Haijawahi kutokea: CCM hawaamini kama wanaondoka, kwa haya lazima waondoke Jumapili

MMASSY

JF-Expert Member
Jan 13, 2011
290
193
Wakati nchi yetu ikiwa kwenye kampeni za lala salama za kuwapata viongozi mbali mbali watakaoongoza serikali ya awamu ya tano, tunafanya hayo tukitazama masuala kadhaa ambayo yamefanyika na baadhi ya wanaotaka kutuongoza tena na hata kuona wale wanaotaka kuingia madarakani.

Nimepata fursa ya kuchambua sehemu ya kashfa zilizohusisha upotevu wa mabilioni ya fedha za walipa kodi wa Tanzania.Naendelea kuchambua na kuonyesha namna ambavyo wale waliohusika na vyama vilivyohusika visivyostahili kupewa tena dhamana ya kutawala nchi hii.

Nimeanza kwa kuainisha hizi tano,pitia na uwape elimu wengine kadiri Mungu atakavyokuwezesha.

1.RADA
Mwaka 2011 Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ilikumbwa na jinamizi la ufisadi kwa mara nyingine tena,huku Magufuli akiwa mjumbe kwenye baraza la mawaziri. Safari hii uliibuka ufisadi wa mabilioni ya shilingi kupitia ununuzi wa rada chakavu (kuukuu) kutoka)Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza. Ununuzi wa rada hiyo unadaiwa kutofuata taratibu sahihi,sheria ya manunuzi serikalini na kanuni nyinginezo, uliligharimu taifa Sh29.5 bilioni, wakati gharama halisi ilikuwa Sh21 bilioni.Kwa maana nyingine ni kuwa,serikali ya Chama cha Mapinduzi ilijitaia isivyo halali kupitia kwa makada wake zaidi ya Billioni 9.

Serikali ya Uingereza iliamua kurudisha fedha hizo kama chenji baada ya wanaharakati kadhaa kuandamana uingereza wakidai Tanzania imedhulumiwa.Serikali ya uingireza ilijiridhisha kuwa vongozi waandamizi wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi walipiga dili huku ikisisitiza kuwa watuhumiwa wote wa hapa nchini waliohusika na ununuzi wa rada hiyo mtumba, washitakiwe Tanzania au Uingereza kutokana na kubainika dosari kwenye ununuzi huo.

Wakati Uingereza ikitaka watuhumiwa hao wafikishwe mahakamani, mtandao wa Wikileaks unaosifika kwa kufichua siri za ndani ya mataifa mbalimbali duniani, ulibaini kuwepo kwa harakati nchini za kutowafikisha mahakamani wahusika wa ufisadi huo.Mikakati hii ilisukwa kwa ustadi mkubwa na Viongozi waandamizi ndani ya Chama Cha Mapinduzi wakati huo huyu anayegombea leo na anayetuambia CCM Ni ile ile akiwa serikalini tena kwenye chombo cha juu cha maaamuzi ya nchi.

Kuna wimbo unaendelea kupigwa sasa katika mikutano ya CCM ikisisitiza kuwa CCM ile ile.Mimi nasema na watanzania wanisikie.CCM ni ile ile ya Radar chakavu na ni ile ile iliyowaibia Watanzania ila wazungu wakawaonea huruma Watanzania kuliko kuliko CCM wanaowania kuendelea kuwaibia watanzania.

2. EPA
Mwaka 2008 iliibuka kashfa nyingine ya wizi wa mabilioni katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu (BoT), ambapo vigogo kadhaa walitumia mbinu chafu kuchota zaidi ya Sh133 bilioni katika akaunti hiyo.Chama cha Mapinduzi hadi sasa hakijakana kuhusika na wizi ule kupitia Makada wake maarufu.Waliofungwa juzi ni kiini.

mamcho tu,sheria zenyewe wamezitunga wao.Haiwezekani mtu unaiba zaidi ya billioni kumi unapigwa faini ya Millioni tano.Huu ni utani kabisa.Utani huu wameufanya CCM kwa sababu viongozi wake waandamizi wanajua watanzania ni Malofa,hawawezi kuipitisha katiba ya tume ya Warioba,hawawezi hata siku moja kuikataa CCM kwa kuwa eti kunguni akiingia kitandani huwezi kuchoma kitanda.

Hizi ni kejeli, ni utani kwetu na ni hatari zaidi kwa maslahi mapana ya taifa letu.Nchi inapofikia katika hali hii,usalama wa taifa wanatakiwa wasaidie nchi kuliko chama.Hadi leo, fedha za wananchi zinaibwa na CCM, Taarifa za CAG kila mwaka zinaanika wizi na hakuna anayewajibishwa. CCM Wanajua watanzania ni "Business as usual".Katika wizi huo ulioitikisa nchi, wahusika walitajwa kutumia vivuli vya siasa katika kupitisha nyaraka bila kufanyiwa uhakiki wa nyaraka hizo.

Magufuli anayegombea leo,w izara anayoiongoza hadi sasa imeshutumiwa mara kadhaa kwa ushahidi wa documents kutoka kwa Mkaguzi wa hesabu za Serikali na hajawahi kusimamia uadilifu katika wizara yake. Leo hii CCM wanataka kurudi Ikulu eti wataunda mahakama maalum ya wezi.Ni nani kasema na ni wapi iliandikwa kuwa suluhisho la wizi wa fedha za nchi hii ni mahakama?

CCM wanavyotuaminisha kuwa wataunda mahakama maalumu ya rushwa ni kutaka kutuambia kuwa CCM hawana imani na mfumo wa mahakama wa Tanzania au hata majaji walioko kwenye mahakama zetu nao wamekuzwa kwenye mfumo wa rushwa chini ya uratibu wa CCM?.

3. RICHMOND
Mwaka 2006 baada ya Rais Jakaya Kikwete kuingia madarakani kulitokea tatizo kubwa la uhaba wa umeme.
Hapo ndipo Serikali ilipoanza kufanya mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutafuta njia za dharura za kutatua tatizo hilo.Waziri Mkuu wa wakati huo Edward Lowassa alikuwa mstari wa mbele katika mikakati hiyo ndipo Kampuni ya Richmond Development (LLC) ilipewa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura na kuliuzia Shirika la Ugavi wa Umeme nchini Tanesco.

Lowassa hakufanya vile kwa kuwa alikuwa anamaslahi binafsi kama wanavyosema akina Mwakyembe,hakufanya hivyo kwa sababu ni mtu korofi kama anavyosema Samuel Sitta.Alifanya hivyo kwa kuwa yeye ni kiongozi anayeamini katika utekelezaji na uwajibikaji.Lowassa hakwenda Marekani kutafuta Richmond.

Yeye kazi aliwapa wataalamu katika wizara,wakatafuta Kampuni, wakafanya taratibu wanazojua wao.Alichokifanya Lowasa kwa mujibu wa nyaraka nilizonazo ni kuharakisha umeme kupatikana.Aliingilia kati kutaka umeme haraka.Alichokifanya si kigeni.Kiongozi yeyote anayethubutu lazima achukue hatua za haraka kutatua tatizo.Richmond ilianza kuzalisha umeme na kupunguza makali ya mgao wa umeme kama tulio nao sasa.Hadi leo Richmond ipo bado Tanzania na inafanya kazi.

Lowassa amejiuzulu mwaka 2008,leo ni 2015.Serikali ya CCM inayombakizia Lowasa mzigo wa Richmond haijachukua hatua yeyote dhidi ya wanayemwita mwenye Richmond. Jana tu Kikweke kasema eti mwenye Richmond ni Lowasa. Naona Kikwete anapima hasira za watanzania. Hivi? Kati ya Lowassa na Kikwete nani anaongoza serikali?

Kama Kikwete anajua Lowasa ndiye mwenye Richmond, kwanini Kikwete kama amiri jeshi mkuu asiamuru kukamatwa na kushtakiwa Lowasa mara moja kama mhujumu uchumi?Kama Lowasa ndiye mwenye Richmond,ilikuwaje baada ya yeye kujiuzulu ikaendelea kufanya kazi na hata
Kikwete akamwalika Obama kuja kukagua mitambo hiyo na Kikwete akamzawadia Obama barabara iliyokuwa ya uhuru ikaitwa "Obama Drive?"Kikwete ndiye mamlaka ya juu ya nchi hii.

Kwa mujibu wa sheria,yeye ndiye raia namba moja.Ikawaje akubali Richmond iendelee kuwepo nchini baada ya kujiuzulu mwenye nayo?Ilikuwaje Lowasa akataja mamlaka ya juu ya nchi ndiyo ilimzuia kuvunja mkataba wa Richmond na hajachukuliwa hatua yoyote hadi sasa?

Kikwete anasahau kuwa Mwakyembe aliyeongoza kamati iliyomsulubu Lowasa bila kuhojiwa ndiye anayemiliki kampuni binafsi ya kuzalisha umeme wa upepo anaowauzia TANESCO.Yeye Mwakyembe hakutangaza maslahi aliyonayo Kama sheria inavyomtaka.Hakueleza bungeni kuwa ana maslahi na suala analolichunguza kwa kuwa tayari alishatofautiana na Lowasa pale alipotaka kuiuzia TANESCO umeme.

Sababu iliyomfanya Lowasa akatae ni moja na iko wazi kisheria, Kiongozi yeyote wa umma hawezi kufanya biashara na serikali kwa kuwa yeye mwenyewe ni mwamuzi katika serikali hiyo.Hili Mwakyembe halisemi kwa sababu anajua kosa lake.Wiki mbili zilizopita Mwakyembe huyu huyu ameibuka na kusema eti atazunguka nchi nzima kuonyesha uchafu wa Lowasa kwenye suala la Richmond.

Kabla Mwakyembe hajaanza atueleze kinagaubaga kwanini yeye na kamati yake walilichukulia suala la umeme ni la "Uwaziri Mkuu" zaidi kuliko wizara?.Aje atueleze kwanza,kwanini hakutangaza mgongano wa maslahi katika kamati na bungeni na hata kwa wananchi?.Yaani ni hivi vjana wenzangu;Huwezi kumchunga mwanamke(dada) uliyemtongoza akakukatalia na sasa unataka kumchunguza kuwa mahusiano aliyonayo sasa ni sahihi au si sahihi.

Plato anaelezea binadamu kama" Selfish creature" na maamuzi yote anayofanya mtu lazima atangulize maslahi yake mbele.Leo hii tunakaa na kukubali kijana aliyekeataliwa alipokuwa anamtongoza binti eti aende kuchunguza uhalali wa kukubaliwa kijana mwenzake.It is simply cannot be done.Naziri Karamagi na IBRAHIMU MSABAHA iliwalazimu na ilikuwa ni laizma wajiuzulu kwa sababu walishiriki mchakato wote uliogubikwa na utata.Lakini Lowasa ilimpasa kujiuzulu kwa makosa ya watendaji wake.Hili ni jambo la kawaida katika siasa na uongozi.

Mwinyi alijiuzulu uwaziri wa mambo ya ndani baada ya polisi kuua wananchi.Yeye hakushika bunduki wala hakuendesha oparesheni ile.Lkini baadaye alikuwa Rais wa Tanzania.Kosa liko wapi?Je Mwakyembe hakuwa bungeni katika sakata la Escrow?Kama mwanachama na waziri na mwana harakati mchukia rushwa,alikuwa wapi wakati CCM kupitia mawaziri na wabunge wakiibia nchi?Au fedha za Richmond ndio zilimuuma kuliko za Escrow?

Ni Mwakyembe huyu huyu!..aliyesema Richmond sio halali lakini sasa anashangilia uhalali wa Simbion, mitambo ni ile ile, umeme ni ule ule, mkataba ni ule ule na capacity charge ni ile ile! na Watanzia tumenyamaza. Ni Mwakyembe huyu huyu!..ambaye amelithibitishia bunge kuwa Richmond ni kampuni feki, hivyo kisheria kitu kikisha kuwa feki yaani batili, then ni batili tangu mwanzo kumaanisha hakipo na hakijawahi kuwepo, 'void ab initio' kitu ambacho ni uongo wa wazi wa mchana kweupe kwa sababu hata kama Richmond ni kampuni feki, ufeki wa Richmond ni kwenye makaratasi tuu, ile mitambo ya Richmond sio mitambo feki, na ule umeme wa Richmond sio umeme feki, ni mitambo real na inafua umeme real, hivyo Watanzania tulidanganywa!
Ni Mwakyembe huyu huyu!aliyezawadiwa uwaziri kwa kazi nzuri ya kumhifadhi mmiliki halisi wa Richmond, na kiukweli japo ameboronga kule Uchukuzi, lakini ameendelea kubebwa kwa kuwekwa kwenye wizara ambayo ni insignificant na haina impact!

Hatuoni Treni za Mwakyembe. Tunachoona ni mabehewa feki na Skrepa za treni. Ni Mwakyembe huyu huyu aliyejiapiza kuwa Tanzania isilipe tozo hiyo na kamwe haitalipa!, lakini ukweli Tanzania imeishalipa tozo ile, hivyo Mwakyembe ameisababishia Tanzania hasara ya mabilioni!, Tanzania ingekuwa ni Uchina, saa hizi Jina la Mwakyembe lingeisha kuwa ni historia siku nyingi kwa 'alikuwa!

Lowassa analalalamika hadi leo kwamba tatizo lilikuwa uwaziri mkuu.Kila mmoja anajua kuwa Lowasa alikuwa ndiye meneja wa kampeni za Kikwete.Tunajua kuwa Samuel Sitta alikuwa mtu wa karibu na mwenye nguvu kisiasa japo hakumfikia Lowasa.Wafuatiliaji wa mambo tunajua fika kuwa Samuel Sitta alitegemea kuwa waziri mkuu badala ya Lowasa.

Tunajua kuwa vita ilianza baada ya Kikwete kumtosa Sitta na kumpa uwaziri mkuu Lowasa.Kwa hesabu za CCM,waliamrisha wabunge wao kumchagua haraka Samuel Sitta kuwa Spika ili kumlipa fadhila.Samuel Sitta hakupenda sana cheo hiki,yeye aliona anastahili kuwa Waziri Mkuu.kwa hiyo mbeleko pekee aliyokuwa nayo Samuel Sitta ni kummaliza Lowasa ili aukwae uwaziri Mkuu jambo ambalo pia halikumsaidia sana.kwani mtoto wa Mkulima(Pinda ) akaokota pochi ya mzungu.Samuel Sitta akawa ameishia kwenye Uspika na hakuingia kwenye orodha ya watu waliowahi kuwa Mawaziri wakuu wa Tanzania.Mwakyembe aje hapa na azunguke Tanzania nzima sasa akituambia namna gani yeye na Sita wanavyolifahamu suala la Richmond.

Lakini pia asisahau kutuambia ni nani mmiliki wa kweli wa Richmond? Ni kiasi gani kimelipwa kwa Richmond(na sasa Dowans),kiasi hicho amelipwa nani? Mwakyembe atueleze wazi kuwa,kwanini yeye hakujiuzulu uwaziri na uanachama wa CCM baada ya serikali ya chama chake kumwalika Obama Tanzania na kuja kukagua mitambo ya Dowans iliyoridhiwa toka Richmond ambayo alijiapiza kuwa ni feki.

Atueleze yeye kama Waziri Mwandamizi Serikalini na kwenye chama,alikuwa wapi wakati Tanzania inashtakiwa mahakamani na kulipa kiasi kikubwa cha fedha kutokana na maamuzi ya bunge kuhusu Richmond?Ni kwanini ugomvi wa kisiasa wa makada wa CCM unaligharimu taifa mabilioni ya fedha kwa tamaa ya kulipiza visasi na kusaka madaraka?

4. OPERESHENI TOKOMEZA UJANGILI
Operesheni Tokomeza Ujangili iliyoanzishwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi kupambana na ujangili wa wanyama nchini mwaka 2013 iliwang'oa madarakani mawaziri wanne ambao wizara zao zilielezwa kushindwa kusimamia vizuri utekelezaji wa operesheni hiyo.Kung'oka kwa mawaziri hao kulitangazwa bungeni na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliyeeleza kuwa Rais Jakaya Kikwete ametengua uteuzi wao baada ya kuwasiliana naye kwa mashauriano akiwa nchini Marekani.

Ni nchi pekee duniani inaitwa Tanzania ndiko Rais anaweza kuwa nje ya nchi wakati wananchi wake wanauawa kama sisimizi wanavyokanyagwa.Ni Chama Cha Mapinduzi pekee duniani kinachoweza kutetea serikali yake pale watendaji wake wanaposimamia mauaji ya wananchi kwa kiwango cha operesheni tokomeza.Mawaziri waliong'olewa kutokana na ripoti ya kamati hiyo iliyoongezewa shinikizo na michango ya wabunge wengi hasa wale wa upinzani wakishirikiana na wachache wa CCM wanaojitambua ni Waziri wa Maliasili na Utalii,

Khamisi Kagasheki na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi. Wengine ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.Baada ya kujiuzulu kwa Mawaziri hao,hakuna hata mmoja aliyechukuliwa hatua za kinidhamu wala za kisheria kwa kuwa sio kawaida ya viongozi wa serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi kuwajibishwa kutokana na makosa waliyofanya kwa maslahi yao.

Mimi naamini hawachukuliani hatua kwa kuwa kila mmoja anajua ana makosa kiasi gani.Kuna wanaojua ni kwanini tembo wanaisha nchini kila kukicha,kuna ambao wanajua ni kwa nini biashara ya madawa ya kulevya yanashamiri kila kukicha Tanzania,kuna ambao wanajua kwanini pembejeo hazifiki kwa wananchi maskini,kuna ambao wanajua kwanini Twiga kiumbo ni warefu kuliko ndge lakini wanasafirishwa kwa magari na kwa ndge hadi nje ya nchi.Kuna ambao wanajua ni kwanini Tanzania ina madini mengi,Gesi na vyanzo kadhaa vya maji lakini umaskini hauishi.CCM ni mfumo ndugu zangu watanzania.Usipoondoa mfumo huwezi kufanya mageuzi yoyote ya maana.

Yaani ninachomaanisha hapa,sheria nyingi nchi hii zimetokana na serikali ya CCM, zimetokana na wabunge wa CCM na zimetekelezwa na Mahakama zinazofadhiliwa na SeRIKALI YA Chama Cha Mapinduzi.Mimi narudia sana kusema kuwa,Kama Chama cha mapinduzi kisipoondoka madarakani watanzania wasitegemee lolote katika maendeleo ya nchi hii.Kashfa ya Tokomeza ni tone tu.Zipo nyingi ambazo bunge limetumika kufunika.Kwa mfano,kuna taarifa ya maasi ya wananchi huko Mtwara na Lindi ambayo Spika aliahidi ingewasilishwa lakini mpaka mama Makinda anasema nendeni na amani pale Dodoma haikuwah kuonekana imetupwa wapi.

Sote tunajua bila kificho kuwa,baadhi ya wananchi wa Mtwara waliuawa,waliteswa na kubughudhiwa na serikali yao.Polisi haikuweza kuwatuliza wananchi pale walipodai kuwa wanaibiwa rasilimali gesi yao.Jeshi liliingia kazini na kuwakamata,kuwapa mkong'oto vijana na wanaume na akina mama wakakamavu.Leo hii CCM inajinasibu kwa wimbo wao maarufu kuwa CCM ni ile ile.Na mimi nasema kweli CCM ni ile ile iliyowaeleza wanamtwara na lindi kuwa gesi itaenda Dar Es Salaam kwa gharama zozote.WanaLindi na Mtwara wameminywa,wakakanyagwa,na gesi hatimaye ikaenda Dar Es Salaam chini ya uratibu wa Chama Cha Mapinduzi.

Leo hii CCM wale wale wako kila mahali nchini ikiwemo Mtwara na Lindi ikiwaimbia Wananchi "CCM ni ile ile" na wanataka wachaguliwe tena kuwaamrisha wananchi na rasilimali zao kwa gharama yoyote ile.Sio hivyo tu,wananchi wa Nyamongo wanauawa kila uchao na wamiliki wa mgodi,wanakunywa maji yenye sumu toka kiwandani yanayoigia kwenye vyanzo vya maji,wanapambana na kuuawa na polisi bila huruma.Mwaka 2012 wananchi kadhaa waliuawa. PAUL SARYA miaka 26 wa kijiji cha nyangoto na RODGERS MWITA miaka 18 wa kijiji cha kimusi walipigwa Risasi na kufariki mwaka 2012.

Sio serikali wala polisi wala mmiliki wa mgodi wa ABG waliowajibika kwa mauaji haya.Operesheni tokomeza inadaiwa kukiuka haki za binadamu ikiwamo watu 13 na askari sita kuuawa, utesaji wa kutisha watuhumiwa, ubakaji, rushwa na uporaji wa mali za wananchi.Hakuna sehemu utakayogusa nchi hii ambapo kuna mwekezaji ukose sokomoko kati ya wananchi na mwekezaji huyo.Hii inatokana na ukweli kwamba,sera za uwekezaji za Chama cha Mapinduzi ni hatari kwa usalama wa taifa.

Wengi mtashangaa kwa sababu mnadhani usalama wa nchi ni usalama wa serikali au wa Chama cha Mapinduzi.Hapana,Usalama wa taifa ni usalama ni ulinzi wa uhai wa wananchi,mali za wananchi,na ustawi wa wananchi na taifa kwa
ujumla.

Kama ni kinyume basi Mwalimu wangu wa chuo Kikuu alinifundisha vibaya,lakini hata mimi nilithibitisha kwa kuangalia nchi zingine zinafanyeje.Serikali huja nahuondoka,Vyama kama CCM huja kama kilivyokuja,na sasa kinaondoka na kitaacha taifa na usalama wa taifa. Serikali yoyote inayotokana na Chama chenye sera mbovu kama CCM ni hatari sana kwa usalama wa taifa.Nyamongo wanauawa kwa sababu tu mgodi upo kwao,Geita kwenye GGM wanauawa kwa sababau mgodi upo kwao na sasa yupo asiyejali maslahi yao, Serengeti wananchi waliuawa kwenye operesheni kwasababu wako kando kando ya mbuga.Hiyo ni baadhi tu ya mifano.

Serikali kupitia kwa katibu Kiongozi ilitokea mbele ya waandishi wa habari na kudai kuwa viongozi wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi waliozembea hadi wananchi kuuawa hawana kosa na kwa maana hiyo ni wasafi.Yaani ni kama wale wananchi waliouwawa sio kitu,ni sisimizi wamekanyagwa na mtembea kwa miguu na kwa hiyo aliyewakanyaga hana kosa.Mimi nilifundishwa na hata Biblia inasema damu huwa inalia,huwa inarudi.Kuna siku damu ya Daudi Mwangozi(Mungu umrehemu) itarudi na kuwalilia CCM na mimi naamini ni siku kama arobaini kutoka leo.

Damu za wananchi waliouawa sehemu kadhaa wakitetea maisha yao na ya Watanzania wenzao itainuka na kuwauliza CCM kwanini mnatumbia mbinu za kimafia kuongoza wananchi?.Damu ya wananchi waliouawa kwenye mkutano wa Chadema Arusha,Damu ya watanzania iliyomwagika Mwaka 2011 Januari tano Arusha zitawalilia CCM.

Ndivyo damu ilivyo.CCM wanajua ni kwanini wanapenda kutumia mgongo wa polisi kuuwa wananchi wanaotetea maslahi yao kule Sanya juu,Loliondo na Dodoma.Sheria zote nchi hii zimetungwa kutokana na sera za Chama cha Mapinduzi.Kwa hiyo hakuna sheria ambayo itaonekana ni nzuri tuache kuwasifia Chama cha Mapinduzi, na hakuna sheria yoyote mbaya tutaacha kuwalaumu na kuwabeza Chama Cha Mapinduzi.Mwaka huu wananchi wanapiga kura kuamua kati ya giza na mwanga.Wanapiga nchi kuamua watawaliwe kwa machungu kama operesheni tokomeza na nyinginezo zilizoambata nazo au watawaliwe kwa Usawa,Demokrasia na utawala bora unaojali haki za binadamu.

Sera za Vyama cya CCM na Chadema/Ukawa zinakinzana sana.Huwezi ukafananisha namna ambayo Lowasa angeongoza nchi akiwa CCM na namna atakavyoiongoza nchi akiwa Chadema.Kuna msemo wa kiingereza ambao tafsiri yake kwa kiswahili ni "Ukienda kwa Waroma,fanya wanayoyafanya waroma".Na CCM ijiandae kwa lolote mwaka huu!!.

5. AKAUNTI YA ESROW
Wakati kashfa ya Richmond haijasahaulika, mapema mwaka 2014,imeibuka kashfa ya upotevu wa mabilioni ya fedha kwenye Akaunti ya Esrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Kashfa hiyo iliyolitikisa Bunge na Serikali, imetajwa kuwa ni mwendelezo wa jinamizi la kashfa ikiwa ya saba kubwa kulikumba taifa hadi sasa.

Akaunti hiyo iliyokuwa na zaidi ya Sh200 bilioni, ilifunguliwa wakati kukiwa kuna mgogoro wa kisheria baini ya wabia wa zamani wa IPTL (VIP Engeneering and Marketing na Mechmar Corporation ya Malaysia) kwa upande mmoja, Tanesco na Independent Power Tanzania, IPT, kwa upande mwingine.Wadau kwenye akaunti hiyo hawakupaswa kuchukua kitu chochote hadi pale mgogoro utakapotatuliwa. Hata hivyo, kitita hicho cha fedha kilichotwa na makada wa Chama Cha Mapinduzi.Ukiachilia mbali Rugemalira ambaye amejinabaisha kama mwanachama
kindakindaki wa Chama Cha Mapinduzi ameonekana kiungo muhimu cha ugawaji wa fedha haramu kwa viongozi waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi,dini na majaji wenye heshima katika taifa hili.

Fedha ziligawanywa kama hazina mwenyewe,Kamati ya bunge ilitueleza kuwa fedha ziligawiwa kwenye mifuko ya rambo,salfeti na hata sandarusi.Wakati hayo yakijiri serikali ya Chama Cha Mapinduzi iliendelea kukomalia kuwa fedha hizo hazikuwa za serikali.Maana yake ni kwamba zilikuwa mali binafsi ya wamiliki wa Escrow.Kinachotushangaza ni kwamba wakati serikali kupitia waziri mkuu na hata Kikwete mwenyewe wakikanusha kuwa hizo sio fedha za walipa kodi,tayari mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali alishakagua fedha hizo na kutanabaisha kuwa zilikuwa fedha za watanzania.Leo nasema,Kikwete kama mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi atokee hadharani na kutuambia fedha za Escrow zilikuwa kwa lengo gani?.Viongozi wa serikali hii akiwemo Magufuli kama mjumbe wa baraza la mawaziri walibariki matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi wa nchi hii.

Leo wanatuambia eti Magufuli naye ni mwana mabadiliko.Enheee heeee nheeeee,yaani kundi la wezi linakaa katika vikao na kulipana fedha za walipa kodi huku wakipitisha maamuzi ya kuliangamiza taifa,leo wanakaa Dodoma na kutuaminisha kuwa Chama Cha Mapinduzi nacho kinataka mabadiliko.Ha ha haaaaaaaa,yaani kumbe hata Ccm na Magufuli wao wanataka mabadiliko?Basi wavunje chama na kuungana na upinzani manake waliosababisha wananchi watake mabadiliko ni wao CCM.Sera mbovu,sheria kandamizi,ufisadi,Upendeleo,Kilimo,biashara,kodi kubwa zinazotozwa na serikali ya CCM Ndizo zilizoifikisha nchi hapa.Ndizo zilizofanya wananchi watake MABADILIKO.Wasichokifahamu CCM ni kuwa wananchi hawataki tu "mabadiliko" bali wanataka MABADILIKO.Wao wanajiita Chama cha Mapinduzi,sijui kwanini kinaitwa Chama Cha Mapinduzi kwa sababu sijui kiliasisi mapinduzi yapi?CCM kilimpindua nani?Vyama vya mapinduzi dunia nzima tunavijua,vimekaa kimapinduzi kweli kweli.Ufisadi uliopo katika Chama Cha Mapinduzi na katika serikali yake,umejenga tabaka na gamba gumu kiasi cha kutokutoka tena.Ni asili na lazima libaki kama lilivyo.Haijalishi ni nani anaingia kuendesha,kama gari ni bovu haliwezi kwenda kama inavyotakiwa. Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Emmanuel Mallya alisema matukio ya ufisadi yanaongezeka nchini kutokana na Serikali kushindwa kuweka bayana hatua zinazopaswa kuchukuliwa watu wanapatikana na makosa hayo, ili iwe fundisho kwa wengine kama ilivyoripotiwa na gazeti la Mwananchi. Alisema kila mara wizi wa fedha za umma unapotokea, Serikali na Chama Cha MApinduzi hupata kigugumizi kuwawajibisha wahusika, hatua inayowafanya watu wengi kuamini kushindwa kwao kunatokana na woga wa kutekeleza azma zao."Hakuna uwajibikaji kama mtu kafanya jambo fulani, kuna kulindana sana, lakini kama wote wangechukuliwa hatua za wazi pengine ufisadi usingekuwa wa kiwango cha juu namna hii," alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (UDSM) Faraji Christoms, alishauri wenye dhamana ya kusimamia masilahi ya taifa wanatakiwa kujitathmini upya.
Alitaja maeneo yanayohitajika kufanyiwa tathmini kuwa ni uzalendo kwa taifa, elimu kwa maana ya uelewa wa mambo ya kisheria, lugha za kimataifa na umakini wakati wa majadiliano ya kimataifa na wanaposoma mikataba ya aina hiyo.
"Unakuta mtu badala ya kutuliza akili akasoma kwa makini mkataba kabla ya kuusaini, anaupeleka kwa msaidizi wake ukisindikizwa na memo (agizo la maandishi) "Please read carefully for advice," (tafadhali soma kwa makini, shauri)," alieleza Christoms.Tumeshuhudia kashfa kuwa waziri mmoja alienda uingereza akasaini mkataba usio na maslahi kwa taifa baada ya kununuliwa whisky.
Alisema katika mazingira hayo, hatima ya usalama wa mkataba huo unakuwa mikononi mwa mwingine, tofauti na aliyepewa dhamana. Christoms alisema mazingira yanaonyesha kuwa wanasheria serikalini wanashindwa na walioajiriwa kwenye kampuni za uwakili, hivyo kusababisha Serikali kupata hasara kwa kuingia katika mikataba isiyo na masilahi kwa taifa.
Profesa Gaudence Mpangala, wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO) alisema historia ya ufisadi nchini inamnyima mtu yeyote makini, ujasiri wa kuishauri Serikali mbinu za kudhibiti vitendo hivyo vya rushwa. Profesa Mpangala alisema vitendo vya rushwa haviepukiki katika jamii, lakini Serikali inapochukua hatua zinazothibitisha kuwa inavipiga vita, hali inakuwa shwari tofauti na ilivyo nchini ambapo rushwa ndogo na ufisadi vimeota mizizi huku hatua zinazochukuliwa zikiacha maswali mengi bila majibu.
Alitoa mfano wa serikali ya awamu ya kwanza, ilivyoshughulikia rushwa iliyokuwa inaelekea kwenye ufisadi kwa kuchukua hatua kali, chini ya hayati Edward Sokoine na Mwalimu Nyerere ambapo waliothibitika kuhusika pamoja na adhabu ya kifungo jela, walitakiwa kuchapwa viboko wakati wa kuingia na kutoka gerezani.
Tujitokeze kwa wingi siku ya jumapili kupiga kura na kuondoa uozo huu.
MMASSY JEROME
Mchambuzi
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom