Full Text: Hotuba ya Baba Askofu Severine Niwemugizi, mbele ya Rais Samia kwenye sherehe ya Jubilei ya miaka 25 ya Uaskofu, 22 Februari 2022 Ngara

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,807
11,969
HOTUBA MBELE YA MGENI MAALUM RAIS SAMIA SULUHU HASSAN KWENYE SHEREHE YA JUBILEI YA MIAKA 25 YA UASKOFU, TAREHE 22 FEBRUARI 2022, NGARA

1645603867245.png

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mwadhama Kardinali Anthony Kambanda, Askofu Mkuu wa Kigali

Mhashamu Askofu Flavian Kassala, Makamu Rais wa TEC

Wahashamu Maaskofu Wakuu, Wahashamu Maaskofu

Mheshimiwa Jenerali Venance Mabeyo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi

Waheshimiwa Wawakilishi wa Maaskofu

Mheshimiwa Padre Ovan Mwenge, Makamu wa Askofu Rulenge-Ngara

Mheshimiwa Meja Jenerali Charles Mbuge, Mkuu wa Mkoa wa Kagera

Mheshimiwa Mathias Kahabi DC wa Ngara

Waheshimiwa Ma DC wa Biharamulo, Chato na Viongozi wote wa serikali

Waheshimiwa Mapadre

Waheshimiwa Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Watawa wote

Mheshimiwa Shehe wa Wilaya na Viongozi wa dini wote mliopo

Waheshimiwa Wabunge

Waheshimiwa Ndugu, jamaa na Marafiki Wapendwa Waamini

Waheshimiwa Wananchi na wageni wote wenye mapenzi mema

Amani na salama!

“Shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu” (1 Thes 5:18). Naomba mniruhusu nianze na Shukrani kwa Mungu Baba. Namshukuru sana kwa upendo, huruma, msamaha, na uvumilivu wake kwangu kwa miaka hii 25 ya utumishi. Hakuna ninachoweza kumpa kikatosha kwa yote aliyonijalia kwa miaka yote hii. Nasema tu ASANTE SANA MUNGU.

Pili nikushukuru wewe Mheshimiwa Rais, Mama Samia. Tarehe 16 Februari 1997 nilipewa heshima kubwa ya kuwa na Hayati Baba wa Taifa Mwl. Nyerere na Hayati Benjamin Mkapa, Rais wan chi yetu wakati huo nilipopewa uaskofu na kusimikwa. Leo umenipa heshima wewe Mheshimiwa Rais ambayo haitatoka moyoni mwangu.

Nakushukuru sana kwa heshima kubwa sana uliyonipa, kuhudhuria adhimisho la Yubilei ya utumishi wangu wa kiaskofu kwa miaka 25. Asante sana, Mungu akubariki. Nakupa pole kwa safari ndefu ya ughaibuni, lakini nakupongeza pia kwa kuliwakilisha taifa letu vizuri katika mikutano ya kimataifa. Kutojihurumia kusafiri tena baada ya safari hiyo ndefu ya nje ya nchi, na kutenga muda ukiacha majukumu yako mengine ufike Ngara kwenye adhimisho hili ni alama ya heshima na upendo mkubwa kwangu na kwa wanajimbo la Rulenge-Ngara. Asante sana kwa upendo wako. Kufika kwako hapa Ngara kwenye adhimisho hili ni ishara ya wewe kutaka kuwa karibu zaidi na kushirikiana na viongozi wa dini zote, kusikilizana nao na kushauriana nao katika masuala muhimu ya kulijenga taifa letu. Niko tayari kukuunga mkono, kushirikiana na serikali yako kwa kuzingatia ukweli na kukuza haki na amani nchini mwetu.

Tarehe 19 Machi utatimiza mwaka mmoja ukiwa madarakani kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa nchi yetu. Nachukua fursa hii kukupongeza sana kwa kazi kubwa nzuri uliyoifanya katika kipindi hiki ukiliongoza taifa letu, na kutekeleza miradi mingi mikubwa yenye tija na manufaa makubwa kwa watanzania. Hongera sana.

Mgeni njoo mwenyeji apone. Kuna msemo huko Biharamulo kuwa: “Umkutapo Mfalme ndipo unamsalimia”. Kwa kweli ni kusema ukipata bahati ya kukutana na Mfalme umweleze hapo hapo shida zako zote! Maana ni mara chache fursa hii kujirudia. Wapo wapiga kura wako wengi wenye changamoto zinazowaumiza mioyo lakini hawana namna ya kuzifikisha kwako. Zikitolewa huku chini zinazimwa. Nitawapa wasaidizi wako baadhi ya hizo. Naomba hapa nikuombe haya yafuatayo:

1. Eneo la ardhi lilipojengwa Kanisa kuu la jimbo sehemu yake iliazimwa kuweka majengo ya shirika la kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) miaka ya 1994-1996, kwa maafikiano kuwa wakiondoka eneo litarudishwa kwa Kanisa. Lakini Shirika lilipotaka kurudisha eneo hilo, kwa ubabe Halmashauri wakalichukua. Nilipoanza uongozi wa jimbo nilimwandikia Mkuu wa Wilaya wa wakati ule juu ya hili eneo, Mh. Kanali Mstaafu Evans Balama. Naye akaandika kuthibitisha kuwa eneo tutarudishiwa. Tunaomba turudishiwe eneo hilo. Sambamba na eneo hilo, ni eneo mbele ya Kanisa kuu, nalo tulinyang’anywa isivyo haki na Halmashauri. Lakini ndipo lilipokuwa kanisa la awali. Tunaomba maeneo yote mawili turudishiwe. Kihistoria maeneo haya mawili yalikuwa kiwanja kimoja. Lakini ilipobidi barabara ya lami ipite katika eneo hili, kiwanja kikagawanywa! Mkononi ninavyo vielelezo vya historia ya eneo husika ninalozungumzia.

2. Katika jimbo ninaloliongoza tunazo hospitali 2 na zahanati 4. Miaka ya nyuma tulikuwa pia na kituo cha afya Chato, lakini kikachukuliwa na serikali na kugeuzwa kuwa hospitali ya wilaya. Hospitali za Biharamulo na Rulenge kama viambajengo vya pembezoni zinahudumia watu maskini wengi. Wengi wanashindwa hata kulipia huduma ndogo wanazopewa, inabidi tu kuwasamehe. Hata hivyo bado tunaelemewa na madeni ya TRA, na uwezo wa kulipa madeni hayo hatuna. Hospitali hizi hazifanyi biashara. Kile kinacholipwa kidogo ni kuziwezesha ziendelee kutoa huduma. Kwa hakika zikifungwa wananchi wataumia sana. Tunaomba madeni hayo ya nyuma toka mwaka 2015 hadi mwaka 2020 yasamehewe. Biharamulo CDH inadaiwa shs. 113,027,693.=; na hospitali ya Rulenge inadaiwa shs. 213,098,525.=. Kwa kuwa hospitali hizi zinawahudumia raia wako, ikiwezekana pia naomba utusaidie kupata vibali vya ajira ili tuboreshe huduma kwa kuwa na idadi ya watumishi kiasi cha kuwezesha kutoa huduma bora.

3. Ngara ina shida kubwa ya maji. Kwenye mkutano wa hadhara hapa Ngara tarehe 20 Septemba mwaka 2017 Mheshimiwa hayati Rais Magufuli aliahidi kutoa milioni 500 ili maji yavutwe toka chanzo cha kudumu, mto Kagera, na kupandishwa kwenye tanki kubwa juu ya mlima Shunga. Na kutokea hapo maji yangesambazwa wilaya nzima bila shida. Nakuomba niungane na mwakilishi wa jimbo la Ngara la Uchaguzi kuomba mradi huo utekelezwe ili shida hii iishe.

4. Baadhi ya waumini wangu wengi ni wakulima. Wakiwa maskini sana watashindwa kumtolea Mungu sadaka na zaka. Naomba sana wasaidie kuwaokoa kwa kuhakikisha vyama vya Ushirika vinavyonunua mazao yao havifinywi na kuuawa na wanyonyaji kwa kofia ya wawekezaji, hasa wale wanaokwenda kununua mazao yao yakiwa shambani kabla ya kuvunwa kama kahawa na mpunga kwa bei ndogo sana. Kuna kitu kinaitwa KUNUNUA BUTURA. Hii inafanywa na wanunuzi binafsi wengine wakivaa kofia ya wawekezaji, wanaotaka kwenda moja kwa moja kwa mkulima mmoja mmoja wakiwa na lengo la kununua kahawa kwa bei isiyo ya ushindani, ili wao wakatengeneze faida kubwa. Viongozi wa vyama vya ushirika wanapita katika wakati mgumu kwa kuwatetea wakulima wasinyonywe katika mkoa huu. Nitakupa ushahidi wa chama kimojawapo cha wakulima wa Ngara.

5. Dokezo dogo kuhusiana na mradi wa Uchimbaji Nickel: Kuna uvamizi wa eneo la mradi, uvamizi unaofanywa na watu toka nje ya Ngara wakitafuta fidia kwa mazao feki. Wengi wa hawa wanawaonea sasa wakazi wa eneo kwa kuwanyang’anya maeneo na kupanda migomba porini. Nimepata hakikisho toka kwa viongozi wa mkoa na wilaya kufahamu tatizo hili na utayari wa kulifanyia kazi. Nimetaka ulijue kwani linaweza kuchelewesha utekelezaji wa mradi lisipotatuliwa kwa wakati.

6. Matukio ya mauaji, watu kujiua, na vifo vingi vya ajali za barabarani yametia doa kubwa sana taswira ya nchi yetu. Shida kubwa nionavyo mimi mara nyingi tunajishughulisha na matokeo badala ya kutatua chanzo cha matokeo. Jambo hili linahitaji mjadala wa kitaifa. Katika makundi tutafakari na tujadiliane kutafuta sababu au chanzo ni nini na nini tufanye ili kuzuia yasiendelee kutokea. Imefika mahali dhamiri za watu wengi kama zimekufa kabisa, watu hawaoni maisha na utu wa wengine kama ni tunu takatifu za kuheshimiwa na kulindwa kwa gharama yoyote. Watu wanaona ni jambo jepesi kuua au kujiua. Hii ni alama ya kuwa kuna kosa mahali fulani. Kwa vyovyote dini na maadili kutofundishwa ipasavyo au kuyapuuza maadili ya dini zetu kunachangia katika hili. Ni imani yangu serikali ikiwa na dhamira ya dhati kushirikiana na viongozi wa dini tutapunguza kwa kiasi kukubwa tatizo hili.

Nichukue fursa hii kuwaalika umoja wa viongozi wa dini Ngara tukutane tarehe 30 Machi ili tuzungumzie changamoto hii na kutafuta cha kufanya. Tutafurahi uongozi wa serikali ukiwa nasi, na ikipendeza tuwaalike pia viongozi wenzetu wa wilaya jirani ndani ya mkoa huu.

7. Ninao mradi wa ujenzi wa nyumba ya mapadre. Nyumba hii pamoja na kuwa na jina hilo itawapokea pia wageni wetu hata wa serikali wanaotaka mahali tulivu pa kufanya tafakari. Inakadiriwa kugharimu Tshs. Bilioni moja hadi kukamilika. Si rahisi sana kupata ufadhili wa nje, tunasuasua kupata raslimali za kuendeleza ujenzi. Ikikupendeza tunaomba utuunge mkono katia kazi hii.

Sisi viongozi wa dini ifahamike ni sauti ya Mungu katika jamii. Mungu anasema na watu wake wote kupitia midomo yetu. Tunapaswa pia kuwasemea wasio na sauti bila kuwa wanasiasa. Ni wajibu wetu kukemea na kuonya pale watu wakikengeuka, lakini pia kufundisha watu waishije katika nyanja zote za kidini, kijamii, kisiasa, kitamaduni, kiuchumi, nk. maisha yanayompendeza Mungu. Tunalaani matukio hayo ya mauaji na matendo yote ya ukatili na ukiukwaji wa haki za watu. Lazima tuendelee kuonya kuwa Mungu anachukizwa na hayo maovu, na tusishangae ghadhabu yake ikiwaka dhidi ya wote wanaowatenda mabaya watu walioumbwa kwa sura na mfano wake.

Kazi ya Askofu ni kufundisha kama Nabii, kutakatifuza kama Kuhani na kuongoza kama Mchungaji. Hii ndiyo kazi nimeifanya kwa miaka 25, nikikumbana na changamoto za aina mbali mbali. Hata hivyo kwa neema ya Mungu nimesimama bado. Namwomba Mungu neema yake izidi kunisindikiza nisitetereke na kumsaliti Kristo aliyenituma.

Wahashamu Maaskofu wakuu na Maaskofu, asanteni sana kwa sadaka kubwa mliyoitoa kuahirisha shughuli zenu ili kuungana nami katika adhimisho hili. Lakini niwashukurunu sana kwa ushirikiano mlionipa katika kutimiza majukumu yangu kama Askofu katika Baraza letu la Maaskofu, na katika majukwaa mengine kama Jukwaa la Wakristo, CSSC, Interfaith Forum, na mengine. Tuendelee kushikamana ili kumtumikia Mungu kwa kuwatumikia watu wake. Badiliko la ratiba ya tukio hili limewaathiri wengi waliojipanga kufika hapa Ngara sasa wameshindwa, nimewaelewa.

Nawashukuru wote walionisaidia katika kutimiza wajibu wangu: Mapadre, Watawa, Walei, viongozi wa serikali, viongozi wa dini, kila mmoja kwa namna yake mmenisaidia iwe kwa sala au kwa kubeba baadhi ya majukumu yangu au kunipunguzia adha iliyoelekea kunikwamisha. Lakini nawashukuru hata wale waliojaribu kuwa vikwazo katika njia yangu ya kuwajibika kwa Mungu na kwa jamii. Hao nao wamenisaidia kwa namna hiyo ili nijue kuwa utumishi huu ni msalaba. Wengine hawapendi uubebe msalaba, uyatimize majukumu yako vizuri ili wokovu usipatikane! Mungu awabariki wote hao.

Naishukuru Kamati iliyoratibu mipango ya sherehe hii. Najua mmefanya kazi kubwa sana bila mimi kujua nini kinaendelea. Hongereni Makamu wa Askofu kwa hekima na busara yako kama Mwenyekiti, na wote ulioshirikiana nao kufanikisha na Mungu awabariki.

Namshukuru kila mmoja wenu mliofika kuungana nami kwenye adhimisho hili. Natambua sadaka mliyoitoa kuacha shughuli zenu ili kuwa hapa leo. Asanteni sana kwa zawadi zenu kila mmoja kwa nafasi yake. Mmenionyesha upendo mkubwa sana, na hata kunishangaza kwa kujua vizuri nini nahitaji kwa maisha na utume wangu kuliko mimi mwenyewe. Asanteni sana.

Mwisho, Mheshimiwa Rais, namalizia nikikuombea uwe na afya njema, uwe mnyenyekevu. Pamoja na madaraka makubwa uliyo nayo, usikubali kamwe kulinganishwa na Mungu kwa namna yoyote ile. Mungu akusaidie kukuza upendo kati ya watanzania unaotuongoza, ukuze haki, nayo haki izae amani na utulivu na kukuza demokrasia; ukuze mshikamano wa watanzania ili hatimaye utumishi wako utukuke na kuacha alama itakayonenwa kwa vizazi. Mungu akujalie hekima na uvumilivu wa kusikiliza hata yale yasiyopendeza masikioni mwako, hasa ushauri wenye nia njema ya kulijenga taifa letu liendelee kuheshimika ndani na nje ya mipaka yake.

Natanguliza shukrani kwa kutusaidia katika hayo niliyokuomba. Nakutakia utumishi mwema na Baraka nyingi za Mungu. Karibu sana Ngara.

+Severine Niwemugizi

ASKOFU WA JIMBO LA RULENGE-NGARA

NIWEMUGIZI NI NANI?


Na Askofu Flavian Matindi KASSALA, Jimbo Katoliki la Geita, Tanzania.

niwe.jpeg

Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki Geita, ambaye pia ni Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika makala hii, anapenda kumpongeza na kumshukuru Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara aliyezaliwa tarehe 3 Juni 1956 huko Katoke. Tarehe 16 Desemba 1984 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 8 Novemba 1996 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Rulenge na kuwekwa wakfu na Askofu mkuu Anthony Peter Mayalla kuwa Askofu tarehe 16 Februari 1997. Tarehe 22 Februari 2022, Sikukuu ya Ukulu wa Mtume Petro anaadhimisha kilele cha Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu. Askofu Flavian Matindi Kassala anapembua kwa umakini mkubwa uongozi wa Askofu Niwe kama Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kati ya Mwaka 2000 hadi mwaka 2006 na siasa za wakati ule. Awamu ya Pili kati ya Mwaka 2012 hadi mwaka 2015. Askofu Flavian Matindi Kassala anasema, shangwe na nderemo zilizosikika tarehe 16 Februari 1997 zinavuma tena kwa namna ya pekee hapo tarehe 22 Februari 2022, ikiwa ni mara ya 25 tangu pale Mama Kanisa alipopiga kengele za shangwe kumpokea mwanaye, Padre Sererine Niwemugizi kama mojawapo wa Makhalifa wa Mitume.

Miaka hii 25 ya utumishi wa kiaskofu inafumbatwa na majitoleo mengi na utendaji wa Askofu Severine Niwemugizi katika eneo la Jimbo la Rulenge-Ngara, Kanisa la Tanzania na ulimwengu kwa ujumla katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifu watu wa Mungu ndani nje ya Tanzania. Baba Niwemugizi: Askofu wa Rulenge na Rulenge-Ngara. Kama Askofu wa Jimbo la Rulenge, wakati huo, Askofu Severin ni mrithi wa aliyejulikana kama Baba wa Mkamilishano, Baba Askofu Christopher Mwoleka. Baba Askofu Severin anaweka historia Jimboni Rulenge pale ambapo mwaka 2008 aliamua kubadilishwa kwa jina na Jimbo toka Jimbo la Rulenge na kuwa Jimbo la Rulenge-Ngara. Mabadiliko haya yalihusisha hasa sababu za kichungaji. Hayakuwa maamuzi mepesi, lakini ulikuwa ni uamuzi ambao ulilenga katika kutanua mtandao wa huduma za Kanisa Kijimbo na Imani kwa Ujumla katika eneo la lililokuwa Jimbo la Rulenge. Pamoja na kubadilisha jina la Jimbo, pia makazi ya Askofu Jimbo yalihamishwa kutoka eneo la Rulenge na kupelekwa mjini Ngara. Pia Kanisa Kuu la Jimbo na Kiti cha Kiaskofu vilihamia katika eneo hilo la Ngara.

Hata hivyo ikumbukwe kuwa eneo la Jimbo halikubadilika kutokana na mabadiliko haya. Moja wapo ya mafanikio makubwa ya kuhamishwa kwa Makao Makuu ya Jimbo ilikuwa ni pamoja na urahisi wa kufikika kwa huduma zilizodai kufanyika katika ofisi za kiaskofu, kutoka maeneo mbalimbali ya Jimbo. Mahali yalipo makao makuu ya Jimbo kwa sasa yanatoa pia nafuu kubwa kwa mawasiliano na sehemu nyingine za taifa na dunia kwa ujumla, ikizingatiwa kuwa kuwepo kwa Makao Makuu Rulenge, wakati huo, kulizuia kufikika kwa kutumia huduma mawasiliano kama vile simu pengine hata Internet. Uwepo wa Askofu katika eneo la Ngara inafungua pia mahusiano ya karibu na mamlaka mengine tendaji ya kitaifa na kimataifa, kwani ofisi za kiserikali kwa ngazi ya wilaya zinapatika mjini Ngara.

Askofu Niwemugizi anayo mengi ya kushuhudia katika maisha na utume wake kama Askofu.
Askofu Niwemugizi anayo mengi ya kushuhudia katika maisha na utume wake kama Askofu.

‘Baba Niwe’: Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC. Jina ‘Baba Niwe’ nimekuwa nikilisikia sana katika mahusuano yetu ya urika tunapokuwa katika shughuli mbalimbali za ki-Baraza. Ni jina ambalo litumikapo hunipatia vionjo vya upendo, unyenyekevu na upendo kitumishi kwa ndugu zake. Kitaifa, Askofu Niwemugizi ameliongoza Baraza la Maaskofu la Tanzania, TEC, kama Rais wake kwa kipindi cha miaka sita (2000 hadi 2006). Kihistoria ninakumbuka kuwa ni kipindi cha sherehe za za Maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo. Kumbe, alikuwa kinara wa kusimamia maadhimisho hayo ambayo yalikuwa ya namna yake katika Kanisa Katoliki ulimwenguni. Kama kiongozi wa Baraza wakati huo aliliongoza Kanisa la Tanzania kutafakari hitimisho la maadhimisho Barua ya Kichungaji “Mwenye Nguvu Amenitendea Makuu, na Jina Lake ni Takatifu” (Lk 1:49)’ barua ambayo iliwaalika Waamini na Taifa la Mungu kwa ujumla nchini Tanzania kuyaishi mafanikio na mafundisho makubwa yaliyopatikana katika adhimisho la Jubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo.

Rais wa Baraza na Siasa wa Wakati: kipindi cha uongozi wa Askofu Severine kama Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kilikuwa na changamoto zake kisiasa. Kilikuwa ni kipindi cha mabadiliko makubwa kiuchumi, ambapo Kanisa lilihitajika kusimamia haki, ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wote. Hivyo, matarajio mengi wa waamini na wasiowaamini yaliwekwa katika Maaskofu, ambao yeye alikuwa Kiongozi na msemaji wao. Ni kipindi ambapo alishuhudia mabadiliko ya Marais wawili: Mhe. Ali Hasan Mwinyi akimalizia muda wake na Mhe. Benjamin Willim Mkapa akiingia katika awamu ya kwanza ya madaraka yake. Uongozi wake ulihakikisha mahusiano ya Kanisa na Serikali yanalindwa na kudumishwa hali kila upande ukilinda misingi yake. Ikubukwe kuwa Baba Niwemugizi naingia katika uongozi wa Baraza muda mfupi tu baada ya Baraza, kwa niaba ya Jamii, kuhoji hali fulani zenye utata katika mabadiliko makubwa yaliyokuwa yakitokea ndani ya nchi. Katika barua yao “WHAT WE SEE AND HEAR: The Opinion of the Tanzania Episcopal Conference on Certain National Issues.” (Ref. Raymond Saba (Ed), Compendium of Major Pastoral Letters, Guidelines and Statements of the Catholic Bishops in Tanzania: 1953-2018, 2018, pp. 325-330.)

Maaskofu walikuwa wamehoji kuhusu: hali wakulima, soko huria, mabadiliko katika mfumo wa elimu sanjari na kukosekana fursa za ajira kwa vijana. Barua hiyo iliyohoji pia kuhusu mfumo wa demokrasia nchini ilikuwa ni utekelezaji wake katika kipindi cha uongozi wa Baba Niwemugizi. HAIKUWA KAZI RAHISI. Hii ilikuwa ni “patashika nguo kuchanika.” Mhashamu Askofu Severine: Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC. Pamoja na kumaliza kipindi chake cha uongozi hapo 2006, Askofu Severine hakusita pale ndugu zake Maaskofu wa Tanzania walipomwomba kushiriki tena katika uongozi wa Baraza. Askofu Severine alilitumikia Baraza kwa nafasi hiyo toka mwaka 2012 hadi 2015. Ni katika kipindi hicho pia aliongozana na Maaskofu wenzake kwenda kwenye hija ya Kitume: “Ad Limina Apostolorum Visitatio” na kwa kifupi, “Ad Limina.” Wakiwa katika ziara hii, alibahatika kuwa ni kati ya Maaskofu wa wachache sana duniani kuzungumza ana kwa ana na Mtakatifu Yohane Paulo II katika siku za mwisho za uhai wake. Ni wazi bahati na baraka hiyo haikosi nafasi yake katika maadhimisho haya ya miaka 25 ya utumishi wa Kitume.

Baada ya utumishi huo wa nafasi ya uongozi katika Baraza, Baba Severine amekuwa mnyenyekevu katika nafasi mbalimbali alizotumwa na Kanisa la Tanzania katika Baraza la Maaskofu Katoliki. Kati ya nafasi alizotumikia hivi karibuni ni pamoja na kuongoza Kamati cha Mahesabu na Maadili ya Baraza. Kwa sasa Baba Askofu Severine ni Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Bugando (CUHAS), “Catholic University Of Health And Allied Sciences, CUHAS, Bugando, Mwanza. Tafakari hii fupi ya Baba Niwe ni sehemu ya pongezi kwa Baba Askofu Severine Niwemugizi katika kutimiza miaka hii 25 ya utumishi, ambayo ameendelea kuipokea kama zawadi toka kwa Muumba wake. Hali tukimpongeza ni nafasi yetu pia ya kutoa matashi mema kwa sehemu iliyo mbele yake ya utumishi. Tunamwombea baraka, amani na utulivu katika kuyapokea mapenzi ya Mungu yaliyopo mbele yake. Hali tukielekeza macho, masikio na miguu yetu huko Ngara hushuhudia hayo makuu ya Mungu,

Katika utumishi,

+ Flavian Matindi Kassala, Askofu wa Jimbo la Geita. (Jirani wa Rulenge-Ngara).
 

Attachments

  • Niwemugizi.mp3
    10.6 MB
Inategemeana!

Hangaya mwenyewe kwanza hawapendi sana hao rc hivyo maombi yao yatakuwa yameshatpwa kapuni

Sent from my SM-T295 using JamiiForums mobile app
hizi imani bhana wakati mwi gine zina changamoto sana, yaan ukiisoma iyo speech mpaka msomaji unaingia ukakasi maana Askofu ameomba msaada wa vitu vingi sana

Askofu ameomba arudishiwe viwanja viwili alivyolorwa na halmashauri , hilo ni jambo jema sana

ameomba wasamehewe deni linalokaribia milioni 400 toka tra

ameomba kibali cha ajira

Na mwisho ameomba aungwe mkono kwenye jengo lenye thamani ya bilioni moja

Sasa hapo serikali imsaidie kipi iache kipi maana hizo figure sio masihara
 
Hii ndy hotuba ilifaa wabunge kwenye maeneo yao wasemee wananchi wao. Matokeo yake huishia kusema tu asante na tunashukuru Mh Rais ili awape Promotion. Hongera Askofu kwa hotuba maridhawa kabsaa.
 
Back
Top Bottom