Habari Huduma ya kwanza kwa mtoto aliye na joto kali

Sema Tanzania

JF-Expert Member
May 18, 2016
251
465
Aghalabu, kupanda kwa joto la mtoto au homa kali kwa lugha ya kitabibu husababisha wasiwasi mkubwa kwa wazazi ama walezi walio wengi hususan katika miezi michache ya kwanza ya maisha ya mtoto baada ya kuzaliwa. Hata hivyo, ni vyema kutambua kwamba baada ya mtoto kuzaliwa, mfumo wake wa kinga huwa bado mchanga na mara nyingi hauna ufanisi sana katika kupambana na maambukizi.

Kwa nini joto la mwili wa mtoto hupanda?

Joto la mtoto huweza kupanda kutokana na kasi kubwa ya mashambulizi ya wadudu inayoathiri sehemu ya ubongo inayojulikana kama “hypothalamus”. Sehemu hii ndiyo inayoratibu masuala ya joto la mwili hivyo pindi inapozidiwa nguvu na kushindwa kutawanya joto ipasavyo, ndipo joto la mwili linapoongezeka na mtoto hupata joto kali ambalo mwishowe hupelekea homa.

Wataalamu wa afya ya mtoto hueleza kuwa mtoto atakuwa na homa kali iwapo joto la mwili wake litaongezeka na kufikia nyuzi joto 38 au zaidi katika kipimo cha sentigredi. Pamoja na kuwa homa yoyote kwa mtoto ni dalili ya wazi ya kuwepo kwa maambukizi kwa mtoto, joto la mtoto mchanga linaweza kuwa juu kufuatia nguo nyingi alizovikwa katika mazingira ya joto kiasi.

Sababu kuu inayopelekea mtoto kupandwa na joto kali ni ugonjwa wa malaria. Nyingine ni pamoja na magonjwa ya njia ya mkojo, magonjwa ya kifua, masikio na mengineyo. Shida ipo kwetu wazazi, kwani wengi wetu tuna changamoto ya namna ya kutambua ikiwa joto la mwili la mtoto linatosha kuitwa homa ili kuchukua hatua madhubuti. Hii ni kutokana na wengi wetu kutumia njia za zamani zilizozoeleka zinazohusisha kugusa au kuitazama miili ya watoto wetu badala ya kutumia kifaa maalum cha kupimia joto yaani; kipimajoto ama ‘themometa’ kama wengi wanavyokiita.

Ni muhimu kuelewa kwamba homa ni dalili ya tatizo lililo ndani ya mwili wa mtoto. Kama wazazi, pindi itokeapo hali ya namna hiyo kwa watoto wetu swali muhimu zaidi tunalopaswa kujiuliza ni je, mtoto ana hali gani? Swali hili linatupa nafasi ya kujiridhisha zaidi na hali walizonazo watoto pindi wanapougua ili kusudi tuchukue hatua za haraka ikiwemo kuwakimbiza katika kituo cha afya mara tu hali zao zinapobadilika.

Unamhudumiaje mtoto alie na joto kali?

Kutokana na mazoea, jadi na mapokeo kutoka kwa wazazi walitutangulia, utolewaji wa huduma ya kwanza kwa watoto wenye joto kali huelezwa tofauti na umekua ukiwakanganya wazazi na walezi walio wengi. Kutokana na mkanganyiko huo, ni muhimu sasa kufanya yafuatayo kwa minajili ya kuwapatia watoto huduma ya kwanza ya uhakika inayopendekezwa:-

Mosi, ili kuhakikisha tunawapatia huduma ya kwanza watoto walio na joto kali mahali popote kabla ya kuwafikisha katika kituo cha afya, ni muhimu tukatambua haja ya kumiliki kipimajoto ili kitusaidie katika kutambua joto walilonalo watoto wetu badala ya kukisia.

Pili, Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa ni vyema mtoto afutwe kwa maji ya uvuguvugu. Yawe maji ya kawaida tunayotumia kuwaogesha watoto, loweka kitambaa na umfute mtoto taratibu mwili mzima. Njia hii husaidia kushusha joto na kufikia kiwango ambacho ubongo utatambua joto hilo na kuendana nalo.

Aidha, unaweza ukayatumia maji haya ya uvuguvugu kwa kumuogesha mtoto moja kwa moja badala ya kumfuta kwa kitambaa. Usitumie maji ya baridi kwani maji hayo hayawezi kutuliza joto na badala yake hulishusha ghafla isivyotakiwa na huweza kupelekea athari kubwa kwa mtoto ikiwa ni pamoja na kupoteza fahamu.

Ieleweke kwamba, joto la mtoto linapopanda pasipo kushushwa huweza kupelekea mishipa midogo modogo ilio kwenye ubongo kupasuka na kusababisha damu kuvujia ndani na kupelekea mtoto kupoteza maisha. Ugonjwa wa degedege pia ni matokeo ya kupanda kwa joto ama homa kali katika mwili wa mtoto. Tunahitaji umakini mkubwa katika kulinda afya na maisha ya mtoto. Mtoto ni tunu ya wazazi, familia na Taifa. Tumlinde!

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom