Fimbo ya Malkia Elizabeth yatua Tanzania kwa siku mbili

IshaLubuva

JF-Expert Member
Dec 4, 2008
250
11
Doris Maliyaga

FIMBO ya Malkia Elizabeth wa Uingereza inayozunguka nchi mbalimbali wanachama wa Jumuia ya Madola imewasili nchini jana kwa ziara ya siku mbili.

Akipokea fimbo hiyo, Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki (TOC), Filbert Bayi alisema ujio wake changamoto kwa taifa kuanzia vyama vya michezo, serikali na wadau mbalimbali kutambua na kuthamini michezo.

Alisema; ''Hii ni changamoto kwetu na hasa ukizingatia ukweli kuwa Tanzania inakabiliwa na michuano hiyo ya Jumuiya ya Madola mwakani ni muda mfupi ambao tumebakiwa nao.

''Ili kufanikisha mashindano hayo ni lazima wadhamini wajitokeze kwa wingi ili kudhamini michezo hiyo kwa kuwa itakuwa changamoto kwa wanamichezo wetu na wahusika wengi kuwapa moyo wachezaji ili warejee na zawadi.

''Lakini, pia vyama vinatakiwa kujiandaa mapema kwa kuwa ni miezi michache tuliyobakiwa nayo kuhakikisha wanaandaa timu zao mapema, sio zikibaki siku chache ndiyo timu zinaanza maandalizi.

''Wachezaji wetu, pia wanatakiwa waonyeshe kiwango kwa kujituma kwa nguvu zao zote kuhakikisha wanaiwakilisha vyema nchini yao,''alisema Bayi.

Wakati huo huo, mkuu wa msafara huo, Kuldeep Banshtua alisema amefurahi kufika Tanzania na hasa mapokezi waliyoyapata walipowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.

Fimbo hiyo ilianzishwa kwa ushirikiano wa nchi za Uingereza na India na ikiwa nchini ujumbe wake utakuwa kwenye hoteli ya Holiday Inn. Leo, fimbo hiyo itapita mitaani kabla ya kwenda Ikulu ambako itakabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete.

Baada ya hapo, fimbo hiyo ya malkia itakuwepo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ili kuwawezesha Watanzania kuishuhudia.

Fimbo hiyo ilipokelewa na viongozi wa vyama mbalimbali vya michezo akiwamo Rais wa TOC, Gulam Rashid, afisa utawala wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Idd Mshangama, balozi wa India nchini, Nguckham Ganglte na mratibu wa mbio hizo nchini, Charles Nyange.

Michezo ya Jumuiya ya Madola inayojumuisha michezo mbalimbali ikiwemo kuogelea, riadha, inatarajiwa kufanyika Desemba jijini New Delhi, India.

Chanzo: Mwananchi


Hivi hiki kifimbo kitatuwezesha kupiga hatua katika medani ya michezo au ndo mauzauza mengine tena? Na kale kafimbo ka Mwalimu vipi?
 
Back
Top Bottom