Full Text: Hotuba ya Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Lazaro Nyalandu katika bunge la bajeti leo(2015/16)

Imran K

Member
Apr 11, 2015
43
46
HOTUBA YA WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII
MHESHIMIWA LAZARO SAMUEL NYALANDU (MB),
AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2015/2016


Dodoma Mei, 2015




1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba, kufuatia taarifa iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Bunge lako sasa lipokee na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa Fedha 2015/2016.

2. Mheshimiwa Spika, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali na kuniwezesha kuingoza Wizara hii. Aidha, namshukuru Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuniamini na kunikabidhi dhamana ya kuiongoza Wizara ya Maliasili na Utalii. Aidha, namshukuru Dkt. Mohammed Ghalib Bilali, Makamu wa Rais na Mhe. Mizengo K.P. Pinda (Mb.) Waziri Mkuu kwa msaada wao na uongozi wao ulioniwezesha kufanikisha majukumu yangu kama Waziri.

3. Mheshimiwa Spika, naishukuru kwa dhati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira chini ya Mwenyekiti wake Mhe. James Daudi Lembeli (Mb.) ambayo ilijadili na kutoa ushauri madhubuti uliofanyiwa kazi kwa utimilifu na Wizara, hivyo kupelekea kupitishwa kwa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2015/2016.

4. Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza waheshimiwa Innocent. R. Sebba (Mb.) na Dkt Grace K. Puja (Mb.) walioteuliwa na
Rais, kujiunga na Bunge lako Tukufu. Kwa masikitiko napenda kutoa pole kwa Bunge lako Tukufu kwa kuondokewa na Hayati Kapteni John Damian Komba aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi. Nasi Wizara ya Maliasili na Utalii katika kutekeleza majukumu yetu tumepoteza watumishi katika maeneo mbalimbali. Nachukua fursa hii kutoa pole kwa watumishi wetu waliofariki wakati wakitekeleza majukumu yao.


5. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia ufinyu wa muda wa kuwasilisha hotuba hii, naomba hotuba yote kama ilivyoandikwa kwenye randama iingizwe kwenye hansad kama kumbukumbu rasmi za uwasilishaji wa wizara yangu. MAJUKUMU YA SEKTA YA MALIASILI NA UTALII

6.
Mheshimiwa Spika, maeneo yaliyohifadhiwa kisheria kama hifadhi za Misitu na Wanyamapori yana jumla ya hekta milioni 28, sawa na asilimia 33 ya eneo la Tanzania. Jukumu la msingi la Wizara ni kusimamia Uhifadhi wa Maliasili, Malikale, na Maendeleo ya Utalii kwa kushirikiana na wadau. Jukumu hili linatekelezwa na Sekta ndogo za Wanyamapori, Misitu, Ufugaji Nyuki, Utalii na Malikale kama ilivyoainishwa katika aya ya 6 hadi 10 ya kitabu cha hotuba. TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI YA CCM 2010 - 2015 NA MPANGO WA BAJETI YA MWAKA 2014/2015

7.
Mheshimiwa Spika, Wizara imetekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2010 – 2015); Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 – 2015/2016), Mpango wa Bajeti wa mwaka wa fedha 2014/2015, mikataba ya Kimataifa ambayo Tanzania imeridhia, ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge na maelekezo ya Serikali.

8. Mheshimiwa Spika, katika hatua ya kuwashirikisha wananchi katika Uhifadhi wa Maliasili na Malikale na Ufugaji wa Nyuki, wizara imetenga eneo lenye ukubwa wa hekta milioni 7.7 katika mpango shirikishi. Kati ya hizo, hekta milioni 2.4 ni misitu ya jamii na hekta 5.3 milioni ni misitu inayosimamiwa kwa ubia kati ya Serikali na wamiliki wengine.

9. Mheshimiwa Spika, kati ya mwaka 2010 hadi 2015 Wizara imeanzisha maeneo mapya ya Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori (Wildlife Management Areas - WMAs), Jumuiya hizo ni ILUMA (Kilombero na Mahenge), Ndonda (Nachingwea) Rindilen (Monduli), Kidoma, (Kilosa) na Mchimalu (Nanyumbu).

10. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015, jumla ya wananchi 7,320 waliokuwa wamejiunga katika vikundi 921 vya Ufugaji Nyuki katika vijiji 242 katika Wilaya 30 nchini walifundishwa mbinu bora za ufugaji nyuki. Tumegawa mizinga 14,076 kwa wananchi katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Mbeya, Rukwa, Iringa, Tabora, Shinyanga, Katavi, Ruvuma, Mtwara, Lindi, Kilimanjaro, Tanga, Arusha, Singida, Manyara na Dodoma.

11.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Tanzania inakuwa kinara cha Utalii Barani Afrika, kwa kupitia Bodi ya Utalii, tumeanzisha Kauli mbiu "Utalii uanze kwa mtanzania mwenyewe"; na tumefanikiwa kuongeza idadi ya watalii wa ndani kutoka 567,062 mwaka 2010 hadi 1,003,496 mwaka 2014/2015.

12.
Mheshimiwa Spika, Tanzania imetajwa kwenye taarifa ya utafiti duniani iliyorushwa na kituo cha runinga cha CNN hivi karibuni kuwa nchi ya kwanza kwa kuvutia watalii wanaokuja kuangalia Wanyamapori Barani Afrika, ikifutiwa na Botswana, Kenya, Zambia, Afrika Kusini, Namibia, Uganda, na Zimbambwe.

13.
Mheshimiwa Spika, Idadi ya watalii kutoka nje wanaotembelea nchi yetu imeongezeka kwa asilimia 4 kutoka watalii 1,095,884 Mwaka 2013 hadi watalii 1,140,156 mwaka 2014, pamoja nakumekuwepo na changamoto za athari za gonjwa la Ebola Magharibi mwa Afrika, tishio la Ugaidi Ukanda wa Afrika Mashariki na kuporomoka kwa sarafu ya Euro Barani Ulaya.

14.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Benki Kuu ya Tanzania, Utalii sasa unaongoza katika kuliingizia Taifa fedha za kigeni kwa kiwango cha asilimia 25, na kwamba mchango wa tasnia ya utalii kwenye pato la Taifa sasa umekadiriwa kupita asilimia 17. Aidha, takwimu zinaonyesha kuwa utalii umeajiri wafanyakazi 500,000 (direct employment), na zaidi ya watu 2,000,000 wananufaika na biashara ya Utalii kwa namna moja au nyingine.

15. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inapenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuhusu mpango mkubwa na wa Kihistoria tulioufikia na Benki ya Dunia wa kuendeleza Utalii Kusini mwa Tanzania (Southern Tanzania Tourism Development Initiative) ambao tumepanga kuutangaza mjini Mbeya, tarehe 8/06/2015. Mpango huu wa Kitaifa utahusisha wadau mbalimbali, ikiwepo sekta ya umma na sekta binafsi na utagharimu zaidi ya dola milioni mia moja za Kimarekani au sh. 200 bl kujenga miundombinu muhimu ya kusaidia kuinua soko la Utalii katika mikoa ya Kusini mwa reli ya Kati; ikiwa ni pamoja na mpango wa utunzaji wa vyanzo vya maji, utunzaji wa maeneo yaliyohifadhiwa, Utalii wa fukwe, Utalii wa kiutamaduni na ujenzi wa miundombinu muhimu kwenye utalii. Aidha, kupitia Benki ya Dunia na Ofisi ya Waziri Mkuu wizara inakamilisha taratibu za kufanya utafiti wa kubuni fursa zote za utalii zilizo katika nchi yetu na kuandaa mpango mkakati wa utekelezaji.

16.
Mheshimiwa Spika, nafurahi kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa, kama nilivyoahidi kwenye hotuba ya Bajeti ya 2014/2015, tumekamilisha mpango wa kuhuisha mtazamo wa Dunia kuhusu Tanzania (Re-branding), na Tangazo la Tanzania sasa limekamilika na linatarajiwa kuzinduliwa tarehe 15 Juni, 2015 kwa kutegemea Ratiba ya Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tangazo hili litaanza kurushwa na vituo vya CNN na BBC kuanzia tarehe 1 Julai, 2015, na limezingatia vivutio vya utalii vilivyopo Tanznaia Bara na Zanzibar.

17. Mheshimiwa Spika, Tangazo hili litaiweka Tanzania katika ramani ya Utalii ulimwenguni na litaelezea kwa ufanisi uzuri wa nchi, maajabu yake na ukarimu wa watu wake katikati ya mataifa. Nchi yetu Tanzania, kwa maneno na vitendo, kwa historia na duru za Taifa, imekuwa HERI KWA MATAIFA. Nchi yetu ndio chimbuko la amani, udugu, utu na wema na kama vitabu vilivyoandika zamani, "moyo wa Daudi ulikuwa karibu sana na moyo wa Mungu kutokana na rejea za maisha", Tanzania imekuwa heri kwa mataifa na sasa itajulikana miongoni mwa nchi zote ulimwenguni kuwa ndio moyo wa Afrika "Tanzania, the Soul of Africa".

18.
Mheshimiwa Spika, kupitia TTB tumeanzisha maonesho ya Kimataifa ya Swahili International Tourism Fair, ambayo kwa mara ya kwanza yalizinduliwa hapa nchini na Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, tarehe 01 – 04 Oktoba, 2014 na yanafanyika kwa ushirikiano na INDABA ya Afrika ya Kusini. Maonesho haya yatafanyika Jijini Dar es Salaam Oktoba kila mwaka.

19. Mheshimiwa Spika, tunaendelea kuimarisha maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya KARIBU TOURISM FAIR yanayofanyika mjini Arusha kila mwaka, kwa ushirikiano na wadau wa Utalii TATO na kesho 29 Mei, 2015 nitahudhuria ufunguzi rasmi wa maonesho hayo yanayotarajiwa kuhudhuriwa na wadau kutoka kote ulimwenguni.

20. Mheshimiwa Spika, kama nilivyoitaarifu Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, baada ya kutia saini Tangazo la Serikali (GN) Na. 206 la Mei 2015 kuhusu tozo zinazolipwa na hoteli na loji zilizopo ndani ya TANAPA; Wizara inatarajia kupanua wigo wa Hoteli na Loji zote ziingizwe kwenye mfumo rasmi wa ulipaji wa tozo kupitia GN mpya. Aidha, Wizara inakamilisha maandalizi ya kupata fomula ya kudumu itakayosaidia kukokotoa viwango vya tozo hii, ili kuleta uwiano utakaondoa malalamiko kutoka kwa wawekezaji. UHIFADHI

21.
Mheshimiwa Spika, Wizara imejikita katika kutatua migogo inayotokana na changamoto za kuongezeka watu karibu na maeneo yaliyohifadhiwa na ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba maeneo yaliyohifadhiwa yanakuwa salama na wananchi, hususan wafugaji wanakuwa salama kwa kufuga kwa tija na katika maeneo yasiyokiuka sheria za nchi.

22.
Mheshimiwa Spika, tarehe 09 Mei 2015, nilikutana na Chama cha Wafugaji katika Mji mdogo wa Lamadi, Simiyu na kuwahakikishia kuwa Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi zimejipanga kusikiliza kero zao, na kutafuta njia shirikishi za kuwawezesha kufuga mifugo yao kwa amani katika maeneo yaliyotengwa mahsusi kwa kazi hiyo. AIDHA, niliwahakikishia wafugaji kuwa Serikali haitavumilia vitendo vyovyote vya uvunjwaji wa Sheria au Kanuni kunakosababisha baadhi ya matukio kama ng`ombe kupigwa risasi, mateso kwa wafugaji, kulipishwa tozo zisizo na risiti, ama uwepo wa matukio ya wahifadhi kujeruhi au kuumiza na pengine kuua raia. Wizara imeagiza pande zote zinazohusika kutii sheria za nchi. Aidha, watumishi watakao kiuka sheria kwa makusudi watachukuliwa hatua za kisheria mara moja.

23. Mheshimiwa Spika, nimeagiza kwamba ni marufuku kwa mgeni yeyote kutoka nje ya nchi kuingiza mifugo katika maeneo yaliyohifadhiwa nchini, na kwamba tutaitaifisha mifugo yao na kuipiga mnada na fedha zake zitatumika kujengea maabara au shule nchini.

24.
Mheshimiwa Spika, Wizara imekamilisha zoezi la kuyatambua baadhi ya maeneo yaliyokuwa sehemu ya Mapori Tengefu ambayo yamepoteza sifa, yataondolewa na kuruhusiwa matumizi mengine. Jumla ya mapori tengefu 16 kati ya 42 yameanishwa na ripoti imepelekwa Waziri Mkuu kwa hatua zaidi.

25.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeanzisha Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa Tangazo la Serikali Na. 135 la Mei, 2014, na imeipa nguvu ya kisheria kupitia Tangazo la Serikali Na. 20 la tarehe 15 Januari, 2015. TAWA itakuwa na Makao yake Makuu Mjini Morogoro na itaanza kazi rasmi Julai, 2015.

26.
Mheshimiwa Spika, katika kupambana na vita dhidi ya ujangili nchini, wizara imechukua hatua shirikishi zikiwemo zifuatazo:- Mwezi Februari, 2014, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alitangaza mjini London uamuzi wa Tanzania wa kupiga marufuku biashara ya meno ya Tembo nchini; hatua hii iliifanya Tanzania kuungana na Botswana, Gabon, Ethiopia na Chad kama mataifa kinara katika kupambana na ujangili barani Afrika. Mnamo mwezi Mei 2015, Wizara iliitisha Mkutano wa Kitaifa kuhusu Ulinzi wa Tembo Jijini Dar es Salaam ambako wadau muhimu ikiwepo Benki ya Dunia, UNDP, Marekani, Ujerumani, China, EU, Japan, Benki ya Maendeleo ya Afrika na Mashirika kama FZS, WCS na ICCF walikubali kujiunga kusaidia Mpango Mkakati wa Taifa kupambana na ujangili. Aidha, mwezi Juni 2014, Wizara iliamua kufanyika upya kwa zoezi la kuidadi tembo nchi nzima (sensa ya tembo) ili Taifa lipate uhakika kuhusu idadi ya tembo tulionao katika mifumo yote ya Kiikolojia nchini. Hatua hii ilikuwa na lengo la kuweka uwazi katika jitihada zetu za kuhifadhi mifumo yetu yote ya Kiikolojia, na sensa hii imekamilika kwa kuendeshwa kwa pamoja kati ya TAWIRI, Vulcan (USA) na FZS (Ujerumani); na nitatangaza matokeo ya sensa hiyo Juni 01, 2015 Mjini Arusha.

27.
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na UNDP ilikamilisha Mpango Mkakati ambao uliweka mipango ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu ya kupambana na ujangili. Mwezi Novemba 2014, Wizara iliitisha Mkutano wa Kikanda kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa UNDP na Taasisi ya Uhifadhi wa ICCF, ambapo mataifa 11 yalihudhuria, yakiwemo Mashirika ya Kimataifa na Nchi Wahisani. Mkutano huo ulifikia kutolewa kwa AZIMIO LA ARUSHA ambapo Mataifa yalikubaliana kushirikiana kiintelijensia katika vita dhidi ya ujangili na kupinga biashara haramu ya nyara za Pembe za ndovu. Mkutano huu ulifanikiwa kuipatia nchi yetu rasilimali mbalimbali zikiwemo fedha na vifaa vitakavyoendelea kutusaidia katika mapambano dhidi ya ujangili.

28.
Mheshimiwa Spika, nafurahi kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa, tarehe 25 Mei, 2015 Tanzania na Msumbiji zilitia saini Makubaliano ya ushoroba wa Selous-Niassa, ambapo nchi hizi sasa zitashirikiana kulinda ushoroba uliokuwa kituo kikubwa cha majangili wa kutoka pande zote mbili. Aidha, makubaliano ya Selous-Niassa yanalinda eneo kubwa lililohifadhiwa kuliko eneo lolote la hifadhi ya wanyamapori duniani, lenye jumla ya ukubwa wa takriban kilomita za Mraba 120,000.

29. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili, 2015 wizara imefikisha jumla ya maaskari wa wanyamapori 3,198 katika maeneo yote yaliyohifadhiwa nchini. AIDHA, kuna jumla ya maaskari wa kujitolea ….. katika Pori la Akiba la Selous.

30.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2014/15, kwa kushirikiana na wadau wa Maendeleo, Wizara imepata magari, ndege, helicopters, silaha, vifaa vya Maaskari kama mahema, bionuculars na GPS ikiwa ni hatua ya kuongeza nguvu kwa askari wetu na kwa vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika vita kubwa ya kupambana na ujangili. Serikali ya China, Ujerumani, Marekani, Uingereza, UNDP, World Bank pamoja na taasisi za HBF, FZS, WSC, Friedkin Conservation Group, OBC na TAWISA, zimekuwa mstari wa mbele kutoa rasilimali mbalimbali.

31. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Machi, 2015 jumla ya watuhumiwa 1,802 wa ujangili walikamatwa na jumla ya kesi 988 zilifunguliwa. Aidha, nyara za Serikali zilizokamatwa ni nyamapori yenye kilogramu 9,658.5 na meno ya tembo 182 yenye uzito wa kilogramu 256. Nyara nyingine ni kucha za samba 451; meno ya samba 65; ngozi 60 za wanyamapori mbalimbali; ndege hai 65 aina mbalimbali; kenge 149; lita 10 za mafuta ya simba na matenga 50 ya samaki. Mifugo na mali nyingine zilizokamatwa ni pamoja na ng'ombe 17,489; mbao 1,828; magogo 130 na magunia ya mkaa 915. Aidha, silaha 132 za aina mbalimbali zilikamatwa, kati ya hizo bunduki 84 ni za kivita.

32. Mheshimiwa Spika, jitihada za utatuzi wa migogoro katika hifadhi za wanyamapori zinaendelea ambapo kumekuwa na hatua za maridhiano kati ya Wizara na wadau. Katika kufikia maridhiano, Kamati za wilaya na wananchi zimehusishwa. Baadhi ya maeneo yenye migogoro ya muda mrefu iliyotatuliwa ni Hifadhi ya Taifa Mikumi, Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Pori la Akiba Mkungunero na Msitu wa Hifadhi Kazimzumbwi. Aidha mgogoro kati ya Pori la Akiba Mkungunero na Hifadhi ya Jumuiya ya Makame ulisuluhishwa kwa kurejesha eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 50.5 kwa wamiliki wa Hifadhi hiyo ya jamii. Wizara kwa kushirikiana na wadau wanaendelea kutatua migogoro iliyosalia.

33.
Mheshimiwa Spika, asilimia 53 ya misitu iko kwenye Mamlaka ya Halmashauri za Vijiji na Wilaya, wakati Serikali Kuu inasimamia asilimia 34.6 ya misitu yote nchini. Aidha, inakadiriwa kuwa jumla ya hekta 372,000 za misitu zinapotea kila mwaka kutokana na uharibifu wa shughuli za binadamu katika maeneo yanayosimamiwa na Halmashauri za Wilaya. Kwa mwaka, jumla ya Tani milioni 1.7 za mkaa hutumika kama chanzo cha nishati kuu na asilimia 50 ya mkaa inatumika katika Jiji la Dar es Salaam.

34.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2014/15, TFS imepanda hekta 8,200 kwenye mashamba ya miti, na kufikisha jumla ya hekta 40,000 zilizopandwa tangu TFS kuanzishwa hapo mwaka 2011/12. Ongezeko hilo limewezesha kufikia hekta 95,000 za mashamba ya miti nchi nzima. Kwa mantiki hii, ili kuliepusha Taifa na janga la kugeuka kuwa jangwa na kwa kuzingatia mahitaji makubwa ya mazao ya misitu, na ili kufanikisha azma ya serikali ya kuwepo matumizi endelevu ya raslimali za misitu, Wizara imeanza mchakato wa kupandisha hadhi Wakala wa Misitu ili iwe Mamlaka kamili ya Misitu Tanzania.

35. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuimarisha sekta ndogo ya Malikale kupitia program mbalimbali. Ninayo furaha kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, baada ya kufanyia ukarabati eneo la magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara limerejeshewa hadhi yake ya kuwa katika Orodha ya Urithi wa Dunia. Maamuzi hayo yalifikiwa katika Mkutano wa 38 wa Kamati ya Urithi wa Dunia chini ya UNESCO uliofanyika tarehe 15 hadi 25 Juni, 2014 nchini Qatar. Aidha, Ukumbi wa Nkurumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam umeingizwa katika Orodha ya Urithi wa Taifa.





UKUSANYAJI WA MADUHULI

36.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2014/15 Wizara ilikadiria kukusanya jumla ya Sh.158,790,010,023 kupitia Idara, Mifuko na Taasisi zilizo chini yake.Hadi Machi 2015, Wizara ilikusanya jumla ya Sh.112,004,867,786 sawa na asilimia 71 ya lengo. CHANGAMOTO ZA SEKTA NA MIKAKATI YA KUZIKABILI

37.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu ya Wizara Changamoto mbalimbali zilijitokeza. Baadhi ya changamoto hizo ni ujangili na biashara haramu ya nyara; migogoro ya mipaka, uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa, na matumizi yasiyo endelevu ya mazao ya maliasili. Changamoto nyingine ni uvunaji haramu wa mazao ya misitu na ukwepaji ulipaji tozo za utalii; ubovu wa miundombinu kama barabara, nyumba za watumishi, viwanja vya ndege na madaraja katika maeneo yaliyohifadhiwa; na uhaba wa watumishi na vitendea kazi. Kutokana na tishio la ugaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na milipuko ya magonjwa, kwa Ebola, baadhi ya wageni waliahirisha safari za utalii.

38. Mheshimiwa Spika, Wizara imejipanga kushirikisha wadau katika uhifadhi na matumizi endelevu ya maliasili, malikale na maendeleo ya utalii. Ili kutatua migogoro ya mipaka na uvamizi na maeneo yaliyohifadhiwa, Wizara itaendelea kurekebisha na kuweka alama za kudumu za mipaka, kufanya doria na kuelimisha Umma. Aidha, Wizara itaendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji na ufuatiliaji wa maduhuli. Vilevile, Wizara itaendelea na jitihada za kuongeza idadi ya watumishi, kutoa mafunzo na kuongeza vitendea kazi. Katika kutangaza utalii, kampeni za Kimataifa zitatumika kuwatoa hofu wageni kuhusu usalama wao nchini. MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA 2015/2016

39.
Mheshimiwa Spika, mapendekezo ya mpango na bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016 yamezingatia maelekezo yanayolenga kutekeleza sera na mikakati ya Serikali. Malengo na kazi za Wizara yamejikita katika maeneo sita ya kipaumbele yaliyoainishwa katika Mpango Mkakati wa Wizara (2013-2016). Kwa muhtasari, Wizara imejipanga kutekeleza yafuatayo:
Sekta Ndogo ya Wanyamapori

40.
Mheshimiwa Spika, katika sekta ndogo ya wanyamapori, Wizara itatekeleza kazi zilizoainishwa katika aya ya 106 hadi 113 ya Kitabu cha Hotuba. Baadhi ya kazi hizo ni: kutafuta maeneo kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu ya TAWA na Ofisi za Kanda; kufanya tathmini ya mali za wananchi ili kulipa fidia kwa waliohamishwa kutoka Pori la Akiba Mkungunero; na kufanya tafiti za mwenendo wa magonjwa ya wanyamapori na magonjwa ya maambukizo baina ya binadamu, wanyamapori na mifugo.

41.
Mheshimiwa Spika, ili kupunguza tatizo la huduma ya malazi ndani ya hifadhi za taifa, TANAPAitajenga mabanda ya watalii yenye uwezo wa vitanda 230 katika Hifadhi za Taifa Tarangire, Serengeti, Saadani, Ruaha, Mikumi, Kilimanjaro na Rubondo. Aidha, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) itaendelezamradi wa kuboresha mifugo na kukamilisha mradi wa Kijiji cha Jema walikohamishiwa wananchi waliotolewa hifadhi na kuukabidhi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro. Vilevile, Mamlaka itanunua magunia 30,700 ya mahindi kwa ajili ya jamii zinazoishi katika Hifadhi.
Sekta Ndogo ya Misitu na Nyuki


42.
Mheshimiwa Spika, katika sekta ndogo ya Misitu na Nyuki, kazi zitakazotekelezwa mwaka wa fedha 2015/16 zimeainishwa katika aya ya 114 hadi 128 ya Kitabu cha Hotuba. Baadhi ya kazi hizo ni kuotesha miche ya miti milioni 18 itakayopandwa kwenye mashamba yenye ukubwa wa hekta 11,774 katika maeneo mapya na maeneo yaliyovunwa. Ili kusimamia na kutambua maeneo yaliyovamiwa, Wizara itafanya mapitio ya soroveya na kusafisha mipaka ya misitu ya hifadhi na kuweka maboya na mabango ili kutoa tahadhari kwa jamii kuhusu maeneo yaliyohifadhiwa.


43.
Mheshimiwa Spika,katika juhudi za kulinda uoto wa asili kampeni za kuzuia moto zitafanyika kwa viongozi wa vijiji 112 vilivyo kando ya misitu ya hifadhi 20. Elimu ya usimamizi na matumizi ya rasilimali za misitu itatolewa kwa kamati 89 za maliasili za vijiji na pia kuwezesha kuanzishwa kwa kamati 18. Aidha, elimu itatolewa kwa wafugaji nyuki 610, vikundi 400 vya ufugaji nyuki, wachakataji na wafanyabiashara wa mazao ya nyuki katika kanda saba za Wakala wa Misitu. Vilevile, Wakala utawezesha usajili na kuanza kazi kwa Chama cha Kuendeleza Ufugaji Nyuki Tanzania.

44. Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kushirikisha jamii katika kuhifadhi misitu,Mfuko wa Misituutatoa ruzuku kwa miradi 217 ya wadau wa misitu na ufugaji nyuki ikiwemo miradi mipya 139. Sekta Ndogo ya Utalii


45.
Mheshimiwa Spika,Wizara itaendelea kuboresha mazingira ya kuendesha biashara ya utalii na kuongeza ukusanyaji mapato. Ili kuwezesha jamii kunufaika na biashara ya utalii, Wizara itafanya tathmini kuhusu uendeshaji wa biashara za utalii kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati katika mikoa ya Pwani, Kilimanjaro na Arusha.

46.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa maendeleo ya sekta ya utalii, Wizara kwa kushirikiana na Benki ya Dunia inaandaa mradi wa kusimamisha usimamizi wa maliasili na maendeleo ya utalii kusini mwa Tanzania. Mradi huo utakaogharimu dola za kimarekani milioni 100, utatekelezwa na Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, Wizara ya Kilimo na Chakula, OWM-TAMISEMI na Sekta Binafsi. Mradi huu unalenga kuimarisha usimamizi wa maeneo ya vilindimaji (catchment areas), kuboresha miundombinu ndani ya maeneo ya hifadhi, kuimarisha sekta binafsi na kuboresha uchumi wa wananchi kupitia Sekta ndogo ya Utalii. Kupitia mradi huu, Wizara imejipanga kuboresha Muundo wa Sekta ya Utalii, Sera na Mikakati ya kuendeleza utalii na mifumo ya usimamizi.

47. Mheshimiwa Spika,Bodi ya Utaliiitaongeza jitihada za utangazaji katika nchi zinazoinukia kiuchumi kama vile China, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), India na Brazil. Vilevile, Bodi itaendelea kusimamia na kuendeleza onesho la kimataifa la Utalii la Swahili International Tourism EXPO. Aidha, Bodi inatarajia kuongeza idadi ya mabalozi wa hiari kutoka watatu hadi saba. Mabalozi hao watatoka katika nchi za Italia, Uingereza, Ujerumani na China.

48. Mheshimiwa Spika,kumekuwepo na tofauti ya mafunzo yanayotolewa na vyuo vingi vya utalii vinavyochipukia nchini. Wakala wa Chuo cha Taifa cha Utaliiutafanyia kazi matokeo ya utafiti uliofanywa na mtaalamu ili kubaini suluhisho la changamoto hiyo. Maelezo zaidi kuhusu kazi zitakazotekelezwa katika sekta ndogo ya utalii yako katika Kitabu cna Hotuba aya ya 129 hadi 133. Sekta Ndogo ya Malikale

49. Mheshimiwa Spika, kama ilivyoainishwa katika aya ya 134 na 135 ya Kitabu cha Hotuba, Wizara itaandaa miongozo ya uhifadhi wa miji ya kihistoria ya Kilwa Kivinje, Mikindani na Pangani. Kazi nyingine ni kufanya ukarabati wa Boma la Pangani. kuanza ujenzi wa Kituo cha Taarifa na Kumbukumbu cha Amboni. Aidha,Shirika la Makumbusho ya Taifa litaendelea kuitangaza Makumbusho na kusogeza huduma kwa jamii. Shirika litatoa elimu na ushauri wa kitaalamu kwa jamii, kufanya utafiti na kuhifadhi mikusanyo. Uratibu, Utawala na Maendeleo ya Rasilimaliwatu

50.
Mheshimiwa Spika, Wizara inatarajia kuajiri watumishi 1,091. Kati ya hao, 965 ni wa kada ya Wahifadhi Wanyamapori na Misitu. Aidha, itafanya mapitio ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Wizara (2013-2016) na kuandaa Mpango Mkakati (2016-2021). Wizara itaratibu na kusimamia mfumo wa kielektroniki utakaowezesha kuunganisha taarifa za maduhuli kupatikana katika kituo kimoja. Katika kutoa elimu kwa umma, Wizara itaendelea kuchapisha jarida na vipeperushi mbalimbali vya kuelezea Sera, Sheria na Kanuni. SHUKRANI

51.
Mheshimiwa Spika, kabla ya hitimisho la hotuba yangu, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa wapigakura wa Jimbo langu kwa kunichagua kuwa Mbunge wao kwa kipindi cha miaka 15. Nashukuru kwa ushirikiano walionipa katika kuendeleza jimbo la Singida Kaskazini na mkoa wa Singida kwa ujumla.

52.
Mheshimiwa Spika, majukumu yote niliyoyaeleza yametekelezwa kwa ushirikiano mzuri kati ya viongozi na watumishi. Shukrani za pekee nazielekeza kwa Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa-Naibu Waziri, Mbunge wa Mufindi Kaskazini; Dkt. Adelhelm James Meru-Katibu Mkuu na Bw. Selestine Gesimba-Naibu Katibu Mkuu kwa ushirikiano wanaoutoa kwangu. Nawashukuru kwa dhati watumishi wote wa Wizara na wadau wa sekta kwa juhudi wanazoonesha katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara.

53. Mheshimiwa Spika, Wizara imetekeleza majukumu yake kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo kutoka nchi na asasi mbalimbali za kitaifa na kimataifa na sekta binafsi.Nichukue fursa hii kuwashukuru wote na kutaja baadhi ya wadau kama ifuatavyo: Marekani, Ujerumani, Uingereza, Sweden, Ufaransa, Ubelgiji, Japan, Norway, Finland, Jumuiya ya nchi za Ulaya, DANIDA, UNDP/GEF, FAO, UNWTO, ILO, World Bank, KfW, GIZ, IUCN, UNESCO, ICCROM, JICA, ICOMOS, ICOM, WMF, BTC, HBF, WWF, FINNIDA, FZS, AWF, AWHF, SNV, AFD, USAID, Trade Aid na NORAD. HITIMISHO

54. Mheshimiwa Spika, naomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha makadirio ya matumizi ya jumla ya Sh. 81,964,541,000 kwa mwaka 2015/2016. Kati ya fedha hizo, Sh. 74,255,391,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Sh. 7,709,150,000 ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Fedha za Matumizi ya Kawaida zinajumuisha Sh.45,235,955,000 za Mishahara ya watumishi na Sh.29,019,436,000 za Matumizi Mengineyo. Fedha za Miradi ya Maendeleo zinajumuisha Sh.5,709,150,000 fedha za nje na Sh.2,000,000,000 fedha za ndani.

55.
Mheshimiwa Spika, Naomba kutoa Hoja.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom