Hadithi: Maisha yangu nyuma ya pazia jeusi

Nakuombeni radhi Sana nyote mliokuwa mnafuatilia Riwaya hii. Nilitoa taarifa kuwa ratiba ya mwezi jana isingekuwa rafiki Sana kwa mimi kupata nafasi ya kendelea kuleta simulizi hii. Mwezi mgumu umeshaisha Ila bado Kuna vitu vichache naviweka sawa na hatimaye tutaendelea.
Barry will return soon.
 
Mie nashangaa tyuuuh kimya sion muendelezo, kulikoni tena the author?
 
Nakuombeni radhi Sana nyote mliokuwa mnafuatilia Riwaya hii. Nilitoa taarifa kuwa ratiba ya mwezi jana isingekuwa rafiki Sana kwa mimi kupata nafasi ya kendelea kuleta simulizi hii. Mwezi mgumu umeshaisha Ila bado Kuna vitu vichache naviweka sawa na hatimaye tutaendelea.
Barry will return soon.
Najua tatizo limeanzia huko unakocopy.
 
Najua tatizo limeanzia huko unakocopy.
Tunatofautiana mazingira, si kila wakati utakuwa unapata masaa 4-5 kwa ajili ya ya kuandaa simulizi. Kuna maisha mengine nje ya jf na ndiyo yanayofanya tupate nguvu za kuingia humu.

Ila si vibaya kama unapafahamu huko ninapo'copy na wewe uende uka'copy na kisha ukaja uka'paste mwendelzo hapa, utakuwa umetusaidia sana.
 
MAISHA YANGU NYUMA YA PAZIA JEUSI

SEHEMU YA 19

KUMRADHI

Napenda kukuombeni radhi kwa wasomaji na wafuatiliaji wote wa simulizi hii ya ‘Maisha yangu nyuma ya pazia jeusi’ kwa kushindwa kuleta mwendelezo kwa kipindi cha karibu mwezi na nusu. Hata mimi sikuwa najisikia vizuri kabisa kwa hili lakini sikuwa na jinsi maana nilikuwa katika mazingira ambayo unapaswa kutumika kwa masaa mengi kila siku na muda pekee uliokuwa unapatikana ni wa kupumzika na kujiandaa kwa ajili ya ratiba ya siku inayofuata. Kwa sasa nipo katika mapumziko ya siku kadhaa, hivyo nitajitahidi angalau kila siku tupate sehemu moja na baada ya mapumziko kupita tutarudi kwenye ratiba yetu ya awali ya mara mbili kwa wiki.

Asanteni nyote.

Ilipoishia…..

Nilitaka nitangaze kuwa kama kuna mtu alikuwa ameisahau lakini nikaona ni vyema nikaona kilichomo ndani kwanza, na kwa kuwa nilikuta imechomekwa kwenye daftari langu ilifanya nihisi huenda ilikuwa ni ya kwangu. Nikajaribu kuifungua, ilikuwa ‘sealed’ nikasita kidogo kuendelea kuifungua. Nikatulia na kufikiri kidogo kama niifungue ama niachane nayo kwanza. Baada ya kufikiri kwa muda nikapitisha maamuzi ya kuifungua, nikaingiza mkono kutoa kilichokuwa ndani, ilikuwa leso, tena mpya kabisa. Niligundua kuwa leso ilikuwa mpya kwa sababu ilitoa harufu Fulani ya upya upya, nadhani utakuwa umenielewa. Nikaangalia ndani ya bahasha ili kuona kama kulikuwa na vitu vingine vilivyosalia. Kweli, kulikuwa na vitu vingine ndani ya bahasha ukiachana na ile leso ambayo nilikuwa nimeshaitoa.

Endelea…..

Niliingiza mkono tena ili nichukue vile vingine ambavyo vilibaki kwenye bahasha. Kabla sijavitoa nilisikia mtu akiniongelesha.

“oya barry, twende MPH tukapoteze muda, mi sijisikii kusoma kabisa” alikuwa ni Fadhili, rafiki yangu ambaye tulikuwa tunasoma darasa moja. (The) Multi-Purpose Hall au MPH kama tulivyozoea kupaita, ulikuwa ni ukumbi ambao ulikuwa unatumika katika shughuli mbalimbali pale shuleni. Kwa siku kama hiyo ya ijumaa kuanzia saa 1 usiku kulikuwa na sala na nyimbo zikifanyika humo MPH na wanafunzi waliokuwa katika imani ya kisabato kwa ajili ya kuikaribisha siku ya sabato. Japokuwa sala hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya wasabato, wanafunzi wa dini nyingine walikuwa wanaenda ili kukwepa kukaa darasani na kujisomea. Hata mimi ambaye ni mkatoliki lakini mara kadhaa nilikuwa naenda katika sala hiyo ya jioni.

Kwa kuwa kutokuwepo kwa Jennifer darasani kulikuwa kumeanza kunifanya niwaze ni nini anakipitia huko aliko na ile bahasha ambayo ilikuwa na vitu ambavyo sikuwa nimeviona baadhi, nilikuwa na mtanziko wa mawazo hivyo niliamua kukubali wazo la kwenda MPH ili kupoteza masaa. Nilirudisha ile bahasha ndani ya meza yangu, mara hii nikiipachika katikati mwa daftari lililokuwa chini kabisa kisha nikafunga na kunyanyuka kwenda huko MPH pamoja na rafiki yangu huyo.

Tulifika MPH tukawakuta wakiimba, nasi tukajiunga nao. Tulisali na kuimba na wasabato hadi ilipofika muda wa kulala, saa nne na dakika zake ishirini. Baada ya hapo tulitoka moja kwa moja na kwenda zetu mabwenini ili kulala huku tukiingojea siku nyingine mpya. Tulifika mabwenini na kama ilivyokuwa kawaida, ilikuwa ni lazima tutumie dakika kama ishirini au thelathini kupiga story za hapa na pale ili kuukaribisha usingizi.

Wakati tukiwa tunaongea haya na yale mara tulianza kusikia kelele kutoka katika mabweni ya wasichana. Ulikuwa ni utaratibu wa mara kwa mara kwa wanafunzi kupiga kelele mara kadhaa nyakati za usiku au hata nyakati za mchana kwa sababu mbalimbali hasa michezo na labda kama kulikuwa na ugomvi au mambo mengine yanayoshabihiana na hayo.

Lakini kelele za siku ile zilikuwa ni za tofauti sana. Zilikuwa ni kelele za hali ya juu. Ilitubidi tutulie kimya ili tusikilize ni nini kilikuwa kinaendelea. Walisikika wasichana wakipiga mayowe kiasi tukaanza kuwaza huenda kulikuwa na wezi walikuwa wamewaingilia au labda walikuwa wamemuona 'msela nondo'. Msela nondo lilikuwa ni jina maarufu sana pale shuleni lililotumika kumtaja mwanaume wa kufikirika ambaye iliaminika kuwa alikuwa akiwaingilia wasichana kimaumbile nyakati za usiku kwa kutumia njia za kishirikina. Japokuwa hakukuwa na ushahidi wa wazi juu ya uwepo wa mtu au kiumbe huyo lakini hiyo haikuzuia jina hili kuwa maarufu pale shuleni kwetu.

Wakati huo wote kelele ziliendelea huku tukijipa moyo pengine zingekoma baada ya muda Fulani mfupi, lakini haikuwa hivyo. Kelele zilizidi kuongezeka kiasi kila mtu aliyekuwa amelala aliamka na kukaa kitandani na kusikiliza kwa makini ni nini kilikuwa kinaendelea. Watu walianza kutoka na kusimama nje ya mabweni ili angalau waweze kusikia vizuri zaidi ni nini kilikuwa kinaendelea.

Kelele bado hazikukoma; mayowe, vilio vilisikika kutoka katika mambweni ya wasichana. Uzalendo na uvumilivu vilitushinda. Tukajikuta tunaanza kusogea taratibu katika mambweni ya wasichana. Ilikuwa ni mwiko wanafunzi wa jinsia moja kwenda katika mambweni ya jinsia nyinginne isipokuwa katika siku ya jumamosi asubuhi ambapo kulikuwa na ukaguzi wa usafi wa mabweni. Siku hiyo, viongozi wa usafi pamoja na smart boy na smart girl wa wiki hutembelea mambweni yote kukagua usafi. Hii ndiyo ilikuwa nafasi pekee ya mwanafunzi wa jinsia moja kwenda katika mabweni ya jinsia nyingine. Watu walijitahidi sana kuwa nadhifu siku ya alhamisi ili wachaguliwe kuwa smart boy na smart girl wa wiki ili tu wapate nafasi za kwenda katika mambweni ya wanafunzi wa jinsia ya pili, lakini kama ilivyo kawaida kwa watu wa nchi yetu hata hao ma’smart boy na ma’smart girls walikuwa wakichagulia kwa kujuana. Kama kiranja wa usafi alikuwa ni rafiki yako basi ulikuwa na nafasi ya kuchagulia mara kwa mara.

Baada ya kufika katika maeneo ya mabweni ya wasichana tulikutana na hali ambayo ilionyesha wazi kuwa hakukuwa na usalama kabisa eneo hilo. Wasichana wengi walionekana kurundikana katika moja ambalo ilionyesha jambo lililokuwa likisababisha kelele hizo lilikuwa limetokea hapo. Walimu na walinzi walisikika wakiwazuia wanafunzi wasisogee mbele zaidi. kingine na kikubwa kabisa nilisikia wasichana wakilia huku wakitaja jina la Jennifer. Mapigo yangu ya moyo yalianza kuongezeka baada ya kusikia baadhi ya wasichana wakilia huku wakitaja jina la Jennifer. Nilianza kutetemeka kwa kuwa nilihisi huenda kuna jambo baya sana limetokea kwa Jennifer. Nilianza kupiga hatua huku nikiomba Mungu kuwa kile ambacho nilikuwa nimeanza kukihisi kuhusu Jennifer kisiwe kweli. Baada ya sekunde chache nilifika katika eneo hilo ambalo lilikuwa na mti wa mkwaju. Huku nikiwa najaribu kujipenyeza katikati ya kundi la watu, nilikuwa naangalia kwenye huo mti kwa maana ilionekana hapo ndipo kilipokuwa kiini cha tukio lote hilo. Niliweza kuona shuka likiwa limefungwa kwenye moja ya matawi ya mti huo. Mapigo ya moyo yalizidi kwenda kasi baada ya kuona kwenye shuka hilo kulikuwa kuna mtu akining’inia. Kwa kifupi ni kuwa kuna mtu alikuwa amejinyonga.

Kwa kuwa nilishaanza kusikia watu wakitaja jina la Jennifer, nilikuwa naomba kimoyomoyo kuwa asiwe Jennifer Yule ambaye nilikuwa namfikiria mimi. Lakini haikuwa hivyo, kwa sababu nilivyokazia macho yangu kuelekea kumwangalia mtu aliyekuwa ananing’inia, alikuwa ni Jennifer, tena Jennifer niliyekuwa namfikiria mimi.

Nilihisi miguu yangu kukosa nguvu ya kuubeba uzito wa mwili wangu. Mwili mzima ukawa unatetemeka, machozi yalianza kunilenga. Kwa hakika sikuweza kuamini kile nilichokuwa nakiona. Nilitamani tukio hilo liwe ni ndoto na niamke kutoka usingizini, lakini sekunde zilizidi kusonga huku hali ikiwa ile ile. Nilijaribu kujipenyeza ili nifike mahala mwili wa Jennifer ulipokuwa unaning’inia ili nikajaribu kumtikisa pengine angeamka, lakini sikuweza kufanikiwa kwa kuwa walizi na baadhi ya walimu wa kiume walikuwa wanawazuia wanafunzi wasikaribie eneo hilo.

Baada ya jaribio langu hilo kushindwa nilisogea pembeni huku nikitafakari kama tukio lile ni la kweli ama lah. Moyo wangu ulikuwa mzito sana kuamini kama Jennifer angeweza kujinyonga. Kwa nini ajinyonge? Kwa nini achukue uamuzi wa kukatisha uhai wake kikatili hivyo, bado sikuona sababu. Tafakari hiyo haikutosha kunifanya nijisikie afueni, bali ilizidi kutengeneza hisia zilizozidi kutafuna moyo wangu kwa kasi.

Nikiwa bado sijielewi elewi, nilisikia kengele ikigongwa. Hii ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kusikia kengele ikigongwa saa nne usiku. Walimu na walinzi walianza kutuamrisha sote tukakusanyike ‘paredi’. Wanafunzi taratibu tulianza kuondoka. Kundi la wanafunzi lilisindikizwa na sauti za vilio na kwikwi kutoka hasa upande wa wasichana. Mimi kwa upande wangu nilikuwa na huzuni kubwa moyoni huku bado nikiwa siamini kama lile tukio kweli lilitokea.

Tulifika paredi, na kukuta wanafunzi wengine wakiwa wamesimama huku kukiwa na sauti mchanganyiko. Wapo waliokuwa wanalia kwa sauti, wapo waliokuwa wanalia kwa chinichini, wapo waliokuwa wanaongea kwa sauti kubwa na wakunong'onezana pia walikuwapo. Hivyo mchanganyiko huo wa sauti ulizaa sauti moja ambayo isingeweza kueleweka. Lakini kila mmoja alionekana akiwa katika hali ya kuzuni, ni wachache sana waliokuwa katika hali ya kawaida kama ilivyokuwa kwa siku nyingine.

Tulisimama pale tukisubiri kuambiwa kile ambacho walitaka kutuambia. msaidizi wa mkuu wa shule alifika na kusimama pale mahali pa kutolea matangazo.

"jamani naomba tusikilizane" alisema mwalimu lakini sauti yake haikuwa imesikika vyema kwa sababu ya kuzidiwa na kelele za wanafunzi. "naomba tusikilizane...naomba tusikilizane jamani huko nyuma naombeni mtulie" aliendelea baada ya kuona wanafunzi walikuwa hawanyamazi bado, na mara hii aliongea kwa sauti kubwa. taratibu kelele zilianza kupungua na hatimaye kuisha kabisa lakini sauti za vilio vya chinichini hasa kutoka kwa wasichana viliendelea kusikika.

"jamani , najua kila mmoja wetu ameshikwa na taharuki kutokana na jambo ambalo limetokea leo katika shule yetu. mimi na uongozi mzima tumelipokea kwa masikitiko mkubwa sana na tukio hili kama ilivyo kwenu....." wakati anaongea kelele zilianza kurudi upya hali iliyomfanya kutunyamazisha tena kisha akaendelea "naombeni tutulie, najua mna majonzi lakini naombeni tusikilizane kidogo tu. tumepokea kwa masikitiko sana jambo hili. lakini naombeni tuwe watulivu, tunasubiri polisi waje wafanye uchunguzi ndipo taratibu nyingine ziendelee, hivyo katika kipindi chote hiki tunakuombeni tuwe watulivu..sawa jamani....na kama ikitokea mtu yeyote kati yenu akahitajika kutoa maelezo kwa polisi naomba muwape ushirikiano wa kutosha. kwa hiyo nawaomba muende mabwenini na muende mkalale ili tuone ni nini kitaendelea kesho. sitarajii kuona watu wakipiga kelele usiku..haya mnaweza mkatawanyika" alisema mkuu wa shule msaidizi kisha wanafunzi tukaanza kutawanyika.

Lile tangazo kutoka kwa msaidizi wa mkuu wa shule lilipigilia msumari wa moto katika nafsi yangu. Nilikuwa sitaki kukubali kama kweli Jennifer alikuwa amefariki kwa kujinyonga, lakini tangazo lake lilihitimisha kuwa ni kweli Jennifer hakuwa pamoja nasi tena.

Nikiwa katika kundi la wanafunzi wanaaoenda bwenini huku nilikiwa katika lindi la mawazo na huzuni, kuna kitu nilikikumbuka. Kuna bahasha ambayo ilikuwa na vitu ambavyo baadhi sikuvifungua. Nafsi yangu ikanisihi kuwa ni lazima nikaviangalie vile vitu ndipo niende bwenini. Huku nikiwa na simanzi kubwa ndani ya moyo wangu, nilijikaza na kuanza kurudi darasani kwa kasi ili nikaviangalie vile vitu vilibyokuwa kwenye ile bahasha.

Nilifika darasani na nikapitiliza moja kwa moja kwenye meza yangu. Nikafungua meza na kupekenyua huku akili yangu ikiwa nusu kamili nusu hayawani, nikafanikiwa kuipata hiyo bahasha. Huku mikono yangu ikiwa inatetemeka niliingiza mkono wa kulia kutoa vitu vilivyo ndani a kwa kuwa nilifanya hivyo kwa papara hali iliyofanya bahasha ichanike kasehemu kakubwa tu kutoka juu hadi karibu na kati, sikujali. Nikavitoa vilivyokuwa ndani. Kulikuwa na leso ambayo nilikuwa nishaiona tayari kwa hiyo sikuwa na mpango nayo tena. Nilitoa macho kuviangalia vitu vilivyosalia ambavyo sikuviona hapo awali.

Kitu cha kwanza ilikuwa ni picha na cha pili ni karatasi iliyokuwa imekunjwa. Niliishika ile picha na kuitazama, alikuwa ni Jennifer. Alionekana akiwa amevalia sare nadhifu za shule yetu na ile picha ilionyesha kuwa alipiga palepale shuleni. Alikuwa amesimama, huku akiwa ameachia tabasamu mwanana usoni mwake. Nikiwa natizama picha hii nilijikuta machozi yananibubujika bila kutarajia. Kwa hakika nilikuwa napitia kipindi kigumu sana katika maisha yangu. Kwa kishingo upande niliacha kuangalia kitu cha mwisho kilichokuwamo katika ile bahasha. Ilikuwa ni karatasi iliyokunjwa. Nilichukua na kuikunjua haraka haraka.

Macho yangu yakakutana na mwandiko niliokuwa naufahamu, ulikuwa ni mwandiko wa Jennifer. Mikono iliaza kutetemeka. Sikuwa najua ni nini Jennifer alikuwa amekiandika mule. Nilikazia macho yangu katika karatasi ili niweze kuzoma, lakini nikashindwa kwa sababu akili yangu haikuwa imetulia kabisa. Niliziona herufi, maneno na sentensi lakini sikuweza kuelewa chochote kwa wakati ule.

Baada ya zoezi la kusoma ujumbe ule kuwa gumu, nilifumba macho yangu huku nikiomba kujaaliwa nguvu na ujasiri wa kusoma kilichokuwa kimeandikwa. Baada ya kufumbua macho tena nikaikazia macho karatasi ile huku mikono yangu ikiwa bado inatetemeka, nilianza kusoma. Iliandikwa:

'habari mpenzi wa nafsi yangu, barry.

Natumaini uko mzima wa afya. Najua leo utakuwa unajiuliza ni wapi nilipo mimi kipenzi chako. Nipo, lakini najiandaa kuondoka. Barry, najua mimi nawe tumepitia katika milima na mabonde mengi sana, na yote yalisababishwa na ugumu wa nafsi yangu. Nakiri kuwa nilikukosea sana. Mara zote nilipenda ujisikie vibaya.

Lakini katika namna ambayo hata sasa sielewi, mimi na wewe tukawa watu wa karibu, watu wa karibu sana na baadaye penzi tamu lilichipua kati yetu. Binafsi niliona hiyo ndiyo nafasi ya mimi kukusahaulisha maumivu yote niliyokusababishia hapo nyuma. Nikakupa moyo wangu na mwili wangu kwa sababu ya mapenzi tu na nilikuamini kuwa wewe ni sehemu ya maisha yangu hivyo hakuna siri kati yangu nawe.. Nikakupa na picha yangu ya utupu ili kudhibitisha kuwa mimi na wewe hatufichani kitu. Nilijua kuwa siri za mwili wangu ungezitunza kama nitunzavyo zako. Lakini haikuwa hivyo, kumbe wewe haukuwa umenisamehe bado. Msamaha wako ulikuwa wa uongo, kumbe ulisubiri upate nafasi ili ulipe kisasi mara elfu zaidi. ukaniita malaya, kahaba. na ukatishia kuudhihirisha ukahaba wangu kama ningejaribu kulitetea penzi langu.

Pengine nastahili haya yote, ila nimekosa uwezo wa kuyahimili. Barry, naondoka. Kule ninakoenda kuna giza totoro, sijui ni nini kitanitokea huko. Lakini naona ni afadhali kuliko utumwa wa hisia. Giza linatisha, ila utumwa wa kihisia unatisha na kuumiza kwa pamoja.

Barry, naondoka na sitorudi tena ila nakuachia picha yangu, picha ambayo angalau itakufanya ukumbuke mema yangu machache niliyokutendea. picha itakayoficha ukahaba wangu japokuwa haitobadili ukweli ulionao kunihusu. Barry najua wewe ni mtu mwenye moyo mgumu na hauwezi kusikitishwa wala kudondosha chozi, lakini kama ikitokea ukalia kwa sababu yangu naonyesha mchamgo waku wa kukupoozesha machungu utakayokuwa unayapata kwa sababu yangu kwa kukuachia leso yangu uitumie kufutia machozi yako kwa kuwa sitakuwa na uwezo wa kukufuta machozi wakati natakapokuwa nimeozea udongoni.

Barry, kama hutalia leo basi hutalia kamwe ila kama utalia leo, amini nakuambia utalia maisha yako yote. Na kumbuka uliniita malaya, wacha niende nikakumbane na adhabu yangu stahiki. Ila wewe katubu kwa kuwa ulizini na kahaba..nawe utakuwa mweupe kama theluji.

Kaburi ni chumba kidogo kitoacho faraja kwa waikimbiao dunia pana.

kwa heri kipenzi cha nafsi yangu...'

nilimaliza kusoma huku nikiwa nabubujikwa na machozi, kwikwi nayo haikuniacha mbali. Maneno aliyoyaandika jenifer yalikuwa mazito na magumu mno. Nilitamani ningekuwa na uwezo wa kurushisha wakati nyuma ili nisahihishe makosa yangu na Jennifer abaki kuwa hai na mwenye furaha, lakini uwezo huo sikuwa nao. Uwezo niliokuwa nao wakati huo ni kulia tu.

Nilikaa kwenye kiti huku nikiwa nimeshikilia ile barua ya Jennifer huku nikilia kwa sauti. Kwa kuwa ulikuwa ni wakati wa usiku, sauti kidogo tu ingeweza kufika mbali lakini hilo halikuwa kichwani mwangu, majonzi ya kumfanya Jennifer aikimbie dunia yaliizonga nafsi yangu pasi na kuipa nafasi ya kutafakari.

Nikiwa katikati ya kilio mara nikasikia mtu akiita kutoka dirishani. Niligeuka kwa hamaki kubwa kuangalia alikuwa ni nani. Lahaula..! alikuwa ni mlinzi mkuu wa shule.

“unafanya nini huku peke yako? Eeh?” alisema kwa ukali. Mwili ulizidi kuishiwa nguvu. Nilikuwa katikati ya majonzi lakini hili nalo lilikuwa ni tatizo jipya tena. Hakika siwezi kukisahau kipindi hiki katika siku zite ya maisha yangu. Ni kipindi ambacho moyo wangu ulibeba mzingo wa maumivu na huzini kupita kiasi.

Nikiwa bado sijui ni nini nifaye, nilisikia mlinzi akifoka tena.

“we mwanafunzi nakuomba hivyo ulivyo nyanyuka uje hapa.” Kauli hii ilikuwa ni msiba mwingine kwangu. Kwa hakika nilijua kuwa ile siri iliyokuwa imejificha nyuma ya kifo cha Jennifer ingeenda kufichuka punde.

Itaendelea….
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom