Gharika Kuu kashfa ya Escrow bungeni Dodoma

Candid Scope

JF-Expert Member
Nov 8, 2010
11,879
1,250  • Pinda atakiwa kuachia ngazi kwa kuzembea
  • Werema kinara wa kufanikisha uchotwaji fedha
  • Wote watakiwa kung'oka, pia yumo Maswi, Maselle
Gharika la ‘Tegeta Escrow' limeikumba serikali baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na viongozi waandamizi kadhaa wa serikali kubainika kuhusika katika sakata la uporwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 ya fedha katika akunti hiyo iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Aidha, imependekezwa kwamba viongozi wa umma waliopata mgawo wa fedha hizo wafilisiwe na kuvuliwa nyadhifa zote mara moja.

Akiwasilisha mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), bungeni jana, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deo Filikunjombe, alisema uchunguzi umethibitisha kwamba Pinda alikuwa anaujua mchezo mzima kwa kuwa alikuwa akijulishwa kila hatua iliyokuwa ikiendelea, lakini hakuchukua hatua.

UHUSIKA WA PINDA
Filikunjombe alisema kamati hiyo ililazimika kupitia kwa umakini Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 iliyoainisha kazi na mamlaka ya Waziri Mkuu na kubaini kuwa, kwa mujibu wa Ibara ya 52 (1): Waziri Mkuu atakuwa na madaraka juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa siku hata siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Alisema Ibara ya 52 (2), inasema; Waziri Mkuu atakuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni.Alisema baada ya kusoma Ibara hizo, Kamati ilijiuliza maswali kadhaa ikiwamo (a) Je, Waziri Mkuu alikuwa anajua sakata la utoaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow? (b) Je, Waziri Mkuu alitimiza wajibu wake kwa mujibu wa Ibara ya 52(1)?

(c) Je, Waziri Mkuu wakati akitoa matamshi yake Bungeni alikuwa akitimiza wajibu wake kwa mujibu wa Ibara ya 52 (2)?
(d) Je, nini maana, uzito na ukweli wa matamshi ya mara kwa mara ya Waziri Mkuu ndani na nje ya Bunge kuhusiana na suala hili?
(e) Je, Waziri Mkuu alitoa maamuzi au maelekezo yoyote ya kuzuia jambo hilo lisifanyike?

Mheshimiwa Spika, baada ya kupitia vielelezo vilivyomo kwenye ripoti ya CAG, kamati imejiridhisha pasipo shaka kuwa, Waziri Mkuu, alikuwa ana taarifa zote kuhusiana na mchakato mzima wa kuchotwa fedha kutoka katika akaunti ya Escrow.

Alisema ushahidi uliopelekwa na CAG kwenye kamati unaonyesha kuwa Waziri Mkuu alikuwa akipata taarifa za jambo hilo lakini hakuchukua hatua zozote kuzuia muamala huo usifanyike.

Alisema kamati imethibitisha kwamba Waziri Mkuu alikuwa analijua jambo hilo vizuri na kwamba aliridhia muamala huo ufanyike na ndiyo maana katika maelezo yake ya bungeni mara kadhaa alithibitisha kuwa fedha za Escrow hazikuwa fedha za umma.

"Ni wazi kwamba maneno ya Waziri Mkuu hapa Bungeni yaliuaminisha umma kuwa fedha zile siyo fedha za umma kiasi kwamba gazeti la Serikali la Daily News la tarehe 1 mwezi Mei, 2014, likachapisha habari yenye kichwa kikubwa cha habari ‘IPTL clean Deal – Pinda'. Na ofisi ya Waziri Mkuu haikukanusha."

"Ni jambo la kushangaza kuona kwamba, jambo kubwa na zito kama hili lingeweza kufanyika bila ya mamlaka za juu, hususan Waziri Mkuu kufahamu."

Filikunjombe alisema kutokana na uzito na unyeti wa jambo hilo kwa vyovyote vile, Waziri Mkuu anapaswa kuwajibika kwa kauli zake na kwa kutokutekeleza wajibu wake wa kikatiba ipasavyo, ili kurejesha imani ya wananchi kwa serikali yao na viongozi wao wa kisiasa.

WAZIRI MUHONGO
Filikunjombe alisema Kamati imethibitisha kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, ndiye alikuwa dalali mkuu aliyewakutanisha Harbinder Singh Sethi na James Rugemalira, tena katika ofisi ya umma.

"Waziri wa Nishati na Madini alifanya udalali huo akijua dhahiri kuwa Sethi hana uhalali wa kisheria kufanya biashara kwa jina la IPTL," alisema Filikunjombe.

Alisema iwapo Waziri wa Nishati na Madini angetimiza wajibu wake ipasavyo, Fedha za Tegeta Escrow zisingelipwa kwa watu wasiohusika, na nchi ingeweza kuokoa mabilioni yaliyopotea kama kodi za VAT, Capital Gain Tax na Ushuru wa Stempu ambazo ni takribani Sh. bilioni 30.

"Mheshimiwa Spika, kamati inapendekeza kuwa kamlaka yake ya uteuzi itengue uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini kutokana sababu hizo zilizoelezwa."

MASWI
Katika mapendekezo hayo, kamati imetaka Maswi avuliwe wadhiwa wake na Takukuru imfikishe mahakamani haraka kwa kuikosesha serikali mapato, matumizi mabaya ya ofisi na kusaidia utakatishaji wa fedha haramu.

Alisema kamati imethibitisha kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini aliingia makubaliano ya kutoa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow bila kujiridhisha kikamilifu kuwa maamuzi ya hukumu ya ICSID 2 yalikuwa bado kutolewa na hivyo kusababisha fedha kutolewa bila kukokotoa upya gharama za ‘capacity charges', jambo ambalo limesababisha kupoteza fedha za umma.

"Vile vile, kamati imebaini kuwa, Katibu Mkuu hakufanya uchunguzi wa kina (due diligence) kujiridhisha uhalali wa kampuni ya Mechmar kuuzwa kwa Piperlink na baadaye kuuzwa kwa PAP, na hivyo kusababisha fedha za akaunti ya Tegeta Escrow kulipwa kwa asiyestahili na kinyume cha mkataba wa akaunti ya Escrow."

Filikunjombe aliongeza kuwa: "Kwa maana hiyo, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, pengine kwa uzembe wake ama kwa kukusudia kwa sababu anazozijua yeye mwenyewe zaidi, amesaidia uchotwaji na hatimaye utakatishaji wa fedha haramu."

Alisema kamati pia imethibitisha uzembe wa hali ya juu uliofanywa na Maswi kushindwa kujiridhisha kama masharti ya Sheria ya Kodi ya Mapato Sura ya 333, Kifungu cha 90(2) ambacho kinaitaka mamlaka ya ‘approval'' ya uhamishaji wa makampuni kutotambua kampuni mpaka kwanza kodi za uhamishaji ziwe zimelipwa na hati za malipo ya kodi zimetolewa na mamlaka ya kodi.

BODI YA TANESCO
Alisema kamati imejiridhisha kuwa Bodi ya Shirika la Ugavi wa Umeme Nchini (Tanesco) bila sababu zozote za msingi ilikataa mapendekezo ya menejimenti ya shirika ya kutoruhusu uchotwaji wa fedha kutoka BoT akaunti ya Tegeta Escrow na hivyo kusababisha kulikosesha shirika fedha zake inazohitaji sana kutokana na hali mbaya ya Shirika.

"Kamati inaitaka serikali kuvunja mara moja Bodi ya Tanesco na Takukuru iwafungulie mashtaka ya matumizi mabaya ya ofisi wajumbe wote waliohusika kupitisha maamuzi hayo ya kifisadi, ili iwe fundisho kwa wajumbe wengine wa bodi za mashirika ya umma kwamba watahukumiwa kwa maamuzi mabovu wanayoyafanya.

STEPHEN MASELE
Kuhusu Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Filikunjombe alisema kamati imethibitisha kuwa alisema uongo bungeni kwa kutamka kauli ambazo zilizokuwa na lengo la kupotosha umma kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow, ikiwamo kauli ambazo zingeweza kusababisha nchi kuingia kwenye mgogoro wa kidiplomasia na nchi ya Uingereza.

"Kamati inapendekeza kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini achukuliwe hatua kali za kinidhamu ikiwamo kutenguliwa uteuzi wake. Kamati pia inapendekeza kuwa Naibu Waziri huyu afikishwe mbele ya Kamati ya Bunge ya Maadili ili aadhibiwe kama Mbunge kwa kusema uwongo bungeni ili liwe fundisho kwa wabunge wengine kuhusiana na kauli wanazotoa ndani ya Bunge lako tukufu."

AG JAJI WEREMA
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, ametajwa kuhusika katika kashfa hiyo kwa kutoa ushauri ulioipotosha BoT kuhusiana na hukumu ya Jaji Utamwa.
Imebainika pia kuwa Jaji Werema, alitumia madaraka yake vibaya na kuagiza kodi ya serikali yenye thamani ya Sh. 21 bilioni isilipwe na hivyo kuikosesha serikali mapato adhimu.

"Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kujua na kwa makusudi alilipotosha Bunge na Taifa kwamba mgogoro uliopelekea kufunguliwa kwa Akaunti ya Escrow ulikuwa ni mgogoro wa Wanahisa wa IPTL badala ya mgogoro kati ya Tanesco na IPTL. Kamati inapendekeza kuwa uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali utenguliwe mara moja na kisha afikishwe mahakamani kwa matumizi mabaya ya Ofisi yaliyopelekea Serikali kupoteza mabilioni ya fedha.

HUKUMU YA JAJI UTUMWA
Kamati hiyo imesema kuwa hukumu ya Jaji Utamwa ya kukabidhi masuala yote ya IPTL kwa Kampuni ya PAP, ilitafsiriwa vibaya na Harbinder Singh Sethi mwenyewe na baadaye ikatafsiriwa vibaya pia na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na hata baadhi ya viongozi wakuu wa Serikali akiwamo Waziri Mkuu.
Filikunjombe alisema uchunguzi ulibaini kuwa Kampuni ya PAP haikuwa na uhalali wowote wa umiliki wa IPTL wakati inalipwa fedha za kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.

HARBINDER
Kamati imependekeza kuwa Takukuru na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) wamkamate mfanyabiashara Harbinder Singh Sethi na kumfikisha mahakamani kwa makosa ya Anti money laundering, ukwepaji kodi na wizi.

Kamati pia inaelekeza Serikali kutumia sheria za Nchi, ikiwamo sheria ya ‘Proceeds of Crime Act' kuhakikisha kuwa Harbinder Singh Sethi anarejesha fedha zote alizochota kutoka Benki Kuu ya Tanzania."

MENGINEYO
Filikunjombe alisema Kamati imethibitisha bila chembe ya mashaka kwamba mchakato mzima wa kutoa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow uligubikwa na mchezo mchafu na haramu wenye harufu ya kifisadi ulioambatana na udanganyifu wa hali ya juu ambao kwa kufuata sheria tu ungeweza kugundulika na kuzuiwa.

Alisema kutokana na mchezo huo mchafu, mfumo mzima wa Serikali ni kama ulipata ganzi au uliganzishwa ili kuwezesha uporwaji huo wa Sh. bilioni 306 na kutakatishwa kupitia Benki mbili hapa Nchini na baadhi ya mabenki ughaibuni.

Kamati hiyo pia imependekeza kuwa kutokana na kukua na kukomaa kwa vitendo haramu vya wizi wa fedha ama mali za umma na kukua ama kukomaa kwa vitendo vya rushwa kubwa na uhujumu uchumi, inapendekezwa kwamba Bunge lako Tukufu liridhie kuitaka Serikali kuanzisha kitengo maalumu cha kushughulikia rushwa kubwa (grand corruption) kitakachokuwa na nguvu ya kuendesha mashtaka kwa uhuru kamili, na kwamba Bunge lako Tukufu liridhie kuanzishwa kwa Mahakama Maalum ya kushughulikia Rushwa kubwa itakayoshughulikia kesi za rushwa zitakazokuwa zikipelekwa kwake na kitengo maalum cha kushughulikia rushwa kubwa.KUNA KITU KINAKUJA HAPA MAONI YA WABUNGE
Wabunge wametoa maoni tofauti kuhusu taarifa maaumu ya PAC kufuatia matokeo ya ukaguzi wa CAG katika akaunti ya Tegeta Escrow, baadhi wakiiunga mkono na wengine wakisema inahitaji ufafanuzi zaidi.

Walitoa maoni hayo baada taarifa hiyo kuwasilishwa na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe na Makamu wake, Deo Filikunjiombe, bungeni.

DK. LIMBU
Mbunge wa Magu (CCM), Dk. Festus Limbu, alisema pamoja na kazi ya PAC kutimiza hadidu rejea walizopewa na Spika wa Bunge, kuna mambo yanayohitaji kutolewa ufafanuzi, ikiwamo kuelezwa waliopokea fedha hizo kutoka kwa waliochota kama nao pia waliohojiwa na kamati au la.

LEMBELI
Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli, aliunga mkono taarifa ya PAC na kusema wote waliotajwa kila mmoja abebe msalaba wake kwa kuwa hakuna kitu anachokichukia duniani kama wizi.

BULAYA
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Esther Bulaya, alisema jambo hilo ni zito sana na kwamba, wabunge bipa kujali itikadi zao, walipiganie suala hilo na hatakubali kuona mwizi akiendelea kuwamo ndani ya Bunge bila kuchukukiwa hatua.

MASELE
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele, alisema haoni uhusiano wa mgogoro kati yake na balozi kuhusishwa na suala la Tegeta Escrow, hivyo ameshangazwa kuona anatajwa katika taarifa hiyo, ambayo haikuwamo kwenye hadidu za rejea.

NGELEJA
Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja, alisema ripoti ipo bungeni inasubiri kujadiliwa na taarifa itatolewa na makubaliano yatakubaliwa.

MBOWE
Mbunge wa Hai (Chadema), ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema taarifa ya PAC ni nzuri, lakini akasema ilipaswa kwenda mbali zaidi kwani kuna shinikizo kibwa lilikuwa likitoka kwa baadhi ya watendaji wa Ikulu katika uchotwaji wa fedha hizo.


Chanzo:Nipashe

 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom