Steve Dii
JF-Expert Member
- Jun 25, 2007
- 6,402
- 1,261
Ifuatayo ni habari njema kwa Watanzania, adha ya usafiri wa anga natumaini itapungua sasa..
Source: Mwananchi.co.tz
SteveD.
Kampuni ya Precisionair kuingiza ndege saba mpya Tanzania
Na Andrew Msechu
KWA mara ya kwanza nchini, Kampuni ya Precision Airlines imeingiza ndege moja mpya kati ya saba aina ya ATR 72-500, ikiwa ni sehemu ya mkataba wa Dola za Kimarekani 129milioni (zaidi ya Sh150 bilioni).
Ndege hiyo ni sehemu ya mkataba ambao ulisainiwa hivi karibuni kati ya Precision na Kampuni ya ATR ya Toulouse, nchini Ufaransa kwa ajili ya kuingiza ndege saba mpya na vifaa vya ndege za ATR kwa nchi zote za Afrika.
Akizindua ndege hiyo kwa niaba ya Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge jana, Kaimu Mkurugenzi wa Usafirishaji katika wizara hiyo, Kirenga Ndomino alisema hatua hiyo ya Precision, ni changamoto mpya katika sekta ya usafiri wa anga nchini, hasa katika kuimarisha sekta ya uzalishaji na utalii wa ndani.
Ndomino alisema uamuzi wa Precision kuingia mkataba huo mkubwa zaidi kati ya Precision na ATR ambao haujawahi kusainiwa na kampuni yoyote binafsi ya ndege nchini, hasa kwa ajili ya kuingiza ndege mpya saba ndani ya miaka mitatu, ni mfano wa kuigwa katika juhudi za kuboresha sekta ya usafirishaji wa anga nchini.
"Hii si ndege ya kwanza kuzinduliwa na Precision, lakini ukweli unabaki pale pale kuwa hii ni kampuni ya kwanza kuingiza ndege mpya nchini, pia imeweka historia ya kuwa kampuni ya kwanza Afrika Mashariki na kati kuagiza ndege mpya kutoka kiwandani baada ya kampuni ya Kenya Airways. Kampuni nyingine zimekuwa zikitumia ndege zilizokwishatumika," alisema Ndomino.
Aliongeza kuwa kwa kutambua mchango wa kampuni hiyo katika kuboresha sekta ya usafirishaji wa anga nchini, serikali inaendeleza juhudi za kufanya maboresho makubwa kwenye viwanja vya ndege nchini kwa kuanza kwa awamu ya pili ya ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Kiamataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, kuanzia mwezi ujao kwa gharama ya zaidi ya Euro25 milioni.
Kaimu Mkurugenzi huyo alisema ukarabati huo unaodhaminiwa na Benki ya Dunia, pia utaviwezesha viwanja vingine saba vya Arusha, Mafia, Bukoba, Shinyanga, Tabora, Kigoma na Sumbawanga kufanyiwa ukarabati mkubwa, mradi ambao tayari umeshaanza.
Mkurugenzi wa kampuni ya Precision, Alphonse Kioko alisema uamuzi wa kuwapo kwa sasa usafiri wa anga nchini unaweza kuwa rahisi zaidi kutokana na uamuzi wao wa kuingiza ndege mpya kutoka kiwandani, ambazo zitahakikisha usalama na mazingira mazuri zaidi kwa wateja na wao.
"Siku hii ya leo si ya kawaida kwetu, ni siku mpya katika utaratibu mzima wa utoaji wa huduma kwa wananchi wa Tanzania, tuna uhakika wa kuwahakikishia huduma bora zaidi, kwa haraka na raha zaidi, tunawashukuru wadau wetu wote waliotuwezesha kufika hapa tulipo leo" alisema Kioko.
Akizungumza katika makabidhiano ya ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 70, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Precision, Michael Shirima alisema ndege hiyo inaungana na ndege nyingine nne za Precision ambazo zinaendelea kufanya kazi nchini.
"Tunaamini kuwa kutokana na uhusiano mzuri uliopo baina ya Precision na serikali na wateja wake ni moja ya sababu kubwa ya kutufanya tuwepo hapa leo, pia uthabiti wa ndege hizi za ATR unatufanya tujisikie fahari ya kuwakaribisha na kuwahakikishia usalama na raha kila mnaposafiri na sisi," alisema Shirima.
Kampuni hiyo iliyoanzishwa mwaka 1996 pia inatarajia kuingiza ndege nyingine aina ya Boeing 737-300 mwishoni mwa mwezi huu, pia imethibitishwa na Shirika la Viwango vya Usalama wa Anga Duniani na kuwa mwanachama wa IOSA.
Source: Mwananchi.co.tz
SteveD.