingi kabisa kwa ajili ya Elimu bora (Connell, 1993). Kama mfumo wa jamii utawatendea visivyo haki baadhi ya wanafunzi katika jamii hiyo, ubora wa elimu ni wazi utakuwa na kasoro kubwa. Connell(ibid) anapendekeza uwepo wa mitaala ambayo mizizi yake imejikita katika haki na demokrasia. Mitaala hiyo iwe na uwezo wa kufungua fikra za wanyonge ili kuweza kifikia usawa katika jamii husika.

Katika elimu, kama ilivyo katika taasisi nyinginezo za huduma za jamii mamlaka yote yamefungamana na haki.
Wazazi, watoto, viongozi wa kisiasa na jamii kwa ujumla wana matarajio ya ni kitu gani shule zikifanye na ni jinsi gani kifanyike ili kufanya maisha ya mwanadamu yawe bora.

Wengi huitazama shule kama taasisi ambayo mazao yake hayana budi kuujenga uchumi na kuiboresha jamii. Shule hususan za umma zipo kwa ajili ya kutumikia na kujenga maslahi ya umma nay a mtu mmoja mmoja.

Masuala ya usawa na demokrasia ni miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele na mfumo haki wa kijamii.

Ujenzi wa Haki ya kijamii kupitia Elimu
  • Sharti pawepo vipengele vya kujenga haki ndani ya mitaala
  • Kuwepo kwa mipango ya kielimu ya kujenga mfumo haki (Education for Justice Programs; EFP)
  • Kuwezesha uwepo wa fursa kwa wanafunzi kushiriki katika matukio na vitendo vinavyolenga kujenga Elimu ya Haki ya Kijamii.
  • Ziwepo njia za ufundishaji darasani zinazotoa fursa kwa wanafunzi kujadili kanuni za haki katika Ulimwengu wa sasa.
  • Masomo ya uraia/sayansi ya siasa yalenge kujenga ufahamu wa vitendo vilivyo kinyume na haki na ni jinsi gani watawala wanapaswa kijenga haki.
  • Elimu ijenge fikra na mitazamo kuntu kuhusu masuala ya jamii, ukoloni, ubaguzi wa rangi, haki za binadamu, umaskini na mengineyo.
  • Elimu isisitize na kuamsha tabia ya kujali haki za wanyonge katika jamii, yaani maskini, walemavu, makabila madogo, wanawake, watoto, ambao hawajazaliwa, na mataifa madogo katika Ulimwengu wa ushindani kiuchumi.
  • Elimu isaidie kujenga maadili mahali pa kazi, uhusiano mwema baina ya mwajiri na mwajiriwa, mtumishi na mtumishi mwenzake, mtoa huduma na mteja n.k
  • Elimu iongoze jitihada za ujenzi wa haki ndani na nje ya darasa.
  • Elimu ifundishe kanuni za gawio haki na stahili ya kila mmoja.
  • Elimu ijenge mazingira ya usawa wa kijinsia, iendeleze wasichana kwa kuwapa fursa katika michepuo yote ya sayansi asili na sayansi ya jamii.
  • Elimu iwe ya fursa sawa kwa wote.
SEHEMU YA KUMI
MFUMO SHERIA ZITENDAZO HAKI (JUST LAWS)

Chini ya itikadi ya haki, sheria zote katika nchi sharti zizingatie haki za binadamu na viumbe hai wengine. Sheria zote sharti zipimwe kwa viwango vya haki kama zinavyozingatiwa na katiba ya nchi na katika miafaka/ matamko ya kimataifa.


nategemea criticism toka kwa kila atakayesoma makala hii. Ikibidi niandikie moja kwa moja.

George Kahangwa
kahangwagl@udsm.ac.tz
 
Ndugu Kahangwa, karibu sana. Huko ndiko hapa JF kunaitwa kumkoma nyani gladi (chini ya uasisi wa mkuu FMES). Ngoja tusome, tutafakari, tutarudi. Ni mara chache tunakutana na nondo kama hizi. Haya Kasheshe et al., si huwa mnataka itikadi, sera, etc za vyama mbadala, haya hizo hapo, zizodoeni sasa!
 
Bwana Kitila na wengine,
Nimesubiri kwa hamu kuzodolewa, nashangaa kimya. Tafadhali timiza ahadi yako,kwamba utayasoma haya mawazo na utarejea na maoni.Nayatamani sana maoni hayo
 
Mzalendohalisi na Mzee Mwanakijiji,
Nawashukuruni sana kwa shukrani mlizonitumia kuhusiana na mada hii
 
Hi

Ahsante Kwa Kutuletea Mada Hii Hapa Lakini Nasikitika Kukuambia Kwamba Umeleta Mada Katika Sehemu Ya Siasa Ambapo Watu Wengi Wanatilia Zaidi Mkazo Katika Kuikosoa Serikali Na Watendaji Wake Na Sio Kutafuta Ufumbuzi

Wewe Umekuja Na Mada Yenye Ufumbuzi Ni Vizuri Mada Hii Ungepeleka Katika Hoja Nzito Au Katika Sehemu Nyingine Inayohusika Na Usomaji Kama Elimu Hili Naona Kama Zinahusiana Hapa Wengi Ndio Hivyo Kukosoa Serikali Na Watu Wake Bila Suluhisho

Tafadhali Angalia Makala Za Mwanakijiji Nyingi Ziko Katika Hoja Nzito Zile Zenye Suluhisho Nafikiri Umenielewa .

Mwisho Napenda Kuchangia Kidogo Katika Mada Yako Nina Maneno Machache Ya Kusema

- Haki Haiwezi Kuwa Haki Kama Mwenye Haki Asipopata Nafasi Ya Kujua Haki Zake Ni Zipi Pamoja Na Za Wengine , Hii Inachangia Wakati Mwingine Na Mila Na Desturi .

Mfano Katika Nchi Za Kiarabu Wana Mila Na Desturi Zao Tofauti Na Hapa Tanzania Kwahiyo Kitu Ambacho Ni Haki Yako Hapa Tanzania Ukienda Saudi Arabia Inaweza Kuwa Sio Haki Yako Kutokana Na Mila Na Desturi Za Kule Pia Kutokana Na Wewe Mwenyewe Kutokupata Taarifa Na Elimu Husika Kuhusu Haki Hizo

Nakutakia Weekend Njema Nimeaad Email Yako Katika Mailing List Yangu , Ahsante Hope Utaendelea Kutuleta Makala Na Mada Zingine Moto Moto Zenye Kuleta Changamoto Kwa Vijana Na Taifa Zima La Watanzania Mada Zinazoleta Suluhisho Katika Jamii Husika

Ahsante Tena Na Tena
 
Ahsante sana ndugu Yona kwa mchango wako katika mada hii. Tayari nimekumbushwa au nimejifunza kitu kutoka kwako, kwamba tafsiri ya haki yaweza kuwa katika mazingira ya jamii husika (social context), kama vile yalivyo maadili ya jamii moja yasivyofanana na maadili ya jamii nyingine. Hata hivyo naamini yapo masuala ambayo yanaweza kukubalika katika ngazi ya jamii ndogo, yakakubalika kitaifa na kimataifa pia, matharani haki za binadamu ambazo mataifa wanachama wa umoja wa mataifa wameziridhia (Tanzania ikiwemo)

Kuhusu watu kutofahamu haki zao, hapo ndipo elimu ilipo na wajibu wa kutimiza. Ndio maana katika mada yangu nimeionesha nafasi ya elimu katika kujenga haki.

Utaniwia radhi kwa kuweka mada hii katika eneo ambalo hujapenda. Kwangu mimi siasa si uwanja wa kukosoana tu, na sina hakika kwamba katika historia ya mwanadamu ukosoaji peke yake uliwahi kufanya mabadiliko katika jamii. Nashukuru kwamba umenikumbusha kwamba tunalo pia jukwaa la hoja nzito, panapo majaliwa nitalitumia pia. Natarajia kupata mengi kutoka kwako, kupitia JF na kama ulivyosema, kupitia e-mail yangu. Karibu
 
Hi

Ahsante Tena Kwa Kujibu

Sikumaanisha Jukwaa La Siasa Ni Katika Kukosoana Pekee Lakini Ukiangalia Wengi Wanaochangia , Kusoma Au Kuleta Lolote Wengi Wanapenda Kuchambua Mambo Mabaya Yaliyofanywa Na Serikali Au Watu Wake Bila Kutoa Njia Mbadala Za Kushugulikia Mambo Hayo

Ndio Maana Nikasema Ikienda Hoja Nzito Ndio Muafaka Kwa Sababu Hii Hoja Tena Nzito Na Ina Fikira Mbadala Zinazoweza Kuibadilisha Jamii Kwa Njia Moja Au Nyingine Hata Kama Sio Leo Ni Kesho Au Kesho Kutwa Au Hata Kama Sio Tanzania Hata Sehemu Zingine Watu Wanazotembelea Au Kusoma Vitu Hivi .

Hapa Niliposasa Ni Usiku Kidogo Na Ninajiandaa Kwenda Sehemu Fulani Wacha Nichangie Kidogo Kuhusu Elimu Ya Haki Za Mwanadamu , Unaona Watu Wengi Hawapati Haki Mpaka Pale Anapokumbwa Na Msuko Suko Fulani Katika Maisha Yake Ndio Anaenda Kuelimishwa Kuhusu Haki Zake

Huoni Kwamba Sasa Watu Inabidi Kujifunza Haki Na Sheria Zao Toka Shuleni Na Wanavyokuwa Pia ??
 
kahangwa:
Sijasoma kwa kina mchango wako mhimu ulioubandika hapa; lakini nimeona kabla ya kujiwekea muda mzuri wa kuutumia katika kusoma makala hii, nikupe uzoefu wangu na wasomaji na wachangiaji katika ukumbi huu.

Panapokuwa na hoja nzito kama hii yako, na ikiwa na urefu wa kiasi hiki, wengi wa wasomaji hukwepa kutumia muda wao mwingi kusoma makala yote kwa pamoja. Kwa hiyo unakuta uchangiaji na usomaji unakuwa kidogo ni hafifu. Sio kwa sababu hoja ni dhaifu, hapana, ni kwa urefu wa hoja yenyewe, na pengine uzito wake ndio inayowaogopesha wengi.

Njia mojawapo ambayo imewahi kutumika kwa ufanisi mzuri, kwa hoja ndefu kama hii ni kama ile ambayo huwa anaitumia Marshall Field ES, kwa kuikata kata hoja na kuiwasilisha kama vipande huku mjadala ukiendelea. Sisemi kuwa hiyo ni njia bora zaidi kwa mjadala mzito kama huu, lakini ni wazo tu la kukufanya ufikirie kama kuna njia nyingine nzuri zaidi ya hii uliyoitumia hapa.

Hayo aliyoyasema Shy ya kulaumu tu serikali bila ya kutoa ufumbuzi mimi sikubaliani naye. Njia za ufumbuzi wa matatizo yetu ya kimaendeleo zinatolewa humu kila siku.
 
Ndugu Shy,
Haja ya watu kuelimishwa kuhusu haki zao ipo tena ni kubwa sana. Watu wengi wanaonewa au wanapoteza haki zao kwa kutokuwa na elimu hiyo. Nizidi kusisitiza kwamba, chini ya falsafa na itikadi hii, elimu itolewayo mashuleni kuanzia ngazi ya chini, haina budi kuwa na mada za haki katika mitaala yake.
Ndugu Kalamu,
ahsante kwa angalizo la kwamba watu hawana mazoea ya kusoma mada ndefu. Nitajitahidi kuzingatia hilo panapobidi(kadri ninavyodumu kuwa mwanaJF)
Natamani ujaliwe muda wa kuisoma, ili uweze kuona kama ina mantiki au kasoro zake zimejikita wapi, (you never know, one day Tz might say this is our road map) Nitafurahi sana tukishirikiana kuijadili kwa kuiboresha.
 
Bwana Kahangwa,

Usitiwe hofu wala kufikiri hoja yako haifai hapa mahali pa siasa. Taratibu naipitia kama ile mada yako kwenye Dira ya Elimu (by the way, Mwalimu Selina Mushi anatoa shukrani), nami nitakuja kujibu hoja.
 
Hii mada ni nzuri sana.. na ninaomba niendelee kuimeza wakati chembechembe za ubongo wangu zinafanya kazi ya ziada..
 
Mzee Mwanakijiji,
Ahsante kwa comment yako kuhusu uzuri wa mada hii. Nabakia mwenye subira,nikitarajia kupata tafakuri na mapendekezo ya wanaJF wote
 
Mchungaji,
Ahsante kwa kuniondoa hofu. Shukrani zangu pia kwa Mwalimu Celina.Sina shaka utakalokuja nalo baadaye katika hoja hii litakuwa la manufaa sana.
 
Kahangwa,
Nimesoma kwa makini makala yako hii hadi ikanivutia kujiunga na JF ili pamoja na kuwa mchangiaji mtarajiwa katika hoja za JF,nikupongeze kwa mawazo mazito na mazuri sana kiasi hiki.Natamani ungetufafanulia zaidi itikadi hii.Lakini usiiishie tu katika kuifafanua,kama wana JF wataniunga mkono,tukubariki ukaipendekeze kwa vyama vya siasa viifanyie kazi ili panapo majaliwa iwe ndio itikadi ya taifa letu. Anza na hicho chama ulichoomba kutokitaja. Na kama wewe bado ni mwanasiasa jitokeze tukusikilize,si ajabu ukawa ndo wale tunaowatafuta watuondolee jinamizi la viongozi mafisadi.Tunahitaji HAKI iinue Taifa letu.
 
Kahangwa,
Nimesoma kwa makini makala yako hii hadi ikanivutia kujiunga na JF ili pamoja na kuwa mchangiaji mtarajiwa katika hoja za JF,nikupongeze kwa mawazo mazito na mazuri sana kiasi hiki.Natamani ungetufafanulia zaidi itikadi hii.Lakini usiiishie tu katika kuifafanua,kama wana JF wataniunga mkono,tukubariki ukaipendekeze kwa vyama vya siasa viifanyie kazi ili panapo majaliwa iwe ndio itikadi ya taifa letu. Anza na hicho chama ulichoomba kutokitaja. Na kama wewe bado ni mwanasiasa jitokeze tukusikilize,si ajabu ukawa ndo wale tunaowatafuta watuondolee jinamizi la viongozi mafisadi.Tunahitaji HAKI iinue Taifa letu.
Ndugu Waridi,
Ahsante kwa pongezi. Nakubali jukumu ulilonipa la kufafanua zaidi.Ni vizuri basi yangeulizwa maswali hapa ili iwe rahisi kwangu kutambua mahali pa kutolea ufafanuzi.
Kuhusu baraka za wanaJF,naona mpaka sasa michango iliyotolewa hadi huu wa kwako ni positive,basi tusaidiane kuueneza ujumbe wake kwa watu wengi zaidi.
 
Nipo,nimetingwa na uandishi wa academic theses kidogo, lakini bado kitambo kidogo nitamaliza.Tegemea kupata mchango wangu wa hoja soon.
Well, tunatarajia zaidi toka kwako.

Nakutakia ufanisi katika kazi zako. Mungu akujaalie ufanikiwe
 
Back
Top Bottom