Geranimo E.K.I.A: Kutoka Makao Makuu ya CIA Langley, Oparesheni Ya Kukamatwa Osama Bin Laden

Jina lako la "NI MTAZAMO TU", limesadifu uzi wako.

Aiseeeeh, bora uombe mods waufute huu uzi maana ni aibu.

Maana, ni mataputapu kabisa.
 
Haha ni kama kukwapua simu Ubungo mataaa halaf unaenda kumuuzia mtu Mbezi kumbe ndio mwenye simu!
Mbona Shigongo na makala zake mlikuwa mnanunua sana au mnafikiri alikuwa anataka wapi ,ok ila mimi naamin katika akili 2 huleta uhuru wa kifikra.
 
Binadamu wengine bana.....wewe umekopi kazi ya mtu wa humu humu, tena umeikopi humu humu, halafu mbaya zaidi ukaileta humu humu, unataka tukupe likes, na comments za kutosha

Hayo ni mambo ya kike ndugu yangu usipende vya mteremko, utakuja pakatwa siku moja..

Shwain......
 
Twende pamoja sasa.
Mwaka 2001, mwezi Desemba katika milima ya
Tora Bora baada ya mapambano ya siku kumi na
moja toka tarehe 6 hadi 17 na mabomu kadhaa
kudondoshwa katika milima hiyo hatimaye askari
wa miguu walianza zoezi la kuikagua milima hiyo
kuangalia kama kuna masalia yoyote muhimu
yanayoweza kuwapa fununu ya kuielewa vita
waliyoianzisha kati yao Majeshi ya Marekani na
Wanamgambo wa Taliban.
Katika mchakato huo wa ukaguzi wanajeshi wa
marekani walifanikiwa kumuokota kijana mmoja wa
umri wa mika 21 akiwa hai. Baada ya kumuokota
wanajeshi kadhaa wakampakia katika chopa ya
kivita na kurudi nae katika kambi ya kijeshi ya
Bagram Air Base iliyo nchini Afghanistan.
Baada ya kufika katika kambi ya Bagram wanajeshi
wakaanza kumuhoji kijana huyo ajieleze yeye ni
nani na alikuwa anafanya nini katika milima ya Tora
Bora.
Baada ya kujitambulisha kijana huyo akawaeleza
kuwa alikuwa anawinda katika milima hiyo ya Tora
Bora na kwa bahati mbaya akajikuta ameingia
kwenye eneo ambalo hakujua kuwa kulikuwa na
mapigano ya kijeshi.
Maafisa wote wa kijeshi hawakuamini maelezo
haya na waliendelea kumuhoji kwa siku kadhaa
lakini yule kijana alishikilia maelezo yake yale yale
kuwa alikuwa anawinda milimani.
Baada ya kutokuwepo kwa mafanikio yoyote ya
kumuhoji kijana huyu Maafisa wa ngazi za juu wa
kijeshi katika kituo cha Bagram wakawasiliana na
maafisa wa CIA waliopo nchini Afghanistan na
kuwaeleza juu ya tukio hilo. Maafisa hao
wakawashauri kuwa kijana huyo wakabidhiwe wao
ili wamuhoji wao kwa kina.
Siku tatu baadae kijana huyo akakabidhiwa kwa
maafisa wa CIA na wao wiki moja baadae
wakamsafirisha kutoka Afghanistan mpaka kwenye
jela za siri (Black Sites) za CIA zilizopo ulaya katika
nchi ya Romania na baadae akaamishiwa jela za siri
nchini Poland.
Baada ya kijana huyo kufikishwa huko mahojiano
yakaendelea na akaendelea kushikilia msimamo
wake kuwa alikuwa anawinda kwenye milima ya
Tora Bora. CIA ikaamua kupanua wigo wake zaidi ili
wamtambue. Wakachukua alama zake za vidole na
kuziingiza katika mfumo wa alama za vidole wa nchi
karibia zote za kiarabu lakini wakapata matokeo
sifuri, hakukuwa na taarifa zozote zinazoshabihiana
alama za vidole za kijana huyo.
Hii ilikuwa na maana nyingi lakini maana moja
kubwa ni kwamba kijana huyu hakuwa na rekodi
yoyote ya uhalifu katika maisha yake, alikuwa ni
'raia mwema'!
CIA wakaanza kuhisi labda kijana huyu kweli
hakuwa na hatia yoyote. Lakini kabla hawajalipa
nafasi wazo hilo kukua kwenye vichwa vyao,
wakaakua wafanye kitu cha kubahatisha,
wakaingiza alama za vidole za kijana huyo katika
mfumo wa kiusalama wa nchini kwao marekani na
matokea ambayo waliyapata hakuna ambaye
aliweza kuamini.
Kumbukumbu za mifumo ya kiusalama ya nchi za
marekani zilionyesha kuwa mtu mwenye alama hizo
za vidole zinafanana kabisa na mtu ambaye alijaribu
kuingia nchini marekani siku ya tarehe 3 Agosti
2001 katika uwanja wa ndege wa Orlando, Florida
akitokea Dubai.
Maafisa wa uhamiaji wa uwanja wa ndege
wakamkataa kuingia nchini marekani kutokana na
sababu kadhaa. Kwanza kijana huyo alikuwa na
fedha dola 2,800 pekee na hii iliwapa shida maafisa
wa uhamiaji kuelewa angewezaje kuishi nchini
marekani? Pili kijana huyu alikuwa amekata tiketi ta
kwenda pekee (one way ticket).
Sababu hizi mbili zilipelekea maafisa wa uhamiaji
wa uwanja wa ndege kuhisi kijana huyu alikuwa na
mpango wa kuwa muhamiaji haramu kwani dalili
hizo zilionesha kuwa hakuwa na mpango wa kurudi
tena kwao. Hivyo basi maafisa hao wa uhamiaji wa
uwanja wa ndege wa Orlando wakamkataa kijana
huyo juingia nchini marekani na wakamrudisha
alikotokea.
Maafisa wa CIA walishitushwa na jambo hili na
wakawasiliana na vyombo vingine vya usalama
nchini Marekani na pasipo kupoteza muda maafisa
kutoka shirika la upelelezi la FBI wakafika katika
uwanja wa ndege wa Orlando, Florida ili wapate
taarifa zaidi kuhusu nini hasa kilitokea siku ya
Agosti 3 2001 siku ambayo kijana huyo alikataliwa
kuingia nchini marekani.
Baada ya FBI kufika uwanja wa ndege waliomba
kuzungumza na maafisa uhamiaji waliokuwepo siku
ya tarehe 3 Agosti pia waliomba wapatiwe mikanda
ya video ya kamera za ulinzi za uwanja wa ndege.
Baada ya kuangalia mikanda hiyo ya video, FBI
waligundua jambo kubwa zaidi ambalo
hawakulitegemea kabisa. Kamera za ulinzi zilizo nje
ya uwanja zilirekodi gari inayomilikiwa na Mohamed
Atta likiwa limepaki nje ya uwanja wa ndege.
Kwa wasiomfahamu Mohammed Atta ndiye alikuwa
mtekaji kiongozi wa watu walioteka ndege za
kimarekani na kwenda kuzigongesha katika
magorofa ya WTC siku ya tarehe 11, Septemba
2001. Pia ndiye aliyeendesha moja wapo ya ndege
hizo zilizotekwa.
Kwahiyo FBI wakang'amua kuwa siku hiyo
Mohammed Atta alifika uwanja wa ndege kumpokea
kijana huyo lakini kwa bahati mbaya maafisa
uhamiaji walimkataa asiingie Marekani.
Hii ilikuwa na maana kwamba kama kijana huyu
asingelitiliwa shaka na maafisa wa uhamiaji basi
alitakiwa kuwa mojawapo ya washiriki walioteka
ndege na kuzilipua katika majengo ya WTC siku ya
Septemba 11, 2001.
Taarifa hizi ziliishitua FBI na pasipo kuchelewa
wakawataarifu maafisa wa CIA katika jela ya siri
nchini Poland ambako kijana huyu alikuwa
anashikiliwa, na baada ya maafisa hawa kupata
taarifa hii mara moja wakawasiliana na Makao
Makuu ya CIA Langley, Virginia nchini Marekani.
Mara baada ya taarifa hizi kufika Makao Makuu ya
CIA, Mkurugenzi wa CIA Bw. Leon Panetta
akaamuru kijana huyo awekwe 'mahali salama' kwa
ajili ya 'mahojiano' zaidi.
Ndege ikaandaliwa na safari ya kuelekea gereza la
Guantanamo Bay ikaanza.
Jina halisi la kijana huyu anaitwa Mohammed al-
Qahtani kipindi anakatwa alikuwa na umri wa miaka
21 na kwa sasa ana miaka 36 na ni mfungwa
namba 63 (ISN 10063) katika gereza la Guantanamo
Bay.
NDANI YA GUANTANAMO: 'MAHOJIANO' ZAIDI
Baada ya kijana al-qahtani kufikishwa katika gereza
Guantanamo ambapo aliwekwa selo katika jengo
lililoitwa Camp Delta 'mahojiano' zaidi yakaendelea.
Licha ya mambo yote ambayo vyombo vya usalama
viligundua juu yake lakini kijana yule aliendelea
Kushikilia msimamo wake kuwa alikuwa anawinda
kwenye milima ya Tora Bora.
Ilifikia hatua mpaka Katibu mkuu kiongozi wa
makamu wa rais wa kipindi hicho Bw. David
Addington pamoja na mshauri wa ikulu Bw. Alberto
Gonzales walifika binafsi katika jengo la Camp Delta
ndani ya gereza la Guantanamo mahsusi kwaajili ya
kuongea na kijana al-qatani ili aeleze ukweli lakini
kijana huyo akashikilia msimamo kuwa yeye ni
muwindaji.
Ndipo hapa ilipofikia hatua hii Waziri wa Ulinzi wa
Marekani wa wakati huo akaidhinisha 'Mbinu za
Mahojiano Zilizoboreshwa' (Enhanced Interrogation
Techniques) zitumike kumuhoji kijana huyo.
Mbinu hizi zilizoboreshwa zilikuwa zinajumuisha
kwa mfano kutesa mfungwa kwa kumnyima pumzi
kimateso kwa kumiminia maji (waterboarding),
mikao ya msongo (stress positions), kumnyima
usingizi n.k.
Uamuzi huu ulikuja kuleta mushkeli na watu wa haki
za binadamu miaka iliyofuata.
Baada ya maafisa waliokuwa wanamuhoji kupewa
idhini ya kutumia 'mbinu zilizoboreshwa'
inasemekana kwamba kijana al-Qahtani ndiye
mmoja wa wafungwa wa Guantanamo waliovunja
rekodi kwa kuhojiwa muda mrefu zaidi kwa 'mbinu
zilizo boreshwa'. Inasemekana kijana al-Qahtani
alihojiwa kwa siku 48 mfululizo!
Baada ya 'mahojiano ya kina' yaliyochukua siku 48
kwa kutumia 'mbinu zilizoboreshwa' hatimae al-
Qahtani akafunguka na kueleza ukweli.
Kwanza akakiri kuwa jina lake ni Mohammed al-
Qahtani na ni raia wa Saudi Arabia.
Pia akakiri kuwa ni yeye ndiye aliyekataliwa kuingia
nchini Marekani siku ya Tarehe 3, Agosti 2001 na
akaeleza kuwa alipewa maagizo na mtu anayeitwa
Khalid Sheikh Mohammed ili aje marekani kwaajili
ya kazi maalumu. Pia alieleza kuwa aliwahi
kupatiwa mafunzo maalumu ya utendaji wa
kishushushu na mawasiliano ya usiri (Operational
training in Covert Communications) na aliyempatia
mafunzo hayo alijulikana kama Abu Ahmed al-
Kuwait.
Baada ya kupewa maelezo haya ilikuwa ni hatua
kubwa kiasi kwa CIA lakini bado kulikuwa na
mambo kadhaa hayakuwa sawia.
Kwa upande Khalid Sheikh Mohammed (KSM) mtu
ambaye kijana huyu alimtaja kuwa ndiye
alyemuagiza aje Marekani, mtu huyu alikuwa
anafahamika vizuri na CIA. Walimfahamu kuwa
ndiye moja wa Lutenati wa ngazi za juu wa kikundi
cha Al Qaeda na ndiye 'mchora ramani' wa
mashambulizi ya septemba 11, 2001.
Lakini mtu wa pili (Abu Ahmed al-Kuwait) aliyetajwa
na huyu kijana kuwa ndiye aliyempatia mafunzo
kijana juu ya ushushushu na mawasiliano ya siri,
mtu huyu CIA walikuwa hawamfahamu. Ndio ilikuwa
mara yao ya kwanza kulisikia jina hilo.
Hivyo basi kipaumbele kikawekwa kwamba kijana
huyu 'ahojiwe' zaidi ili atoe taarifa zitakazofanikisha
kumpata KSM (Khalid Sheikh Mohammed) 'mchora
ramani' wa mashambulizi ya Septemba 11.
Mahojiano kwa kutumia mbinu zilizobordshwa
yakaendelea.
Kwa msaada wa maelezo waliyoyapata kutoka kwa
kijana al-Qahtani maafisa wa CIA kwa kushirikiana
na maafisa wa ISI (Inter-Service Intelligence - Idara
kuu ya masuala ya usalama na ushushushu nchini
Pakistani) walifanya oparesheni maalumu ya
kumkamata KSM (Khalid Sheikh Mohammed) baada
ya kumuwinda kwa muda mrefu sana na hatimae
siku ya Machi 1, 2003 walifanikiwa kumkamata KSM
akiwa hai katika katika jimbo la Ralwapindi nchini
Pakistani.
Baada ya kukamatwa tu na taarifa hiyo kufika
makao makuu ya CIA Langley, Mkurugenzi mkuu
Bw. Panetta akaamuru KSM awekwe 'mahali
salama' mara moja. Na pasipo kupoteza muda siku
hiyo hiyo CIA wakampandisha ndege KSM na
kumpeleka gereza la Guantanamo. Na baada ya
KSM kupokelewa Guantanamo alipewa selo kwenye
jengo mojawapo la Guantanamo linaloitwa Camp
Echo na akatambulika kama mfungwa namba ISN
10024.
Kesho yake 'mahojiano ya kina' yakaanza kwa
kutumia 'mbinu zilizoboreshwa'.
Haikuchukua siku nyingi za 'mahojiano' KSM
akaanza kufunguka na kusema ukweli. Kwanza
akakiri kuwa yeye ndiye 'mchora ramani' wa
shambulizi la Septemba 11, na ni moja ya
malutenati wanaotegemewa na Al Qaeda katika
kueneza propaganda za kikundi hicho. Akakiri
kuhusika kutafuta vijana watakaotekeleza
shambulizi hilo, akakiri kusaidia baadhi yao kupata
mafunzo ya urubani na akakiri kusaidia kuwaingiza
marekani vijana hao.
Maafisa wa jeshi na CIA walimbana zaidi KSM
aeleze ni namna gani wanaweza kuwapata viongozi
wa ngazi za juu wa Al-Qaeda na hasa hasa kiongozi
mkuu lakini jibu la KSM liliwashangaza kila mtu.
KSM akawaeleza kuwa hata yeye afahamu kiongozi
mkuu yuko wapi au anapatikanaje.
Mwanzoni walihisi anawadanganya lakini baada ya
'kumbana' zaidi wakagundua kuwa anamaanisha
kuwa hajui 'kiongozi mkuu' yuko wapi wala namna
ya kumpata.
KSM akawaeleza kuwa kiongozi mkuu, Osama Bin
Laden aliacha kutumia simu toka mwaka 1998
maada ya mawasiliano yake ya simu ya satelaiti
kudukuliwa na CIA na kuponea chupu chupu
kuuwawa na wanajeshi wa kimarekani.
Akawaeleza kuwa tangu hapo aliacha kutumia na
mawasiliano ya simu na mawasiliano yote mengine
ya kisasa na kwa upande wa mawasiliano akawa
muumini wa falsafa ambayo imekuja kutumiwa na
karibia maafisa wote wa ngazi za juu wa vikundi
vya wapiganaji katika mashariki ya kati, kwamba;
"If you live like you are in the 'past', the 'future' will
never find you"! (Ukiishi kama upo kwenye nyakati
za zamani, usasa hautakukamata kamwe).
Kwa hiyo mawasiliano yote yalikuwa yanafanyika
kwa mdomo kutoka kwa mtu kwenda kwa mtu au
kwa barua za kuandika kwa mkono.
CIA wakambana zaidi aeleze je yeye alikuwa
anapataje maagizo kutoka kwa kiongozi mkuu na
akawajibu kulikuwa na mtu mmoja tu ambaye
alikuwa anaaminika kwa asilimia mia moja na
kingozi mkuu na ndiye aliyekuwa 'mpambe' wa
karibu wa Bin Laden na kwamba kwa miaka kadhaa
wapiganaji wa Al-Qaeda wala malutenati wa ngazi
za juu walikuwa hawajawahi kumuona Bin Laden
wala hawajui alipo na maagizo yote waliyapata kwa
mdomo kutoka kwa mtu mmoja pekee aliyeitwa Abu
Ahmed al-Kuwait.
Maafisa wote wa jeshi na CIA waliduwaa. Hii ilikuwa
ni mara ya pili wanasikia jina hili. Mara ya kwanza
walilisikia kutoka kwa kijana al-Qahtani kuwa
alipatiwa mafunzo ya ushushushu na Abuu Ahmed
al-Qahtani na sasa wanaelezwa na KSM ambaye ni
lutenati wa ngazi za juu kabisa wa Al Qaeda kuwa
hajawahi kumuona kiongozi mkuu kwa miaka
kadhaa na maagizo yote yalikuwa yanaletwa kwake
na mtu anayeitwa Abu Ahmed al-Kuwait.
Kitu kilichowasahangza zaidi CIA ni kwamba
walikuwa wanawafahamu viongozi na malutenati
wote wa ngazi za juu wa Al Qaeda lakini jina hili
lilikuwa jipya kwao. Hawakuwahi kumsikia Abu
Ahmed al-Kuwait.
Wakiwa bado wapo kwenye mshangao wapigani wa
kikurdi kutoka nchini Iraq wakawasiliana na serikali
ya marekani kuwaeleza kuwa wamemkamata
Hasaan Ghul moja ya mawakala wa Al Qaeda
anayetegemewa nchini Iraq.
CIA wakampakia Hassan Ghul kwenye ndege na
kumpeleka kwenye jela za siri nchini Romania.
Baada ya 'kumuhoji' kwa siku kadhaa Hassan Ghul
akawaeleza kuwa maagizo yote kuhusu
mashambulizi na mipango mingine anayapata
kutoka kwa kiongozi mkuu Osama Bin Laden kupitia
kwa mtu anayemfahamu kwa jina la Abu Ahmed al-
Kuwait.
Mshangao wa CIA ukageuka kuwa kitendawili. Huyu
Abu Ahmed al-Kuwait ni nani na wanawezaje
kumpata?
Mkurugenzi Mkuu wa CIA akaamuru kuwa
kumtambua na kumkamata Abu Ahmed al-Kuwait
kiwe kipaumbele namba moja..
Baada ya mchakato wa muda mrefu hatimae
mwaka 2007 CIA walifanikiwa kumtambua Abu
Ahmed al-Kuwait ni nani! Wakafanikiwa kupata jina
lake halisi (Ibrahim Saeed Ahmed) na kwamba
mwanzoni alikuwa ni mwanafunzi wa KSM kabla
hajapanda ngazi kuwa mpambe wa Bin Laden.
Baada ya kumfahamu kwa kiasi CIA wakaanzisha
mpango maalum wa kumchunguza ili wapate taarifa
zaidi juu yake. Ili waweze kumpata kirahisi CIA
wakafanya zoezi maalum la kuwatambua ndugu
zake mbali mbali waliokuwa wanaishi kwenye nchi
tofauti tofauti za kiarabu.
Baada ya kuwatambua ndugu hao CIA wakafanya
kazi ya kudukua mawasiliano ya simu ya ndugu
zake na katika kitu kimojawapo ambacho
walikigundua ni kwamba ndugu zake hao walikuwa
na desturi ya kuwasiliana na namba za simu tofauti
tofauti lakini zote zikiwa ni za Pakistan. Hii
ilipelekea CIA kuhisi kwamba namba hizi ni za al-
Kuwait lakini alikuwa anazibadilisha mara kwa mara
ili kuepuka kugundulika.
Kwahiyo walichofanya CIA ni kusubiri siku ambayo
ndugu yoyote wa al-Kuwait akipiga simu yoyote
kwenda nchi ya Pakistan basi wataifuatilia namba
hiyo ili wafahamu ni nani aliyekuwa anaongea naye.
Siku hiyo haikukawia sana kwani mwaka 2010
ndugu mmoja wapo alipiga simu kwenda Pakistan
katika mji wa Pashwar. Kwa kutumia Wapalestina
waliokuwa wanafanya kazi kwaajili ya CIA
waliifuatilia simu hiyo mjini Pashwar na kuthibitisha
kuwa aliyekuwa anaongea na simu hiyo alikuwa ni
Abu Ahmed al-Kuwait. Baada ya al-Kuwait kumaliza
kuongea na simu aliingia ndani ya gari na kuondoka
na wapelelezi hao wakamfutilia kwa makini wajue
anakoelea.
Pasipo kujua kuwa anafuatiliwa al-Kuwait
aliendeshe gari mpaka mji wa Abbottabad. Na
alipofika Abbottabad akaingia kwenye Jumba moja
la kifahari. Jumba hili lilikuwa na muonekano na
ulinzi uliotia shaka. Na hii ikapelekea CIA kuamini
kuwa ndani ya jumba hilo hakuwa al-Kuwait pekee
anayeishi bali kuna uwezekano mtu wa hadhi ya juu
zaidi alikuwa anaishi humo ndani. Pengine labda
kiongozi mkuu wa Al Qaeda, Osama bin Laden labda
alikuwa ni mkazi humo ndani.
Waziristan Haveli
Baada ya CIA kugundua nyumba hii na kuitilia
mashaka kuwa kuna uwezekano inamuhifadhi
kiongozi wa hadhi ya juu wa Al Qaeda pengine labda
Osama bin laden mwenyewe, hivyo wakaingiza
wapelelezi katika mji wa Abbottabad ambao
walinunua nyumba mjini hapo kama raia mwingine
wa kawaida. Baada ya wapelelezi hao kufanikiwa
kufanya mkazi mjini Abbottabad wakaanza kazi ya
kukusanya taarifa juu ya jumba hilo na wakazi
wake.
Wapelelezi hao ambao walikuwa ni raia wa Pakistan
wanaofanya kazi kwa niaba ya CIA wakaanza
kuwadodosa majirani na wakafanikiwa kupata
taarifa za kutosha kiasi.
Kwanza majirani waliwaeleza kuwa jumba hilo
linamilikiwa na mtu wanayemfahamu kama Arshad
Khan (Abu Ahmed al-Kuwait) ambaye anaishi na
kaka yake pamoja na familia zao. Majirani
wakaeleza kuwa Arshad amewaeleza kuwa kuwa
yeye ni msimamizi wa biashara za Hoteli za familia
yao zilizopo Dubai. Pia majirani walimueleza kuwa
Arshad (al-Kuwait) alikuwa ni 'mtu wa watu' na
alikuwa anahudhuria karibia kila msiba mtaani
kwao.
Pia walielezwa kuwa licha ya kuwa na uwezo wa
kifedha huwa anapenda kufanya manunuzi ya
mahitaji yake ya nyumbani hapo hapo mtaani na
mara kwa mara hutoka na watoto wake kwenda
kuwanunulia mikate kwenye duka la uokaji (bakery)
mtaani hapo.
Pia majirani waliwaeleza kuwa wamezoea kuliita
jumba hilo Waziristan Haveli (Waziristan Mansion
(Kasri la Waziristan)) kwani waliamini kuwa wakazi
wa jumba hilo wanatokea Waziristan.
Baada ya CIA kupata taarifa hizi kutoka kwa
wapelelezi waliojipenyeza mtaani hapo wakaamua
wapanue wigo zaidi kwa kuwahusisha kitengo
Maalumu cha Taifa la Marekani chini ya wizara ya
ulinzi (DOD) kinachohusika na kukusanya taarifa na
Ushushushu wa kijiografia (National Geospatial-Intt
elligence Agency - NGA) ili wafahamu nukta baada
ya nukta ya jumba hilo.
Kwa kutumia picha za satelaiti na kukusanya picha
kwa kutumia ndege inayojiendesha yenyewe (drone)
NGA walipata taarifa zote muhimu kuhusu jumba
hilo kuziwasilisha CIA.
Taarifa yao ilieleza kuwa jumba hilo lililoitwa
Waziristan Haveli lipo umbali wa takribani kilomita
moja na nusu kutoka kituo cha mafunzo ya kijeshi
cha Abbottabad cha jeshi la Pakistan. Mtaani
ambao jumba hili lilikuwepo ulikuwa na makazi ya
wastaafu wengi wa jeshi la Pakistan.
Jumba hili lilichukua eneo kubwa zaidi kuliko
nyumba nyingene za jirani kwani jumba lilijengwa
kwenye eneo la ardhi lenye ukubwa la takribani
mita za mraba 3,500.
Jumba hili lilizungukwa na ukuta wenye urefu wa
futi 12 lakini ndani yake ukiingia unakutana na eneo
la wazi tupu alafu anakuta ukuta mwingine wenye
urefu wa futi 18. Kuta zoto hizi juu yake zilikuwa na
waya za miba miba na umeme.
Pia jumba hili lilikuwa na ghorofa tatu na katika
balkoni ya gorofa ya tatu ilikuwa na ukuta wake wa
kuikinga wenye urefu wa futi 7. Pia kulikuwa na
kamera za ulinzi katika kila kona ya jumba hili.
Pamoja na hayo pia NGA waligundua kuwa ndani ya
jumba hilo kulikuwa na bustani kubwa iliyopandwa
mboga mboga, pia kulikuwa na kuku zaidi ya 100,
sungura pamoja na ng'ombe mmoja.
Pia jumba hili lilikuwa na mdirisha madogo na
machache kiasi kwamba ukiliangalia haraka haraka
unaweza kudhani halina madirisha kabisa.
Pia idara ya ushushushu wa kijiografia ya Marekani
NGA ilifanikiwa kukusanya taarifa za wakazi wa
jumba hilo ambapo walifanikiwa kung'amua kuwa
Kasri hilo lilikuwa na wakazi wapata 22 wanaoishi
ndani yake wengi wao wakiwa ni watoto. Pa
waling'amua kuwa kulikuwa na takribani wakazi
watani ambao kamwe walikuwa hawatoki nje ya
jumba hilo.
Baada ya NGA kuwasilisha taarifa yao kwa CIA
kuhusu vile walivyovibaini kuhusu jumba hili,
Mkurugenzi Mkuu wa CIA Bw. Leon Panetta alizidi
kushawishika kuwa Kasri hili lilikuwa linamuhifadhi
kiongozi wa hadhi ya juu wa Al Qaeda na pengine ni
Bin Laden mwenyewe anaishi humo.
Hivyo basi akaamuru ufanyike uthibitisho wa
mwisho kuhakiki kama ni kweli kile anachokihisi.
CHANJO FEKI
Mkurugenzi Mkuu wa CIA Bw. Pattena alitaka
kwanza kuhakiki kama hisia zao ni za kweli kuwa
Bin Laden anaishi kwenye Kasri hilo. Hivyo basi
maafisa wa CIA wakaja na mpango kuwa wafanye
uhakiki wa uwepo wa familia yake na kama familia
yake ipo kwenye jumba hilo basi hapana shaka Bin
Laden atakuwepo ndani ya hilo Kasri.
Kwahiyo maafisa hao wakaemweleza mkurugenzi
wao wanachotakiwa ni kupata sampuli za vinasaba
(DNA) za watoto wanaoishi ndani ya jumba hilo.
Kwahiyo mkakati ukawekwa kwamba ifanyike
chanjo feki ili wapate fursa ya kuingia kwenye
jumba hilo kuwahudumia watoto na wakifanikiwa
kuingia watatumia mbinu kadhaa kuchukua sampuli
za vinasaba za watoto eidha kwa kubakiza damu
kiduchu za hao watoto kwenye sindano ya kutolea
chanjo au mbinu nyinginezo.
Ili kufanikisha azma hii CIA walimuendea Daktari
Bingwa aliyeitwa Shakil Alfridi ambaye alikuwa
ndiye daktari mkuu katika maeneo ya Khyber
mpakani na Afghanistan.
CIA wakafanikiwa kumshawishi daktari Hugo
ashiriki kwenye mpango huo wa kutoa chanjo hiyo
feki.
Baada ya kufanikiwa kumshawishi Dk. Shakil
matangazo yakawekwa kuhusu mpango wa kutoa
chanjo katika eneo hilo kwa mwezi February na
Mwezi April 2011. Ili kuwapiga chenga serikali ya
mji wa Abbattobbad wasihusike kwenye zoezi hilo
Dk. Shakil alieleza kuwa amepata ruzuku kutoka
mashirika ya kimataifa ili atoe chanjo hiyo bure na
chanjo hiyo ni ya kuwakinga watoto dhidi ya
Hepatitis B.
Hivyo basi alifanya zoezi lake kwa Uhuru pasipo
kuingiliwa na watu wa serekali za mitaa na manesi
ambao walijumuika nae kutoa chanjo hiyo walipata
posho iliyoshiba.
Ili kuepuka watu kuanza kuuliza maswali na kuwa
na wasiwasi, alianza kutoa chanjo hiyo katika mitaa
wanayoishi masikini kama vile mitaa ya Nawa Sher.
Alifanya hivyo kwa mwezi February na aliporejea
tena alitoa chanjo hiyo katika mtaa wanaoishi watu
matajiri katika mji wa Abbattobad yaani mtaa wa
Tabil ambapo ndipo kulikuwa na hilo jumba
linalotiliwa mashaka.
Ilipofika zamu ya kutoa chanjo kwa watoto waliopo
ndani ya hilo jumba walikaribishwa kwa ukarimu na
Dk. Shakil mwenyewe akabaki nje getini na
akamruhusu nesi aliyeitwa Bakhto aingie ndani ya
kasri atoe 'chanjo' kwa watoto.
'Chanjo' ikatolewa, zoezi likaisha Dk. Shakil na
manesi wake wakarejea Khyber na kukabidhi
sampuli walizozipata kwa CIA.
Sampuli zikasafirishwa mpaka marekani,
zikafanyiwa uchambuzi wa DNA kisha
ikalinganishwa na DNA ya dada yake Osama Bin
Laden aliyefariki dunia mwaka 2010 jijini Boston
nchini Marekani kwa uvimbe kichwani.
Baada ya sampuli hizo za DNA kupimwa na
kulinganishwa, majibu yakapelekwa mezani kwa
Mkurugenzi Mkuu wa CIA Bw. Pattena. Baada ya
Pattena kuyaona majibu hayo akatabasamu mpaka
ufizi wa mwisho, akainua simu ya mezani na kupiga
ikulu ya Marekani na kuomba kuongea na Rais
Obama.
Mara baada ya kuunganishwa na Rais Obama,
Pattena akampa taarifa Rais, taarifa iliyosubiriwa
muda mrefu na kwa shauku kubwa, kwa kifupi
akamueleza Rais kwa furaha "we got
him.!" ("Tumempata.!")
OPARESHENI NEPTUNE SPEAR
Baada ya kupatikana uhakika kuwa Osama Bin
Laden anaishi ndani jumba hilo lililopo Abbottabad,
CIA wakafanya kikao maalum na Jemedali Msaidizi
(Vice Admiral) William H. McRaven ambaye ni
kamanda wa kitengo maalum kinachosimamia
oparesheni maalum zinazofanywa na majeshi yote
ya marekani ( Joint Special Operations Command -
JSOC) ambapo katika kikao hicho CIA walimpa
taarifa wa kila wanachokifahamu kuhusu makazi
hayo waliyoyagundua.
Baada ya kupewa taarifa hiyo, Admiral McRaven
akapendekeza kuwa wanaweza wakatuma kikosi
cha makomando kufanya uvamizi kwenye jumba
hilo lakini akawa na wasiwasi inaweza kuleta
mushkeli na jeshi la Pakistan ambalo lipo kilomita
moja na nusu tu kutoka makazi ya siri ya Bin Laden.
Baada ya majadiliano ya kina Admiral McRaven
akawaagiza maafisa kadhaa kutoka Jeshi la
Wanamaji (U.S. NAVY) kitengo cha Maandalizi ya ya
Mapigano/vita Maalum ( Special Warfare
Development Group - DEVGRU) kwamba waweke
ofisi ya muda makao makuu ya CIA Langley na
washirikiano kuandaa mpango maalumu utaoenda
kupendekezwa kwa Rais juu ya kushugjulikia
makazi yaliyoaminika kumficha Osama Bin Laden.
Baada ya miezi miwili ambayo DEVGRU waliitumia
kuaandaa mpango kwa kushirikiana na CIA
hatimaye wakawasilisha mapendekezo yao kwa
Mkurugenzi wa CIA Bw. Pattena na kwa waziri wa
ulinzi Bw. Robert Gates.
Kisha Rais Obama akaitisha kikao maalum cha
Baraza/kamati ya usalama ya Taifa ili kujadili suala
hilo.
Baada ya majadiliano marefu kwenye kikao hicho
ilionekana kuwa Rais Obama alipendelea zaidi
pendekezo la kulipua makazi hayo kwa bomu
kutoka angani. Lakini maswali yakaibuka je ni vipi
kama kuna handaki kwenye jumba hilo na Osama
labda huwa anakaa chini ya hilo handaki. Katika
upelelezi wao wote CIA hawakuweza kung'amua
kama kulikuwa na handaki katika jumba hilo ama la.
Kwa kuzingatia hivyo basi (uwepo wa handaki)
kama wataamua kulipua makazi hayo kwa bomu
basi itawabidi watumie bomu lenye uzito
usiopungua Kg. 910 ili liweze kusambaratisha
kabisa makazi hayo pamoja na handaki kama lipo.
Lakini pendekezo hili nalo likawa na changamoto
zake kwani kama litatumika bomu lenye nguvu
kubwa hivyo, kulikuwa na nyumba kadhaa za
majirani ambazo zitakuwa ndani ya kipenyo cha
mlipuko (blast radius). Pia kama makazi hayo
yangelipuliwa kwa bomu kusingekuwa na ushahidi
wowote wa kujiridhisha kuwa Osama ameuawa
kwenye shambulio hilo.
Baada ya kubainishwa kwa changamoto hizi katika
kikao kilichofuata cha kamati ya Usalama wa Taifa,
Obama akasitisha mpango huo wa kulipua makazi
kwa bomu usitekelezwe.
Chaguo la pili lilikuwa kwa makomando wa kikosi
cha Wanamaji (Navy) SEALs, wavamie makazi hayo
kwa kutumia helikopta maalum zinazoruka bila
kutoa kelele na sio rahisi kuonekana na Rada ya
adui. Chaguo hili lilikuwa ni zuri lakini lilikuwa na
changamoto moja kubwa. Kumbuka makazi haya
yapo karibu kabisa na kituo cha Kijeshi cha
Pakistani, itakuwaje kama wakishtukiwa kabla
hawajamaliza kutekeleza oparesheni?
Baadhi ya watu waliokuwepo kwenye kikao
akiwemo waziri wa ulinzi Bwa. Robert Gates
akapendekeza kuwa labda wawashirikishe watu wa
kitengo maalumu cha ushushushu cha Pakistan
(ISI). Wazo hili likapingwa vikali na Rais Obama
kuwa hawaamini hata chembe Wapakistani na
endapo wakiwaeleza kuhusu oparesheni hiyo basi
siku hiyo hiyo Osama ataamishiwa sehemu
nyingine.
Obama akapendekeza kuwa kama ikitokea
makomando wao wamekamatwa kabla
hawajamaliza oparesheni yao basi Admiral
McRaven atatakiwa ajiandae kumpigia simu Mkuu
wa Majeshi Pakistani Ashfaq Parvez Kayani
kumshawishi kuwaachia makomando hao wa
Marekani.
Lakini pia Obama akamuagiza Admiral McRaven
awaandae makomando wake kwa mapambano ya
kijeshi kama ikitokea wamepewa upinzani na
wanajeshi wa Pakistan na hawataki kuwaruhusu
waondoke.
Watu wote waliohudhuria kiako hicho cha kamati ya
usalama wakakubaliana na mpango huo wa
kuvamia makazi ya Bin Laden kwa kutumia
helikopta isipokuwa Makamu wa Rais Joe Biden
pekee aliupinga mpanga huo kwa asilimia zote.
Licha ya Makamu wa Rais kuupinga mpango huo,
siku ya tarehe 19 April kamati ya Usalama wa Taifa
ilipokutana tena Rais Obama akatoa idhini ya awali
kukubali oparesheni hiyo itekelezwe. Na ikapewa
jina Oparesheni Neptune Spear.
Kesho yake McRaven pamoja na kikosi chake cha
SEALs wakaondoka marekani kuelekea Afghanistan
ambapo walitumia takribani wiki mbili kufanya
mazoezi kuhusu oparesheni waliyoenda kuifanya.
Kikosi hiki kilifikia katika kambi ya Bagram nchini
Afghanistan na hapo palitengenezwa mfano wa
nyumba kama ile inayosadikiwa kumuhifadhi bin
laden na kikosi cha SEALs wakafanya wazoezi ya
kutosha jinsi watakavyotekeleza zoezi hilo.
Ilipowadia siku ya tarehe 29, Rais Obama alimpigia
simu Kamanda McRaven kumuuliza juu ya
maendeleo ya maandalizi. Pia akamuuliza kama
alikuwa na angalau ya chembe ya shaka kuhusu
kufanikiwa kwa oparesheni hiyo na kama alikuwa
na shaka yoyote basi oparesheni hiyo itahairishwa.
McRaven akamjibu kuwa vijana wake wako tayari
kwa kutekeleza Oparesheni.
Obama akawapa idhini ya mwisho kuwa
amewaruhusu kufanya oparesheni hiyo siku
itakayofuata yaani tarehe 30 April.
Kesho yake Obama akataarifiwa kuwa oparesheni
imehairishwa kwa muda wa siku moja kutokana na
hali ya hewa kutokuwa rafiki na badala yake
itafanyika kesho yake tarehe 1.
Jioni ya siku hiyo Obama akampigia simu tena
McRaven kumtakia kilala kheri yeye na makomando
wake wa SEALs na akwashukuru kwa kujitoa kwao
kwa ajili ya Taifa lao.
Siku ya tarehe 1 May ilipowadia wajumbe wa kamati
ya usalama wa taifa walikusanyika katika chumba
maalumu cha ikulu ya marekani (situation room)
kufuatilia oparesheni hiyo kupitia kwenye runinga
iliyokuwa inaonyesha picha za moja kwa moja
zilizokuwa zinachukuliwa ndege ya kujiendesha
(drone) iliyokuwa inafuatilia tukio zima la
oparesheni hiyo.
Usiku wa manane Makomando wa SEALs wapatao
79 waliruka na helikopta za kijeshi kutokea kambi
ya kijeshi ya Bagram mpaka eneo la mpakani
Jalalabad. Walipofika hapo wakagawana.
Makomando wapatao 24 pamoja na mbwa aina ya
Belgia Malinois aliyeitwa Cairo waliingia kwenye
helikopta mbili aina ya Black Hawk ambazo
zimeboreshwa kuzuia kuonekana na Rada ya adui
na kutotoa sauti.
Makomando waliosalia waliingia kwenye chopa
kubwa za kijeshi aina ya Chinook.
Makomando ambao walipanda kwenye chopa za
kivita aina ya Black Hawk hawa ndio walipewa
jukumu la kuvamia makazi ya Bin Laden.
Makomando wengine ambao walipanda kwenye
chopa kubwa za kivita aina ya Chinook hawa
watakaa maili kadhaa kutoka eneo la tukio kama
tahadhali ikitokea wenzao wakahitaji msaada zaidi.
Baada ya kujigawanya hivi safari ya kuelekea
kwenye makazi ya siri ya Bin Laden ikaanza.
Baada ya kuyafikia makazi ya Bin Laden Chopa
moja ilitua eneo la mbele ya jengo na nyingine ilitua
nyuma kwa juu na makomando wakashuka kwa
spidi ya haraka kwa kutumia kamba.
Chopa ambayo ilitua mbele ya jengo, rubani aliiweka
chini kwa makosa kidogo na kusababisha mkia wa
helikopta kugonga uzio wa ukuta wa nyumba na
almanusuura ipinduke chini juu lakini kwa ustadi
akaiweka sawa na makomando wakashuka salama
ingawa helikopta tayari ilikuwa imeharibika.
Baada ya makomando wote kufanikiwa kuingia
ndani ya uzio wakaanza kuisogelea mlango
mkubwa wa nyumba. Pembeni ya nyumba kubwa
kulikuwa na vyumba vichache vimejengwa kwa ajili
ya wageni na ndani yake walitokea wanaume wawili
waliokuwa na bunduki aina ya AK-47 na
kuwafyatulia risasi makomando wa SEALs.
Kabla watu hao hawajaleta madhara yoyote
makonmando wa SEALs waliwadondosha chini kwa
risasi mbili kila mmoja. Watu hawa wawili walikuja
kutambulika baadae kuwa ni Abu Ahmed al-Kuwait
pamoja na kaka yake aliyeitwa Abrar.
Kisha makomando wakaingia ndani ya nyumba. Na
baada ya kuingia ndani kuna kijana akaonekana
akikimbia kupandisha ngazi kwenda ghorofa ya juu.
Naye akadondoshwa chini kwa risasi. Kijana huyu
naye alikuja kutambulika kama mtoto mkubwa wa
kiume wa Osama Bin Laden.
Baada ya kijana huyo kupigwa risasi mlango wa
chumba kilichopo ghorofa ya juu ulionekana
kufunguliwa na mtu akachungulia. Pia naye
akafyatuliwa risasi kadhaa zikamkosa lakini moja
ikampata ubavuni. Mtu huyo aligeuka haraka na
kurudi ndani chumbani lakini kabla hajaufunga
mlango wa chumba vizuri komando wa SEALs
alifanikiwa kuruka na kubiringika mpaka ndani ya
chumba hicho.
Katika kujitahidi kujificha mtu huyo (Bin Laden)
alimnyakua mwanamke mmoja aliyekuwepo humo
chumbani (mkewe Mdogo) na kumsukumia kwa
komando wa SEALs lakini komando alifanikiwa
kumkwepa mwanamke huyo na akafanikiwa
kufyatua risasi iliyompata Osama kwenye paji la
uso.
Papo hapo komando mwingine naye alikuwa
ameshaingia chumbani naye akafyatua risasi
iliyompata Osama kifuani. Bin laden akadondoka
chini na komando mmoja akamfyatulia risasi
nyingine kifuani akiwa hapo hapo chini. Pale pale
roho ya Osama Bin Laden ikaach mwili.
Komando mmoja akatoa simu ya mawimbi ya
kijeshi na kuwasiliana na kamanda McRaven
aliyekuwa amebaki kwenye kambi ya Bagram.
Baada ya kupokea tu simu komando akamueleza
kamanda wake kwa kifupi tu "Geranimo".
Kamanda wake nae akaitafsiri taarifa hii kwa watu
waliopo Ikulu marekani pamoja na Rais Obama
wakifuatilia Kupitia Satelaiti, kamanda McRaven
akawaeleza "For God and for the country, Geranimo
Geranimo Geranimo" kisha akamalizia "Geranimo
EKIA" (EKIA - Enemy Killed In Action (Aduai
ameuawa kwenye mapambano)). Geranimo ndio
lilikuwa jina la fumbo (code name) la kumtambua
Osama Bin Laden katika oparesheni hii.
Seneta Hillary Clinton kipindi akiwa kama waziri wa
mambo ya nje wa Marekani naye siku alikuwepo
Ikulu ndani ya situation room anaeleza kuwa mara
baada ya Rais Obama kusikia taarifa hii kwa
msisimko na hisia kubwa akaongea maneno
machache tu, "we got him" ("tumempata/
tumemmaliza").
Baada ya kutoa taarifa hiyo kuwa wamefanikiwa
kumuua Bin Laden, makomndo wa SEALs
wakawakusanya wanawake na watoto wote
waliowakuta ndani ya nyumba hiyo na eakawafunga
kwa pingu za plastiki na kuwaacha hapo hapo.
Kisha wakaubeba mwili wa Bin Laden na kuupakia
kwenye Chopa.
Lakini kabla ya kuondoka wakailipua ile chopa
iliyopata itilafu kwani isingeweza kuruka tena na
hawakutaka watu wajue teknolojia yao ya siri
inayotumika kwenye chopa hizo.
Zoezi lote hili lilipangwa kutumia dakika 40, lakini
kutoka na umahiri wa hali ya juu wa makomando
wa SEALs liliisha ndani ya dakika 30 pekee. Risasi
16 tu ndizo zilifyatuliwa na watu 5 waliuwawa
(Osama, mtoto wake wa kiume, Abu Ahmed al-
Kuwait, Abrar (kaka wa al-kuwait), na mke wa
Abrar).
Baadaya ya hapo wakaruka mpaka kambi ya
Bagram kisha mwili wa Bin laden ukapakiwa tena
kwenye chopa na kupelekwa kwenye manowari ya
kivita ya NAVY iliyoko baharini. Huko sampuli za
DNA zikachukuliwa na mwili ukapigwa picha. Baada
ya hapo mwili ukavilingishwa shuka jeupe alafu
ukatumbukizwa kwenye mfuko mkubwa na imara,
vikawekwa na vyuma vizito ndani yake, mfuko
ukafungwa, ukatumbukizwa baharini. Huo ukawa
mwisho wa Bin laden Duniani.
HOTUBA YA UTHIBITISHO
Jioni ya siku hiyo Rais wa marekani Barack Obama
alitoa hotuba ambayo itakumbukwa kwa vizazi vingi
vijavyo. Alisema;
"Habari za jioni, usiku huu napenda kuwataarifu
Wamarekani na Ulimwengu wote kuwa Marekani
imeendesha oparesheni iliyofanikiwa kumuua
Osama Bin Laden kiongozi wa Al Qaeda na Gaidi
anayehusika na vifo vya maelfu ya wanaume,
wanawake na watoto wasio na hatia......"
Ulimwengu ulisimama kwa sekunde kadhaa na
wengine hawakuamini masikio yao na mpaka sasa
wapo wasio amini na kumeibuka nadharia nyingi
mno. Lakini hiki nilichokisimulia ndicho
wanachoamini CIA na serikali ya Marekani, kuwa
siku ya Tarehe 1 mwezi May mwaka 2011;
"Geranimo E.KI.A..... Adui aliuwawa katika
mapambano.
 
Wote wanaiga the bold nae anatoa huko google anatafsiri tu,hakuna mwenye mali hapo,wakija walioandika hizo makala sijui mtasema nini
Wanatoa tu mapovu mengi yasiyo na msingi au sijui fikra finyu kuna wengine hawajui km uzi anao upost ulishapita humu

Kingine km unavyosema hii story kwa humu haina mwenyewe si nani wala cha nani kila mtu kanyapia mahali ndo kuipost,niliona hii kitu channel ya Discovery history kwa picha na videos documentary nzima sasa ile sijui ilikopiwa humu!!!??

Haiwezekani mtu amwibie mtu uzi humu aupost tena humu humu,huyu labda ni wa juzi tu jf au hajui km hii nyuzi ilishawahi kupita humu....yani wengine wanamsakama bure jamaa ka copy uzi ili sijui tuwajue km mpo so active
 
Back
Top Bottom