Hadithi: Uchawi wa bilionea Bazoka

NYEMO CHILONGANI
UCHAWI WA BILIONEA BAZOKA
0718069269
SEHEMU YA 21.

Naye akauparamia na kutokea upande wa pili, akaanza kuondoka kuelekea mbele, alihitaji kujua mahali mtu huyo alipokwenda. Alitembea mpaka alipofika sehemu iliyokuwa na njiapanda, akasimama na kuangalia kila upande.
Aliangalia kila kitu alichotaka kuangalia na baada ya kumaliza, akaondoka zake urudi ofisini. Alichanganyikiwa, kilichomchanganya zaidi ni zile alama ambazo zilionekana ubavuni mwa Bi. Semeni, nini kilitokea mpaka kuzipata alama hizo?
Akafikisha taarifa ofisini, bosi wake, Kamanda Masumbuko naye alishangaa, hizo alama alizokuwa amezipata na mazingira ya kujeruhiwa na kisu vilikuwa vitu viwili tofauti kabisa.
Maganza alitulia ofisini kwake, hakuwa sawa, ilikuwa ni lazima kuhakikisha muuaji anampata na kumfikisha mbele ya sheria. Akiwa hapo, akili yake ikaanza kudadavua vitu, mtu kama mpelelezi akili yake ilitakiwa kuwa sawa kila wakati.
Hapo ndipo akakumbuka aliambiwa wapangaji waliogopa kupanga kwa sababu ya ushirikina wake lakini mara ya mwisho kuna kijana alipanga humo, naye yakamkuta yaliyomkuta na kuondoka zake.
Alihitaji kuanza upelelezi wake kwa kuanzia na kijana huyo, alihisi kabisa inawezekana kulikuwa na kitu alichokuwa amekiona, labda kuwa na maadui ama mtu aliyekuwa akiwasiliana naye sana.
Haraka sana akasimama kutoka kitini na kuondoka ofisini hapo, alimwambia Kamanda Masumbuko kwamba kulikuwa na kitu alichokifikiria na hivyo angekwenda na majibu yake haraka sana.
Akaondoka na kuelekea huko Magomeni, alipofika, akaanza kuulizia kuhusu mpangaji huyo na watu walimwambia hakuwa amezoeana na mtu yeyote zaidi ya kijana Frank aliyekuwa akiishi jirani naye.
Akataka kuonana na huyo Frank, kweli akakutana naye na kuanza kuzungumza. Alimuuliza kuhusu huyo mpangaji, alichokuwa akihitaji ni kuonana naye na kuzungumza mambo mengi ambayo sasa alihisi ndiyo ungekuwa mwanzo wa kupata alichokuwa akikihitaji.
“Jamaa alihama,” alimwambia.
“Naye alirogwa na kukimbia kama wapangaji wengine?” aliuliza.
“Hamna! Kwa huyu jamaa ilikuwa ni tofauti kabisa!” alimjibu, kidogo Maganza akajiweka vizuri kitini.
“Ilikuwaje?”
“Alifukuzwa!”
“Na nani?”
“Marehemu Bi. Semeni!” alimjibu.
“Ilikuwaje akamfukuza?”
“Sijajua! Ila nahisi jamaa alikuwa mchawi zaidi yake!” alimjibu.
“Mh! Nyie si mnasema huyu bibi alishindikana, sasa ilikuwaje mpaka apate mpinzani wake?”
“Mambo haya yanatofautiana kaka! Kuna wenye cheti cha kidato cha nne, wengine cha sita, wengine wana diploma na wengine digrii,” alijibu Frank na wote kuanza kucheka.
“Huyo jamaa una namba yake ya simu?”
“Ninayo!” alijibu na kuchukua simu yake, akatafuta jina la mtu aliyeambiwa na kumpa.
“Mara yako ya mwisho kuonana naye ilikuwa lini?” aliuliza Maganza.
“Majuzi tu alivyohama!”
“Na nitampataje?”
“Nina namba yake.”
“Naiomba.”
Frank akampa Maganza namba ya Bazoka na kumpigia simu, akaanza kuongea naye na kuomba kuonana kwani kulikuwa na jambo alitaka kuzungumza naye.
Hilo halikuwa tatizo kwa Bazoka, akamwambia aelekee katika kituo cha polisi na kuelekea huko, alipofika, akaomba kuonana naye na kupelekwa ofisini kwake.
Moyo wake ulikuwa na hofu na kitu alichokuwa akikifikiria ni lile tukio la mauaji alilolifanya kwa Bi. Semeni, hakuamini kama kungekuwa na mtu ambaye angegundua kwamba yeye ndiye aliyemuua Yusufu kutokana na mazingira aliyomchukua kutokumshtukiza mtu yeyote yule.
Akatulia! Kabla ya kuanza kumuuliza kitu chochote kile akatulia kwenye kiti chake, alikuwa akimwangalia Bazoka kana kwamba aliwahi kumuona mahali fulani lakini pia alikuwa akifanya hivyo kwa kuwa alihitaji kumsoma kabla ya kuanza kuzungumza naye.
“Kwa nini ulihama kwa Bi. Semeni?” aliuliza Maganza huku akimwangalia.
“Nilihama kwa sababu alinifukuza!” alimjibu.
“Kwa nini alikufukuza?”
“Hata sababu siijui kwa kweli. Nililala, nilipoamka akaniambia nichukue kila kilicho changu niondoke,” alimjibu.
“Kuna tetese zilisema kwamba mwanamke yule alikuwa mchawi, ulilifahamu hilo?” aliuliza Maganza.
“Niliambiwa lakini sikuwahi kuthibitisha!”
“Na ulipokuwa ukiishi kwake hukuwahi kupata vitisho?”
“Vipi?”
“Vya kichawi!”
“Kwa kweli sikuwahi!”
“Bi. Semeni aliwahi kuwa na maadui?”
“Sijui kwa kweli!”
“Kuna mtu alikwishawahi kuingia nyumbani kwake katika kipindi chote ulichokuwa ukiishi pale?” alimuuliza.
“Yaani hilo ndilo lililokuwa likiniumiza kichwa!”
“Kivipi?”
“Ile nyumba hapakuwahi kuingiwa na mgeni yeyote yule,” alimjibu.
“Kwa nini?”
“Hata mimi sifahamu!”
“Sasa na kwa nini na wewe hukupeleka wageni?”
“Sasa kama mwenyeji haleti wageni, mimi nitaletaje wageni?” aliuliza na kuanza kucheka.
“Na unahisi marehemu aliwahi kuwa na maadui?”
“Marehemu gani?”
“Bi. Semeni!”
“Bi. Semeni! Amekufa? Amekufa lini? Imekuwaje? Mbona sina taarifa!”
“Niyo nimekupa. Ameuawa chumbani kwake!”
“Ameuawa? Bi. Semeni ameuawa?”
“Ndiyo!”
“Na nani? Nani alithubutu kuingia ndani kwake?”
“Kwa nini watu washindwe sasa!”
“Si nasikia mchawi sana!”
“Ila hapo kabla umeniambia huku ukifahamu kama Bi. Semeni alikuwa mchawi, sasa hivi unaniambia ulisikia kwamba ni mchawi, niamini lipi?” aliuliza Maganza, kidogo Bazoka akagundua alifanya kosa.
“Labda hukunielewa mkuu!”
“Kukuelewa lipi?”
“Uliniuliza kama nilishawahi kupata vitisho vya kichawi, nikakujibu sikuwahi ila sikukwambia kwamba Bi. Sehemu hakuwa mchawi,” alisema Bazoka, ikambidi kwanza Maganza atulie kidogo, akagundua mtu aliyekuwa akizungumza naye hakuwa wa kawaida kwenye kujibu maswali.
“Umeoa?”
“Ndiyo!”
“Unaishi wapi?”
“Kijitonyama!”
“Peke yako ama na familia yako?”
“Na familia yangu!”
“Sawa! Nashukuru kwa muda wako!”
Baada ya kuzungumza naye, akamruhusu Bazoka kuondoka ofisini hapo na yeye kubaki huku akijifikiria ni kitu gani alitakiwa kufanya.
Akaanza kuyapitia majibu ya Bazoka, kwa jinsi alivyojua lingekuwa jambo gumu sana kwa kumfahamu mtu ambaye alifanya mauaji kwa Bi. Semeni.
Alizungumza na Bazoka lakini majibu yake yalionyesha kama alishtushwa na kifo cha Bi. Semeni. Kwa taarifa za majirani zilisema ilikuwa ni vigumu kwa watu wengine kuingia ndani ya nyumba hiyo, sasa ilikuwaje mpaka muuaji aingie humo na kumuua mwanamke huyo.
Huku akiwa anafikiria hilo, ghafla akapata mawazo juu ya mambo fulani aliyowahi kumuuliza Bazoka, haraka sana akachukua simu yake na kuanza kulitafuta jina la Frank, alipolipata, akampigia kwani alitaka kuzungumza naye.
“Frank...” alimuita hata kabla ya salamu.
“Niambie mkuu!”
“Bazoka alikuwa akiishi na nani hapo kwa Bi. Semeni?” aliuliza.
“Wawili tu, yeye na Bi. Semeni.”
“Hakuwahi kuishi na mkewe?”
“Hapana! Sikuwahi kumuona!”
“Sawa.”
Akakata simu. Moyo wake ukaanza kuwa na shauku na huyo Bazoka, akahisi kabisa kulikuwa na kitu kilichokuwa kimetokea, ilikuwa ni lazima kumpeleleza huyo Bazoka kwa sababu kulikuwa na kila dalili za kuhusika na mauaji hayo.
Kwa nini?
Aliambiwa kwamba Bazoka alipanga chumba kwa Bi. Semeni, alikuwa akiishi hapo lakini alipomuuliza alipokuwa akiishi, alimjibu kwamba ni Kijitonyama, na familia yake.
Kama alikuwa akiishi Kijitonyama na familia yake, kwa nini alikwenda kupanga kwa Bi. Semeni? Kama alifanya hivyo huku familia yake ikiwa haipo jijini Dar, yaani kabla ya kwenda kuishi huko Kijitonyama, pia alihitaji kufahamu hilo.
Kitu cha kwanza kabisa alichokifikiria ni kuwasiliana na Bazoka na kumwambia anamuhitaji aende ofisini kwake, ila baada ya kufika hapo na kuzungumza naye kwa dakika chache, amruhusu aondoke lakini alitakiwa kumfuatilia.
Alihitaji kupafahamu alipokuwa akiishi ili iwe rahisi kwake kwenda nyumbani hapo na kumuhoji mke wake vitu vichache, yaani alihitaji kufahamu kila kitu kilichokuwa kimetokea.
Lilikuwa jambo gumu mno kwa mtu kuwa na nyumba, kuishi na familia yako halafu uende kupanga. Hilo liliwezekana kwa wanaume wasiokuwa waaminifu ambao mbali na nyumba yao, hupanga chumba sehemu kwa lengo la kufanyia ufuska, ingekuwa rahisi kwa Bazoka kuwa hivyo lakini cha kujiuliza zaidi, kwa nini alipanga nyumba ya mchawi? Kama kweli alitaka kufanya mambo hayo, asingekwenda kupanga kwenye nyumba ya Bi. Semeni.
Akahisi kulikuwa na kitu na kwa sababu alikuwa mpelelezi, ilikuwa ni lazima kujua kila kitu kilichotokea, ila pale ambapo angekwenda kuzungumza na mke wa Bazoka, mwanaume huyo hakutakiwa kufahamu hilo hata kidogo.
“Nitajua la kufanya!” alijisemea, kidogo tabasamu likaanza kuonekana usoni mwake.

Je, nini kitaendelea?
 
Hili la kuwa na familia kisha kupanga chumba linakwenda kumharibia Bilionea
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom