Sir Lindege
Member
- Sep 10, 2013
- 34
- 180
MKURUGENZI Mtendaji wa Makampuni ya Global Group, Eric Shigongo amempongeza Rais Dk John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kipekee wa kutoifunga Tanzania (lockdown) katika kipindi hiki cha Ugonjwa wa COVID-19 na kuwataka wananchi wake kuendelea kuchapa kazi huku wakichukua tahadhari za kujikinga na janga hilo kama mamlaka za afya zinavyoelekeza ili kunusuru uchumi wa Taifa letu.
Akizungumza na Shirika la Habari la Sauti ya Amerika (Voice of America- VoA), Shigongo amesema uamuzi wa Rais Magufuli ni wa kijasiri kwa kiongozi yeyote shupavu na kwamba hali hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa kutokushusha uchumi wa Taifa licha ya janga hilo kutikisa dunia nzima.
“Kwa kweli ninaweza kusema Rais Magufuli ana maono makubwa, amesema siwezi kukopi na kupesti njia wanazotumia wengine, badala yake ni kuwaruhusu wananchi waendelee kuchapa kazi huku wakichukua tahadhari. Jifikirie Tanzania ifungwe hata kwa miezi mitatu au sita, hali ya uchumi wake itakuwaje? Sisi tutaendelea kumuunga mkono kwa kila jema anachokifanya kwa manufaa ya Tanzania yetu," alisema Shigongo.
Akizungumzia hali ya biashara katika janga hili la Corona, Shigongo amesema Global Publishers imeanzisha mifumo mbalimbali ya biashara zake mitandaoni kwa njia za kidijitali ambapo wasomaji wa magazeti yote yanayochapishwa na kampuni hiyo; Uwazi, Amani, Risasi, Ijumaa, Ijumaa Wikienda, Championi na Spoti Xtra sasa wanaweza kuyapata kupitia Application ya Global App wakanunua na kusoma kirahisi kabisa kwa njia ya simu au kompyuta zao hata kama wakiwa nyumbani.
Licha ya hivyo, Shigongo amebainisha pia kuwa, Global Group ina Televisheni ya Mtandaoni ya Global TV Online na Radio ya Mtandaoni ya +255 Global Radio, kurasa za mitandao ya kijamii ya Facebook, Twitter na Instagram ambazo zote kwa pamoja zimekuwa zikiwapasha habari wananchi kwa njia ya mtandao.
Akijibu swali la Mtangazaji wa VoA, Paul Ndiho kuhusu iwapo ataingia kwenye siasa mwaka huu, Shigongo amesema ikimpendeza Mungu atagombea Ubunge katika Jimbo la Buchosa, Sengerema mkoani Mwanza kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu (2020).
“Ikimpendeza Mungu nitawawakilisha Bungeni wananchi wenzangu wa Jimbo la Buchosa kupitia chama changu cha Mapinduzi (CCM), ninaaamini ninao uwezo mkubwa wa kuongoza, wananchi wa Buchosa wananihitaji niwatumikie, kupitia Ubunge nitaweza kupaza sauti zao na kuwasemea Bungeni..... na kwa kuishirikiana na Serikali yetu pendwa kupeleka maendeleo makubwa Buchosa na Tanzania kwa ujumla,” alisema Shigongo.