Google yatishia kusitisha huduma zake Australia ikiwa Serikali haitabadili sheria mpya ya malipo ya maudhui, Facebook yafuata mkumbo

Sam Gidori

Senior Member
Sep 7, 2020
165
414
Kampuni ya Google imetishia kufunga huduma zake nchini Australia ikiwa Serikali ya nchi hiyo haitabadili muswada unaoitaka kampuni hiyo kulipia maudhui yanayotoka nchini humo.

Mkurugenzi Mtendaji wa huduma za Google Australia, Mel Silva aliiambia kamati ya Senate kuwa hatua hiyo ya serikali inawalazimu kuwafungia watumiaji wa huduma zao Austalia.

Muswada huo uliwasilishwa bungeni mwaka jana ili kulazimisha makampuni ya Google na Facebook kuvilipa vyombo vya habari vya Australia kwa kuchapisha maudhui yao la sivyo walipe mamilioni ya dola kama faini, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha makampuni makubwa ya kiteknolojia yanaendana na sheria za nchi hiyo. Sheria hiyo haitagusa mitandao ya Instagram na YouTube.

Kampuni ya Facebook nayo imeipinga sheria hiyo, ikisema haitaweza kufanya kazi katika hali yake ya sasa, ikitishia kuwa ikiwa itatekelezwa, itaacha kuchapisha maudhui ya habari kutoka Australia.

Facebook imefafanua kuwa wateja wake wa Australia wataendelea kupata huduma, ila hawataweza kuona maudhui ya habari kutoka Austalia.

Waziri Mkuu, Scott Morrison, ambaye serikali yake ilikubaliana na matakwa ya makampuni makubwa ya habari nchini humo kukabiliana na makampuni makubwa ya kiteknolojia ya Marekani ameonesha kukasirishwa na tishio hilo.

"Australia inaamua vitu gani mnaweza kuvifanya ndani ya Australia. Hilo linafanyika ndani ya bunge letu," Morrison aliwaambia Google.

Hatua hiyo ya Australia inatazamwa kwa ukaribu na vyombo vingi vya habari duniani ambavyo kwa siku za hivi karibuni vimekumbana na changamoto ya kukosa mapato yanayotokana na matangazo kwenda kwa makampuni hayo ya teknolojia. Sheria hiyo ya Australia ilitokana na utafiti uliogundua kuwa kwa kila dola 100 inayotumika katika matangazo, Google inachukua dola 53 na Facebook inachukua dola 28.

Tishio la Google linakuja muda mfupi baada ya kampuni hiyo kusaini mkataba wa dola bilioni 1.3 (Tsh trilioni 3.015) na makampuni ya habari ya Ufaransa kwa muda wa miaka mitatu kwa ajili ya kusambaza maudhui mtandaoni.
 
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom