Freeman Mbowe: Mapendekezo ya marekebisho muhimu ya Katiba na Sheria ili kuwezesha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2020 kuwa huru, wa haki na halali

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Mar 9, 2015
14,243
34,899
Tutawaletea Moja kwa Moja Mkutano wa Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na Wandishi wa Habari wa Tanzania na wakimataifa Kuhusu Mambo mbalimbali ya Nchi

Updates
------------

Mbowe atahadharisha hali ya hatari uchaguzi mkuu, Amlima Barua Rais
-------------

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amemwandikia barua Rais John Magufuli akimwambia kuwa asije akalaumiwa kwa yatakayotokea katika uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu asisitiza kuwa subira ina mwisho wake.

Kwa mujibu wa Mbowe katika barua hiyo amemwambia Rais Magufuli umhimu wa kufanya marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ili kupatikana kwa Tume huru ya uchaguzi.Image result for mbowe na magufuli

Pia, katika barua hiyo iliyotumwa Januari 29, Mbowe ametaka uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 24 mwaka jana ufutwe na kuanzisha mchakato wa maridhiano ya kitaifa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Februari 3 jijini Dar es Salaam, Mbowe amesema mambo hayo yasiposhughulikiwa Chadema isilaumiwe kwa yatakayotokea wakati wa uchaguzi.

“Huu ni mwaka wa uchaguzi. Kwa hali ilivyo kuna kila aina ya kiashiria cha kutokea machafuko ya kisiasa, kama hatutazika viburi vyetu vya kiitikadi na badala yake kusimama pamoja,” alisema Mbowe.Image result for mbowe na magufuli

Kadhalika amekumbusha wito wake wa kutaka maridhiano alioutoa Desemba 9,2019 jijini Mwanza na kauli ya Rais Magufuli kwa mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka huu akisema kila jambo Lina wakati wake.

“Ukimya wetu sio woga. Tuna wanachama wengi tunaofanya kazi ya ziada kuwatuliza. Subira ina mwisho, siku yakifika ya kufika tusilaumiwe,” alisema.

Kuhusu uchaguzi wa Serikali za mitaa, Mbowe alisema ametaka ufutwe na urudiwe kupotia Tume huru ya uchaguzi.

“Kufutwa kwa uchaguzi huu kutahalalisha kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakiwa huru na wa haki. Uchaguzi huu ukafanyike sambamba na uchaguzi wa madiwani, wabunge na Rais,” alisema na kuongeza:

“Kama CCM ikitupeleka kwenye uchaguzi kama ilivyokuwa wakati wa serikali za mitaa, hii nchi haitakuwa salama.”Image result for mbowe na magufuli

Kuhusu maridhiano, alisema wamemwandikia Rais afikirie kuunda Tume ya maridhiano ili kisikiliza malalamiko ya wananchi.

Alitaja malalamiko hayo kuwa pamoja na watu kupotea na wengine miili yao kukutwa kwenye fukwe za bahari, kesi za kisiasa na wakosoaji wa serikali na kuwepo kwa makatazo ya kufanya siasa nchini.

=====

C/HQ/MS/11/144 29 Januari, 2020

Mheshimiwa,

Dr. John Pombe Joseph Magufuli,

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

S.L.P 1102,

1 Julius Nyerere Road, Chamwino, DODOMA .



MAPENDEKEZO YA MAREKEBISHO MUHIMU YA KATIBA NA SHERIA ILI KUWEZESHA UCHAGUZI MKUU WA OKTOBA, 2020 KUWA HURU, WA HAKI NA HALALI
_______________________________________________________________

Mheshimiwa Rais,


Utakumbuka kwamba wakati tukiwa kwenye maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa nchi yetu yaliyofanyika Jijini Mwanza tarehe 09 Disemba, 2020, ulinipa heshima ya kusalimia wananchi na wageni waalikwa ambapo pamoja na mambo mengine nilieleza kwamba unalo jukumu la kuliunganisha Taifa letu kutokana na changamoto mbalimbali tunazokabiliana nazo kwa sasa.

Aidha, hivi karibuni wakati wa kikao chako na Mabalozi wanaowakilisha Nchi mbalimbali nchini ulitoa ahadi kwamba uchaguzi ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu utakua huru na wa haki. Kauli yako hii, ukiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama katika nchi yetu, ilipokelewa kama ishara njema ya kwanza kwa wewe kukiri na kutambaua umuhimu wa Uchaguzi ulio huru, wa haki, na halali. Tunakushukuru kwa ahadi hii; ambayo kwa hakika ikitekelezwa itakuwa moja ya msingi imara wa AMANI, Utengamano na Mshikamano wetu katika Taifa.

Mheshimiwa Rais,

Taifa letu linapitia katika sintofahamu kubwa. Kuna viashiria vingi vinavyoashiria hatari ya kutengwa na Jamii ya Kimataifa; wakati huo huo mfarakanao mpana ukiendelea kuutafuna kwa kasi umoja wetu wa ndani kama Taifa. Hali hii haipaswi kuendelea kama ilivyo.

CHADEMA, kama Chama Kikuu cha upinzani kinaamini kuna kila sababu sasa kuanza kuchukua hatua za makusudi na shirikishi kukabiliana na changamoto hizi; na wewe kama Rais, una mamlaka yote ya kuanzisha mchakato wa kurudisha utengemano wa nchi yetu.

Mheshimiwa Rais,

Huu ni mwaka wa uchaguzi. Kama ujuavyo, mwaka wa uchaguzi huhitaji busara, uelewa na uvumilivu ili kuivusha nchi salama. Kwa hali ilivyo sasa, kuna kila aina ya kiashiria cha uwepo wa machafuko ya kisiasa kabla, wakati na baada ya uchaguzi; kama hatutazika ‘viburi’ vyetu vya kiitikadi na badala yake kusimama pamoja, kama Taifa kuruhusu Haki na Demokrasia ya kweli kutamalaki.

Mheshimiwa Rais,

Kwa mukhtaza huo, CHADEMA tunaleta kwako mapendekezo ya awali ya kuanza kutukwamua katika sintofahamu hii inayolinyemelea Taifa ambayo yamejikita kwenye maeneo Makuu Matatu;

Marekebisho madogo ya Katiba na sheria mbalimbali za uchaguzi ili kuwezesha upatikanaji wa Tume huru ya Uchaguzi.

Kufutwa na kurejewa kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 2019.

Kuunda Tume ya Maridhiano ya Kitaifa.

Mheshimiwa Rais,

Nina hakika tunahitaji maridhiano ya Kitaifa. Kama viongozi tuna wajibu huo mbele ya wananchi wenzetu na hata mbele ya Mungu; na wewe kama Kiongozi Mkuu wa nchi yetu una turufu na wajibu wa kipekee kuwezesha matamanio haya ya haki kupatikana.

Mheshimiwa Rais,

Pamoja na barua hii, naambatanisha hapa maelezo ya kina ya vifungu mbalimbali vya Katiba na sheria tunavyoshauri kurekebishwa. Nina hakika wadau wengine katika Taifa letu nao watakuwa na mawazo ya kuchangia katika kuutafuta mustakabali mwema.

Natanguliza shukrani, nikiamini Mwenyezi Mungu atakujalia busara na hekima nyingi katika kupokea, kutafakari na kuchukua hatua sahihi na stahiki mapendekezo yetu ili kulihakikishia Taifa letu AMANI ya kudumu na ustawi wa watu wake wote.

Wako katika Demokrasia na Maendeleo.
____________________

Freeman Aikaeli Mbowe,

MWENYEKITI WA TAIFA

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (Chadema) KIAMBATANISHO:

MAPENDEKEZO YA MABADILIKO YA KATIBA NA SHERIA MBALIMBALI ZIHUSIANAZO NA UCHAGUZI KUWEZESHA UPATIKANAJI WA TUME HURU YA

UCHAGUZI


1.0 TUME YA UCHAGUZI


Tume ya Uchaguzi imeundwa na ibara ya 74 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kiutendaji wakati wa uchaguzi, mamlaka ya Tume hutekelezwa na Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa, Miji na Halmashauri za Wilaya na watendaji mbali mbali walio chini yao. Hii ni kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi wa Taifa.

1.1 Maeneo ya Katiba na Sheria ya Uchaguzi yanayohitaji Marekebisho kuhusu Tume

Ibara ya 74(1) inayompa Rais wa Jamhuri ya Muungano mamlaka ya kuteua Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume.

Ibara ya 74(5) inayompa Rais mamlaka ya kumwondoa madarakani mjumbe yeyote wa Tume kwa sababu ya kushindwa kutekeleza kazi zake, ama kutokana na maradhi au kwa sababu yoyote au kwa tabia mbaya au kwa kupoteza sifa za kuwa mjumbe.

Ibara ya 74(12) inayonyang'anya Mahakama mamlaka ya kuchunguza jambo lolote lililofanywa na Tume katika kutekeleza madaraka yake.

Ibara ya 75 (1) na (2) inayoizuia Tume kugawa majimbo ya uchaguzi na kuweka mipaka yake bila kupata kibali cha

Rais.

Ibara ya 75 (6) inayokataza Mahakama kuchunguza jambo lolote lililofanywa na Tume katika kutekeleza madaraka yake ya kugawa majimbo ya uchaguzi na kuweka mipaka yake.

Ibara ya 74(7) ikisomwa pamoja na kifungu cha 6 (1) cha Sheria ya Uchaguzi inayompa Rais mamlaka ya kuteua Mkurugenzi wa Uchaguzi, ambaye ni mtendaji mkuu wa Tume, kutoka miongoni mwa watumishi waandamizi wa serikali watakaopendekezwa na Tume.

Kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Uchaguzi kinachowapa Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa, Miji na Halmashauri za Wilaya mamlaka ya kuwa wasimamizi wa uchaguzi unaofanyika katika majimbo ya uchaguzi.

Kifungu cha 7 (2) na (3) cha Sheria ya Uchaguzi kinachoilazimisha Tume kuteua mtumishi mwingine yeyote wa serikali kuwa msimamizi wa uchaguzi.

1.2 Mfumo Huu wa Usimamizi wa Uchaguzi Sio Huru na

Hauwezi Kuendesha Uchaguzi Huru, Wa Haki
na Halali.

Kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma, Wakurugenzi wa Halmashauri za Serikali za Mitaa ni wateule wa Rais (Wakurugenzi wa Majiji); au wa Tume ya Utumishi wa Umma (Wakurugenzi wa Manispaa, Miji na Halmashauri za Wilaya). Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Umma, kama ilivyo kwa Tume nyingine zote, ni wateule wa Rais kwa mujibu wa ibara ya 36 (3) ya Katiba. A

Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Serikali za Mitaa waliopo madarakani kwa sasa wameteuliwa na Rais.

Mkurugenzi wa Uchaguzi na wasimamizi wa uchaguzi wote wanaweza kuondolewa madarakani wakati wowote na Rais mwenyewe chini ya ibara ya 36 (4) ya Katiba; au na Tume ya Utumishi wa Umma ambayo imeteuliwa na Rais.

Wasimamizi wa uchaguzi wa ngazi zote sio watumishi wa Tume kwa maana ya uteuzi na uwajibikaji wao kiutendaji na kinidhamu. Ni 'watumishi wa Tume' kwa matakwa ya Sheria ya Uchaguzi na kwa wakati wa uchaguzi tu.

Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume hawana ulinzi wowote wa kikatiba wa ajira zao. Hii ni tofauti kabisa na ulinzi wa kikatiba wa ajira walionao Majaji wote wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania; Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

1.3 Maeneo ya Katiba na Sheria ya Uchaguzi yanayohitaji

Marekebisho


Matokeo ya Rais yapingwe Mahakamani na Rais asiapishwe mpaka shauri lililofunguliwa kwa hati ya dharura liamuliwe. Tunapendekeza ibara ya 41(7) ya Katiba ifanyiwe marekebisho.

Ibara ya 74 (1) ya Katiba irekebishwe ili kuviwezesha vyama vya siasa na asasi na taasisi za kiraia, ambao ni wadau wakuu wa uchaguzi, kupendekeza majina ya Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi kwa ajili ya uteuzi wa Rais, baada ya kukidhi masharti ya kitaaluma na kiutendaji yaliyowekwa na Katiba.

Ibara ya 74 (5) ifanyiwe marekebisho ili kuwapatia Wajumbe wa Tume ulinzi wa kikatiba wa ajira zao, sawa na Majaji, Wajumbe wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Ibara ya 74 (7) na kifungu cha 6(1) cha Sheria ya Uchaguzi virekebishwe ili kuwezesha Mkurugenzi wa Uchaguzi kuteuliwa na Tume, bila kujali ni mtumishi mwandamizi wa serikali au la, ili mradi ametimiza masharti ya kitaaluma na kiutendaji yaliyowekwa na Katiba au Sheria ya Uchaguzi.

Ibara za 74 (12) na 75 (6) irekebishwe ili kuondoa kinga dhidi ya mashtaka kwa Tume kutokana na utekelezaji wa madaraka yake na ugawaji wa majimbo ya uchaguzi kwa mujibu wa Katiba na Sheria ya Uchaguzi.

Kifungu cha 7 cha Sheria ya Uchaguzi kirekebishwe ili kuipa Tume mamlaka ya kuteua wasimamizi wote wa uchaguzi wenye sifa za kitaaluma na kiutendaji bila kujali ni watumishi wa serikali au la. Tume iwe na mamlaka pekee ya uteuzi wa watumishi wake wote.

1.4 Mchakato wa Kutoa na Kurudisha Fomu za Uteuzi wa Wagombea
Kifungu cha 38 (6) cha Sheria ya Uchaguzi kinawaelekeza wasimamizi wa uchaguzi kutoa na kumpatia mgombea au mpiga kura yeyote idadi ya fomu za uteuzi wa wagombea atakazohitaji.

Kifungu cha 38 (7) kinamtaka kila mgombea au mdhamini wa mgombea kuwasilisha fomu za uteuzi kwenye ofisi ya msimamizi wa uchaguzi kabla ya saa 10 jioni ya siku ya uteuzi wa wagombea.

Hakuna masharti yoyote ya kisheria yanayomlazimu msimamizi wa uchaguzi kuwepo ofisini kwake wakati wote wa kutoa na kurudisha fomu za uteuzi. Aidha, hakuna masharti yoyote ya kisheria ya kumlazimisha msimamizi wa uchaguzi kutoa au kupokea fomu za uteuzi za wagombea wa vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki kwenye uchaguzi.

Kumekuwa na matukio mengi ya wasimamizi wa uchaguzi kutoa au kupokea fomu za uteuzi kwa wagombea wa CCM na kisha kukimbia ofisi zao ili wasitoe au kupokea fomu za uteuzi kwa wagombea wa vyama vya upinzani.

Kumekuwa na matukio mengi yaliyoshuhudiwa wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa, 2019 ya wasimamizi wa uchaguzi kuongeza herufi au namba kwenye fomu za wagombea wa upinzani kwa lengo la kuziharibu na hivyo kuwafanya wakose sifa za kugombea .

1.5 Maeneo ya Sheria ya Uchaguzi yanayohitaji Marekebisho Kuhusu Mchakato wa Kutoa na Kupokea Fomu za Uteuzi wa Wagombea.

Kifungu cha 38 (6) cha Sheria ya Uchaguzi kirekebishwe ili pale ambapo msimamizi wa uchaguzi anapokuwa hayupo ofisini kwake wakati wote wa zoezi la kutoa fomu za uteuzi; au anapotoa fomu za uteuzi kwa mmoja au baadhi tu ya wagombea, basi zoezi zima la kutoa na kurudisha fomu za uteuzi litasimama hadi hapo msimamizi wa uchaguzi atakapotoa fomu kwa wagombea wote wanaohitaji fomu za uteuzi.

Hii itaondoa tabia mbaya ya wasimamizi wa uchaguzi kukimbia ofisi zao ili kukwepa kutoa fomu za uteuzi kwa wagombea wa vyama vya upinzani.

Kifungu cha 38 (7) kirekebishwe ili pale ambapo msimamizi wa uchaguzi hayupo ofisini kwake wakati wote wa zoezi la kurudisha fomu za uteuzi kwa sababu yoyote ile; au anapoondoka ofisini baada ya kupokea fomu za uteuzi za mgombea mmoja au baadhi tu ya wagombea, basi zoezi zima la kurudisha fomu za uteuzi na hatua nyingine zinazofuata litasimama hadi hapo msimamizi wa uchaguzi atakapopokea fomu za uteuzi za wagombea wote waliochukua fomu hizo.

Hii itaondoa tabia ya wasimamizi wa uchaguzi kukimbia ofisi zao ili kukwepa kupokea fomu za uteuzi za wagombea wa vyama vya upinzani.

Kifungu cha 38 kirekebishwe kwa kuongeza kifungu kidogo kitakachowalazimisha wasimamizi wa uchaguzi kutoa au kupokea fomu za uteuzi za wagombea wa vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki kwenye uchaguzi kwa pamoja au kwa wakati mmoja.

Hii pia itaondoa tabia ya wasimamizi wa uchaguzi kutoa au kupokea fomu za uteuzi kwa wagombea wa CCM tu na kisha kukimbia ofisi zao ili kukwepa kutoa au kupokea fomu za uteuzi za wagombea wa vyama vya upinzani.

Kifungu cha 38 kirekebishwe kwa kuongeza kifungu kidogo ili kuwezesha wagombea waliopoteza au kunyang'anywa fomu za uteuzi kupatiwa fomu nyingine za uteuzi ili waweze kushiriki kwenye zoezi la uchaguzi.

Hii itaondoa tabia inayojitokeza kwa kasi ya wagombea wa vyama vya upinzani kutekwa nyara na kisha kunyang'anywa fomu zao za uteuzi na hivyo kushindwa kuzirudisha kabisa, au kuzirudisha nje ya muda uliopangwa kwa ajili hiyo.

Tunapendekeza kuwepo kwa marekebisho ya sheria ili kuiwezesha Tume kuweka kwenye mtandao fomu zote za uteuzi wa wagombea na hivyo kila mgombea kuwa na fursa ya kupakua fomu hizo kuzijaza na kuzirejesha. Fomu irejeshwe kwa msimamizi wa uchaguzi ikiwa na uthibitisho wa Chama cha Siasa kilichomteua na nakala ya fomu hiyo itumwe Tume Makao makuu kwa njia ya mtandao kama uthibitisho wa fomu kurejeshwa na Mgombea. Hatua hii itaondoa tabia ya wasimamizi wa uchaguzi kukimbia ofisi zao siku ya kutoa na kurejesha fomu za uteuzi.

1.6 Sifa na Masharti ya Kugombea Uchaguzi

Kifungu cha 36 cha Sheria ya Uchaguzi kinakataza mtu yeyote kuteuliwa kuwa mgombea wa uchaguzi wa Ubunge mpaka awe na sifa za kuchaguliwa hivyo kwa mujibu wa ibara ya 67 ya Katiba.

Sifa zilizowekwa na ibara ya 67 (1) na (2) ya Katiba ni uraia wa Tanzania; umri wa miaka 21 au zaidi; kujua kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza; kuwa mwanachama na kupendekezwa na chama cha siasa; kutokuwa na hatia ya kosa la kukwepa kodi; kutokuhukumiwa adhabu ya kifo, au kufungwa kwa zaidi ya miezi 6 kwa kukutwa na hatia ya kosa lolote la utovu wa uaminifu; kutokuhukumiwa na Mahakama kwa kukutwa na hatia ya kosa la utovu wa uaminifu au kwa kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma; kutokuwa na maslahi na mkataba wa aina yoyote uliowekewa miiko na kukiuka miiko hiyo; kutokuwa afisa mwandamizi wa serikali; na kutokuzuiliwa kujiandikisha kama mpiga kura katika uchaguzi wa Wabunge.

Nje ya masharti haya ya Katiba, kifungu cha 38 cha Sheria ya Uchaguzi kimeweka masharti mengine ya ziada yafuatayo:

Kupata udhamini wa wapiga kura 25 waliojiandikisha kupiga kura kwenye jimbo husika. (Kifungu cha 38(1).

Kutokukatazwa na Tume ya Uchaguzi kuwa mgombea kwa mujibu wa Sheria ya Gharama za

Uchaguzi. (Kifungu cha 38(2).

Jina, anwani na kazi ya mgombea; majina, anwani za wadhamini na namba za kadi zao za wapiga kura, na hati ya kiapo ya mgombea kuwa yuko tayari na ana sifa za kugombea uchaguzi. (Kifungu cha 38(3).

Hati ya kiapo iliyosainiwa na mgombea mbele ya hakimu kwamba ana sifa na kwamba hajazuiliwa kugombea uchaguzi; picha za mgombea zilizopigwa ndani ya miezi mitatu kabla ya uteuzi, na maelezo binafsi ya mgombea. (Kifungu cha 38(4).

Kifungu cha 38 (5) kinatamka wazi kwamba pale ambapo fomu za uteuzi hazijaambatanishwa na nyaraka zilizotajwa na kifungu cha 38 (4), basi uteuzi wa mgombea husika utakuwa batili.

Hata hivyo, Tume inaweza, endapo itaona inafaa, kuelekeza kwamba fomu za uteuzi za mgombea huyo zikubaliwe kuwa ni halali endapo nyaraka zikizokosekana zitawasilishwa kwa msimamizi wa uchaguzi ndani ya muda wa nyongeza uliowekwa na Tume. (Proviso ya kifungu cha 38 (5).

1.7 Maeneo yanayohitaji Kufanyiwa Marekebisho Kuhusu Sifa na Masharti ya Kugombea.

(a) Kifungu cha 38 (5) cha Sheria ya Uchaguzi kirekebishwe ili fomu za uteuzi zenye mapungufu ya nyaraka zilizotajwa na kifungu cha 38 (4) zisiwe batili. Badala yake, kifungu kipya kielekeze kwamba mgombea husika atapatiwa muda wa kurekebisha mapungufu ya nyaraka yaliyoonekana.

Faida ya pendekezo hili ni kwamba sababu pekee ya kubatilisha fomu za uteuzi wa wagombea itakuwa ni kukosa sifa za kugombea au kuchaguliwa zilizotajwa na ibara ya 67 ya Katiba.

Mapungufu mengine yote yasiyohusu kukosa sifa za kikatiba yataweza kurekebishwa na hivyo kuwezesha wagombea wote wenye sifa za kikatiba kushiriki kwenye uchaguzi.

1.8 Mchakato wa Kuweka na Kuamua Mapingamizi Dhidi ya Uteuzi wa Wagombea.

Kifungu cha 40 cha Sheria ya Uchaguzi kimeweka sababu za fomu za uteuzi wa wagombea kuwekewa mapingamizi, na utaratibu wa kusikiliza na kuamua mapingamizi hayo.

Kifungu cha 50A kimeweka utaratibu wa ziada kuweka mapingamizi wakati wa kampeni za uchaguzi.

Kifungu cha 40 (3) kinawataja watu wenye haki ya kuweka mapingamizi dhidi ya uteuzi wa wagombea kuwa ni wagombea, msimamizi wa uchaguzi, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msajili wa Vyama vya Siasa.

Mapingamizi yote katika hatua hii yanapaswa kuwasilishwa kwa msimamizi wa uchaguzi sio zaidi ya saa 10 ya siku inayofuatia uteuzi wa wagombea. (Kifungu cha 40(2).

Baada ya uteuzi wa wagombea kufanyika na mapingamizi yoyote kuamuliwa, kifungu cha 50A (1) kinamruhusu Msajili wa Vyama vya Siasa kumwekea pingamizi kwenye Tume mgombea yeyote anayekiuka masharti ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi, wakati kampeni za uchaguzi zikiwa zinaendelea.

Baada ya kusikiliza pingamizi hilo, Tume inaweza kumfuta mgombea husika kwenye orodha ya wagombea na kumzuia kuendelea na mchakato wa uchaguzi. (Kifungu cha

50A (2).

Tofauti na utaratibu wa mapingamizi ya awali chini ya kifungu cha 40, hakuna utaratibu wowote wa rufaa kwa mapingamizi yanayowekwa au kuamuliwa chini ya kifungu cha 50A.

Tofauti na utaratibu wa mapingamizi ya awali chini ya kifungu cha 40, utaratibu wa mapingamizi chini ya kifungu cha 50A umeondolewa kwenye mikono ya wasimamizi wa uchaguzi na kupelekwa kwenye mikono ya Tume moja kwa moja. Kwa maneno mengine, mapingamizi chini ya utaratibu huu yatawasilishwa, kusikilizwa na kuamuliwa kwenye ofisi za Tume; badala ya kuwasilishwa, kusikilizwa na kuamuliwa kwenye ofisi za wasimamizi wa uchaguzi walioko majimboni.

1.9 Maeneo yanayohitaji Marekebisho Kuhusu Mchakato wa Kuweka, Kusikiliza na Kuamua Mapingamizi.

(a) Kifungu cha 40 (3) kinachohusu watu wenye haki ya kuweka mapingamizi kirekebishwe ili pale ambapo mweka pingamizi ni msimamizi wa uchaguzi, au Mkurugenzi wa Uchaguzi au Msajili wa Vyama vya Siasa au Mwanasheria Mkuu wa Serikali,

basi pingamizi hilo lisikilizwe na kuamuliwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya au Mahakama ya Hakimu Mkazi ya eneo la jimbo husika la uchaguzi.

Hii itaondoa hatari ya watu wanaohusika na uchaguzi kuwa waweka mapingamizi na waamuzi wa mapingamizi hayo.

Itaondoa pia uwezekano wa Mkurugenzi wa Uchaguzi anayeweka pingamizi kumshinikiza msimamizi wa uchaguzi ambaye yuko chini yake kimamlaka kuamua pingamizi hilo kwa upendeleo.

Aidha, pendekezo hili litaondoa uwezekano wa wateule hawa kula njama za kuwaengua wagombea wa vyama vya upinzani.

Kifungu cha 40 kirekebishwe kwa kuongeza kifungu kingine kidogo kitakachoweka wazi kwamba sababu pekee ya kubatilisha uteuzi wa mgombea aliyewekewa pingamizi ni kama fomu zake za uteuzi zinaonyesha kwamba hana sifa za kugombea au kuchaguliwa zilizotajwa na ibara ya 67 ya

Katiba.

Kifungu cha 40 (6) kirekebishwe ili kuondoa kinga dhidi ya mashtaka kwa Tume kutokana na uamuzi wake juu ya rufaa za mapingamizi ya uteuzi wa wagombea mara baada ya kutolewa uamuzi huo, badala ya kusubiri uchaguzi husika kukamilika kwanza.

Pendekezo hili litawezesha uamuzi wa Tume kuengua wagombea wa vyama vya upinzani kubatilishwa kabla ya uchaguzi kufanyika na hivyo kuwaruhusu kuendelea na kampeni na kushiriki kwenye uchaguzi.

Kwa uzoefu wa mashauri ya mapingamizi kabla ya uchaguzi na mashauri ya kesi za uchaguzi baada ya uchaguzi; ni rahisi zaidi kwa mashauri ya mapingamizi kusikilizwa na kuamuliwa kabla ya uchaguzi kuliko kesi za uchaguzi zinazofunguliwa baada ya uchaguzi kufanyika na washindi kutangazwa.

Kifungu cha 50A kifutwe kabisa kwa sababu kinaweza kutumiwa vibaya kwa kuwaonea wagombea, hasa wa vyama vya upinzani, kwa kuwaengua kabisa kwenye mchakato wa uchaguzi, au kwa kuvuruga kampeni zao za uchaguzi.

1.10 Sheria ya Gharama za Uchaguzi

Sharti na katazo la kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 12 (1), (2), (3) na (4) kinachotaka vifaa vya uchaguzi kuingizwa siku 90 kabla ya uchaguzi lifutwe. Hii ni kutokana na ukweli kwamba katazo hilo halijazingatia uteuzi unaofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwani Tume inateua wagombea ikiwa imesalia siku moja kabla ya kampeni kuanza, inawezekana vipi kwa chama cha siasa kuagiza vifaa bila kuwa na mgombea aliyeteuliwa na Tume. Aidha katazo hili la kisheria halijazingatia ugumu wa kuagiza, kuzalisha na kusafirisha vifaa hivyo kutoka nje ya nchi.

Mapendekezo haya ya marekebisho ya sheria yaende sambasamba na kuboresha Sheria ya uchaguzi wa Madiwani “The Local Government (Elections) Act Ca. 292” kwa sababu uchaguzi huo pia ni muhimu na unafanyika sambasamba na uchaguzi wa Rais na Wabunge.

2.0 UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA ULIOFANYIKA NOVEMBA 2019

Kwa ajili ya kuliunganisha Taifa tunapendekeza uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika tarehe 24 Novemba, 2019 ufutwe na urudiwe chini ya Tume huru ya Uchaguzi baada ya kufanyika kwa marekebisho kama tulivyopendekeza katika sehemu ya kwanza ya barua hii. Hii ni kutokana na sababu kwamba uchaguzi huo kwa ujumla wake ulishindwa kuwapatia wananchi viongozi ambao wamepatikana kidemokrasia kwa sababu ya mapungufu makubwa ya kiusimamizi kama tulivyokuwa tumemuandikia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa umeacha sintofahamu kubwa na mpasuko mkubwa miongoni mwa jamii yetu huko Vijijini na Mitaani. Huku ndipo Umoja na Mshikamano wa Taifa unapozaliwa. Tafadhali fanya maamuzi magumu uliponye Taifa.

Aidha, kufutwa kwa uchaguzi huu kutaonyesha nia yako njema ya kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu unakuwa huru, wa haki na halali.

3.0 TUME YA MARIDHIANO

Kutokana na matatizo mbalimbali ndani ya nchi kwa sasa ni imani yetu kwamba kuna malalamiko mengi kutoka kwa wananchi ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi ili kuliunganisha Taifa. Masuala ambayo kwa sasa tunashauri yafanyiwe kazi na Tume ya Maridhiano itakayoundwa ni pamoja na haya yafuatayo;

Kupotea kwa baadhi ya watu na wengine kuuwawa kikatili na miili yao kuokotwa kwenye fukwe za bahari ya Hindi kwa nyakati tofauti na mpaka sasa hakuna taarifa zozote.

Kufuta kesi zote zenye sura ya kisiasa na zile zinazohusiana na makosa ya uhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha zenye sura ya kisiasa, uonevu na au zinazolenga watu ambao wanaikosoa Serikali kwa mujibu wa Katiba na sheria zetu.

Kufuta makatazo yote ya kisiasa yanayozuia vyama vya siasa kufanya shughuli zake za kisiasa ikiwemo mikutano ya hadhara na maandamano.

Kutafuta muafaka kati ya wananchi na baadhi ya Wakuu wa Wilaya na Mikoa nchini ambao wamekua wakitumia vibaya mamlaka yao ya kuwaweka kizuizini wananchi bila kufuata taratibu, kutoa maagizo mbalimbali kuhusu mali au uwekezaji wa watu binafsi waliofuata misingi ya sheria na au kufukuza Watumushi wa umma bila kuzingatia taratibu na Kanuni za

Utumishi.

Kukamata na kutaifisha mali za wawekezaji nchini bila kufuata taratatibu za kisheria

Uwepo wa mfumo wa kodi ambao sio rafiki kwa wawekezaji na au matumizi mabaya ya madaraka yanayofanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa kusaidiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

Ni matumaini yangu kwamba mapendekezo haya yenye nia njema sana, utayapokea na kuyafanyia kazi kwa msingi wa haraka na dharura kwa ajili ya mustakabali mwema na uendelevu wa nchi yetu.

Kwa heshima na taadhima naomba kuwasilisha.
 
Huyu mkora anajipya gani,biashara ya kula ruzuku na kuuza ngada imebuma?
au ndio wale wa fursa ,baada ya USA na yeye kaona ajitutumue? ujinga kabisa huu
Tutawaletea Moja kwa Moja Mkutano wa Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na Wandishi wa Habari wa Tanzania na wakimataifa Kuhusu Mambo mbalimbali ya Nchi

Updates

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Nimetega duduproof yangu niko chini ya mwembe hapa nataka nifuatilie kwa ukaribu future ya Taifa langu Tanzania ya kweli ijayo sio hii iliyotekwa nyara na hawa Nzige wa CCM.
 
Back
Top Bottom