Full Text: Hotuba ya Kambi ya Upinzani Bungeni kuhusu Muswaada wa Sheria ya dawa za Kulevya

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
25,491
54,884
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA OFISI YA WAZIRI MKUU – SERA, URATIBU NA BUNGE MHE. RAJAB MOHAMED MBAROUK (MB) AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA UDHIBITI NA USIMAMIZI WA DAWA ZA KULEVYA YA MWAKA 2014 (THE DRUG CONTROL AND ENFORCEMENT ACT, 2014)

Inatolewa chini ya Kanuni ya 86(6) ya Kanuni za Kudumu za Bunge,
Toleo la Aprili, 2013.


1. UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika,
Napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia sisi sote uhai na afya njema na kutuwezesha kuwepo katika Bunge hili kuwatumikia wananchi. Aidha, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru pia Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Mhe. Freeman Aikaeli Mbowe kwa kuendelea kuniamini katika nafasi hii ninayoitumikia ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Uratibu na Bunge.

Mheshimiwa Spika,
Aidha, nawapongeza Wenyeviti wa Taifa, Makatibu Wakuu, na Kamati Kuu za vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), yaani vyama vya CUF, NCCR – Mageuzi na NLD na CHADEMA kwa kutumia hekima na busara kubwa kukubali kuweka kando tofauti za itikadi za vyama vyao na kuweka saini makubaliano ya kushirikiana katika shughuli za kisisa kwa lengo la kuleta mabadiliko ya kweli katika mfumo wa utawala wa nchi ambao umekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya nchi yetu kwa miaka 50 iliyopita. Nawaomba watanzania wote popote pale walipo wawaombee dua njema viongozi wetu wa UKAWA ambao kwa sasa wanafanya kazi kubwa ua kuuelimisha umma juu ya umuhimu wa kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Mfumo wa BVR.

Natoa wito kwa wananchi wote kutumia fursa ya kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura pindi Daftari litakapopita katika maeneo yao ili hatimaye kila mwananchi aliyetimiza umri wa kuandikishwa aweze kuandikishwa na hivyo kuwa na sifa ya kuwa Mpiga Kura na kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba mwaka huu wa 2015.

Mheshimiwa Spika,
Baada ya kutoa salamu hizo, naomba sasa nitoe maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Muswada wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya ya Mwaka 2014 kama ifuatavyo:

2. BIASHARA YA DAWA ZA KULEVYA NCHINI

Mheshimiwa Spika,
Biashara haramu ya dawa za kulevya imekua kwa kasi sana hapa nchini miaka ya hivi karibuni licha ya kuwa na vyombo lukuki vya ulinzi na usalama na licha ya kuwa na Tume maalumu ya kudhibiti madawa ya kulevya chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Takwimu za jeshi la polisi zinaonyesha kuwa matukio ya kukamatwa kwa dawa za kulevya hapa nchini ni makubwa sana na kiwango kinachokamatwa kinaongezeka mwaka hadi mwaka . Kwa mfano kwa mwaka 2012 kiasi cha kilogramu 55,499 za madawa aina ya heroin, cocaine, mandrax na morphine zilikamatwa hapa nchini ikilinganishwa na kiasi cha kilogramu 17,776 zilizokamatwa mwaka 2011.

Mheshimiwa Spika,
Ukizungumzia tani 55 na nusu zilizokamatwa hapa nchini ndani ya miaka mitatu iliyopita sio jambo dogo hasa ukizingatia hiki ni kiasi ambacho kimekamatwa na hatujui ni kiasi gani ambacho wafanyabiashara hawa haramu ya dawa za kulevya walifanikiwa kukipitisha bila kukamatwa. Pengine kiasi ambacho hakikukamatwa ni kikubwa zaidi kuliko kile kilichokamatwa. Ikumbukwe pia kuwa kiasi hiki cha dawa za kulevya zolizokamatwa hakijumuishi dawa za kulevya zilizokamatwa kwa mwaka wa 2013 na 2014. Kwa takwimu hizi ni dhahiri kwamba taifa letu lipo kwenye hatari kubwa ya kuangamia kutokana na matumizi ya madawa ya kulevya.

Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Taarifa ya Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda, iliyosomwa na aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera Uratibu na Bunge Mhe. Wiliam Lukuvi tarehe 26 Juni, 2013 siku ya maadhimisho ya kitaifa ya kupiga vita dawa za kulevya hapa Dodoma ni kwamba katika kipindi cha mwaka 2008 hadi 2012 watuhumiwa 10,799 walikamatwa kwa kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya hapa nchini. Aidha, watanzania wapatao 240 walikamatwa na madawa ya kulevya katika nchi za Brazil, Pakistan na Afrika ya kusini na hivyo kutia doa taswira ya Tanzania katika jumuiya ya kimataifa. Kutokana na kukithiri kwa biashara hii haramu, Serikali kupitia maadhimisho hayo ya siku ya kupiga vita madawa ya kulevya duniani ilitangaza kuwa biashara ya dawa za kulevya kuwa ni janga la taifa.

Mheshimiwa Spika,
Ili kudhihirisa usahihi wa ile methali isemayo kuwa "sikio la kufa halisikii dawa", ni kwamba; siku chache tu baada ya Serikali kutangaza kuwa biashara ya dawa za kulevya ni janga la taifa, wasichana wawili – watanzania walikamatwa huko Afrika ya Kusini wakiwa na kilogramu 150 za madawa ya kulevya yenye thamani ya zaidi ya randi milioni 42.6 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 6 za kitanzania.

Mheshimiwa Spika,
Matukio yote haya yametokea katika kipindi cha utawala wa Serikali ya awamu ya nne ambapo kuna viongozi wa juu Serikalini ambao waliwahi kusema kuwa wanawajua watu wanaojishughulisha na biashara haramu ya dawa za kulevya lakini mpaka sasa hawajawataja wahusika na wala hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi ya wahusika.

Mheshimiwa Spika,
Miongoni mwa viongozi wa serikali na taasisi nyingine waliosema kuwa wanawafahamu wafanya biashara ya madawa ya kulevya ni kama ifuatavyo:

i. Rais Jakaya Mrisho Kikwete:
Rais alipiga hatua kubwa zaidi na kusema anawajua hata viongozi wa dini wanaofanya biashara hiyo. Licha ya maaskofu na viongozi wengine wa dini kumtaka Rais awataje wahusika hao wa madawa ya kulevya ili kuuweka ukweli wazi, Rais hajafanya hivyo mpaka sasa.

ii. Kamishna wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya:
Huyu alisema anayo majina ya vigogo (kwa maana ya viongozi) wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya lakini hajaweka majina hayo hadharani na wala haijulikani kama wahusika hao wamechukuliwa hatua yoyote hadi sasa.

iii. Mbunge wa Mwibara: Mhe. Kangi Lugola alisema katika bunge la bajeti 2013/2014 kuwa kama Rais na Kamishna wa tume ya kudhibiti dawa za kulevya wanawajua "kwa majina" watu wanaojihusisha na biashara za dawa za kulevya na hawataki kuwataja watu hao wala kuwachulia hatua yamkini watu hao ni miongoni mwa mawaziri ndio maana kuna kigugumizi cha kuwataja na kuwachukulia hatua. Tangu Mhe. Kange Lugola alihusishe baraza la Mawaziri na kashfa hiyo ya kuhusika na biashara ya dawa za kulevya hakuna hatua yoyote ilivyochuliwa na Serikali kuthibitisha au kubatilisha kauli hiyo.

iv. Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP: Bw. Reginald Mengi aliwahi kutoa taarifa ya wazi kuwa kuna kundi la matajiri wanaoshirikiana na viongozi wa Jeshi la Polisi waliokuwa wanapanga njama za kumwekea mtoto wake dawa za kulevya ili wambambikizie kesi ya dawa za kulevya na hivyo kuchafua heshima ya Bw. Mengi na familia yake. Ndugu mengi alisisitiza katika taarifa yake kwamba yuko tayari kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi na mamlaka nyingine zinazohusika ili kubaini njama hizo na kuchukua hatua stahiki kwa wahusika lakini mpaka leo Ndugu Mengi hakuhojiwa ili kuthibitisha kauli yake jambo linaloashiria kwamba kuna ukweli katika kauli yake.

Mheshimiwa Spika,
Baada ya matukio yote haya na baada ya Serikali kukaa kimya kuhusu matukio hayo, mnamo tarehe 16 Julai, 2013 aliyekuwa Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Vincent Josephat Nyerere (Mb) alizungumza na vyombo vya habari na kutoa tamko kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni:


KWAMBA, Rais Jakaya Mrisho Kikwete awataje na kuwachukulia hatua watu aliosema anawafahamu wanaojishughulisha na biashara ya dawa za kulevya la sivyo akubali kubeba shutuma kwamba Serikali yake ndio Mratibu Mkuu wa biashara ya dawa za kulevya ndio maana anashindwa kuchukua hatua.

NA KWAMBA, Kamishana wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya awajibike kwa kutoa maelezo kwa umma juu ya hatua alizochukua dhidi ya wahusika wa biashara ya dawa za kulevya aloiosema anawafahamu la sivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni italazimika kuwashawishi wananchi kuamini kwamba yamkini na yeye yumo katika mtandao wa wafanya biashara haramu ya dawa za kulevya ndio maana anasita kuwachukulia hatua wahusika hao ambao alishakiri kuwa anawafahamu.

NA KWAMBA, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege awajibike kwa kutoa maelezo kwa umma kuwa ni tatizo gani linaloikabili mamlaka yake hadi kufanya viwanja vya ndege vya Tanzania kuwa ndio njia rahisi ya kuingiza na kusafirishia madawa ya kulevya katika ukanda wa Afrika Mashariki?

NA KWAMBA, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini na Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi wawajibike kwa kutoa maelezo kwa umma kuwa ni kazi ipi wanayofanya ikiwa madawa ya kulevya yanaingizwa nchini na kusafirishwa nje ya nchi kwa kasi kubwa zaidi?

Mheshimiwa Spika,
Napenda kulithibitisha Bunge lako kwamba; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni bado inasimamia tamko hilo na kwamba bado Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahitaji maelezo ya ki-uwajibikaji juu ya maswala yote tuliyohoji Kuhusu kushamiri kwa biashara haramu ya dawa za kulevya hapa nchini.

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inapata tabu kuamini kama sheria hii inayopendekezwa ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya ya mwaka 2014 inaweza kukomesha mtandao wa biashara ya dawa za kulevya hapa nchini. Hii ni kwa sababu tumekuwa na Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya ya Mwaka 1995, tumekuwa na Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, tumekuwa na Polisi miaka yote lakini viwango vya uingizaji na usafirishaji wa dawa za kulevya vimekuwa vikiongezeka.

Mheshimiwa Spika,
Ni vema kama taifa tukatambua madhara ya madawa ya kulevya kwa vijana wetu ambao ndio nguvu kazi ya taifa. Kupuuzia na kutochukua hatua kwa wahusika wa dawa za kulevya ni kuangamiza nguvu kazi ya taifa. Nguvu kazi ya taifa ikishaharibiwa na dawa za kulevya hatuna taifa tena. Hivyo Serikali ifahamu kwamba kuendelea kulifumbia macho jambo hili kwa manufaa ya mafisadi wachache ni kulihujumu taifa na huo ni usaliti dhidi ya kiapo ilichokula cha kulitumikia taifa na kusimamia usitawi wa wananchi wa Tanzania. Aidha, Serikali itambue pia kwamba kuendelea kukaa kimya bila kuchukua hatua yoyote juu ya jambo hili kunatoa dalili kwamba yamkini ya yenyewe inahusika na biashara hiyo.

3. UCHAMBUZI WA JUMLA WA BAADHI YA VIFUNGU VYA MUSWADA WA SHERIA INAYOPENDEKEZWA

Baraza la Taifa la Kudhibiti Dawa za Kulevya

Mheshimiwa Spika,
Kifungu cha 5 (1) na (2) cha muswada wa sheria hii, kinaanzisha Baraza la Taifa la Kudhibiti Dawa za Kulevya na kutaja wajumbe 14 wa Baraza hilo ambapo Waziri Mkuu ndiye atakawa Mwenyekiti wa Baraza hilo. Kwa mujibu wa orodha ya wajumbe wa Baraza hilo, wajumbe wote ni mawaziri. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona ingekuwa bora zaidi kiutendaji na kiufanisi kama Baraza hili lingekuwa na mchanganyiko wa wajumbe kutoka serikalini na katika sekta binafsi. Mchanganyiko huu utaleta taswira ya ushirikishaji wa wadau wengi zaidi katika kupambana na kudhibiti dawa za kulevya kuliko kuiachia serikali yenyewe kufanya kazi hiyo.

Vigezo vya Ajira kwa Watendaji wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kusimamia Dawa za Kulevya

Mheshimiwa Spika,
Kifungu cha 8(2) cha muswada huu kinasema kwamba: " vigezo na masharti ya ajira, mishahara na posho za maafisa na wafanyakazi wa wa Mamlaka baada ya kupendekezwa na Baraza yatapelekwa kwa Rais kwa ajili ya kupata idhini yake"

Mheshimiwa Spika,
Kimsingi Kambi Rasmi ya Upinzani haioni sababu ya kupeleka mapendekezo ya masharti ya ajira, mishahara na posho za wafanyakazi wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kusimamia Dawa za Kulevya kwa Rais ili kupatiwa idhini. Kuna tume ya Utumishi wa Umma ambayo inaweza kufanya kazi hiyo na waajiriwa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kusimamia Dawa za kulevya walipwe mishahara na posho kama Mamlaka nyingine zinavyofanya. Ni rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuwatendea watumishi wote wa umma kwa usawa na wala kusiwe na ubaguzi wa kuwalipa wengine zaidi wakati wote ni watumishi wa umma.

Adhabu ya Makosa Mbali mbali chini ya Sheria inayopendekezwa.

Mheshimiwa Spika,
Muswada huu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya umeweka adhabu ya faini na kifungo kwa makosa mbalimbali yatakayofanyika kuhusiana na biashara ya dawa za kulevya na shughuli nyingine inayohusiana na dawa za kulevya. Kwa mfano kifungu cha 11 kinaweka katazo kwa kilimo cha mimea inayozalisha dawa za kulevya, na ikiwa mtu anapatikana na hatia ya kuendesha kilimo cha mimea ya aina hiyo, atawajibika kulipa faini ya shilingi milioni 20 au kifungo kisichozidi miaka 30 au vyote kwa pamoja. Kifungu cha 15 kinatoa adhabu ya faini ya shilingi milioni 15 au kifungo cha maisha kwa mtu anayepatikana na hatia ya kumiliki, kusafirisha, kununua na kutengeneza dawa za Nakotiki na Saikotropiki.

Kifungu kingine ni kifungu cha 16 kinatoa adhabu ya faini ya shilingi milioni 200 au kifungo kisichopungua miaka 20 na kisichozidi miaka 40 au vyote kwa pamoja kwa mtu aliyepatikana na hatia ya kumiliki mashine, mitambo na maabara za kutengeneza dawa za Nakotiki na Saikotropiki. Kifungu cha 17 hali kadhalika kinatoa adhabu ya faini ya shilinig isiyozidi milioni 10 na kifungo kisichozidi miaka 5 au vyote kwa pamoja kwa mtu aliyepatikana na hatia ya kumiliki kiasi kidogo cha dawa za kulevya ambacho si kwa matumizi binafsi.

Mheshimiwa Spika,
vifungu vingine ni pamoja na kifungu cha 19 ambacho kinatoa adhabu ya faini ya shilingi milioni moja au kifungo cha miaka 10 au vyote kwa pamoja kwa mtu aliyepatikana na hatia ya kuvuta, kunusa au kutumia dawa za Nakotiki. Aidha, kifungu cha 20 kinatoa adhabu ya shilinig milioni 5 na kifungo cha miaka 3 au vyote kwa pamoja kwa mtu aliyepatikana na hatia ya kumiliki jingo, kiwanja au chombo cha usafirishaji kinachotumiwa kutayarisha au kusafirisha dawa za kulevya.

Mheshimiwa Spika,
Kwa ujumla vifungu vya 21, 22,23, 24, 25, 27,28, 35, 40; 43 na vinginevyo, vinatoa adhabu ya faini kati ya shilingi milioni tano hadi milioni 500 na kifungo cha kati ya miaka miezi sita, hadi kifungo cha maisha kwa mtu aliyepatikana na makosa kuhusiana na dawa za kulevya chini ya masharti ya vifungu hivyo.

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haina mgogoro na vifungu hivyo vya adhabu kama kusudio la adhabu hizo ni kukomesha kabisa biashara ya dawa za kulevya hapa nchini. Ila Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawasiwasi kwamba vifungu hivyo hivyo vinaweza kutumika vibaya na kusababisha makosa mengine ya kijinai kama ifuatavyo:

i. Adhabu kali sana zilizotajwa katika muswada huu, zinaweza kuvutia mazingira ya rushwa hususan katika vyombo vilivyopewa mamlaka ya upekuzi na ukamataji wa watuhumiwa wa dawa za kulevya na pia katika mahakama zetu.

Mheshimiwa Spika, ni vema kutambua kwamba biashara hii ya dawa za kulevya ni biashara ya fedha nyingi na mara nyingi wahusika ni matajiri. Hivyo ikiwa mtuhumiwa amekamatwa na kwa mujibu wa makosa yake anajua kwamba anakabiliwa na kifungo cha miaka 30 gerezani au faini ya shilingi milioni 200, yuko radhi kutoa hata milioni 50 kwa afisa aliyemkamata ili asimfikishe kwenye vyombo vya sheria. Na kwa jinsi hali ya maisha ya watumishi wa umma ilivyo duni, ni jaribu kubwa sana kwa afisa mkamataji kukataa shilingi milioni 50 aliyopewa kama rushwa ili asimfikishe mtuhumiwa mahakamani.

ii. Katika mazingira ya rushwa vilevile, mahakimu wanaweza kutoa adhabu za faini pekee bila kifungo kwa watumiwa wa dawa za kulevya watakaopatikana na hatia chini vya masharti ya sheria inayopendekezwa, jambo ambalo linaweza kusababisha biashara ya dawa za kulevya kuendelea kushamiri na kukomaa hapa nchini. Hii ni kwa sababu wafanya biashara wa dawa za kulevya wana uwezo wa kifedha wa kulipa faini hizo bila ugumu wowote.

iii. Kuendelea kutoza faini kwa mtu anayepatikana na hatia ya kujihusisha na dawa za kulevya, ni sawa na kuhalalisha biashara hiyo kwani ni sawa na mfanya biashara kulipia kodi au ushuru wa biashara yake.

iv. Serikali kukubali kupokea faini na kumwachia mtu aliyepatikana na hatia ya kujishughulisha na baiashara ya dawa za kulevya, haina tofauti na kupokea rushwa (iliyogeuzwa jina na kuitwa faini) ili kumwachia mfanyabiashara wa dawa za kulevya kuendelea kuangamiza kizazi cha taifa hili.

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kufuta masharti yote yanayotoa nafasi ya kulipa faini kwa mtu aliyepatikana na hatia ya kujishughulisha na biashara ya dawa za kuelevya na badala yake kuacha masharti ya adhabu ya kifungo pekee. Hii itasaidia sana kukomesha biashara hii haramu ambayo inaangamiza nguvu kazi ya taifa.

Utaratibu wa Kukamata Dawa za Kulevya Bila Kutaifisha

Mheshimiwa Spika,
Kifungu cha 34 kinaeleza kwamba: "Pale ambapo haiwezekani kushikilia vitu vikiwemo mazao yaliyopo ambayo yanastahili kutifishwa, afisa yeyote aliyeidhinishwa chini ya kifungu cha 33 anaweza kumpatia mmiliki au mtu mwenye kumiliki vitu hivyo na kuamuru kwamba hataondoa, au kuachana na vitu hivyo au vinginevyo kujihusisha na vitu hivyo isipokuwa kwa ruhusa ya afisa huyo"

Mheshimiwa Spika,
Huu ni udhaifu mkubwa sana wa sheria inayopendekezwa. Inawezekanaje kumkamata mhalifu na madawa ya kulevya au vifaa vya kutengenezea dawa hizo na kumwachia mhalifu huyo aendelee kutunza dawa hizo au vifaa hivyo kwa sababu tu mamlaka ya ukamataji imekosa uwezo wa kuvishikilia vitu hivyo? Kutakuwa na uhakika gani kwamba mhalifu huyo hataendelea kutumia au kuharibu dawa hizo au vifaa hiyo ili kupoteza ushahidi? Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza masharti hayo yafutwe na ikiwa mhalifu amekutwa na vitu vinavyotakiwa kushikiliwa basi jukumu hilo lisiachwe kwa mhalifu mwenyewe. Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kifungu hiki kifutwe kwa kuwa kinapingana kimantiki na kimaudhui na kifungu cha 36 ambacho kinaeleza kwamba: "Afisa yoyote mwenye mamlaka chini ya sheria hii, anaweza kuamuru kushikiliwa kwa mazao ya mimea ya baruti afyuni, mimea ya bangi, mirungi, mimea jamii ya koka au mimea mingine ya dawa za kulevya iwapo anaamini kuwa imelimwa isivyo halali, na anaweza kutoa amri hiyo, ikiwemo amri ya kuharibu mimea hiyo kama atakavyoona inafaa"

Taarifa ya Ukamataji na Utaifishaji

Mheshimiwa Spika,
Kifungu cha 42 cha Muswada huu, kinasema kwamba: "Endapo mtu yeyote amekamata watuhumiwa au vitu chini ya Sheiria hii, anatakiwa ndani ya masaa arobaini na nane baada ya kukamata au kushikilia vitu hivyo kutoa taarifa kamili ya maelezo ya kukamatwa huko au kushikilia huko kwa afsa wa juu anayemfuatia".

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, haina mgogoro na utoaji wa taarifa za ukamataji kwa afisa wa ngazi ya juu ndani ya masaa 48. Ila upungufu wa kifungu hiki ni kwamba hakitoi mwongozo kwamba watuhumiwa waliokamatwa au vitu vilivyokamatwa au kushikiliwa vinapelekwa wapi?. Hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kuwa hatua zitakazofuata kuhusu watuhumiwa waliokamatwa au vitu vilivyokamatwa au kushikiliwa zitajwe katika sheria.

Mfuko wa Kupambana na Dawa za Kulevya

Mheshimiwa Spika,
Kifungu cha 57 kinaanzisha Mfuko wa Kupambana na Dawa za Kulevya. Vyanzo vya Mapato vya Mfuko huu, vimeorodheshwa katika kifungu cha 58. Kambi Rasmi ya Upinzani haina mgogoro na vyanzo vya mapato vilivyoorodheshwa katika kifungu hicho isipokuwa kifungu kidogo cha (b) ambacho kinataja kiasi cha fedha zitakazopatikana kwa kuuza mali iliyofilisiwa chini ya Sheria hii kuwa mojawapo ya vyanzo vya Mapato ya Mfuko wa Kupambana na Dawa za Kulevya.

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haiungi mkono kutumia fedha zitakazopatikana kwa kuuza mali iliyofilisiwa chini ya sheria hii kuwa sehemu ya mapato ya mfuko wa kupambana na dawa za kulevya. Hii ni kwa sababu feha itakayopatikana kwa kuuza mali hiyo ni fedha haramu kwa kuwa imepatikana kwa kuuza mali haramu (iliyopatikana kutokana na biashara ya kulevya. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua ikiwa mali iliyofilisiwa ni mtambo wa kutengeneza dawa za kulevya, itamuuzia nani na kwa matumizi gani?

Kinga ya kutoashtakiwa kwa Maafisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kusimamia Dawa za Kulevya:

Mheshimiwa Spika,
Kifungu cha 62 cha Muswada kinatoa kinga ya kutoshtakiwa au kuchukuliwa hatua zozote za kisheria dhidi ya mamlaka au afisa yeyote wa Serikali au mtu yeyote anayetumia mamlaka yake chini ya Sheria hii kwa jambo lolote alilolifanya kwa nia njema wakati akitimiza majukumu yak echini ya sheria hii.

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kinga hii ifutwe na badala yake watu wote watakaokuwa wanatekeleza majukumu yao chini ya sheria hii wafuate taratibu, Kanuni na Sheria za nchi. Hii ni kuondoa uwezekano wa watendaji wenye nia ovu kutumia fursa hii kutekeleza nia zao ovu za kutengeneza mazingira ya rushwa au kufanya uonevu kwa raia wema.

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani imeshtushwa na kifungu cha 65 cha Muswada huu ambacho kinaweka katazo kwa Mahakama ya Madai kushughulikia kesi au mwenendo dhidi ya uamuzi wowote unaofanywa au amri inayotolewa na Afisa yeyote au mamlaka chini ya sheria hii katika masuala ya leseni ya ulimaji, upimaji wa ubora nautaifishaji wa mibaruti afyuni, na kasumba.

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina mtazamo kwamba; kuipa Mamlaka ya Kudhibiti na Kusimamia Dawa za Kulevya mamlaka makubwa dhidi ya Mahakama ya Madai ni kuudhalilisha mhimili wa Mahakama ambao ndio chombo kilichopewa mamlaka ya juu kabisa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kusimamia na kutoa haki inayodhulumiwa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kwamba, kitendo cha sheria inayopendekezwa kutoweka chombo kingine cha rufaa ikiwa mtu hataridhika na uamuzi wa mamlaka ya kudhibiti na kusimamia dawa za kulevya ni ukiukwaji wa haki na misingi ya utawala wa sheria, na ni ishara kuwa sheria hii inayopendekezwa ni kandamizi ndio maana haitoi fursa ya kukata rufaa.

4. HITIMISHO

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeonyesha jinsi ambavyo biashara haramu ya dawa za kulevya imeshamiri hapa nchini licha ya kuwa na sheria ya kudhibiti biashara hiyo, tume maalum ya kudhibiti dawa za kulevya na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama ambavyo navyo vina jukumu la kuzuia biashara hiyo. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani imefanya marejeo ya Kauli za viongozi mbalimbali wa Serikali ambao waliwahi kusema kuwa wanawafahamu wafanya biashara wa dawa za kulevya lakini hawakuwataja na hawakuwachukulia hatua jambo ambalo linashawishi watu kuamini kuwa pengine Serikali inahusika na biashara hiyo ndio maana haichukui hatua.

Mheshimiwa Spika
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeendelea kushikilia msimamo wake kwa kuwataka viongozi wanaohusika na udhibiti wa dawa za kulevya wawajibike kwa kuueleza umma hatua walizochukua ili katika kudhibiti dawa za kulevya.

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imepitia Muswada huu kifungu kwa kifungu na bainisha mapungufu mengi na kutoa mapendekezo na ushauri ili kuifanya sheria inayopendekezwa kuwa bora zaidi. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani itawasilisha jedwali la Marekebisho wakati wa Kamati ya Bunge zima.

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaendelea kuitaka kwa msisitizo Serikali kuchukulia suala hili la dawa za kulevya kwa uzito mkubwa. Kupuuzia na kutochukua hatua kwa wahusika wa dawa za kulevya ni kuangamiza nguvu kazi ya taifa. Nguvu kazi ya taifa ikishaharibiwa na dawa za kulevya hatuna taifa tena. Serikali hii ya CCM ifahamu kwamba kuendelea kulifumbia macho jambo hili kwa manufaa ya mafisadi wachache ni kulihujumu taifa, na kunaondoa uhalali wa Serikali hiyo kuendelea kutawala.

Mheshimiwa Spika,
Napenda kuchukua fursa hii kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuvipongeza sana vyombo vya habari nchini katika kuuhabarisha umma juu ya madhara ya dawa za kulevya. Aidha, nawapongeza waigizaji wa filamu hapa nchini ambao nao hutoa maigizo juu ya madhara ya matumizi ya madawa hayo.

"TANZANIA BILA DAWA ZA KULEVYA INAWEZEKANA, TUTIMIZE WAJIBU WETU"

Mheshimiwa Spika,
Baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, naomba kuwasilisha.

Rajab Mohamed Mbarouk (Mb)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
KATIKA OFISI YA WAZIRI MKUU – SERA, URATIBU NA BUNGE
24 Machi, 2015

 
wabunge wameshauri
kifungo cha miaka 30
au faini ya Tsh 1 bilion kwa atakayekutwa na madawa ya kulevya.

iko safi hii...
 
Itatekelezwa?,usihau mahakama zetu zinaongoza kupokea rushwa,na hao watu wa sembe nao ni wahongaji wazuri...tusubili..
 
Tatizo la tanzania ni utekelezaji na ufuatiliaji wala sio sheria.
Ndio maana sisi tunataka lowasa aongoze nchi kwa kuwa ni mchapakazi.sio kama hawa wavivu
 
kwani kabla ya hapo adhabu ilikuwa jela miaka mingapi na faini sh ngapi?
 
hiyo adhabu itazidi ya china?mbona wananyongwa lakini bado wanauzwa na watanzania bado wanapeleka
 
​vipi wale wabunge wenye biashara hiyo hawakuwepo Bungeni nni wakati sheria inapitishwa???
 
Back
Top Bottom