NEEMA ya gesi ambayo imekuwa ikizungumzwa, inatarajiwa kubadili Mkoa wa Lindi, kupitia uwekezaji mkubwa ambao haujawahi kutokea katika historia wa miradi nchini, wenye thamani ya inayofikia zaidi ya dola za Marekani bilioni 60 na kutoa ajira karibu 20,000.
Taarifa za wadau wa miradi hiyo, ikiwemo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), zilizowasilishwa kwa wawakilishi wa wananchi mkoani Lindi wiki hii, zimebainisha kuwa miradi hiyo inahusu ujenzi wa Mradi wa Kusindika Gesi (LNG) na Kiwanda cha Mbolea.
Kwa mujibu wa taarifa za TPDC, tayari ardhi imepatikana hekta 2,071 kwa ajili ya mradi wa LNG, huku hekta zingine 20,000 zinazozunguka eneo la mradi huo, zikitengwa kwa ajili ya viwanda.
Kwa sasa kwa mujibu wa taarifa hiyo, TPDC imeshatwaa ardhi hiyo na kazi inayofanyika ni kufanya uthamini wa mali za wananchi wachache walio katika eneo hilo, kulipa fidia na kuwahamisha.
Mradi LNG
Akizungumza na wawakilishi hao, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk James Mataragio, amesema kwa kuwa gesi iliyogundulika baharini inayofikia kiasi cha futi za ujazo trilioni 47, ni nyingi na ikivunwa mahitaji ya ndani hayawezi kuimaliza, watalazimika kuiuza nje ya nchi na kuongezea Taifa mapato.
Kutokana na umuhimu huo wa kuuza gesi nje, Dk Mataragio alisema kitaalamu rasilimali hiyo inapaswa kutolewa kwenye visima na kufikishwa katika mtambo huo wa LNG, ambao utaigeuza kuwa kimiminika, ili ifae kuingizwa katika matangi na kusafirishwa kwa meli kwenda katika masoko mbalimbali duniani.
Akifafanua zaidi Mkurugenzi wa Utafiti wa TPDC, Kelvin Komba alisema mtambo huo utaipooza gesi itakayovunwa mpaka nyuzi joto sifuri na kuipooza zaidi mpaka nyuzi joto hasi 100, ndipo inakuwa kimiminika na kufaa kusafirishwa kwenda maeneo mbalimbali duniani.
Uwekezaji wenyewe
Taarifa za makampuni yanayoshirikiana katika ujenzi wa mtambo huo ambayo ni TPDC, BG Group, Ophir Energy, Statoil, ExxonMobil na Pavilion Energy, zimeeleza kuwa thamani ya mradi huo ni kuanzia dola za Marekani bilioni 30 mpaka dola bilioni 60.
Akifafanua ukubwa wa uwekezaji wenyewe, Makamu wa Rais wa BG Group Tanzania, Sera, John Ulanga kwa niaba ya wawekezaji hao, amesema Bajeti ya Serikali ya Tanzania ni kama dola za Marekani bilioni 10 mpaka 15, kwa hiyo uwekezaji huo ni sawa na kukusanya mapato ya Serikali kwa miaka minne, yasitumike popote, isipokuwa Lindi.
Ajira Mbali na ukubwa wa mradi kwa maana ya kiwango cha fedha kitakachowekezwa, Mkurugenzi wa Utafiti wa TPDC, Komba alisema wakati wa ujenzi wa mradi huo utakaochukua miaka minne mpaka saba, kutatolewa ajira za moja kwa moja zinazokadiriwa kufikia 15,000.
Baada ya ujenzi, wakati wa uendeshaji wa mradi huo kwa mujibu wa Komba, ajira katika mradi huo zitakazotolewa ni za watu 5,000.
Mbali na ajira, Komba ametaja fursa zingine zitakazotokana na uwekezaji huo unaotarajiwa kuanza wakati wowote, kwamba ni huduma kwa wafanyakazi hao ikiwemo usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.
Nyingine ni fursa za ukuzaji wa biashara mkoani Lindi, upanuzi wa makazi, ongezeko la mahitaji ya umeme, fursa za kampuni za ulinzi na uanzishwaji wa vyuo vya mafunzo mbalimbali ya taaluma zinazohitajika.
Pia kutakuwa na fursa kwa kampuni za ujenzi kwa ajili ya kazi mbalimbali za ujenzi, uunganishaji vyuma, mahitaji makubwa ya vifaa vya ujenzi ikiwemo saruji, vyuma, vifaa vya umeme na mengine.
Mradi huo pia utatoa fursa za huduma za forodha na uhamiaji, huduma za viwanja vya ndege, uboreshaji wa bandari, huduma za benki, afya, elimu, bima, kreni za kupandisha mizigo katika majengo marefu, huduma za mawasiliano na zingine nyingi.
Mradi mwingine Mbali na mradi huo wa kusindika gesi, TPDC kupitia ubia, inatarajia kuanza ujenzi wa kiwanda cha mbolea katika Wilaya ya Kilwa, kitakachohitaji uwekezaji mwingine wa dola za Marekani bilioni 2, ambacho kitatoa ajira zingine 5,000.
Tayari TPDC imeshaingia mkataba na makampuni matatu ya Ferrostaal Industrial Projects GmbH ya Ujerumani, Fauji Fertilizer ya Pakistan na Haldor Topsoe ya Denmark, kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho.
Baada ya mkataba huo kwa mujibu wa taarifa hizo, TPDC na washirika hao wataunda kampuni ya pamoja itakayoitwa Tanzania Mbolea and Petrochemical Company (TMPC), ambayo itazalisha tani 2,200 za mbolea ya ammonia kwa siku na tani 3,850 za mbolea ya urea kwa siku.
TPDC katika mradi huo kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo gazeti hili linazo, itaanza kumiliki asilimia tano ya hisa kwa kutoa eneo lake la ardhi na taratibu, itanunua hisa mpaka kufikia asilimia 40 ya hisa.
Mbolea ya mradi huo, inatarajiwa kuuzwa nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Ikweta, ambazo zimekuwa zikiagiza mbolea nje ya eneo hilo.
Tayari utafiti umeonesha kuwa kiwanda hicho kitakachotumia gesi kuzalisha mbolea, kitakuwa na soko la bidhaa hiyo la nchini linalofikia tani 204,527 za mbolea; Uganda tani 18,510; Kenya tani 276,878; Zambia tani 200,411; Malawi tani 376,862; Madagascar tani 21,157; Afrika Kusini tani 585,419 na Msumbiji tani 48,392.
Source: Habari Leo