Hadithi: Uchawi wa bilionea Bazoka

NYEMO CHILONGANI
UCHAWI WA BILIONEA BAZOKA
0718069269

SEHEMU YA 30.

Maganza alitulia ofisini kwake huku kichwa chake kikiwa na mambo tele, bado alimfikiria Bazoka, mwanaume huyo alimsumbua kwa kuwa kulikuwa na mambo mengi yaliyokuwa yakimvuruga.
Kila alipokuwa akimfikiria, alikosa jibu, kuna wakati alianza kuhisi jamaa alikuwa mchawi lakini wazo hilo hakulitilia maanani kwa kuwa jamaa muonekano wake haukuwa kama wa kichawi hata kidogo.
Alihisi kulikuwa na jambo lililokuwa likiendelea nyuma ya pazia lakini pia hakuona kama kulikuwa na kitu, kichwa chake kilimwambia kulikuwa na jambo jingine lakini si hilo alilokuwa akilifikiria.
Alitulia, huku akiwa amezama kwenye mawazo ndipo akakumbuka kuhusu gari la Bazoka. Siku ya kwanza alipokwenda kufanya upelelezi wa kupotea kwa mtoto Yusufu, alikumbuka aliambiwa kuhusu gari ambalo halikuonekana, ilikuwa ni Noah Nyeupe.
Kengele ikagonga kichwani mwake, huyo Bazoka aliwahi kufika hapo kituo cha polisi akiwa na gari lake, akajitahidi kulikumbuka vilivyo, lilikuwa ni Noa Nyeupe kama alivyoambiwa.
Sasa hapo akaanza kupata picha kwamba inawezekana kabisa huyo Bazoka ndiye yule mwanaume aliyemteka Yusufu na baadaye kukutwa porini akiwa ameuawa kwa imani za kishirikina.
Alipokumbuka hilo, akatulia na kujipa makosa, aliwahi kusikia na kuona kwamba watoto wote waliokuwa na ulemavu wa ngozi walipokuwa wakitekwa, walipokuwa wakipatikana, miili haikuwa na viungo, watu walivitoa na kuondoka navyo, hiyo ilikuwa tofauti na Yusufu kwani alikutwa na viungo vyake vyote.
“Sasa mbona inanichanganya!” alijisemea.
“Ila acha nianze kudili na hii Noah, yaani moyo wangu unaniambia kwamba haya yote anayoyafanya ni Bazoka tu,” alijisemea, akiwa amemaliza kuwa kwenye hali hiyo, mara simu yake ya mezani ikaanza kuita, haraka sana akaichukua na kuipeleka sikioni.
“Halo!”
“Nakuhitaji ofisini,” ilisema sauti ya upande wa pili na kukata simu.
Sauti hiyo ilikuwa ni ya kamanda Masumbuko, aliijua auti yake na hivyo haraka sana akainuka na kwenda huko, alipofika ndani ya ofisi ya mkuu wake, akagonga mlango, akakaribishwa na kuingia ndani, macho yake yakatua kwa makamanda wengine wawili waliokaa kwenye viti vilivyokuwa humo, akapiga saluti.
“Kuna kazi nataka nikupe. Fuatilia mauaji ya mtu fulani,” alisema Kamanda Masumbuko.
“Mauaji gani mkuu?”
“Kuna mtu anaitwa Christopher, ama kwa jina jingine Bonge,” alijibu.
Maganza aliposikia majina hayo tu akashtuka na kumwangalia Masumbuko vilivyo, hayakuwa majina mageni masikioni mwake, aliwahi kuyasikia mahali au hata kufuatilia jambo kuhusu mtu huyo.
Hapo ndipo Masumbuko alipomwambia kwamba mwanaume aliyekuwa ameuawa alikuwa rafiki wa Bazoka, akakumbuka, alikuwa mmoja wa watu aliowahi kuwahoji baada ya kifo cha Sultani kutokea.
Sasa hapo kichwa chake kikachanganyikiwa zaidi, hapo kwa haraka sana akaanza kupata majibu ya kitu fulani, ni kweli alikuwa bize kumuhusisha Bazoka kwenye mauaji ya watu hao lakini inawezekana kulikuwa na watu walioamua kufanya mauaji kwa watu hao na huyo Bazoka naye alikuwa kwenye orodha hiyo.
Marafiki zake waliuawa, kwake haikumuingia akilini kwamba ni Bazoka ndiye aliyefanya mauaji hayo, kwa mara ya kwanza akaanza kukubaliana na Bazoka kwamba kulikuwa na mtu mwingine aliyekuwa akiyafanya hayo yote lakini si yeye.
Hayo yote yalifikiriwa kichwani mwake ndani ya sekunde chache tu, Masumbuko akampa faili kuhusu mauaji ya mwanaume huyo na kurudi nalo ofisini mwake, akalifungua na kuanza kulifuatilia.
Kilichoandikwa humo kikaanza kumtia hofu, alisoma maelezo vizuri na kugundua kwamba mtu aliyefanya mauaji alikuwa mwanamke ambaye baada ya tukio hilo hakuonekana tena.
Mauaji yake yalikuwa sawa na yale ya Sultani, naye aliuawa na mwanamke nyumbani kwake, ila huyo Bonge aliuawa akiwa ofisini mwake. Akachanganyikiwa mno, hakutaka kubaki ofisini, haraka sana akaondoka na kuelekea huko ofisini, alitaka kuliona eneo la tukio.
Alipofika huko, alikuta ofisi ikiwa imefungwa ila tayari alipewa ufunguo kwa lengo la kuingia na kuanza kuchunguza. Aliangalia mpangilio wa ofisi huku mikononi akiwa na glove kwa ajili ya kuacha kila kitu kama kilivyokuwa bila kuweka alama yoyote ile ya vidole vyake.
“Maiti yake ilikutwa hapa, ilikuwa imelala bila shaka,” alijisemea huku akikiangalia kitu, kwenye meza kulikuwa na alama fulani nyekundu, alihisi zilikuwa damu.
“Mwanamke alikaa wapi? Labda kwenye kiti hiki,” alijiuliza na kujijibu.
“Inawezekana ndani kulikuwa wawili tu? Hapana! Ndiyo! Hapana! Ndiyo! Inawezekana kabisa. Sasa baada ya kufanya haya mauaji mwanamke alikimbilia wapi?” alijiuliza huku akiangalia dirisha la vioo tupu, lilikuwa limefungwa vilivyo.
“Hakuweza kupitia dirishani kwa sababu bado lilikuwa limefungwa, kama angepitia hapa basi dirisha lingekuwa wazi,” alijisemea.
“Hebu subiri!” alisema.
Haraka sana akachukua simu yake na kumpigia mtu alikuwa karibu na ofisi yake na kumwambia akaagalie ofisini kwake, kwenye lile faili ambapo kulikuwa na namba ya simu ya dada wa mapokezi.
Haraka sana hilo likafanywa na mwanaume aliyekuwa upande wa pili na baada ya dakika kadhaa, akatumiwa namba ya msichana huyo, haraka sana akaipigia, akaanza kuzungumza naye.
“Nataka nikuone hapa ofisini, hakikisha ndani ya nusu saa uwe umefika,” alimwambia baada ya kuitambulisha.
Baada ya kuzungumza naye, akatulia humo ofisini huku akiendelea kufuatilia kwa karibu na kujaribu kufikiri ni kitu gani kilichokuwa kimetokea. Baada ya dakika ishirini, msichana huyo akafika ofisini hapo na kuanza kuzungumza naye.
Alimuhadithia kila kitu kilichokuwa kimetokea, namna bosi wake alivyofika ofisini hapo na kuzungumza naye, alipoingia ndani na msichana huyo kutokea, naye akaingia.
“Halafu?” aliuliza.
“Baada ya dakika kadhaa, rafiki yake akafika ofisini hapa,” alimwambia.
“Rafiki yupi?”
“Bazoka!”
“Bazoka?” aliuliza huku akiwa na mshtuko kwa mbali.
“Ndiyo!”
“Alifika huku huyo msichana akiwa ndani?”
“NdiyO!”
“Halafu ikawaje?”
“Aliingia na kuongea naye kidogo, hakukaa sana, akatoka, aliniambia anamuacha bosi wake akizungumza na huyo msichana halafu yeye angerudi kwani hakujua kama alikuwa na mgeni,” alimwambia.
“Sawa. Bazoka alivyoondoka, una uhakika msichana huyo aliendelea kubaki humo ndani?” alimuuliza kana kwamba yule msichana alijigeuza Bazoka na kuondoka.
“Ndiyo kwani niliendelea kusikia vicheko vyao ndani ya ofisi!”
“Sawa. Endelea.”
Baada ya lisaa hivi, Bazoka akarudi!”
“Lengo la kurudi?”
“Aliniambia alimuachia uhuru bosi ili afanye yake!”
“Yapi?”
“Kufanya mapenzi na msichana huyo, hivyo aliporudi, tulikuwa tunaongea kwa utani kwamba bado wanaendelea kufanya kwani kulikuwa kimya kabisa,” alisema.
“Sasa nyie mlijuaje kama amekufa?”
“Bazoka alichoka kusubiri, akaamua kuingia ndani! Ndipo alipoikuta hiyo maiti na kuniita,” alijibu.
“Kwa hiyo Bazoka ndiye aliyegundua maiti ya bosi wako?” aliuliza.
“Ndiyo!”
Kwa kipindi hicho kama kulikuwa na watu waliokuwa wamechanganyikiwa kwa matukio mengi yaliyokuwa yakitokea, basi yeye alikuwa wa kwanza. Alitamani kumuhusisha BAzoka kwenye jambo hilo lakini kwa jinsi msichana yule alivyokuwa amesimulia, hakuona ni wapi mwanaume huyo alipokuwa amehusika.
Yeye mwenyewe inaonyesha kabisa hakuwa amejua kilichokuwa kimetokea, aliingia na kukuta maiti, sasa kama kweli alitakiwa kumuhusisha ilikuwa ni lazima kuwa na sababu mahali ama hata uwalakini wa kumuingiza kwenye tukio hilo.
Alipanga kumpigia simu Bazoka na kwenda kuzungumza naye, alihisi inawezekana kabisa akawa anafahamu kilichokuwa kimetokea kwa ukaribu lakini hofu yake ilikuwa moja kwamba asingepata ushirikiano kutoka kwake kwa kuwa alimsumbua sana.
“Kwenye hii kesi acha nifuatilie taratibu,” alijisemea, alihitaji kufanya uchunguzi wa mauaji hayo kimyakimya kabisa, ikiwezekana amfahamu msichana huyo kwanza.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumanne mahali hapa.

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 
NYEMO CHILONGANI
UCHAWI WA BILIONEA BAZOKA
0718069269

Sehemu ya 31

BAADA YA MIEZI SITA.
Bazoka alimaliza kila kitu, alikuwa na mafanikio makubwa kabisa, alikuwa maarufu jijini Dar es Salaam na utajiri wake ulikuwa ukiongezeka kila siku.
Alijulikana kwa wema wake mkubwa, alikuwa akitoa misaada ya kifedha na chakula kwa watu waliokuwa na uhitaji mkubwa. Kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakisema kuwa mwanaume huyo alikuwa na mafanikio ya kishirikina lakini baada ya kuona namna alivyokuwa akiwasaidia watu wengine, kila mmoja aliamini hakuwa na utajiri wa damu kama walivyokuwa wakisema.
Bazoka alipendwa, ilikuwa hivyo ni kwa sababu tu aliamua kuutoa utajiri wake kwa watu waliokuwa na shida mbalimbali. Alitembelea hospitalini, aliwatia faraja wagonjwa na hata wale wasiokuwa na uwezo wa kulipia matibabu, aliwalipia bila tatizo lolote lile.
Bazoka akawa Bazoka. Watu walipenda maisha yake, walivutiwa naye kiasi cha watu wengine kuanza kujipa jina lake kwa kuamini inawezekana nao siku moja wakawa na pesa nyingi kama ilivyokuwa kwa jamaa huyo.
Mguu wake ulikuwa na kidonda kikubwa, kilichochimbika na kuuma mno, kila alipotembea, alichechemea kitu kilichowafanya watu wengi kushangaa na kuhisi inawezekana mwanaume huyo aliwahi kuvunjika mguu kipindi cha nyuma.
Hawakujua mateso aliyokuwa akipitia kila siku, ni kweli alikuwa tajiri mkubwa lakini kidonda kile kilimnyima raha kabisa, kuna wakati alitamani kupoteza kila kitu ili apone lakini kila alipofikiria utamu wa kuwa na pesa, akaamua kuuchuna tu.
Baada ya hiyo miezi sita, hatimaye Bazoka akatokewa tena na jini lililokuwa na muonekano wake. Siku hiyo alikuwa ofisini mwake akiendelea na kazi zake kama kawaida, huku akiwa ameinamia kalkuleta yake, ghafla akasikia salamu kutoka kwa mtu aliyesimama mlangoni.
Akauinua uso wake na kutua kwa jini hilo, hakushangaa wala kuogopa ila hakupenda kumuona tena kwa kuwa mara ya mwisho alipomfuata na kuzungumza naye, alimwambia kitu ambacho mpaka siku hiyo kilikuwa kikimuumiza.
Jini hilo likaanza kumsogelea huku likiwa kwenye sura iliyokuwa na tabasamu, likakaa kitini na kuanza kuangaliana na Bazoka uso kwa uso. Bazoka hakusema kitu na hata ile salamu hakuwa ameiitikia.
“Tunahitaji kutoa tena kafara,” alisema jini yule huku akimwangalia Bazoka.
Bazoka akashtuka kusikia hivyo, hakutaka kabisa kulisikia neno liitwalo kafara kwani kama kutoa, aliwahi kufanya hivyo, tena si mara moja, sasa hakuaka kuua tena kwa kuwa yale mauaji aliyowahi kuyafanya, hakika aliyaona kutosha.
“Hapana! Nimechoka, yaani kila siku kutoa kafara tu,” alisema Bazoka, alikuwa anamaanisha kile alichokisema, hakuwa akitania hata kidogo.
“Bazoka! Huu ni ulimwengu wa kitajiri sana, wanaokupa utajiri wanataka damu zaidi, damu ya thamani sana kutoka kwako,” alimwambia.
“Damu ya thamani kutoka kwangu?” aliuliza huku akimwangalia, alishtuka si kitoto.
“Ndiyo!”
“Unamaanisha nini?”
“Kumuua mtoto wako,” alimwambia.
Moyo wa Bazoka ukapiga paa! Hakuamini alichokisikia, kumuua mtoto wake kilikuwa kitu kisichowezekana kabisa, alimpenda sana, kwake alikuwa kila kitu, kumuua ingeonyesha hakuwa na mapenzi naye hata kidogo.
Ni kweli alihitaji sana kuwa tajiri zaidi lakini kwa lile sharti aliloambiwa, namna ambavyo kafara ilitakiwa kutolewa, hakika hakukubali, alikuwa tayari kupoteza kila kitu lakini si kumuua mtoto wake.
“Nimuue mtoto wangu?” aliuliza huku akiwa haamini alichokisikia.
“Ndiyo!”
“Hivi una mtoto wewe? Hivi unajua maumivu ya kufa kwa mtoto wako mwenyewe?” alimuuliza, jini lile likaanza kucheka.
“Utatakiwa kuilipia kwa kitu kingine!”
“Kitu gani?”
“Uue watu kuanzia ishirini, tena kwa mkupuo,” alimjibu.
“Sijakuelewa.”
“Fikiria, utaelewa tu!”
“Napo haiwezekani!”
“Ila kuna la tatu pia,” alimwambia.
“Lipi?”
“Kama hayo mawili ya mwanzo yatashindikana!”
“Lipi hilo?” aliuliza kwa ukali.
“Kukuua wewe. Utakufa kwa maumivu mazito, utapooza kitandani, thamani yako itashuka, utachekwa, utapitia mateso makubwa mno mpaka kutamani kifo, upo tayari kupokea kifo hicho?” aliuliza.
Bazoka akabaki kimya kwa sekunde kadhaa, alichokuwa ameambiwa hakika kwake kilikuwa ni mtihani ambao hakuamini kama ingetokea siku moja angepewa kwa lengo la kuufanya.
Kwanza hakuwa tayari kumuua mtoto wake, alikuwa na thamani kubwa kuliko kitu chochote kile, ukiachana na huyo, pia hakuwa tayari kuona akiteketeza roho ya mtu mwingine, sasa kipindi hicho aliambiwa aue watu wengi kitu ambacho naye hakutaka kabisa kuona kikitokea
“Utakuwa tayari kwa lipi?” liliuliza jini lile.
“Binadamu hatuna thamani! Hata ukiwa na utajiri kuliko binadamu yeyote katika dunia hii, ni lazima mwisho wako utakuwa mmoja tu, nao ni kifo. Naomba ukawaambie waliokukutuma kwamba binadamu ambaye alikuwa tajiri kuliko wote, na utajiri wake hautokuja kufikiwa alikuwa mmoja tu, mfalme Sulemani, mtoto wa mfalme Daudi, mtoto aliyezaliwa na mwanamke wa nje ya ndoa, unajua nini kilitokea kwa Sulemani? Naye alikufa pamoja na utajiri wake mkubwa, nipo tayari kufa kwa sababu nisipokufa kwa kifo hicho, basi kuna siku isiyokuwa na jina nitakufa, na nitakapoanza kufa, hakuna atakayeniokoa, hata wewe hutoweza kuniokoa. NIPO TAYARI KUFA,” alisema Bazoka huku akimwangalia jini lile lililoonekana kushangaa.
“Una ujasiri mkubwa sana!” alimwambia.
“Ni kwa sababu kifo ndiyo mwisho wetu. Kama umezaliwa na mwanamke, basi mwisho wako ni kifo tu,” alisema Bazoka.
Walibaki wakiangaliana tu, siku hiyo Bazoka alionekana kuwa na ujasiri mkubwa, hakuonekana kuhofia jambo lolote lile, alikubali kufa kwa kuwa hakutaka kuona akimuua mtoto wake wala mtu mwingine.
Aliifahamu thamani ya maisha ya mwanadamu na mwisho wake, hapakuwa na yeyote ambaye aliishi milele, wote waliokuwa wakizaliwa na mwanamke, mwisho wa siku walikuwa wakifa tu, hivyo naye hakuona sababu ya kutaka kuishi milele.
Jini lile likapotea na kumwambia angekwenda kuwaambia waliomtuma kile kitu alichomwambia. Bazoka hakutaka kujali, kwake, kwa muda huo alikuwa tayari kupoteza kitu chochote kile lakini si kuona akiendelea kufanya mauaji kama ilivyokuwa ikitokea.
Maisha yaliendelea zaidi, aliendelea kula maisha, kwa kipindi hicho hakuwa na furaha kama kipindi cha nyuma. Mkewe aliligundua hilo, alimuuliza kilichokuwa kikiendelea lakini hakumwambia kitu chochote kile zaidi ya kusema alikuwa sawa tu.
Alikosa furaha, maisha yake yakaanza kubadilia, akaanza kunywa pombe kwa kuamini labda ingemsaidia kupunguza mawazo, ni kweli alisahau lakini pombe ilipomalizika kichwani, akaanza kukumbuka kila kitu tena na tena.
Kila alipokuwa akimwangalia mtoto wake, Edward aliyaona mapenzi yake mbele yake, alikuwa tayari kufanywa lolote lile lakini si kuona akimpoteza mtu huyo, moyoni mwake alijisikia faraja kubwa na muda mwingine alimkumbatia na kumbusu.
Hiyo ndiyo ilikuwa faraja yake, furaha na tumaini lake kubwa, hakutaka kuona akimuua na ndiyo maana alikuwa tayari kwa kila kitu.


Je, nini kitaendelea?

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 
NYEMO CHILONGANI
UCHAWI WA BILIONEA BAZOKA
0718069269

SEHEMU YA 32.

Maganza alikuwa ofisini kwake huku akiendelea na mambo yake kama kawaida, alikuwa bize, kwa siku hiyo alitaka kuifuatilia kesi ya Yusufu na Bi. Semeni kwa kuamini labda kuna kitu angekipata ambacho kingempa picha kamili.
Alisumbuka sana na kukata tamaa, tayari aliona kulikuwa na jambo kubwa mbele yake, inawezekana alikuwa akipambana na watu ambao hakuwa na nguvu ya kupambana nao. Tena kila alipomfikiria Bazoka, hakika alichanganyikiwa kabisa.
Yaani hakuamini kama mwanaume huyo ndiye aliyekuwa akimsumbua namna hiyo, aliamini kulikuwa na jambo lililokuwa likiendelea lakini hakulijua, ni kama kichwa chake kilifungwa kulifahamu jambo hilo, sasa akabaki akiwa hajui nini cha kufanya.
Kulikuwa na mambo kadhaa ambayo yalimchanganya. La kwanza lilikuwa lile la gari kutokuonekana kwenye mkanda wa video uliokuwa umechukuliwa, la pili ni majeraha ya makucha yaliyokutwa kwenye mwili wa Bi. Semeni, na la mwisho ni kwa namna ambavyo hakupafahamu alipokuwa akiishi Bazoka na wakati alikwenda huko siku chache zilizopita.
Hayo yote yalimchanganya na kumfanya sasa kuhisi kulikuwa na nguvu fulani aliyokuwa akipambana nayo, na haikuwa kawaida hata kidogo. Alitulia huku akifikiria mengi mara akasikia mlango ukigongwa, alipomkaribisha mgongaji, alikuwa kijana wake kwenye kazi ambaye alimwambia kuna mwanaume alifika mahali hapo, alihitaji kuzungumza naye.
Alikuwa bize sana, hakutaka kuonana na mtu huyo, kama alikuwa na jambo la lazima basi azungumze naye yeye lakini si kumwambia aingie humo na kwani kulikuwa na mambo mengi aliyotakiwa kufanya.
“Nisaidie kuzungumza naye, sina muda,” alimwambia.
“Haina shida.”
Kijana yule akatoka na kurudi alipotoka, Maganza alikuwa akiendelea na kazi zake na baada kama ya dakika mbili, mlango ukagongwa na aliporuhusu mgongaji kuingia, alikuwa kijana yuleyule.
“Vipi tena?” alimuuliza.
“Amekataa kuzungumza nami!”
“Kwa sababu gani?”
“Ameniuliza wewe si ndiye unayetaka kufahamu ukweli kuhusu Bazoka?” alimwambia jinsi alivyoambiwa.
Alipolisikia jina hilo ni kama moyo wake ukapiga paa! Alikuwa ofisini humo akifikiria mambo mengi lakini kubwa zaidi lilikuwa la huyo Bazoka, ni kama alihisi kulikuwa na jambo lililokuwa likiendelea, huku akiwa hajamaliza, kukatokea mtu ambaye alionekana kama kufahamu mambo kadhaa kuhusu huyo mtu.
Akashikwa na hamu ya kutaka kumsikiliza, akamwambia kijana wake akamuite, aingie na kuzungumza naye kitu ambacho haikuwa tatizo hata kidogo, akamuita na baada ya dakika moja, mwanaume mtu mzima akaanza kuingia ndani ya ofisi hiyo.
Alimwangalia, alionekana kuwa na miaka kuanzia sitini, alikuwa mtu mzima kabisa, ndevu zake zilikuwa na mvi kwa mbali, akamkaribisha kwa heshima, alisimama kabisa na kumpa mkono.
“Karibu sana,” alimkaribisha.
“Nashukuru sana!”
Mzee huyo akakaa kwenye kiti ofisini mule, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuangalia mandhari ya ofisi ile, ilivutia machoni mwake, ilimfanya kuwa na tabasamu pana.
“Yaani nilikuwa nasikia joto, nilipoingia humu ofisini kwenu, yaani hali imebadilika, ninatamani mpaka nilale humuhumu,” alisema mzee huyo huku akionekana kuwa na furaha.
“Dar es Salaam ina joto sana, ni kama tunaishi kwenye tanuru,” alimwambia.
“Yaani acha tu! Poleni na kazi za kulinda raia na mali zao,” alimwambia.
“Usijali! Nashukuru sana. Ni wajibu wetu pia,” alimwambia.
Walikaa na kuzungumza mawili matatu na ndipo mzee huyo akaanza kumwambia kuhusu Bazoka. Kwanza kitu cha kwanza alichotaka kujua ni kama alimfahamu mwanaume huyo vizuri ama la. Alimwambia hakuwa akimfahamu japokuwa kulikuwa na mambo yaliyokuwa yakimtia hofu.
“Mambo gani?” alimuuliza.
“Mambo kadhaa tu! Wewe unafahamu nini kuhusu Bazoka?” alimuuliza.
“Maisha yake kwa ujumla. Tangu alipokuwa masikini mpaka alipopata utajiri wake,” alimwambia.
“Ooh! Inaonekana ni marafiki sana!”
“Hapana! Sisi si marafiki, na hatukuwahi kuwa marafiki, endapo ningekuwa rafiki yake nisingekuja hapa kwa lengo la kumchoma,” alimwambia.
“Kumchoma? Una maana gani?”
“Bazoka ni mchawi!” alimwambia.
Maganza akakaa kimya kwanza, alimwangalia mzee huyo na kile alichomwambia. Ishu ya kuwa mchawi kwake halikuwa tatizo, alichotaka kujua ni yale maswali ambayo mpaka muda huo hakuwa na majibu nayo.
Uchawi wa Bazoka haukumuhusu, angejuana yeye na Mungu wake ila kitu pekee alichokuwa akihitaji ni kuhusu hayo yote yaliyotokea, baada ya kumwambia hivyo, mzee huyo akaanza kufunguka.
Alimwambia kila kitu, tangu siku ya kwanza Bazoka alipokutana na Sultani, alivyokubaliana naye na hatimaye kwenda kuonana na Bonge na hatimaye watatu hao kuwa kitu kimoja.
Alisimulia mpaka walivyoungana na kuhakikisha mwanaume huyo anakuwa tajiri mkubwa, baada ya hapo akamwambia kuhusu mambo ya kafara, jinsi alivyopewa masharti na mtu wa kwanza kwenda kumuua akiwa Yusufu.
Alimwambia hayo yote mpaka kwa Bi. Semeni. Mud wote huo Maganza alikuwa kimya tu, kile alichokuwa akikisikia kiliusisimua mwili wake, hakuamini kama kulikuwa na watu waliokuwa wakiishi maisha ya kutoana kafara namna hiyo.
Kwake, hizo ziliwahi kusikika kama stori tu kwamba kulikuwa na mtu fulani alikuwa na utajiri wa kichawi lakini hakuwahi kuwa na uhakika hata siku moja, leo hii mzee huyo alikuwa akimwambia kila kitu kuhusu Bazoka.
“Umesema ana kidonda kikubwa?” alimwambia.
“Ndiyo! Kipo mguuni. Kile kidonda ndiyo utajiri wake mkubwa, yaani kadiri kinavyoendelea kuuma ndivyo utajiri wake unavyozidi kuongezeka,” alimjibu.
“Mh!”
“Dunia ina mambo sana. Utashangaa mpaka kiama,” alimwambia.
“Kuna maswali mengi nilikuwa najiuliza kuhusu huyu Bazoka, na maswali yangu yoote umenipa majibu,” alimwambia.
“Na ndiyo maana nimekuja kwako, nikupe majibu!” alimwambia.
“Pamoja na kunipa majibu, pia umeniongezea swali jingine.”
“Lipi?”
“Wewe umeyajuaje haya? Umejuaje kuhusu ishu ya kidonda cha Bazoka, namna jitu la ajabu lilivyopambana na fisi ambapo mmoja alikuwa ni Bi. Semeni, jinsi mwanamke aitwaye kwa jina la Shunie alipokwenda kumuua Bonge na Sultani, yaani wewe umejuaje haya yote?” alimuuliza huku akimwangalia.
“Ni vigumu kuniamini!”
“Na uliniambia wewe sio rafiki yake. Yaani inamaanisha Bazoka alikwambia ama?” alimuuliza.
“Hapana!”
“Sasa wewe umejuaje?” alimuuliza kwa mshangao.
“Ninajua mambo ambayo watu wengine hawayajui!” alimwambia.
“Ila ni ya ndani sana!”
“Najua! Ila ndiyo nayajua, ama unataka mpaka nikwambie mambo yako pia?”
“Kwani kuna yangu unayajua?”
“Ndiyo! Hata usiponiambia, ninayajua yote, kwa kifupi kwangu hakuna siri,” alimwambia.
“Unanichanganya!”
“Mkeo alikuwa na mimba, ikaharibika, iliharibika kwa sababu hukutaka azae, ugomvi wenu mkubwa ni kupata mtoto wa pili, yule mmoja aliona hatoshi ila wewe ukawa unakataa kila siku kuongeza mtoto wa pili,” alimwambia na kuendelea:
“Wakati mkeo akiwa ameshika mimba, siku moja ulichukua dawa iitwayo Phlemotypheric ambayo hutumiwa kuchoropoa mimba, ukainunua kisiri huku dawa hiyo ikiwa hairuhusiwi kuuzwa, ukamuwekea mkeo kwenye juisi, akanywa na kesho mimba ikatoka. Kweli si kweli?” alisema na kumuuliza.
Kimyaaaaaa.
“Hadija amekwambia ana mimba, si mimba yako, ni mimba ya mwanaume aitwaye Maliki. Ameamua kukupa wewe mimba hiyo kwa sababu una uwezo, unaweza kumuhudumia. Suala la mimba ni siri yenu wawili lakini nimekuwa nikifahamu sana. Kwa kukusaidia, ile mimba si yako, ni mimba ya mwanaume mwingine kabisa, hivyo kuwa makini,” alimwambia, Maganza akashangaa zaidi.
“Pesa ulizoingiziwa mwaka jana kwenye akaunti yako kiasi cha shilingi milioni mia moja na hamsini si pesa halali, hakikisha unazirudisha vinginevyo zitakutokea puani. Wenzako waliziita zawadi, ila kiukweli ni rushwa, una nafasi ya kuzirudisha vinginevyo kuna mambo mengi mabaya yatatokea,” alimwambia.
Maganza akawa amekodoa macho tu.
“Mpaka hapa huamini ninachokwambia kuhusu Bazoka? Kama nimejua mambo yako ambayo kila siku umeamini ni siri, vipi kuhusu haya ninayokwambia?” alisema na kumuuliza.
Maganza akabaki kimya, alikuwa mpole kama mtu aliyelowanishwa na maji, kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka, hakuamini yale aliyokuwa ameambiwa na mzee huyo.
Yalikuwa mambo ya siri sana, aliamini hapakuwa na mtu yeyote aliyekuwa akiyafahamu lakini kitu cha ajabu kabisa, mwanaume huyo alikuwa akiyafahamu kila kitu.
Alitulia, alishindwa kujua ni kitu gani alitakiwa kuzungumza mbele ya mwanaume huyo. Tayari alianza kumuogopa, akaanza kuhisi hakuwa mtu wa kawaida hata kidogo, inawezekana hakuwa mtu kutokana na yale aliyomwambia.
Suala la mchepuko wake, Hadija lilimuingia kichwani mwake na kumuumiza mno. Ni kweli alikuwa na mchepuko, ulipata mimba na kumwambia, alikubaliana nao lakini leo hii aliambiwa hiyo mimba haikuwa yake, ilikuwa na jamaa aliyeitwa kwa jina la Maliki.
Kama alitakiwa kumwamini mzee huyo kuhusu Bazoka, pia alitakiwa kumwamini kuhusu huo mchepuko wake. Alimwambia hayo yote lakini pia kukawa na swali jingine lililoibuka, kwa nini aliamua kumwambia hayo?
“Ni kwa sababu unatakiwa kujua mtu unayemfuatilia ni wa aina gani,” alimwambia.
Hilo lilimshangaza sana Maganza. Swali alilokuwa amejiuliza, alijiuliza moyoni mwake lakini kitu cha ajabu kabisa, mwanaume huyo alimjibu kana kwamba alimuuliza kwa sauti.
“Who the hell are you?” (Wewe ni nani?) alimuuliza.
“Huwezi kunijua. Chukua hiki kijiti, kiweke mfuko, nenda nyumbani kwa Bazoka kesho. Utapakumbuka nyumbani kwake, utakachokutana nacho huko usishangae. Hakikisha unakwenda jioni,” alimwambia na kuinuka huku akiwa amekiweka hicho kijiti mezani.
Mzee huyo akaanza kusogea na kuufikia mlango, akaufungua na kutoka Haraka sana Maganza akataka kumfuatilia, naye akaufungua mlango na kutoka, mzee yule hakuonekana.
Alishangaa mno, hakuamini kilichotokea. Mzee huyo alitoka ofisini kwake ndani ya sekunde thelathini tu, na kwa jinsi alivyokuwa akitembea taratibu, asingeweza kutoweka machoni mwake ni lazima angemuona, cha ajabu hakuwa akionekana.
Akaelekea mpaka nje, hakumuona mzee huyo, hilo lilimchanganya sana. Aliwahi kuyaona mauzauza mengi lakini hayo ya siku hiyo yalikuwa kiboko, yaani yalimvuruga kupita kawaida.
Akabaki akijiuliza huyo mzee alikuwa mganga, jini ama mchawi wa kawaida? Kila alichojiuliza akakosa jibu. Haraka sana akarudi ofisini kwake na kutulia, akakichukua kijiti kile na kuanza kukiangalia.
Aliambiwa akichukue na kukiweka mfukoni, angepakumbuka nyumbani kwa Bazoka, amfuate na kuambiwa hakutakiwa kushangazwa na hali ambayo angekutana nayo huko.
Hali gani hiyo?
Napo hakupata jibu.
“Nitakwenda huko. Au nimpigie simu? Hapana! Acha niende nikajionee mwenyewe,” alijiuliza na kujijibu.

Je, nini kitaendelea?

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 
NYEMO CHILONGANI
UCHAWI WA BILIONEA BAZOKA
0718069269

Sehemu ya 33

“Mpigieni simu bosi!” ilisikika sauti ya mwanaume fulani.
“Ndiyo nimejaribu lakini namba yake haipatikani! Jamani jamani! Mmeondoa vitu vilivyosalia?” alisikika mwanaume mwingine.
“Imeshindikana! Tumeshindwa kuondoka kitu chochote kile, yaani moto ulivyoanza kuwaka, sijui milango ikajiloki, yaani haikufunguka kabisa,” alijibu mwanaume wa kwanza.
“Na watu wa zimamoto vipi?”
“Nao wamesema wanakuja, ila cha ajabu mpaka sasa hivi hawajafika,” alijibu.
Kiwanda cha kutengeneza mifuko ya nailoni kilichokuwa kikimilikiwa na Bazoka kilikuwa kikiteketea kwa moto, kila mfanyakazi aliyekuwa ndani ya jengo hilo kubwa akakimbia kuyaokoa maisha yake.
Kila kitu kilichokuwa ndani ya jengo hilo kiliteketea na kitu cha ajabu mpaka magari ya kampuni hiyo yaliyokuwa sehemu ya maegesho nayo yaliteketea kwa moto. Kila mmoja alishangaa, haikuwa kawaida kutokea kwa kitu kama hicho.
Ingekuwa rahisi sana kuokoa kila kitu lakini ilishindikana kabisa, watu walichanganyikiwa na kwa kipindi hicho walikuwa wakipambana kumpigia simu bosi wao, naye hakuwa akipatikana.
Gari la zimamoto lilikuwa njiani kufika mahali hapo, hapakuwa mbali sana na kampuni hiyo ilipokuwa. Ilikuwa maeneo ya Mwenge na gari hilo lilikuwa hapo Fire lakini kutoka hapo mpaka kufika huko Mwenge, kwa siku hiyo hali ilionekana kuwa tofauti kabisa.
Njiani kulikuwa na foleni kubwa, walipata shida sana mpaka kufika huko, walitumia muda wa dakika arobaini na tano, walijitahidi kupiga honi lakini magari mengine kupisha yalikuwa taratibu.
Walipofika hapo, haraka sana wakaunganisha mipira yao kwa lengo la kuzima moto huo, cha ajabu sasa, maji hayakuwepo.
Ndiyo hayakuwepo!
Walishangaa, waliondoka wakiwa na maji ya kutosha, walihakikisha kabla ya kuondoka lakini cha ajabu baada ya kufika hapo, hawakuona maji yoyote yale. Ikawabidi waende nyuma ya gari kuangalia inawezekana yalikuwa yamemwagika lakini napo hapakuwa na tundu lolote lile kwenye tanki, sasa kama maji hayakuwepo, yalikuwa wapi?
“Sasa mmekujaje bila maji?” aliuliza mwanaume mmoja.
“Tulikuwa na maji, tena tulijaza kabisa kabla ya kuondoka,” alijibu mfanyakazi mmoja wa zimamoto.
“Sasa mbona hamna maji?”
“Ndiyo tunashangaa!”
“Isije kuwa mlijaza kwenye gari jingine!”
“Hapana! Tulijaza kwenye gari hili na magari mengine!”
“Sasa maji hakuna, mnasemaje mlijaza?” aliuliza.
Hawakuwa na majibu sahihi ya kujibu mahali hapo, walishuhudia jengo la kampuni hiyo likiteketea moto na kumalizwa kabisa, baada ya moto kumaliza kila kitu na kujizima, ndipo Bazoka akaanza kupatikana kwenye simu.
Meneja alimwambia kilichotokea, haraka sana Bazoka akaondoka nyumbani kwake na kuelekea huko, njiani alionekana kuchanganyikiwa. Alikuwa na kampuni kama tatu lakini hiyo ndiyo ambayo ilikuwa mama, yaani hizo nyingine ziliitegemea hiyo, hazikuweza kujisimamia zenyewe.
Wakati mwingine alihisi kama alikuwa akiota ama kudanganywa, lilikuwa jambo lisilowezekana kabisa kwa kiwanda chake kuteketezwa kwa moto halafu watu wasichukue hatua yoyote ile.
Alitumia dakika kadhaa akafika mahali hapo, akalipaki gari lake na kuteremka, macho yake yalikuwa kwenye mabaki ya kiwanda chake, ilikuwa ni picha ya kutisha machoni mwake, hakuamini kama aliipoteza kiwanda hicho, na kwa maneno ya meneja alimwambia hapakuwa na kitu chochote kile kilichobaki, yaani kila kitu kiliteketezwa kwa moto.
“Ilikuwaje?” aliuliza huku akilengwa na machozi.
“Umeme ulipiga shoti!” alijibu meneja.
“Hata zimamoto hawakuwahi kuja kuzima moto?” aliuliza.
“Waliwahi!”
“Sasa kwa nini hawakuuzima?”
“Hawakuwa na maji!”
“Ilikuwaje?”
“Yaani hebu acha nimuite.”
Jamaa wa zimamoto akaitwa na kumsogelea Bazoka aliyeonekana kuwa kwenye hali ya majonzi tele, akaanza kumuuliza kilichotokea, sababu iliyowafanya kuchelewa na jamaa huyo kumwambia kila kitu.
Bazoka aliposikia maelezo yake tu kwamba waliondoka wakiwa na maji lakini baada ya kufika hapo hawakuwa na maji, tayari akahisi kulikuwa na kitu kilichotokea.
Watu hao walitaka kupambana na nguvu za giza, akagundua hata huo umeme ambao aliambiwa ulipiga shoti, ni kwamba kulikuwa na kitu tu kilichotokea, nguvu za giza zilikuwa na nguvu mno.
Akaamua kwenda pembeni na kutulia, alisimama huku akiyaangalia mabaki ya kiwanda chake. Alikuwa na majonzi tele lakini moyo wake ulimwambia hata kama kingetokea kitu gani, asingeweza kutoa kafara tena maishani mwake.
“Siwezi kutoa kafara!” alijisemea, akaanza kutabasamu.
Akiwa hapo akahisi miguu yake ikikosa nguvu, akasema achuchumae au kukaa na alipofanya hivyo, akashangaa mwili ukianguka na kulala, alitamani kuinuka lakini alishindwa, viungo vyake vyote vikakosa mawasiliano.
Hakujua kilichokuwa kikiendelea lakini akakumbuka maneno ya yule jini aliyomwambia kuna siku angepooza, hapo akapata picha sasa alikuwa akianza kuitumikia adhabu hiyo.
Moyo wake ulimuuma mno, alitulia pale na kumuita meneja. Haraka sana akawahi, alishangaa, bosi wake kulala pale halikuwa jambo la kawaida, je, alichanganyikiwa na kupoteza nguvu ama ilikuwaje?
“Bosi! Kuna nini?” aliuliza.
“Nibebeni mnipeleke hospitali!” alisema.
Vijana watatu wakamsogelea na kumbeba, wakaanza kuondoka naye kuelekea hospitalini. Njiani kila mmoja alishangaa, hawakujua kilichokuwa kimetokea mpaka mwanaume huyo kuanguka na kushindwa kuinuka.
Mawazo yao yaliwaambia Bazoka alichanganyikiwa, akapata mshtuko na kuanguka chini, yaani alichanganyikiwa baada ya kuona amepoteza kila kitu.
Hawakuchukua dakika nyingi wakafika hospitalini, akalazwa kwenye machela na kuanza kuisukuma kuelekea ndani. Kila nesi aliyemuona, alimfahamu mwanaume huyo, alikuwa Bazoka, yule bilionea aliyekuwa na roho nzuri kama malaika.
Akapelekwa mpaka ndani ya chumba kimoja na madaktari kuanza kumpa huduma. Bazoka alijua madaktari hao walikuwa wakijisumbua kwa kuwa hawakujua sababu ya yeye kupooza mwili kiasi hicho, alichohitaji ni kupigiwa simu kwa mkewe, ikafanywa hivyo na baada ya dakika Asha kufika hospitalini hapo.
Alipomwangalia mume wake kitandani pale aliumia mno, alimuuliza kilichotokea, akaambiwa mumewe alipata mshtuko baada ya kukuta kiwanda chake cha kutengeneza mifuko ya nailoni kikiteketezwa kwa moto, hivyo akaanguka na kupooza.
Asha alilia sana, alimwangalia mume wake kwa huzuni kubwa, hakuamini kama alikuwa akipitia kipindi kigumu kama hicho. Bazoka alitulia na kumwangalia mkewe, alichomwambia ni kwamba hakutakiwa kuwa na hofu kwani kila kitu kingekuwa sawa kabisa.
“Nitapona tu mke wangu,” alimwambia huku akimwangalia.
“Pole sana mume wangu! Nitakuombea kwa Mungu akuponye,” alisema mke wake.
Baada ya saa moja, tayari kila mtu alijua kilichotokea. Bazoka alikuwa jina kubwa kwa kipindi hicho, kitendo cha kuambiwa alipooza baada ya kuona kiwanda chake kikiteketea kwa moto hakika iliwafanya watu wengi kumuonea huruma.
Walihuzunika na wengine kutamani hata hali hiyo ingewakuta wao na si Bazoka, huyo alikuwa mtu wa watu, kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakiendesha maisha yao kupitia yeye, hivyo endapo angekufa basi kungekuwa na familia nyingi ambazo zingeteseka.
“Mi’ nipo tayari kuchukua maumivu ya Bazoka lakini yeye apone,” alisema jamaa mmoja, kwa kumwangalia usoni tu ilikuwa rahisi kusema alikuwa na maumivu makali moyoni mwake.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa maisha ya Bazoka kitandani, hakuweza kusimama tena, shughuli zake alikuwa akizifanya mke wake, yeye ndiye aliyekuwa akifuatilia kila kitu kwenye biashara hiyo, ndiyo ambaye aliajiri watu na kufuatilia mpaka mauzo.
Bazoka akawa mtu wa kitandani tu, pale alipokuwa alijuta kwa kuutafuta utajiri ule ambao sasa ulikuwa ukimletea matatizo makubwa, ila pamoja na hayo, moyo wake ulikuwa ukimsifu kwa kukataa kutoa kafara kama alivyokuwa ameambiwa.
Marafiki zake, ndugu na watu wengine walikuwa wakifika nyumbani hapo na kumuona, kila aliyemwangalia, alimuonea huruma, huyu Bazoka wa sasa hivi alikwisha, alikuwa akipungua kitandani pale, alitoa harufu kutokana na kuwa na uchafu mwingi mwilini mwake.
Wafanyakazi walifanya kazi yao lakini mtu aliyekuwa karibu naye zaidi alikuwa mke wake, yeye ndiye aliyebadilisha ndoo ya haja, kumlisha na mambo mengine, wafanyakazi walihusika kwenye usafi tu.
Kwa kuwa muda mwingi alikuwa akilala, mgongo wake ukaanza kuharibika kwa sababu ya joto, mpaka Asha anaambiwa awe anamgeuza mara kwa mara tayari mgongo ulianza kuharibika.
Hilo likamtia huzuni mno, alikuwa akihuzunika lakini kila alipokuwa akimwangalia mume wake, alionekana kawaida tu, yaani hakuwa na huzuni hata kidogo, alikuwa akicheka na hata kutaniana na watu wengine.
Alishangaa! Haikuwa kawaida, hakuamini kama yeye mtu mzima alikuwa na huzuni kuliko hata mgonjwa mwenyewe, kila alipokuwa akimuuliza sababu ya kuwa hivyo, Bazoka hakujibu zaidi ya kumwambia pesa na umaarufu vilikuwa vitu vya kupita tu.
Wakati Bazoka alipokuwa peke yake ndani ya chumba chake, jini lilelile lililokuwa na muonekano wake lilikuwa likimtokea na kuzungumza naye, lilikuwa likimdhihaki kwa kila kitu kilichotokea.
“Jiangalie ulivyo! Umekuwa Bazoka asiyeogopwa tena, na maisha yako yatakuwa kitandani mpaka kifo chako. Ni ujinga wako ndiyo umekufanya kuwa na maisha haya,” lilisema lile jini huku likiwa limesimama karibu naye.
“Kuna kitu gani ambacho masikini anapitia lakini tajiri hapitii?” aliuliza Bazoka huku uso wake ukiwa na tabasamu pana.
“Unajifariji kwa maneno yako tu. Wewe ni wa kufa tu, tena kifo kilichokuwa na maumivu makali mno,” alimwambia.
“Siwezi kusikia maumivu, mwili umepooza, maumivu hayo nitayasikiaje? Mnafanya mambo bila kutumia akili kabisa,” alisema Bazoka, sasa akaongeza tabasamu lake.
Jini lile likaonekana kukasirika, likamsogelea Bazoka zaidi na kumgusa kwenye kidole gumba cha mguuni mwake, baada ya kufanya hivyo, akaanza kusikia maumivu makali mgongoni mwake.
Yalikuwa ni makali mno, alitamani kulia lakini akaona kama angefanya hivyo ungekuwa ushindi mkubwa kwa jini lile kwani alitakiwa kujifanya hakuwa akijisikia maumivu yoyote yale.
“Kuna matajiri wanateseka vitandani zaidi yangu, pesa zao zimeshindwa kuwaokoa, unafikiri kuna jipya la mimi kuteseka kitandani?” alisema Bazoka na kuuliza swali, jini lile likabaki kimya.
Wakawa wanaangaliana, huyu Bazoka alionekana kuwa kiburi, jeuri, aliyetia hasira. Jini lile likapopotea baada ya kuisikia sauti ya Asha sebuleni, likaondoka zake na kumuacha Bazoka chumbani humo.
Alitulia na kuanza kuugulia maumivu makali, japokuwa alipooza lakini yale maumivu yalianza kujisiwa mwilini mwake baada ya kushikwa kidole na jini lile.
“Unajisikiaje?” aliuliza Asha.
“Maumivu tu! Ila usijali mke wangu. Kila binadamu lazima afe,” alimwambia mke wake.
“Usiseme hivyo mume wangu, unaniumiza sana,” alimwambia.
“Mke wangu! Acha nife, inawezekana niliishi maisha ya giza ambayo kila mtu hakuwa akiyajua,” alimwambia.
“Unamaanisha nin?”
Bazoka alijua dhahiri asingeweza kupona kwa kuwa lengo la kwanza la jini lile alilokuwa amemwambia lilikuwa ni kumuua kwa maumivu makali, hivyo hakuwa na jinsi kumwambia mkewe kila kitu kilichotokea.
Hakuwa na siri tena, ilikuwa ni lazima amwambie kwa kuwa tayari mambo yalionekana kuanza kuharibika. Akaanza kumuhadithia kila kitu.

Je, nini kitaendelea?
Bazoka atakufa?
Tukutane Alhamisi hapahapa.

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom