Hadithi: Happy at Last (Furaha Hatimaye)

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Apr 29, 2016
20,744
25,445
Image may contain: one or more people, text that says 'Happy at Last Eric Shigong'

HAPPY AT LAST (FURAHA HATIMAYE)

Eric Shigongo


“Umeolewa?”
“Ndio!”
“Mume wako yuko wapi?”
“Dar es Salaam!”
“Sijawahi kumwona hata mara moja akija hapa hospitali!”
“Ana kazi nyingi sana ofisini kwake, hata hivyo huwa anajitahidi kufika anapopata nafasi!” Maneno hayo yalitoka mdomoni mwa mwanamke mwenye nywele chafu kichwani mwake, ambazo kwa kuziangalia zilionekana siku za nyuma ziliwahi kuwekwa dawa lakini baadaye zikaachwa bila matunzo!

Alivaa fulana yenye rangi ambayo haikuwa rahisi kuijua kati ya kahawia na nyeupe sababu ya uchafu, pamoja na hali hiyo bado kwa kumwangalia vizuri mwanamke huyo zaidi ya namna alivyovaa, haikuwa rahisi kushindwa kuugundua uzuri wa sura yake, alikuwa na macho makubwa ya kuita, urefu wa wastani, kiuno chembamba na matiti yaliyosimama wima kama vile hakuwahi kuwa na mtoto, chini ya kiuno upande wa pembeni kulivimba vitu kama mito ya kulalia chini ya sketi chafu aliyovaa, ambayo ufupi wake uliacha miguu yake kuanzia magotini kushuka chini ionekane wazi, alikuwa na mguu adimu, mguu ambao wengi waliuita mguu wa bia.

“Unaniambia kweli?”
“Ndio daktari!”
“Mbona sijawahi kumwona, anaitwa nani?”
“Gerald!”
“Mh!”Daktari aliguna, alikuwa amehisi kudanganywa, macho na midomo ya mwanamke huyo vilitofautiana kabisa.

Alikuwa ndani jengo la wodi ya watoto katika Hospitali ya Mtakatifu Francis huko Ifakara, mkoani Morogoro. Kitanda namba 9 chumba cha pili. Hali ya hewa nje ya jengo mchana wa siku hiyo ilikuwa ni ya joto tofauti na siku nyingine zote katika kipindi hicho cha Masika. Hakuwa peke yake ndani ya wodi, kitandani alilala mtoto mdogo, mwenye maumbile ya ajabu, kichwa chake kilikuwa kimejaa mabonde na nundu nyingi, viungo vyote mwilini mwake vilikuwa vimevimba!

Alikuwa mtoto mwenye umri wa miaka kumi lakini alionekana kama mtoto wa miaka mitatu kwa jinsi alivyokuwa mdogo kwa umbile.

Alikuwa Genesis, mtoto wa kike wa Blandina, alimwita jina hilo akiwa na maana ya neno ‘Mwanzo’ kama ilivyo kwenye kitabu Kitakatifu kitumiwacho na Wakristo; Biblia, akiamini ulikuwa ni mwanzo wa maisha ya raha aliyoyafikiria na kuyatamani siku zote, kuja kwa Genesis katika maisha yake ulikuwa mwanzo wa furaha! Haikuwa hivyo, hakupanga mipango yake akimshirikisha Mungu, kama ni kosa basi hilo ndilo alilofanya kwani kuja kwa Genesis badala ya kuwa mwanzo wa furaha, kulibadilika na kuwa mwanzo wa matatizo na balaa katika maisha yake kiasi cha kumfanya apoteze hata Imani ya Kikristo aliyokuwa nayo, akamchukia Mungu akisema “Kama kweli Mungu alikuwepo na aliwapenda watu ni kwanini alimpa adhabu aliyokuwa akiipata akiamini hakuwa na kosa alilotenda kustahili mateso hayo!”

Pembeni kwa kitanda alicholalia Genesis, kulikuwa na kabati, juu ya kabati hilo kulikuwa na redio ndogo aina ya National Panasonic, ikirusha matangazo ya Radio One, mtangazaji siku hiyo alikuwa Misanya Dismas Bingi, akili na mawazo yote ya Blandina yalikuwa yameelekea kwa mtoto wake, alitamani siku moja Genesis apone ili arejee tena jijini Dar es Salaam kuungana na familia yake, kwa muda mrefu alikuwa ameishi peke yake, akihama hospitali moja kwenda nyingine ndani na nje ya Tanzania akitafuta uzima wa mtoto wake.

“Leo katika ukumbi wa Mango Garden, Twanga Pepeta watakuwa pale chini ya mwanamuziki Mahiri nchini Tanzania Ali Choki mtoto wa Kibaha, jukwaa litakuwa linashambuliwa ipasavyo, usikose kiingilio ni shilingi elfu mbili…! Ukitoka hapo unaweza kwenda Bilicanas au Police Officers Mess ambako wazee wa zamani watakuwa wakiserebuka na mzee Ndala Kasheba pamoja na King Kiki katika ile miondoko ya Bakurutu…!” Alimaliza Misanya bila kuelewa ni kitu gani alikuwa akikisababisha moyoni mwa Blandina.

Machozi yalimlengalenga, kumbukumbu za Dar es Salaam zilimiminika kichwani mwake, akamwona mume wake Gerald na kuamini alikuwa bado akiendelea na starehe wakati yeye akiteseka na mtoto hospitalini! Ilimuuma.

Alitamani dunia ingebadilika na kurejea ilikokuwa kabla ya kuzaliwa kwa Genesis ambaye alibadilisha kila kitu katika maisha ya Blandina na kumfanya awe mtu wa machozi usiku na mchana, akili yake ilimrudisha nyuma miaka kumi na mbili na kumfanya azikumbuke nyakati ambazo yeye na Gerald walikuwa wapenzi wakitoka karibu kila mwisho wa wiki kwenda sehemu za starehe pamoja, Gerald akimwita majina yote mazuri kama Sweet, Honey , Darling, Baby na mengineyo mengi.

Hali hiyo haikuwepo tena, alikuwa peke yake katika dunia akihangaika kuokoa maisha ya mtoto wake, haikuwa rahisi kuhisi aliwahi kuwa Miss Dar es Salaam kwa jinsi alivyokuwa mchafu, uzuri wa sura na urembo haikuwa na maana tena kwake, kitu cha muhimu kilikuwa mtoto wake Genesis.

“Mom!” (mama!) Genesis aliita katikati ya maumivu mkononi akiwa ameshikilia picha ndogo ya mtoto.
“Yes my darling!”(Ndio mpenzi wangu!)
“Is this my photo when I was small?”(Hii ni picha yangu nilipokuwa mdogo?) Mtoto aliuliza kwa sauti ya huzuni.

“Yes my sweet!”(Ndio mpenzi wangu!)
“No! This is somebody else!”(Hapana! Huyu ni mtu mwingine!)
“Why?”(Kwanini?)
“How comes I am this ugly and shapeless if at birth I was this cute?”(Inawezekanaje nikawa na sura mbaya kiasi hiki kama wakati wa kuzaliwa nilikuwa mzuri namna hii?)

Lilikuwa swali gumu sana kwa Blandina, badala ya kulijibu alijikuta akiangua kilio mbele ya mtoto wake na kumfanya yeye pia ashindwe kuvumilia, wote wawili wakaanza kulia! Picha ndani ya chumba hicho ilikuwa ni ya kuhuzunisha mno na daktari aliyekuwa pembeni akiandika mambo fulani kwenye faili aliyemfariji na kumtuliza Blandina, alielewa mwanamke huyo alikuwa akipita wakati mgumu kiasi gani. Halikuwa jambo rahisi kwa mwanamke wa kawaida kustahimili shida alizokuwa akizipitia, kwa muda wa miezi tisa alikuwa amelazwa katika hospitali hiyo akimuuguza mtoto wake, kabla ya hapo alishalazwa hospitali nyingi tu jijini Dar es Salaam bila nafuu yoyote kwa mtoto wake.

Kifupi katika miaka minane tangu mtoto wake aanze kuugua, labda ni miezi miwili au mitatu tu ndio alikuwa amekaa nyumbani kwake! Siku nyingine zote alikuwa hospitali akihangaika na mtoto wake, hakuwa tayari kukata tamaa mpaka mwisho uonekane na alitaka mwisho wa maisha ya Genesis utokane na Mungu mwenyewe, kwani mara kadhaa alishashauriwa mpaka na watu wa karibu kabisa maishani mwake amuue mtoto wake ili azae mwingine kwani huyo hakuwa na faida yoyote katika maisha yake zaidi ya kuwa mzigo, kauli kama hii ilitoka pia kwa mume wake ambaye hakuwa tayari kabisa kukubaliana na ukweli kuwa yeye na mke wake walikuwa wamepata mtoto mwenye matatizo na hivyo walitakiwa kushikamana.

“Blandina!” Daktari alimwita.
“Ndio daktari!”
“Nimefanya kazi miaka ishirini lakini sijawahi kukutana na mama mwenye moyo kama wako, Mungu akubariki sana!”
“Ahsante daktari!”
“Unampenda sana mtoto wako sio?”
“Sana!”
“Usikate tamaa, iko siku utapumzika…!”
“Ahsante daktari, endelee kuniombea!”
“Genesis!” Daktari alimwita mtoto.
“ Yes!”(ndio!)
“Do you know that your mom loves you?”(Unajua ya kwamba mama yako anakupenda?)
“Yes I do! I love her too, I haven’t seen my father for a long time, but she is always here with me, she is a good mother!”(Ndio najua! Nampenda pia, sijamwona baba yangu kwa muda mrefu sana, lakini yeye yuko hapa pamoja nami siku zote, ni mama mzuri!) Mtoto aliongea akilengwa lengwa na machozi.

Blandina aliona aibu, alichokuwa akijaribu kukificha kilikuwa kimewekwa wazi na mtoto, siku zote hakupenda kumuaibisha Gerald, alikuwa mume wake. Pamoja na upungufu wote aliokuwa nao, bado alitaka kumlindia heshima yake.
“Blandina”
“Ndio daktari!”
“Ulinidanganya?”
“Nini daktari?”
“Kwamba mumeo huwa anakuja hapa kukuona!”
“Samahani daktari, ni habari ndefu!”
“Ningependa kuifahamu!”
“Nitakusimulia kesho!”

Je, nini kitaendelea?
Je, ni mambo gani yalitokea katika maisha ya Blandina na Gerald?

Tukutane Jumamosi mahali hapa.
Hadithi hii itakuwa ikitoka mara mbili kwa wiki. Siku ya Jumatano na Jumamosi
 
Habari mambo naitwa Mr Equator Nimeandika ujumbe huu kuku omba swala moja tu!
Mimi nimetengeza website ya ku share story ambayo ni EquatorStory
Je umekuwa ukipata tabu kupost story zako hapa?
Hili ndo suluhisho lako.
Mimi nataka nkupe nafasi ya kuwa mmoja wapo wa kwanza kutumia hii website
unda account yako na uweze kupost story yako mpya.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom