Fikra zangu juu ya mpira wa Tanzania

Mnyuke Jr

JF-Expert Member
Jul 3, 2021
4,471
6,370
MIMI SIYO “MZALENDO”
Napenda kumshukuru Mungu wangu kwa kunikirimu afya njema bila ya kumfanyia chochote cha maana. Hiyo ndiyo maana kubwa ya neema kwa jinsi ninavyoelewa mimi.

Ahsante sana Mungu wangu kwa neema hii. Naweka msisitizo katika neno “wangu” kwa maana kila mtu ana imani yake juu ya Mungu amuaminiye. Kwa kusema hivyo sitegemei makasiriko wala kukosolewa kokote kuhusiana na imani yangu kwa huyu Mungu wangu.

Ni takribani juma moja limepita sasa toka niwasili katika moja ya majiji makubwa sana duniani; jiji la New York, kwa mapumziko ya kuelekea muhula mwingine kielimu nchini kwetu pale shule zitakapofunguliwa mwanzoni mwa mwezi ujao yaani mwezi wa tisa. Kwa hiyo kama unanitafuta kwa kupiga namba zangu huwezi kunipata na wala kwa sms za kawaida napo huwezi kunipata. Njia pekee ambayo unaweza kunipata ni kwa kupitia fb messenger na whatsapp +255784853280 (siyo muda wote nitakuwa hewani, sina jeuri hiyo. Huwa nadandia tu huduma za WiFi za watu) na kumbuka huku tupo nyuma masaa 7 kwa hiyo mfano ikiwa saa 12 jioni huko ujue huku ni saa 5 asubuhi. Tuachane na hayo maana siyo dhumuni langu kwa leo.

Kuna dhima ya uzalendo ambayo imekuwa ikihubiriwa na watu na viongozi wa kada mbali mbali. Sehemu kubwa ya huo uzalendo sikubaliani nao kwa namna ambavyo unaelezwa. Kwangu mimi ni kama vile unamaanisha uunge mkono kila kitu cha nyumbani mradi kimetolewa na kiongozi wa sekta yoyote ile michezo/ siasa au dini ilimradi ni Mtanzania.

Katika mapumziko haya nimepata fursa ya kutafakari mambo mbali mbali yanayoendelea katika soka letu la nyumbani ambalo limejaa sana msisimko nje ya uwanja kuliko ndani ya uwanja. Ni jambo linalosikitisha lakini linasisimua pia kwa upande fulani na linasaidia kusukuma siku, maisha yenyewe haya magumu sasa kwa nini tuendelee kuyagumisha wakati vilainishi vipo? Siku zote naamini katika kufurahi na kutotilia mkazo sana maisha, ndiyo nilivyo na ndiyo maana kuna vitu vingi ambavyo watu/jamii wanavitegemea toka kwangu na sijavifanya! Ni maisha yangu na simshauri mtu ayaige maana usije ukanilaumu mbele ya safari. Mimi namuamini Mungu wangu kumbuka hilo na amenipitisha katika mengi.

Kabla ya kuendelea ningependa kukufahamisha kuwa mimi ni shabiki wa Yanga nchini na pia ni mwanachama haswa! Lakini kwa nje ni shabiki mkubwa wa Arsenal na kwa mbali Real Madrid. Mkataa kwao ni mtumwa walijisemea waswahili siwezi kusahau kuwa pia ni Kwa timu za taifa mimi muda wote naiunga mkono Taifa Stars na kuishabikia kwa nguvu zangu zote! Ni nchi yangu niliyozaliwa siwezi kuikana hata iweje! Kitovu changu kilizikwa pale Ilala mtaa wa Tabora ingawa makuzi yangu sehemu kubwa yalikuwa Mabibo na wazazi wangu ni wa Urambo. Kwa hiyo Stars ni timu yangu. Kwa nje timu za taifa ninazozipenda namba moja ni Brazili ila kwa Ulaya ni Ureno (Portugal) na kwa Afrka kama Taifa Stars haihusiki basi huwa nashabikia Ghana. Lakini kama USA inacheza dhidi ya timu tofauti na hizo zilizotajwa hapo basi naishabikia USA naachaje kwa mfano wakati ni sehemu ya maisha yangu maana baada ya Tanzania hii ndiyo nchi nimeishi kwa muda mrefu zaidi na marafiki zangu wengi na watu muhimu ni wa taifa hili.

Hebu tuache hilo nisije nikawa nawakwaza baadhi ya watu waliochukua muda wao muhimu kusoma “upuuzi” wangu huu! Nafurahi kwa kuwa timu zimejiimarisha kweli ingawa wasiwasi wangu ni kwamba timu zimeingia gharama kubwa sana kujiandaa lakini sioni kama waamuzi nao watakuwa wamejiandaa kuendana na viwango vitakavyooneshwa na wachezaji. Kama wamejiandaa kuendana na uwekezaji basi litakuwa jambo zuri sana. Waamuzi wengi wana maamuzi ya kidhaifu sana na yanaziumiza timu kubwa kwa ndogo. Inaharibu utamu wa vipaji vinavyokuwepo uwanjani na pia kuleta matokeo yasiyo na haki ndani yake. Sijui ni kiwango chao duni au ni maagizo wanapewa au ndiyo rushwa? Lakini maamuzi hayo pia yanahatarisha afya za wachezaji na kutunyima kushuhudia vipaji vyao kwa kutumia muda mwingi kwenye meza za matibabu kuliko uwanjani. Na hili limekuwa sugu hasa timu za Yanga na Simba zinapokutana na timu nyingine.

Mara nyingi utakuta wale wachezaji wao wanafanyiwa rafu mbaya na za makusudi lakini hakuna hatua zinachukuliwa. Tazama akina Yacouba, Lwanga, Bwalya, Dilunga, Moloka, Chico, Mugalu, Kagere walitumia muda mwingi wakiwa majeruhi kuliko kucheza. Fiston Mayele alikuwa na Mungu wake tu lakini nadhani ndiyo mchezaji aliyewindwa sana kuliko wote. Na hapo kama umefuatilia kwa makini utakuta wengi waliokuwa wahanga ni wachezaji wa kigeni. Hilo si jambo zuri kwa soka letu na wala haiwasaidii wachezaji wetu wazawa.

Nakupa homework fuatilia Yanga au Simba ikiwa inacheza na timu nyingine halafu hao Yanga au Simba wanaongoza kwa magoli mengi; basi utakuta wachezaji wa timu nyingine wanacheza rafu mbaya na marefa wanawachekea tu. Tuache hilo! Mimi siyo mzalendo!

Wote tulikuwa mashahidi ligi ilipokolea kulipotokea mchuano wa kiatu cha dhahabu kati ya Mayele na Mpole! Zilifanyika juhudi za kila namna kuhakikisha Mayele hachukui ingawa ndiyo alistahili na anachukua mzawa! Hata waamuzi wetu nao bahati mbaya waliingia katika dhambi hiyo na kuna waandishi walianzisha mpaka michango kwa ajili ya Mpole. Sijui kama hata zilimfikia huyo Mpole. Tunawaharibu wachezaji wetu na ndiyo maana wanakuwa wazito Kwenda kucheza nje! Waamuzi watende haki kuwasaidia wapambane na kushinda kwa haki! Mimi siyo mzalendo!

Hapa juzi nilipata fursa walau ya kupitia mitandao na kufuatilia kinachoendelea kwenye medani za soka nyumbani. Nimeona jinsi ambavyo matamasha ya vilabu vya Yanga na Simba yalivyofana pale kwa Mkapa. Heshima nyingi sana kwa aliyekuwa mwenyekiti wa Simba SC bw. Hassan Dalali kwa kuja na ubunifu huu wa Simba Day na sisi wananchi tukaamua kukopi na kutengeneza siku yetu; si vibaya kuiga kitu kizuri toka kwa mpinzani wako. Viwanja vilijaa na kupendeza. Ila swali likanijia kichwani huu umati huwa unakuwa wapi pale timu zetu zinapocheza hasa kwenye ligi zaidi ya pale zinapokutana zenyewe kwa zenyewe? Jibu linalonijia ni lile lile kwamba watanzania oooh samahani washabiki wa mpira wa nyumbani tunatilia sana mkazo na kufurahishwa na mambo ya nje ya uwanja kuliko ndani ya uwanja. Sasa sawa tumejaza viwanja je lile tukio lina mchango gani kwenye kuwania makombe? Yaani ingewezekana kwenye mechi inazoshirikisha hizo timu kwenye ligi, Azam confederation wangejitokeza hata nusu ya ule umati ingekuwa nzuri sana. Na hiyo si kwa hao mahasimu wawili tu, subiri uone kama hata hao Singida watapata umati kama ule walioupata zitakapoanza mechi za ligi.

Mpaka Yanga au Simba watakapoenda kucheza huko! Tusubiri muda utaongea! Mimi siyo mzalendo!
Siku chache zilizopita niliona taarifa kutoka kwa mwenyekiti wa TFF ambayo sina uhakika mpaka sasa kuwa ni ya kweli ama la. Nasema hivyo kwa kuwa siamini kama kweli mtu kama yeye mwenye wadhifa mkubwa hivyo kwenye soka letu anaweza kuongea kitu kama hicho! Kukataza watu kupokea timu/vilabu vya nje vinavyokuja kucheza na vilabu vya Tanzania! Real? Kwa nini? Eti uzalendo (patriotism!). Sijui kama alishauriana na viongozi wenzie na kama ni hivyo basi soka letu lipo kwenye mikono hatari sana! Mpira wa vilabu hauna uzalendo hata siku moja na ndiyo maana vilabu vinapokutana nyimbo za taifa hazipigwi! Uzalendo unaingiaje wakati timu zetu zina wachezaji toka mataifa mbalimbali? Lakini pia watanzania hawazuiwi kushabikia vilabu vya nje ya Tanzania! Ningemulewa kama angekataza watu kuzipokea timu za taifa za nchi nyingine zinazokuja kucheza na timu yetu ya taifa lakini napo hapana nisingeunga mkono maana kuna raia wan chi nyingine wanaoishi Tanzania. Hapo mheshimiwa Karia ameteleza. Mimi hata siku moja siwezi kuishabikia Simba ikiwa inacheza na timu yoyote ile labda wakiwa wanacheza na Mbeya City. Hata kama inacheza na timu ya nje. Lakini vile vile sitegemei kumuona shabiki wa Simba anaishabikia Yanga pale inaposhiriki michuano ya kimataifa! Hakuna suala la uzalendo hapo ni ushabiki na utani wa jadi.

Kumbuka Simba akishinda dhidi ya tuseme Kaizer Chiefs mashabiki wake hawatasafiri Kwenda Afrika kusini kuwazomea, watatuzomea sisi. Vivyo hivyo sisi Yanga tukishinda kwa mfano dhidi ya tuseme Highlanders ya Zimbabwe usitegemee mashabiki wa Yanga tutasafiri kwenda Zimbabwe kuwatafuta mashabiki wa Highlanders. La hasha tutawatania walio karibu yetu hata kama hatujacheza nao. Huo ndiyo mpira na huo ndiyo utani wa jadi. Mimi ningependa Yanga inapocheza, Simba wawe mstari wa mbele kuwapokea wapinzani wetu, kuwapa mbinu, na kujaa uwanjani kuwashangilia na kutuzomea Yanga. Ndiyo mpira, tusilete siasa taka kwenye mpira. Waache watu wawe huru kushabikia wanachotaka wasibanwe! Kumbuka maisha yenyewe magumu unataka kuwapangia na jinsi ya kuchagua furaha yao? Kwa mfano wakijitokeza Karia atawafanya nini hao watu? Maana hakuna uvunjifu wowote wa sheria za nchi! Kumbuka mimi siyo mzalendo!

Katika pitapita zangu tena mtandaoni nakutana na tukio la Tundaman kuingia na jeneza siku tamasha la Simba. Watu wamemjia juu kijana wa watu na kumshambulia na kutamani hata kumlaani. Mimi sijaona tatizo kwa kweli kwa Tundaman kufanya vile. Ile ni Sanaa na ubunifu wake. Watu wanalalamika kuwa sijui kaufanya nini ukristo! Jamani hebu tuache kuhamisha hasira zetu binafsi kwa mgongo wa dini. Mazishi ni taratibu tu ambazo zimepangwa duniani na hakuna sehemu kwenye biblia inayoelezea mazishi ya kikristo yafanyike vipi kiasi kwamba hicho kitu kiwe ni kitakatifu. Siku zote tukumbuke kanisa ni la Kristo hakuna mmiliki anayelimiliki kiasi cha kumtaka Tundaman aombe msamaha. Wala sioni umuhimu wa timu ya Simba kuomba msamaha! Hivi kuna watu wangapi wanavaa rozali, wana tattoo za misalaba, wana mikufu ya misalaba na wanafanya mambo ambayo yanakatazwa na Yesu mwenyewe na yameandikwa kwenye biblia? Maskini nasikia mpaka meneja wa uwanja kaondolewa sababu ya tukio hilo! Inasikitisha sana.

Niliwahi kuona siku moja kwenye mieleka ya WWE sijui mwanamieleka gani yule aliingia na jeneza na majoho mbona sikusikia mtu analalamika? Acheni vijana wafanye ubunifu wao. Nilishangaa hata ule wimbo wa Diamond na Zuchu wakaambiwa watoe sijui kipengele cha maudhui ya kanisani! Na Basata nao kweli wakakubali. Na kwenye maigizo je? Hukawii kusikia marufuku kuweka maudhui ya dini. Ningekuwa mimi ndiyo nina sauti kwenye kanisa au kiongozi ningefurahia sana kuwa kumbe hata vijana wa kiislamu wanafuatilia ibada na mambo yetu tunayofanya? Kama Diamond na Zuchu ningeenda na kuwaomba hata watusaidie mifuko ya cement tuna kituo cha watoto tunataka kujenga au labda ningewaomba waje wawanoe kwaya vijana au watoto kuimba hata labda watusaidie kununua majoho au vifaa vya muziki. Au wafadhili watoto yatima hata watano kutoka kanisani na kama vipi unawapiga na neno kwamba wanaonaje wakaingia kabisa kwenye ukristo? Kitu hicho hicho kingeweza kufanyika kwa Tundaman wale vijana naamini kabisa wangefanya mambo makubwa sana kwa kanisa na kama kuna sehemu wamekosea ilikuwa ni kuwaelekeza tu kuwa kitu gani wamekosea na walitakiwa wafanye nini kurekebisha. Yesu ni wa upendo siku zote na anasamehe.

Tuwe na moyo wa upendo kuliko hukumu! Sijui kwa nini nimemkumbuka mr Bean alipoenda kwenye ibada ya harusi kanisani! Nimewaza tu! Mimi siyo mzalendo.
Jicho langu limetupia tena kwingine kuna sakata la Manara na TFF! Shida nini? Manara kafungiwa na TFF kujishughulisha na mpira,yeye kaenda kusherehesha sherehe za tamasha la Yanga! Sijaona kosa mimi hapo. Au TFF siku hizi wanasimamia mpaka ushereheshaji? Au ushereheshaji nao ni mpira? Ningeelewa iwapo chama cha washereheshaji kingewashtaki Yanga kwa kumtumia mshereheshaji ambaye hajasajiliwa na chama chao (iwapo Manara hatambuliki kama mshereheshaji rasmi na chama hicho). Ngoja niishie hapo katika hili.mimi siyo mzalendo!

Naona ngao ya jamii kapewa Sasi awe mwamuzi wa kati. Kwa nilivyomfuatilia mechi kubwa huwa analazimisha sana timu zitoke sare kuna uwezekano na hii akalazimisha sare ili mshindi apatikane kwa matuta! Labda atakuwa kabadilika msimu huu.

Cha mwisho kabisa ningeomba waandishi wa Habari na viongozi kwa jumla pamoja na mashabiki tujitahidi kushika na kutamka majina ya wachezaji au viongozi tukishindwa basi tutumie sifa ya nchi anakotoka mfano Mkenya au Mkongo au Mserbia badala ya neno “Mzungu” huo ni ubaguzi wa rangi. Si jambo jema. Wewe kwa mfano ukaenda kwao halafu wakakuita “Mweusi” utajisikiaje? Mimi siyo mzalendo!
Alamsiki!
 
Cha mwisho kabisa ningeomba waandishi wa Habari na viongozi kwa jumla pamoja na mashabiki tujitahidi kushika na kutamka majina ya wachezaji au viongozi tukishindwa basi tutumie sifa ya nchi anakotoka mfano Mkenya au Mkongo au Mserbia badala ya neno “Mzungu” huo ni ubaguzi wa rangi. Si jambo jema. Wewe kwa mfano ukaenda kwao halafu wakakuita “Mweusi” utajisikiaje? Mimi siyo mzalendo!
Alamsiki!
Hii hulka imeshajengeka Tz na inaota mizizi siku hadi siku, mazingira ya kubaguana sometimes tunayatengeneza wenyewe
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom