Habari Mbaya kwa Watu Wote kama ilivyoandikwa na 'Raia Fulani' | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Habari Mbaya kwa Watu Wote kama ilivyoandikwa na 'Raia Fulani'

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Raia Fulani, Apr 24, 2012.

 1. Raia Fulani

  Raia Fulani JF-Expert Member

  #1
  Apr 24, 2012
  Joined: Mar 12, 2009
  Messages: 10,219
  Likes Received: 83
  Trophy Points: 145
  Ikawa siku ile mbele ya Baraza la saba la kutunga haki akatokea mfuasi machachari kati ya wale wazee 323 wa Baraza akasema, "Je, hawa watajwao kati yetu hawajafanya kosa? Tazama mikono yao ilivyochafuka damu. Wamezitapanya nyara za wana wa nchi na kurarua vifua vyao na kuziteketeza roho za wapiga kura wetu. Wametapanya chakula na kujiogesha na mvinyo wa gharama. Wameivika mioyo yao uziwi na upofu hata wasisikie vilio vya wana wa nchi. Wamezini na kufanya uasherati juu ya katiba na sheria na sera na taratibu na kanuni tulizojiwekea. Je, haiwapasi watu hawa kufungwa jiwe la kusagia shingoni mwao na kutoswa baharini?"

  Ndipo kiongozi wa Baraza aliposimama na kusema, "Lawezaje hili kutendeka, nasi hatuna mamlaka toka juu? Yeye aliyewakweza ndiye atakayewatweza."

  Neno likamjia tena Yule mfuasi machachari kusema. Naye akajawa na Roho wa ujasiri na kunena, "Mama yangu na mkubwa wangu, kama itapendeza mbele ya nafsi yako adhimu, nilete hoja mbele yako ya kumfunga shingoni jiwe la kusagia kiongozi wa mawaziri hawa walio mbele ya Baraza lako tukufu. Huyu tuna mamlaka naye. Na huyu tukushamtosa ndani ya kina cha Nungwi, itampendeza mkuu wa nchi kuvunja Baraza lao na kutenganisha kati ya ngano safi na magugu."

  Ndipo kiongozi wa Baraza aliposimama tena huku akiwa amejawa na ghadhabu. Akasema, "Ewe mfuasi mtukutu, mawazo yako yamejaa ubatili, nayo yanaelekea kushindwa." Akafungua juzuu lililoko mbele yake na kusoma toka huko haya yafuatayo;


  1. Mwanabaraza yoyote anaweza kutoa taarifa ya maandishi kwa kiongozi wa Baraza ya kutaka kuleta hoja ya kutokuwa na imani na kiongozi wa mawaziri kwa mujibu wa aya ya 53A ya juzuu hii;
  2. Hoja yoyote ya kutaka kupitisha Azimio la kumtosa kiongozi wa mawaziri kwenye kina cha Nungwi haitatolewa mbele ya Baraza endapo;
   • Haina uhusiano na utekelezaji wa majukumu ya kiongozi wa mawaziri yaliyoainishwa katika aya ya 52 ya juzuu;
   • Hakuna madai kwamba kiongozi wa mawaziri amevunja sheria ya maadili ya utumishi wa juu, ya wana wa nchi;
   • Haijapita miezi sita tangu alipoteuliwa; au
   • Haijapita miezi tisa tangu hoja kama hiyo ilipotolewa mbele ya Baraza na Baraza likakataa kuipitisha.
  3. Hoja ya kutokuwa na imani na kiongozi wa mawaziri haitajadiliwa na Baraza kama;
   • Taarifa ya maandishi iliyowekwa saini na kuungwa mkono na wanabaraza wasiopungua asilimia 20 ya wanabaraza wote itatolewa kwa kiongozi wa Baraza, siku zisizopungua 14 kabla ya siku iliyokusudiwa kuwasilishwa mbele ya Baraza…

  Nazo siku zilizosalia zilikuwa tatu tu ili Baraza liahirishwe hadi mwezi wa sita wa mwaka.
  Ikawa Yule mfuasi machachari aliposikia hayo, kwa hali ya unyenyekevu kabisa akasimama tena na kunena na kiongozi wa Baraza. Akamwambia, "Kama juzuu isemavyo, Niruhusu mimi na wenzangu 70 miongoni mwetu tukuletee majina na sahihi zetu panapo siku ya Jumatatu ili zipate Baraka na kibali mbele yako ya kutekelezwa kwa hoja yetu yenye azma ya kumtosa kiongozi wa mawaziri katika Baraza lijalo."

  Naye kiongozi wa mawaziri huku akijua anawindwa ili kutoswa kina cha Nungwi, akafanya hila na kupenya kati yao akaenda mahali panapo utulivu huku akifanikiwa kuwakutanisha wale alio na nasaba nao. Akawaambia, "Nafsi yangu imejaa ukiwa hata natamani kulia. Ama nilie?"

  Nao wafuasi wale wakamsihi sana asilie, ndipo alipotulia na kuwaambia, "Chombo chetu ki katika maji ya kina kirefu cha bahari. Nayo bahari imeghadhabika. Mawimbi yanakipiga chombo, nacho kinakaribia kuzama kutokana na wingi wa shehena. Tukimwaga shehena yote baharini hatutapata chakula cha kutufikisha Pwani. Tutafia majini. Sasa basi, kwa kuwa bado chombo kimelemewa, nasi ni wengi himu chomboni, na tupige kura kwa watu nane hivi ili nao tuwatose baharini."

  Ikawa yapata majira ya saa sita hivi usiku hata zoezi la kuwapata wale nane lilipokamilika. Wale wafuasi waliobakia wakawafunga wale nane kwa kamba kuzunguka miili yao. Nao wale waliosalimika wakasimama kwa ahueni na hudhuni, Wakawa wakisubiri amri ya kuwasukumia wale nane baharini toka kwa kiongozi wa mawaziri, ambaye nae alionekana kujawa na huzuni sana moyoni.

  Na tazama, sauti ikasikika toka katika kipaza sauti ndani ya kile chombo. Nao wakataharuki Wakawa wakiisikiliza ile sauti. Sauti ikasema, "Hamna mamlaka ya kutoa uhai wa wenzenu. Mimi ndiye mwenye mamlaka hayo! Tazama, kama itampendeza Yule aliye juu kabisa, dhoruba hii itapita na mambo yatakuwa shwari. Wafungueni wenzenu na muwaache huru. Rudini Barazani walipo mahasimu wenu nami nitatoa maelekezo ya nini cha kufanya."

  Ikawa usiku ikawa asubuhi siku ya Jumatatu. Ndipo Baraza lilipokusanyika tena wakiwapo wale manusuru ambao bado walionekana wangali wakiweweseka. Naye mkuu wa Baraza akaketi mahali pa juu kabisa. Mahali pa mamlaka. Naam, mahali palipotukuka. Naye akishakukaa akatoa dua, kisha agizo kwa Baraza kuanza.

  Nalo Baraza likaanza kuchambua hoja moja baada ya nyingine kwa mapana na membamba na marefu na mafupi yake, na wala pasionekane lolote lililo jipya kati ya yote yaliyozungumzwa.

  Ikawa asubuhi ikawa mchana siku hiyo ya Jumatatu. Naye mkuu wa Baraza akiwa na mamlaka rasmi, alisimamisha Baraza na kuwapa wanabaraza muda wa kutosha wa kwenda kuongeza uhai.

  Ikawa mchana ikawa alasiri siku hiyo ya Jumatatu. Na wana wa nchi toka pande zote wakatega macho na masikio yao katika vyombo rasmi na visivyo rasmi vya taarifa, wakisubiri kwa hamasa na ari na shauku na tashwishi na kiwewe, kuona hukumu ya haki iliyotabiriwa kutokea. Nao wana wa Jamiiforums walikuwa mstari wa mbele katika kupashana habari juu ya yale yanayoendelea ndani ya Baraza lile tukufu.

  Nao wanabaraza wakapewa tena muda wa kuwasulubu wale manusuru kwa hoja na takwimu na data na ushahidi, ya kwamba ni kwa nini wasifungwe

  mawe ya kusagia na kutoswa baharini? Na yote haya yangetekelezwa kwa namna ambayo ingempendeza Jemedari mkuu kuyatolea maamuzi.

  Na muda wao ulipokoma, ndipo mkuu wa Baraza aliposimama na kuwapa manusura muda wa kujitetea. Nao wakajitetea kwa hoja na hisia na huruma, ya kwamba ni chuki na ghiliba na vijiba vya roho na husuda na vivu wa wachache waliokosa nafasi hizo adhimu ndio sababu ya wao kupendekezwa kutoswa baharini kwa namna ambavyo ingempendeza Jemedari mkuu kuyatolea maamuzi.

  Lakini wanabaraza huku wakijawa na jazba na ghadhabu walipiga kelele wakisema, "Na watoswe baharini! Watoswe baharini!"

  Nao umagamba ukaufanya moyo wa mkuu wa Baraza kuwa mgumu, wala asisikilize kilio cha wanabaraza. Akasema, "Niliyosema, nimeshayasema! Ni kwa namna ambayo itampendeza Jemedari mkuu pekee kuyatolea maamuzi. Nami ndiye mwenye kauli ya Mwisho miongoni mwenu."

  Haya yote yalitokea na kutendeka ili lile neno lililoandikwa lipate kutimia.

  Nalo ni hili;

  Ee mkuu mfalme wa kisasi
  Mfalme wa kisasi uangaze!
  Mwenye kuhukumu nchi, ujitukuze
  Uwape wenye kiburi stahili zao.

  Mkuu hata lini wasio haki,
  Hata lini wasio haki watashangilia?
  Ee mkuu wanawaseta watu wako
  Wanawatesa warithi wako

  Nao husema, mkuu haoni
  Mfalme wa wote hafikiri
  Enyi wajinga miongoni mwa watu, fikirini
  Enyi wapumbavu, lini mtakapopata akili?

  Aliyelitia sikio mahali pake asisikie?
  Aliyelifanya jicho asione?
  Awaadhibuye mataifa asikemee?
  Amfundishaye mwanadamu asijue?

  Lakini mkuu amekuwa ngome kwetu
  Na Mfalme wetu mwamba wetu wa kukimbilia
  Naye atawarudishia uovu wao
  Atawaangamiza katika ubaya wao
  Naam, mkuu, Mfalme wetu atawaangamiza.

  Nao wana wa nchi wakiwa hawaamini kwa kile kinachotokea mbele ya macho na masikio yao, ndipo Yule mwana mpendwa wa mkulima, mkuu wa mawaziri aliposimama na kuijongelea mimbari kwa ajili ya kutoa neno la hitimisho. Nayo maneno mengi yakamtoka kinywani. Maneno yaliyoandikwa juu ya gome. Naam, maneno mengi.

  Hapo ilikuwa yapata saa moja usiku, nae alikuwa Akiendelea kushukuru na kupongeza na kushauri na kukemea na kusisitiza na kusihi, wala asijue kuwa wana wa nchi walikuwa na kiu nyingine. Kiu ya kusikia jambo jipya. Kiu ya kusikia habari njema.

  Hata alipofikia tamati, hapakuwako na neno lolote la kuwafariji wana wa nchi kwa maana walitamani mioyoni mwao kusikia, "Yanipasa kujivua gamba", wala wasisikie.

  Naye akiisha kusema hayo, akahitimisha kwa kuahirisha Baraza la saba hadi mwezi wa Juni wa mwaka bila kwa neno la matumaini kwa wana wa nchi. Ndipo waliposema, "Hakika mwana wa mkulima mwoga!"
   

  Attached Files:

 2. Smile

  Smile JF-Expert Member

  #2
  Apr 24, 2012
  Joined: Jul 18, 2011
  Messages: 15,427
  Likes Received: 194
  Trophy Points: 160
  Ikawa mchana ikawa alasiri siku hiyo ya Jumatatu ................................
   
 3. PhD

  PhD JF-Expert Member

  #3
  Apr 24, 2012
  Joined: Jul 15, 2009
  Messages: 3,819
  Likes Received: 818
  Trophy Points: 280
  jamani huyu mtu ni hodari sana wa kutengeneza makala murua kama hii
   
 4. Lukolo

  Lukolo JF-Expert Member

  #4
  Apr 24, 2012
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 5,137
  Likes Received: 76
  Trophy Points: 145
  Duh, mimi nilifikiri nchi imepinduliwa, kumbe ni marudio ya yale yaliyotokea. A good article anyway.
   
 5. Speaker

  Speaker JF-Expert Member

  #5
  Apr 24, 2012
  Joined: Aug 12, 2010
  Messages: 6,357
  Likes Received: 21
  Trophy Points: 135
  Hakuna mbaya zaidi ya hii.

  [​IMG]
   
 6. Raia Fulani

  Raia Fulani JF-Expert Member

  #6
  Apr 24, 2012
  Joined: Mar 12, 2009
  Messages: 10,219
  Likes Received: 83
  Trophy Points: 145
  kwa mambo yalivyo ni kama imepinduliwa tu
   
 7. KOMBESANA

  KOMBESANA JF-Expert Member

  #7
  Apr 24, 2012
  Joined: Jun 18, 2009
  Messages: 862
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 35
  ujumbe ni mzito,mzito mno kwa aina ya wanasiasa tuliowakubalia kuka madarakani!Usitamke hekima kwa mpumbavu,hawezi kuifurahia
   
 8. muonamambo

  muonamambo JF-Expert Member

  #8
  Apr 24, 2012
  Joined: Sep 3, 2010
  Messages: 769
  Likes Received: 44
  Trophy Points: 45
  Tumezunguka sana mlima huu sasa tugeukia upande wa kaskazini
   
 9. Mungi

  Mungi JF Gold Member

  #9
  Apr 24, 2012
  Joined: Sep 23, 2010
  Messages: 16,986
  Likes Received: 443
  Trophy Points: 180
  Kwani nchi kupinduliwa nani kakuambia ni habari mbaya?
  Nchi kupinduliwa ni hatua moja kuelekea kwenye ukombozi.
  Duniani kote, pale jeshi linapogundua serikali imeshindwa kuwatumikia wananchi, na kuna chama ambacho kinatetea maslahi ya umma lakini inashindwa kutokana na utawala wa mabavu, linaipindua hiyo serikali kandamizi, na kuikabidhi kwa wananchi kwa njia ya haki, kwa maana ya kufanya uchaguzi wa kidemokrasia, ambapo taratibu zote za uchaguzi unaratibiwa na jeshi.
  Kwa mfano jeshi letu ukiacha Shimbo na Mwamunyange wakiwemo wafuasi wachache, wanaelewa jinsi serikali yetu ilivyoshindwa kuwatumikia wananchi, wanaelewa jinsi serikali yetu inavyowakumbatia waizi.
   
 10. MNYISANZU

  MNYISANZU JF-Expert Member

  #10
  Apr 24, 2012
  Joined: Oct 21, 2011
  Messages: 7,056
  Likes Received: 41
  Trophy Points: 145
  Well said. Viongozi wa majeshi ndio kikwazo cha mapinduzi nchini. Wanajeshi wa kawaida wanataka sana kuipindua serikali ila viongozi wao ndio stumbling blocks.
   
 11. KML

  KML JF-Expert Member

  #11
  Apr 24, 2012
  Joined: Apr 2, 2012
  Messages: 863
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 35
  great thinker
   
 12. jouneGwalu

  jouneGwalu JF-Expert Member

  #12
  Apr 24, 2012
  Joined: Apr 11, 2011
  Messages: 2,680
  Likes Received: 62
  Trophy Points: 145
  Dah Raia Flani we ni mkali!
  Umenikumbusha Shaaban Robert....
  Ntaidownload nkifika kwa pc!
  Fani ambayo imenogesha sana, kwa haya yaliyotokea kwenye baraza hili kweli yanatakiwa kuwekwa kwenye fasihi....
   
 13. jouneGwalu

  jouneGwalu JF-Expert Member

  #13
  Apr 24, 2012
  Joined: Apr 11, 2011
  Messages: 2,680
  Likes Received: 62
  Trophy Points: 145
  Kwani hii uliyoitoa hapa ni simulizi kamili au ni sehemu tu!
  Natamani nione hyo sehemu ya mapinduzi labda kizazi hiki kinaweza kung'amua kitu!
   
 14. Edson

  Edson JF-Expert Member

  #14
  Apr 24, 2012
  Joined: Mar 7, 2009
  Messages: 9,202
  Likes Received: 720
  Trophy Points: 280
  kuna waandishi wa habari wavivu wa kufikiri ..hii makala utaikuta kwenye magazeti yao ya jumapili....wamekopy na kupaste..  hongera kwa uandish mahiri
   
 15. Raia Fulani

  Raia Fulani JF-Expert Member

  #15
  Apr 24, 2012
  Joined: Mar 12, 2009
  Messages: 10,219
  Likes Received: 83
  Trophy Points: 145
  Angalau nashukuru kwa kunikubali
   
 16. Raia Fulani

  Raia Fulani JF-Expert Member

  #16
  Apr 24, 2012
  Joined: Mar 12, 2009
  Messages: 10,219
  Likes Received: 83
  Trophy Points: 145
  pamoja ssana
   
 17. dudus

  dudus JF-Expert Member

  #17
  Apr 24, 2012
  Joined: Feb 28, 2011
  Messages: 7,765
  Likes Received: 6,087
  Trophy Points: 280

  Ha ha ha ha ha! And all nine bullets hit the target perfectly!
   
 18. Raia Fulani

  Raia Fulani JF-Expert Member

  #18
  Apr 24, 2012
  Joined: Mar 12, 2009
  Messages: 10,219
  Likes Received: 83
  Trophy Points: 145
  Nadhani kwa sasa hiyo inatosha kutufikirisha
   
 19. Elli

  Elli JF-Expert Member

  #19
  Apr 24, 2012
  Joined: Mar 17, 2008
  Messages: 26,822
  Likes Received: 10,120
  Trophy Points: 280
  I wish kufanya sponosrship ili ichapishwe kwene magazeti yooote yanayoyaoona haya....Huyu lazima atakua Naamani na Esther wa kwenye bible
   
 20. Nzi

  Nzi JF-Expert Member

  #20
  Apr 24, 2012
  Joined: Oct 21, 2010
  Messages: 12,858
  Likes Received: 4,537
  Trophy Points: 280

  MNYISANZU. Popote pale penye mapinduzi ya kijeshi, wanajeshi wa kawaida ndiyo wahusika wakuu. Tena wenye vyeo kama kapteni na luteni ndiyo wafanya mapinduzi,kwani wao ndiyo wenye wanajeshi,kupitia vikosi.

  Hivyo wanajeshi wetu hawana ujasiri kama tulivyo sisi raia wa kawaida.
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
Loading...