Gazeti la UHURU Desemba 14: “Hali inaruhusu vyama vingi nchini – Nyerere.”

FrediusSnowden

JF-Expert Member
Joined
Sep 7, 2016
Messages
269
Points
250

FrediusSnowden

JF-Expert Member
Joined Sep 7, 2016
269 250
Kama unakumbuka vizuri mnamo DESEMBA 13 mwaka 1991 Mwalimu Julius Nyerere alizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Msasani, Dar es Salaam, juu ya kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini ambao ulianza mwaka 1992.

Baada ya mazungumzo yale pale nyumbani kwake, Siku iliyofuata, Desemba 14, waandishi wa habari mashuhuri na waandamizi, Salva Rweyemamu (aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu utawala wa Kikwete) na mwenzake Lukas Kisasa, kwa pamoja walichapisha habari katika Gazeti la Uhuru (Gazeti la CCM) likiwekewa kichwa cha habari: “Hali inaruhusu vyama vingi nchini – Nyerere.”

Katika mkutano huo na wanahabari, pamoja na mambo mengi mtawanyiko yaliyozungumzwa, Mwalimu Nyerere alishangaza wengi aliposema; “ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndiyo ulionifanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa vyama vingi.”

“Nilitumaini kuwa tunaweza kupata chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza nchi yetu badala ya CCM, au ambacho kingekilazimisha CCM kujisafisha uongozi wake, kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo, kitashindwa katika uchaguzi ujao.”

Huo ndiyo ulikuwa mtizamo wa Mwalimu Nyerere kuhusu uwepo wa vyama vingi na siasa za ushindani hapa nchini. Mwalimu aliamini kuwa, CCM imara inahitaji upinzani madhubuti.

Ukubwa na ukongwe wa CCM ulikifanya kuanza kubweteka na kushindwa kujibu changamoto mtambuka. Mserereko huo ulimfanya Mwalimu Nyerere kuwa mkosoaji mkubwa wa sera za chama chake.

Mwalimu Nyerere, alikosoa hadharani pasipo woga wala hofu. Huyu ndiye alianza kuasisi dhana ya “chukia makosa, penda wakosoaji” ndani ya chama chake.

Nimelazimika kurejea haya yote mara baada ya kuanza kunusa harufu mbaya ya kuturejesha tulikotoka. Mjadala sasa ni mkali hususan kwenye mitandao ya kijamii.

Watu wanaanza kuhoji iwapo kuna umuhimu wa kurejea kwenye mfumo wa chama kimoja. Mjadala huu unakolezwa na ukweli halisi juu ya hali ya kisiasa hapa nchini.

Malalamiko kwa vyama vya siasa yameongezeka kwa madai kuwa, mazingira ya kufanya siasa kwa sasa ni magumu sana na hatarishi. Orodha ya matukio ya kuzuia shughuli za siasa ni ndefu.

Kuzuia mikutano ya hadhara kwa vyama vya upinzani ni miongoni mwa matamko hatarishi kwa ustawi wa demokrasi yetu changa.

Pamoja na ukweli huo, si sahihi hata kidogo kutamani kurejea au kurejeshwa kwenye mfumo wa chama kimoja. Zipo sababu kadhaa.

Mosi, dunia inahama kwa kasi sana kutoka mfumo wa Chama kimoja kwenda siasa za ushindani. Yeyote anayetamani kurejea huko tulikotoka ni sawa na kutamani kufuta historia ya nchi hii.

Pili, tafiti zote zinaonesha wazi kwamba, maendeleo na demokrasia ni chanda na pete. Huwezi kutenganisha uwepo wa demokrasia na maendeleo.

Uhuru wa watu kuzungumza mambo yao kwa uhuru na uwazi pasipo hofu yoyote ndio injini na kichocheo cha maendeleo.

Hakuna serikali yoyote inayoweza kuwaletea maendeleo wananchi wake pekee yake pasipo ushiriki wa wananchi wake weyewe. Hii ni dhana ya kitafiti.

Kujificha katikati ya dhana kuwa, uchumi na maendeleo ndiyo huzaa demokrasia ni kujidanganya na kujiliwaza kwa kutumia dhana mfu. Ukweli ni kwamba, msingi mzuri wa ujenzi wa maendeleo na ukuaji wa mitaji na uchumi ni uwepo wa demokrasia.

Kujaribu kutenganisha demokrasia na maendeleo ni kutokujua dhana pana ya maendeleo. Hii ni dhana pana inayohitaji mjadala mahususi kwa siku zijazo.

Lakini itoshe tu kusema, kamwe tusitumie kigezo cha maendeleo na ujenzi wa uchumi kwa kuminya uhuru wa watu kutoa maoni na hata kufikiri tofauti.

Wapo baadhi ya makada watiifu wa CCM walau waliobakia na chembechembe za Mwalimu Nyerere, wengi wao walikuwepo Msasani kwenye mkutano wa Mwalimu Nyerere na wanahabari mwaka 1991.

Hawa wanakerwa sana na makatazo ya kuzuia shughuli za kisiasa. Tofauti yao na Mwalimu Nyerere ni moja; Mwalimu alikemea hadharani bila uoga, lakini wao wamebakia kunong’ona chini kwa chini kwenye makorido ya ofisi ndogo ya CCM Lumumba, Dar es Salaam.

Ni vema ikaeleweka kwamba, mnufaikaji muhimu wa uwepo wa siasa za vyama vingi ni CCM yenyewe. Na ni busara kutambua kuwa, kazi ya vyama vya upinzani ni kutafuta makosa ya serikali iliyoko madarakani na kuyaanika hadharani. Vyama vya siasa kusifia serikali iliyopo madarakani ni hiyari si sharti.

Mifano ya CCM kunufaika na ukosoaji wa vyama vya upinzani ipo mingi. Mathalan, tangu serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli iingie madarakani imeweza kujipambanua kwa mambo makuu mawili:

Mosi, ikisema inatenda. Hii ni tofauti kidogo na awamu ya nne iliyoongozwa na Jakaya Kikwete, ilikuwa ikisema haitendi na ikitenda haisemi. Pili, awamu ya tano inashughulika na yote yaliyosemwa na wapinzani katka awamu zilizopita.

Mambo yaliyoibuliwa na wapinzani huko siku za nyuma hususan masuala ya ufisadi na rushwa, ndiyo hayohayo yanayoshughulikiwa na serikali ya awamu ya tano hivi sasa.

Vyama vya upinzani ni sawa na kioo. Kazi ya kioo ni kuonesha kasoro. Huwezi kulaumu au kuvunja kioo baada ya kukuonesha kuwa hujanawa uso vizuri kwa sababu waliokuzunguka hawataki kukwambia ukweli. Tafakari.

Credit: Gululi Kashinde
 

Forum statistics

Threads 1,382,163
Members 526,296
Posts 33,821,056
Top