Hadithi - Mwendo ni kula raha | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Hadithi - Mwendo ni kula raha

Discussion in 'Jukwaa la Lugha' started by SN_VijanaFM, Oct 22, 2010.

 1. S

  SN_VijanaFM Member

  #1
  Oct 22, 2010
  Joined: Mar 25, 2010
  Messages: 58
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Hii hadithi inatoka hapa: http://vijana.fm/tag/jicho-la-tatu/

  "Mwendo ni Kula Raha" ni kisa kutoka kwa kijana anayeitwa Magirini; yaliyotokea tarehe 15 Novemba, 2002.

  ____________________________

  Nilikuwa nasubiri kipindi hiki kwa udi na uvumba; baada ya mtihani wangu wa mwisho wa kidato cha nne, mwendo ni kula raha tu mpaka matokeo yatakapotoka Machi au Aprili mwaka kesho. Lakini mpaka sasa hivi mambo yamekuwa kinyume kabisa na niliyotarajia. Siku mbili nilizokuwa nyumbani bila la maana la kufanya zimeniboa sana, kwasababu marafiki zangu wengi, ambao wanafanya masomo ya biashara, wanamaliza mitihani yao leo Ijumaa.  Tokea saa tisa mchana, muda ambao marafiki zangu watakuwa wanakusanya mitihani yao ya mwisho, nimekuwa nikiitolea mimacho simu yangu. Sijui masela wanapanga kufanya nini leo? Bahati nzuri wimbo mpya wa msanii chipukizi Mangwea“Ghetto Langu” upo hewani na unanipa fikra tofauti kidogo. Nasikiliza mashairi yake huku macho yangu yakiranda-randa kwenye chumba changu. Kuanzia mwanzo wa wimbo hadi mwisho, nimelinganisha ghetto la Mangwea na langu na sijaona chochote kile ambacho kitampagawisha demu ye yote yule! Hata wa Uswazi!  DJ Stevie B anaonekana kaupenda sana huu wimbo na anaamua kuucheza tena. Safari hii naamua kutolinganisha chumba changu na ghetto la Mangwea; nafumba macho yangu taratibu na nayaachia kazi masikio yangu kufaidi midundo mwanana na mashairi.
  Joto linalosababishwa na jua kali la Bongo linanipa uvivu kiasi, na nahisi usingizi unaanza kuninyemelea. Nilichokuwa nasubiri siku nzima kinatokea: napokea ujumbe mfupi kutoka kwa rafiki yangu Deo unaosema, “Magz! 2day ni Billz! Dingi na maza hawapo, so pick-up ni yetu. Mzuka?”  Bila kusita, namjibu haraka-haraka, “U r da man! Tunaanza na kiti moto na nyagi au?”  Ananijibu kwa kizushi, “Unaulizia makonzi kituo cha polisi? Mtu kibao zitazuka. Hadi demu wako HAHAHA!”  “Acha masihara Deo! Mi mgumu, halafu yule wa geti kali simuwezi. Poa mzee, muda ule ule.. Cine Club then BILLZZZ!”


  Deo anapenda sana utani. Napokea ujumbe wake mwingine, “Neema kakuzimia Magz! Ananisumbua kinoma. Nadhani hata ukimpeleka kula mihogo na chachandu hatamaind.. only 4 u! Peace!”  Nashindwa kujizuia kuangua kicheko, ingawa mimi ndiye ninayetaniwa. Nimekuwa muoga kufuata Deo anayosema na kumtokea Neema. Sio kwamba simfagilii. Basi tu; kuingia kichwa kichwa na kupigwa kibuti halafu masela wajue ni noma. Wakati mawazo ya matokeo ya kupigwa kibuti yakijikita kwenye akili yangu, naamua kulala kwenye kitanda na kuegesha kichwa kwenye mto. Natazama kona za dari ambazo zina tando za buibui. Kila siku huwa nasema nitaziondoa kesho, lakini huwa nasahau…  * * *

  “Ngo! Ngo! Ngo! Magirini, chakula tayari! Baba anasema leo tunakula pamoja mezani,” sauti ya binti anayetusaidia kazi za ndani, Hadija, inanizindua kutoka usingizini.
  Namjibu kwa unyonge, “Haya. Ninakuja sasa hivi.” Nanyanyuka kutoka kitandani, nawasha taa na kuangalia muda kwenye simu yangu. Ni saa mbili na nusu; Deo atakuja kunichukua saa tatu hivi, kwahiyo nina dakika thelathini tu za kuongea na baba na mama na kuwaomba ruhusa ya kutoka leo usiku.  Naenda bafuni kunawa uso na kupiga mswaki haraka-haraka kisha najongea sebuleni, baba na mama walipo wakiangalia runinga. “Shikamoo baba, shikamoo mama.”  Wote wananijibu, “Marahaba.” Baba anaendelea, “Yaani tokea tumerudi kutoka kazini ulikuwa umelala? Hukusikia hata mlio wa gari?”


  Namjibu kwa kifupi tu, “Hapana baba.”  Baba ananiangalia kwa jicho ambalo linaashiria amekerwa kiasi, kisha anamuangalia mama. Inaonekana walikuwa wameshajadili wanachotaka kuniambia. Anageuka na kuniangalia huku akiwa amekunja ndita, “OK, leo ndio mwisho wako kukaa nyumbani bila kufanya kitu chochote! Kuanzia kesho shughuli za bustani na vitu vingine nje ni jukumu lako. Nikiona majani yaliyokauka kwenye maua, wa kwanza kukuuliza itakuwa ni wewe.”


  Natingisha kichwa kuashiria kuwa naafikiana naye.


  Baba ananyanyuka kutoka alipoketi na kuelekea mezani kwa ajili ya chakula cha jioni huku akiniambia, “Halafu kitu kingine. Unajua kuendesha gari sasa hivi? Nitakutafutia leseni ili uwe unashughulikia mambo ya shamba kuanzia wiki ijayo. Mtu kama wewe inabidi uwe bize mpaka tutakapoanza zoezi la kukutafutia shule A-level.” Baada ya kuketi na kuanza kupakua chakula, baba anamwambia mama anayevuta kiti ili aketi, “Hivi vidume vikiachiwa uhuru vinaanza kuvuta bangi na kuwapa mimba binti za watu.”


  Mama anamjibu, “Baba mkwe asingekuacha huru baada ya kumaliza kidato cha sita labda tusingekutana baba Magirini!”


  Baba anatabasamu kisha ananiangalia na kuniambia, “Vipi, mbona hukai? Leo hutaki kula makande?”


  Mazingara ya maongezi yamebadilika, na wakati huu utani ukiendelea ni muda muafaka kuomba ruhusa ya kutoka, “Unajua mitihani ilikuwa migumu sana. Nilikuwa napanga kutoka leo. Nitakuwa na Deo na marafiki zangu wengine.”


  Mama anaanza kutabasamu na kumwambia baba, “Si nilikwambia? Haya, mpe hela ya taksi ya kurudia.”  Baba anaanza kunipa nasaha zake kama kawaida, “Usinywe pombe. Sitaki kusikia mambo ya wasichana! Kabisa!” Kwa shingo upande anatoa hela kwenye pochi yake na kunikabidhi, “Unajua cha kufanya, Magirini. Usirudi kwa lifti za marafiki zako walevi. Kukiwa na shida nipigie simu.”


  Sitaki kutibua kitu chochote sasa hivi, kwahiyo napokea hela na kusema, “Ndiyo baba, nitafuata maelekezo yako yote.”


  Kabla sijaondoka baba ananiambia, “Halafu niliona buibui kwenye chumba chako leo asubuhi. Unasubiri mimi, mama yako na Hadija tukusaidie?”


  Bahati mbaya mazingara ya maongezi yanageuka ghafla, lakini mama anaokoa jahazi kwa kumkata kauli baba, “Baba Magirini, mwache.”  Bila kusita baba anamwambia mama, “Mbona unamtetea sana? Angekuwa dada yake hapa maongezi yangekuwa tofauti kabisa.”


  Mama anamjibu, “Huo mjadala mwingine. Haya Magirini toka hapa kabla baba yako hajabadili mawazo.”


  Nakimbia chumbani kwangu kuvaa nguo kwa ajili ya usiku kama wa leo. Kabla ya kutoka, najipulizia manukato halafu naangalia simu yangu ambayo ina ujumbe kutoka kwa Deo, “Am on my wei. Neema naye atakuwepo.. HEHEHE!”


  Ile kutoka tu nje ya geti, naona Deo anawasili akiendesha gari kwa mwendo mkali huku akitimua vumbi. Nafungua mlango na kungia ndani ya gari, kisha namwambia, “Mzee una fujo! Yaani mzee mzima nimejipinda kupendeza, halafu kichaa unakuja kunitimulia vumbi?”


  Tunaanza safari ya kuelekea Cine Club huku akiniambia, “Sorry mzee. Mzuka umenipanda kupita maelezo leo. Nina uhakika nitapata msonge kwenye pepa la Commerce


  “Sio mchezo mzee! Endesha taratibu basi, Deo. Kichaa kama huoni matuta vile. Kumbuka hauna leseni, na tukipigwa mkono sasa hivi kila kitu kitaharibika. Usiku mrefu kinoma na starehe zote zinatusubiri.”


  Deo anacheka huku akiniambia, “Mzee wa busara unaongea kama dingi yako siku hizi.” Bahati nzuri anapunguza mwendo. Baada ya ukimya wa sekunde kadhaa, anaanza utani, “Ohh! Mzee, kuhusu suala la starehe, nadhani unajua kuwa Neema atakuwa nasi. Fanyia kazi mzigo ule. Oh hooo, Magirini!”


  “Acha uzushi mzee. Umenikomalia siku nzima. Umetumwa nini?”


  Ananiangalia huku akitabasamu bila kusema lolote, kisha anageuka kuangalia tunapokwenda. Tunatoka Mikocheni na kuingia kwenye barabara ya Old Bagamoyo. Upepo mwanana wa bahari unaingia kwenye pick-up ya Deo. Naamua kuwasha redio na kusikiliza muziki ili kuanza starehe rasmi.


  Deo ananiambia, “Hii pick-up ya shamba mzee. Redio yake haikamati hata Clouds FM!”
  Sote tunaangua kicheko. Namwambia, “Haya basi, ngoja nitafute hata RTD nimsikilize Deborah Mwenda na hadithi zake za mazimwi!” Nafanikiwa kudaka mawimbi ya Clouds FM, halafu namwambia, “Nilikuwa naogopa kichizi hadithi za mazimwi. Sijui zimwi lina macho matatu.”  Deo anacheka huku akiniambia, “Nazikumbuka zile. Mi’ nilikuwa naimaind ile hadithi ya Binti Chura. Mpaka leo bado naikumbuka.”


  Taratibu tunawasili karibu na kituo cha basi cha Warioba. Deo anapunguza gia, anakata kona kuingia Cine Club na anafanikiwa kuona sehemu ya kuegesha gari.


  Baada ya kuegesha gari, kuzima redio na kufunga vioo, tunaanza kuelekea sehemu ambapo marafiki zetu walipo. Mwanga ni hafifu, lakini namuona Neema akiwa amekaa kwenye meza moja na marafiki zetu. Kasi ya mapigo ya moyo inaongezeka lakini najitahidi kuficha hisia na kuvaa uso wa mbuzi.

  Nahesabu haraka-haraka watu waliopo mezani ni kama sita hivi. Namuona Jimmy, Dullah, Issa, Kingo, Neema na binti mwingine ambaye nadhani ni rafiki yake. Tunafika mezani na kuwasalimia, “Vipi mambo?”  Karibia kundi zima linajibu kwa mpigo, “Poa!”  Deo anatoa salamu nyingine, “Kina dada mliopendeza, vipi mambo? Mbona meza tupu?”  Neema na rafiki yake wanatabasamu tu, ila Dullah huwa haishiwi na maneno akikutana na Deo, “Hebu kaa chini kwanza, Deo! Mbona mmechelewa? Si tusha’oda mbuzi katoliki na pawa nyagi. Vinywaji vinakuja sasa hivi!”  Deo anamjibu, “Ah! Huyu mzee wa busara Magirini nd’o kanichelewesha. Safari nzima ananipa nasaha kama dingi yake. Mara endesha gari taratibu, Deo. Tunakaribia kufika, anaanza kuniambia zile hadithi za mazimwi za Deborah Mwenda!”  Wakati watu wote wakinicheka, nawaambia, “Jamani! Deo si ulikuwa unaniambia unapenda ile hadithi ya Binti Chura? Au sio wewe? Kuanzia leo jina lako la utani litakuwa Binti Chura.” Kauli yangu ya mwisho inasababisha vicheko zaidi, na tunapata fursa ya kuchukua viti vilivyopo kwenye meza tupu ya jirani na kuketi. Dullah yuko upande wangu wa kuume na Deo yuko upande wa kushoto. Naangalia nyuso za vijana wenzangu; sura zao zimejawa na furaha, utani na vicheko vimetawala na wanajihisi kama wako kwenye dunia nyingine.


  Mhudumu analeta vinywaji mezani, anaweka chupa nne za konyagi katikati ya meza, glasi nane, fanta moja, chupa za coca-cola mbili na club soda kama nne hivi. Baada ya mhudumu kuondoka, Deo anauliza, “Nani kaagiza fanta? Mizengwe tu, inaleta nzi na nyuki mezani!”


  Dullah anadakia, “Mimi nilifika wa kwanza hapa na nd’o nikaagiza kila kitu. Deo, hiyo fanta ni ya kwako mzee. Binti Chura huwezi mambo ya wakubwa. Tuache sisi tunywe mpaka mzee nyagi ashushe mikono!”


  Issa anamuunga mkono Dullah, “Tuache utani jamani. Binti Chura… Samahani. Deo, ujue wewe ndio mwenye usukani leo, kwahiyo huruhusiwi kupata kilaji kama unavyojua. Masela walitaka kukununulia coca sijui, mi’ nikawaambia hata hiyo itakulewesha kichwa panzi. Nd’o tukaamua kununua fanta kwa ajili yako Binti Chura!”


  Kwa jinsi Deo anavyopenda kutania watu, ni ahueni kumona yeye akitaniwa. Uzuri wake ni kwamba hana hasira. Baada ya vicheko kutulia na watu kuanza kunywa, anatuambia, “Kweli leo mmeniamulia. Kiti moto kikiletwa hapa ninajua watu wangu wa kuwatania.” Sote tunajua anawaongelea Dullah na Issa, ambao wote wanacheka kwa sauti tu. Deo anaendelea, “Yule mnyama, kama sikosei, anaitwa nguruwe. Lakini watu wamembatiza majina ya ajabu-ajabu.”


  Dullah anamjibu, “Nguruwe ndio nini tena? Mi’ sijawahi kumsikia!”


  Issa naye, “Aaaah, nadhani anaongelea mbuzi kibonge tuliyeagiza. Tena huyoooo analetwa! Deo… Samahani, Binti Chura. Yule mnyama anaitwa mbuzi katoliki!”


  Mimi huwa muongeaji sana, ila muda kama huu nadhani huwa nafaidi zaidi kukaa pembeni na kuwasikiliza kina Deo, Dullah na Issa wakitupiana vijembe. Ni burudani tosha kusema ukweli; huwa wananikumbusha ile michezo ya kuigiza ya kina Majuto, Mzee Small na Mwanachia.


  Kelele zinapungua baada ya kiti moto kuletwa mezani. Napata fursa nyingine ya kuwaangalia watu wote walio mezani. Taratibu naangalia mtu mmoja-mmoja kwa kuanzia upande wa kulia Dullah alipokaa, Kingo, Issa, Jimmy, rafiki yake Neema; naongeza mwendo na kumruka Neema na nakutana na uso kwa uso na Deo, ambaye anatabasamu. Nadhani nimetegua bomu!


  Deo anapayuka, “My bway Maaaagzzz! Magirini, mbona umekuwa kimya sana leo?”
  Nadhani mimi na Deo tu ndio tunaojua kinachoendelea. Namjibu, “Mshika mawili moja humponyoka. Acha nifaidi msosi.” Deo anaashiria kuwa ameona jinsi ninavyomkwepa Neema na kuendelea kula.  Tunamaliza kula na kuendelea kunywa taratibu huku watu wakiendelea kutaniana, pombe ikisaidia watu zaidi kujiunga kwenye vita ya kutupiana vijembe. Labda kutokana na kutoruhusiwa kunywa pombe, Deo pekee ndiye anaonekana ameboreka, “Jamani, muda umefika. Malizieni kunywa tuzuke kiwanja. Leo patafurika kinoma.”


  Jimmy anasema, “Kama Bills pamejaa, tuzuke The Place uwanja wa nyumbani.”


  Karibia wote tunampinga kutokana na sababu zetu tofauti, ila Dullah anaamua kutuambia sababu yake, “The Place ina masista duu. Kuna siku nilienda pale, sasa DJ akacheza ule mpini “Sonia” wa Sir Nature, mi’ nikajitoa muhanga kwenda kumuomba dada mmoja mkali kucheza naye. Unajua alichoniambia? ‘Eti wimbo huu hauchezeki.’ Tokea siku ile nikasema sikanyagi tena pale! Ile kitu classic hata viziwi wanaucheza baba’ake!”


  Leo nadhani nimecheka sana, lakini kituko cha mwisho cha Dullah kinaniumiza mbavu zangu, “Dullah, unajua wewe ni msanii. Basi tu Bongo michosho. Ungekuwa nchi za watu, nina uhakika ungekuwa mwandishi wa vipindi vya vichekesho. Mzee una matani balaa.”


  Deo ananijibu, “Aaah, wapi! Huyu? Dullah anapenda kuku wa kienyeji ndio maana hapapendi The Place. Hicho alichokwambia ni kisa cha kweli lakini.” Ananyanyuka na kutuambia, “Haya jamani tulipe tuondoke hapa. Usiku umeshakuwa mnene.”


  * * *

  Kama tulivyotegemea, Club Billicanas pamefurika. Bahati nzuri foleni sio ndefu sana, kwahiyo tunafanikiwa kuingia baada ya muda mfupi tu. Ndani tunakuta vijana, wengi wao nina uhakika wamemaliza mitihani yao ya kidato cha nne. Mwendo ni kula raha tu kama nilivyotegemea. Tunajaribu kutafuta sehemu ambayo watu wote nane tunaweza kukaa pamoja lakini juhudi zetu zinagonga mwamba na hatuna budi kutawanyika.

  Dullah, Issa na Deo wanaamua kwenda kucheza pool. Nawakumbusha, “Hakikisheni Deo hanywi. Sana sana mwachieni labda coca moja tu!”

  Deo anaonekana hajafurahishwa, “Jamani, yaani siku kama ya leo mnataka nisipate hata matone mawili matatu ya mkojo wa mende? Acheni hizo masela.” Anatuangalia lakini hatusemi lolote. “Poa tu. Twen’ zetu tukacheze pool

  Waliobakia wanaonekana bado hawajui pa kwenda, hivyo nawaacha, napanda ngazi na kwenda juu kuona nini kinaendelea. Ukiwa juu unaona vitu vingi; ukumbi umejaa, sehemu ya kucheza muziki imejaa pomoni, kuna watu wanaocheza juu ya spika kubwa na wengine wamekaa kwenye viti na kulonga. Najisikia vizuri tu, ila nadhani chupa tatu hivi za bia zitafanya siku hii iwe nzuri zaidi na kuniondolea soni.

  Muziki umekolea na najisikia mwepesi baada ya kuongezea kinywaji! Naamua kushuka chini kuwakusanya marafiki zangu niliokuja nao (pamoja na Neema na rafiki yake) na kuelekea sehemu ya kucheza muziki. Baada ya kucheza nyimbo kama tano hivi mfululizo, DJ anacheza wimbo “Wife” wa Daz Baba. Wenzangu wanaamua kuondoka, Deo ananinong’oneza, “Nyimbo kama hizi kucheza na masela sio ishu wala nini. Wewe baki hapa na Neema. Zali!”

  Mimi naupenda sana huu wimbo na nilikuwa napanga kubaki kucheza, ila ishu ya kubaki mwenyewe kucheza na Neema au rafiki yake haiingii akilini. Kwahiyo naamua kuondoka. Deo na Dullah wananiona nikiwafuata na wananisukuma kunirudisha nilipotoka na kuishia mbele ya Neema, ambaye ananiambia, “Vipi, hutaki kucheza na mimi?”

  Mimi kidume bwana! Nitaogopaje kucheza na demu? Namjibu, “Hapana, nilikuwa nataka kwenda kununua kinywaji kwanza.”

  Anasema kitu lakini nashindwa kumsikia kutokana na kelele za muziki. Hivyo nainamisha kichwa na kutega sikio karibu na mdomo wake ili aninong’oneze, “Umekuwa unanikwepa leo. Tucheze basi…” Sauti yake nyororo ikiambatana na joto la pumzi yake inatua kwenye sikio langu la kulia. Natabasamu tu na kumsogelea ili tucheze pamoja. Neema anaweka mikono yake kwenye mabega yangu. Mimi namshika… No! Siwezi kukwambia nilipoweka mikono yangu kwasababu dingi anasomaga hadithi zangu!

  Tokea nitoke nyumbani mpaka sasa hivi siku imekuwa inaenda haraka sana. Lakini burudani ninayoipata sasa hivi inafanya muda usimame; nahisi kila kitu, nasikia kila mdundo, naona uso wa Neema ukiwa na tabasamu na jasho kidogo kwenye paji la uso. Wakati wimbo unayoyoma, Neema ananishika mkono wangu wa kushoto na kunivuta karibu, kisha ananiambia, “Nasikia joto. Twende nje tukapunge upepo.”

  Neema ananivuta hadi nje ya ukumbi huku akiwa bado amenishika mkono. Kufika tu nje kwenye nuru, anaamua kuniachia. Naongeza ukubwa wa hatua kadhaa ili tuweze kutembea sambamba, bega kwa bega, Neema akiwa upande wangu wa kushoto. Nageuka na kumuangalia usoni kwa udadisi; ingawa nimelewa kidogo, kwa mara ya kwanza naona vizuri uzuri na urembo wa Neema. Naiambia nafsi yangu, binti kama huyu hahitaji kujipodoa. Sielewi kwanini kajipaka rangi nyeusi kwenye kope za macho.


  Wakati tukiwasili kwenye kontena lililopo kama mita 20 kutoka kwenye malango ya Club Billicanas, Neema ananiambia, “Vipi, unaonekana wewe sio muongeaji sana?”


  Natabasamu tu. Pamoja tunakaa kwenye ukingo wa sakafu ya saruji iliyopo mbele ya kontena mbali kidogo na sehemu madereva taksi walipo, naamua kumuuliza, “Mitihani yako ilikuwaje?”


  Neema anaangua kicheko, ananimbia, “Deo was right! Wewe Magirini kweli mzee wa busara. Kila wakati unaongelea mambo serious! Huwezi kuongelea vitu vingine? Lakini… Bahati yako unajua kucheza muziki.”


  Nacheka tu bila kusema chochote. Naangalia chini, kisha nanyanyua uso wangu polepole na kutazama sketi nyekundu aliyovaa, na saa yake ya kiganjani: ni saa nane na nusu usiku. Naendelea kunyanyua uso wangu, nguo aliyovaa inanipa mwanya wa kuona ngozi kwenye mabega yake; inaonekana anasikia baridi. “Vipi, unasikia baridi?” Namuuliza huku nikivua shati langu haraka-haraka na kubakia na fulana. Kwa moyo mkunjufu namkabidhi shati langu, “Jifunike mabega na hili shati. Najua unasikia baridi.”


  Bila kusita Neema anachukua shati langu na kujifunika. “Asante Magz. You are so kind.” Ananimbia huku akitabasamu.


  Kabla ya kufungua kinywa changu, nasikia mtu akituita kwa sauti, “Magiriniiiii, Magiriiiniiiii! Neeema, Neeeema!”


  Naitikia, “Naaam! Niko hapa!” Nanyanyuka, naangalia sehemu sauti inapotoka na kumuona Deo akija sehemu mimi na Neema tulipo huku akipepesuka.


  “Mzee Magirini, I am gonna miss you, man! Neema, this is my real friend right here! Msikilize sana!” Nadhani Deo amekunywa pombe ndio maana anaropoka. “Magirini, najua utaenda shule nyingine. Ninavyomjua dingi yako, he will send you to some stupid nerdy boarding school. Mimi mzee wa Commerce nitabaki Dar. Itaboa kinoma mchizi wangu.”


  Ni kawaida ya Deo kuchanganya lugha akiwa amekunywa. “Deo, tulia kwanza. Kaa chini hapa.” Baada ya kukaa na kutulia, namuuliza, “Mzee, umekunywa ngapi?”


  “Acha hizo mzee. Moja tu.” Sisemi chochote, baadae anasema, “Nimekunywa mbili tu. Niamini.”


  Neema anaingilia, “Vipi Magirini, mbona anaonekana yuko alright tu. Mwache.”
  Namuangalia Neema kwa jicho kali bila kufungua kinywa kwa sekunde kadhaa. Kisha nageuka na kumuambia Deo, “Nipe funguo za pick-up


  Deo ananijibu, “Tuliza boli mtoto wa mama. I am OK. I can drive mzee. Unanijua mimi mzee. Bia nne hazinipelekeshi.”


  Tunaendelea kuzozana kwa dakika kama tano hivi, lakini Deo anagoma kabisa kunipa funguo za gari. Neema anaondoka na kutuacha mimi na Deo tukiendelea kutupiana maneno. Usiku umebadilika ghafla; dakika chache zilizopita kila mtu alikuwa anatabasamu, sasa hivi nyuso zetu zimejaa ndita.


  Punde kundi zima, likiongozwa na Dullah na Neema, linakuja tulipo. Dullah anauliza, “Wazee, vipi tena?”


  Namjibu, “Huyu Binti Chura nadhani kanywa pombe. Sitaki aendeshe gari.”


  Nawaangalia na bahati mbaya hakuna yeyote anayeniunga mkono. Kingo ananiambia, “Achana na Deo. Mi’ nilikuwa nae. Hajalewa wala nini. Au wewe ndio umelewa?” Wote wanaangua kicheko.


  Najihisi kama popo; walimwengu wananitaa ndege ingawa nazaa. Lakini sina jinsi, nainamisha kichwa changu na kuzama kwenye ziwa la fedheha.


  Deo ananiambia, “Ndio maana wazazi wako wakakupa jina Magirini.”


  * * *

  Kwa mbali nasikia sauti ya baba, “Magirini, amka. Amka!”

  Inaniwia vigumu kuamka haraka-haraka kutokana na kaubaridi ka asubuhi. Kwahiyo nageukia upande wa pili dirisha la chumba changu lilipo, nalivuta shuka na kujifunika kichwa. Nilitegemea kusikia tena sauti ya baba akinisihi niamke. Lakini kimya. Nasikia kishindo kidogo cha miguu yake akielekea kwenye dirisha na kufungua pazia. Ingawa mwanga wa jua la asubuhi ni hafifu, unapenya kwenye shuka langu na kutua usoni. Usingizi unatokomea kwa kasi.

  “Magirini, amka, kapige mswaki. Nahitaji kuongea na wewe.”

  Nakumbuka kuwa sijamsalimia. “Shikamoo baba!”

  “Marahaba,” ananijibu huku akingalia nje ya dirisha. “Haya nenda kapige mswaki.”​
  Sio kawaida ya baba kuniamsha Jumamosi asubuhi, hasa kama anajua nilikuwa nimetoka usiku uliopita. Wakati napiga mswaki, nashindwa kujizuia kujiuliza maswali lukuki. Vipi, baba anajua kama jana nilikunywa pombe? Au amesikia kelele za marafiki zangu wakati Deo aliponirudisha kwa gari ya wazazi wake? Labda amekasirika kwasababu sikurudi nyumbani kwa taksi kama alivyoniagiza?

  Baada ya kunawa uso na kupiga mswaki, narudi chumbani na kumkuta baba akimalizia kuondoa tando za buibui kwenye dari. Kuna kitu hakiko sawa; ameamua hadi kutandika kitanda changu! Nashikwa na bumbuwazi na kubaki nimesimama mlangoni. Baba anaketi kwenye kitanda na kuniambia, “Njoo hapa ukae,” huku akinyoosha mkono kuniamuru nikae kitandani karibu naye.

  “Niambie, jana ilikuwaje? Ulirudi kwa usafiri gani?”

  “Samahani baba, niliamua kurudi na gari ya Deo. Sitarudia tena.”

  Nilitegemea ataanza kupaza sauti kunigombeza, lakini anaendelea kuhoji kwa upole, “Deo nd’o alikuwa anaendesha gari? Alikuwa kwenye hali gani? Usijaribu kunilaghai mwanangu.”​
  Moyo wangu unaanza kuwa mzito, lakini mapigo yanaongeza kasi. Sielewi kinachoendelea. “Alikunywa kidogo tu nadhani… Kwani vipi?”

  Baba anainamisha kichwa chini kuangalia sakafu huku akitingisha kichwa, ananiuliza, “Yeye nd’o alikurudisha hapa na wenzako wengine?”

  “Ndio… Kwani vipi?”

  Ananyanyua uso wake na kuniangalia usoni. Na mimi namuangalia usoni. Nadhani leo ndio mara ya kwanza kumuona baba yangu akilengwa na machozi. Ananiambia, “Baba Deo kanipigia simu kutoka Moshi… ” Ananyamaza kwa muda mfupi na kumeza mate. “Baba Deo alinipigia simu kunitaarifu rafiki yako Deo aligonga nguzo ya nyaya za simu iliyoko karibu na nyumbani kwao. Alikuwa mwenyewe kwenye gari.”

  Siamini ninayosikia kutoka kwenye kinywa cha baba. Namuuliza, “Haiwezekani. Nadhani aliwarudisha marafiki zangu… Kesha’pelekwa hospitali?”

  “Pole sana mwanangu. Baba Deo anadhani alifariki pale pale alipopata ajali. Pole sana Magirini.”

  Naanza kutokwa na machozi, huku baba akijaribu kunifariji, “Pole sana mwanangu. Ndio maisha haya. Mimi na mama yako tuko hapa kukufariji kwenye kipindi hiki kigumu.”

  “Baba, siamini unachoniambia. Niache mwenyewe kwa muda. Nitakuja sebuleni…”

  Anabaki akiniangalia kwa dakika kadhaa, mkono wake wa kuume ukiwa juu ya bega langu la kushoto. “Sawa. Mama yako yuko sebuleni. Mimi itanibidi niende Muhimbili kumsaidia mjomba’ake Deo na mipango ya mazishi na vitu vingine mpaka baba Deo atakaporudi kutoka Moshi jioni.” Ananyanyuka, anatoka chumbani na kufunga mlango polepole.​


  Nashindwa kujizuia kububujikwa na machozi na kupiga mayowe. Maisha ya ujana ni kama kishada kinachopepea kwenye anga karibu na ufukwe wa bahari. Mara nyingi upepo huonekana ni mwanana kwenye macho ya wengi. Lakini, mara chache, kamba ya kishada ikikatika, sote tunaona jinsi kishada kinavyobebwa na upepo na kutoweka. Kibaya zaidi, najihisi kama mimi ndiye nilikuwa nimeshika kamba ya kishada. Lakini nitafanya nini sasa. Nitabaki na kuishi na majuto…

  MWISHO   
Loading...