Fikra hizi za Msekwa ni dalili ya matatizo yetu ya Katiba | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Fikra hizi za Msekwa ni dalili ya matatizo yetu ya Katiba

Discussion in 'KATIBA Mpya' started by Mzee Mwanakijiji, Feb 7, 2011.

 1. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #1
  Feb 7, 2011
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,360
  Likes Received: 6,377
  Trophy Points: 280
  MAKOSA YA HOJA ZA MSEKWA KUHUSIANA NA KATIBA


  Na. M. M. Mwanakijiji


  Ni vizuri tujitahidi kutenganisha watekelezaji na Katiba. Katiba inaweka tu vyombo vinavyoingiza watekelezaji hao…Hilo la kutenganisha kati ya watendaji waliowekwa na katiba hiyo na katiba yenyewe - Pius Msekwa.


  Naam! Zama hizi ni zama mpya. Ni zama ambazo hata wakongwe wa kisiasa wanaanza kuchanganya maneno na hata fikra zao zinaanza kuonekana zimechanganyikiwa; kiasi cha kutufanya wengine tuanze kujiuliza hawa watu wameweza vipi kuliongoza taifa letu hadi hivi leo. Mzee Msekwa amefanya makosa makubwa ambayo ni muhimu ayasahihishe yeye mwenyewe kwani yakikubaliwa yatarudisha kwenye matatizo yale yale ambayo tunajaribu kuondokana nayo leo hii.


  Nina uhakika wengi ya wasomaji wangu walipata nafasi ya kufuatilia mjadala wa Katiba Mpya uliorushwa na ITV mwishoni mwa juma ambapo Makamu Mwenyekiti wa CCM Bw. Pius Msekwa alikuwa ndiye mzungumzaji mkuu. Nami pia nilifuatilia kipindi chote. Nilijikuta napiga kelele mbele ya luninga langu baada ya kugundua kuwa Mzee Msekwa alikuwa anaeneza fikra potofu kabisa juu ya katiba na utawala. Mwanzoni nilifikiria amezungumza vibaya lakini mara kwa mara alikuwa anarudia kauli moja ambayo kama ndio msimamo wake tangu miaka ya sitini basi naweza kusema kuwa sasa naelewa kwanini tuna matatizo mengi ya Kikatiba! Maana kama yeye ni miongoni mwa watu walioshiriki katika kukusanya maoni ya wananchi kuhusiana na Katiba ya Tanganyika na baadaye ya Muungano basi ndugu zangu, kweli CCM iko matatani.


  Mara kadhaa Mzee Msekwa alikuwa anawaasa wasikilizaji wake kuwa “katiba inaweka vyombo tu, lakini watendaji wakitenda kinyume na katiba hiyo siyo kosa la katiba ni kosa la watendaji”. Alirudi kauli hiyo mara kwa mara kiasi cha kunifanya niamini kabisa kuwa Mzee Msekwa amefungwa katika fikra za miaka ya sitini ambapo Katiba aliiona kama mashine tu ambayo watu wanajiundia na wakishaunda basi inatosha. Kama mashine inafanya kazi au la hilo halimhusu yeye. Mzee Msekwa alitaka wasikilizaji waamini kuwa mara katiba inapoweka vyombo muhimu vya utawala basi inatosha. Ndio maana alijaribu kuelezea kuwa katiba yetu imeweka vyombo mbalimbali na kwa vile imeviweka basi tusiingalie tena bali tuwalaumu watendaji.


  Hivyo, kosa la kwanza alilolifanya mzee Msekwa ni kutokuelewa uhusiano wa Katiba na Watawala. Katiba ni uanisho wa mpango na mfumo wa mahusiano kati ya watawala na watawaliwa. Wengi wanasema ni “mkataba wa kijamii”; nadhani ni zaidi ya “mkataba wa kijamii”. Katiba ni roho inayoshikilia jamii hiyo (nchi) pamoja kwa kuweka bayana yale ambayo watawala wanaweza kufanya na ambayo hawawezi kufanya na nini kitatokea wakifanya kile wasichoweza kufanya. Kwa hiyo, Katiba haiweki tu vyombo halafu ikakaa kimya jinsi vyombo hivyo vinafanya kazi. Katiba haiwezi kuwa kama fundi ambaye analeta kijijini kitu ambacho anasema ni “mashine ya kusaga”. Wote tukaiona, kweli imekaa kama mashine ya kusaga, ikiwe na sehemu zake zote na ikawa imeandikwa juu “mashine ya kusaga”. Ukweli wa mashine hauji katika kusoma kile ambacho mashine inaweza kufanya. Njia pekee ya kujua kama kweli hii ni mashine ya kusaga, ni kuweka nafaka na kuiwasha kuona kama inasaga.
  Sasa kweli nafaka zinaweza kuingizwa zikazungushwa na kutokea upande wa pili lakini watu wanachotaka kuona ni unga na siyo nafaka zisizosagwa. Kama ilikuwa ni mashine ya kukoboa basi watu wanataka kuona nafaka imekobolewa. Sasa mashine isiposaga au kukoboa hatuwezi kuwalaumu waendesha mashine hao na kusema kuwa ni kosa lao. Ndio maana huitwa mafundi kuangalia mashine ina matatizo gani, na kama mashine imepitwa na wakati - kwa mfano kuna mashine zinazosaga na kukuboa vizuri zaidi, kwa haraka zaidi na kutumia nishati pungufu zaidi kwanini watu wang’ang’anie mashine ambayo inabidi uache nafaka yako hadi kesho uje kufuata!? Hasa kama kwenye kijiji kingine watu wanasikia kuna mashine mpya ambayo wenzao kule wanaifurahia.


  Katiba ni zaidi ya mashine, ni mfumo mzima wa mahusiano kati ya wananchi na viongozi, kati ya viongozi na viongozi, kati ya wananchi na wananchi, kati ya vyombo mbalimbali vya nchi n.k Sasa inatakiwa kimsingi kabisa iwe inayoanisha vizuri na bayana nani ana nguvu gani, nani anatakiwa kufanya nini, nini kisipofanywa au kikifanywa kinatokea nini. Sasa, Katiba haiweki tu vyombo au haisemi “fulani ateuliwa” halafu ikae kimya mtu yule aliyeteuliwa anapovurunda! Ndio maana Katiba imeweka hata utaratibu wa kumuondoa madarakani Rais, Waziri Mkuu n.k Kwa hiyo, hatuwezi kabisa kutenganisha Katiba na Watendaji wanaotokana na Katiba hiyo.


  Kosa la Pili ambalo nalo ni kubwa ambalo Mzee Msekwa alilifanya ni katika kuzungumzia (na linatokana na hilo la kwanza) na kushindwa kuelezea uhusiano wa Katiba na Sheria za Nchi. Mara kwa mara tunawasikia watu wanasema “Katiba ndio sheria mama” wakimaanisha kwamba sheria nyingine zote zinatokana na Katiba hiyo. Sasa sheria za nchi zinazotungwa na Bunge ni lazima zipatane au niseme zikubaliane na katiba. Katiba basi ndicho kiwango cha juu kabisa cha sheria nchini na sheria yoyote inayopingana na Katika au sehemu ya sheria yoyote inayopingana na katiba basi inakuwa imekosewa. Sasa ni muhimu kwa watu kutambua uhusiano huu mkuu kati ya Katiba na Sheria.


  Sasa kama chombo, mtu, mbunge au kiongozi yoyote au mtu yeyote akisema au kufanya jambo ambalo linapingana na Katiba mtu au chombo hicho kina makosa. Hivyo, Katiba ni lazima iwe wazi kabisa juu ya nini kinaweza kufanywa au sheria gani inaweza kutungwa kwani ikikaa kimya basi watu wanaweza kujiandikia sheria zenye madudu kama tulizo nazo leo hii. Nitatoa mfano kwa kutumia Katiba ya Marekani. Mabadiliko ya kwanza ya Katiba ya Marekani yalikataza mambo mbalimbali mojawapo ni kukataza Bunge la nchi hiyo kutunga sheria yoyote itakayerasmisha dini fulani au kukataza watu wasifuate dini fulani. Kutokana na kipengele hicho Wamarekani hawana dini rasmi na hawawezi kuja na sheria inayoonesha kwa namna yoyote upendeleo wa dini fulani. Kwa hiyo kile ambacho Katiba inakataza hakifanywi. Kumbe basi sheria zinazosimamia watendaji mbalimbali zitafanya kile ambacho Katiba inataka au haitaki. Kwa mfano, Katiba yetu inasema kutakuwa na tume ya Uchaguzi itakayoongozwa na mtu mwenye sifa ya ujaji atakayeteuliwa na rais. Matokeo yake ndivyo ilivyo; lakini Katiba ikisema kutakuwa na tume ya uchaguzi ambaye mkuu wake atakuwa ni jaji atakayeteuliwa na Rais na kuidhinishwa na Bunge maana yake ndivyo itakavyokuwa.


  Kosa la tatu la mzee Msekwa kwenye hoja yake linatokana na kile alichokisema kuwa sababu ambazo zinaweza kusababisha watu kutaka kuwa na katiba mpya. Alitoa sababu mbili ya kwanza alisema pale ambapo utawala unabadilishwa (change of sovereignty) na sababu ya pili alisema kuwa ni tawala zinapounganishwa (merger of sovereignty). Sovereignty ni ile asili ya madaraka ya kutawala. Wafalme wanaitwa “sovereign” kwa maana ya kwamba asili a madaraka yote katika nchi yanatoka kwa mfalme; na jamii zinazoamini utawala wa Mungu wanaamini kuwa Mungu ndiye Asili Kamili ya Madaraka (Absolute Sovereign). Sasa sababu zile mbili za kubadilisha katiba zinazungumzia - asili ya madaraka zinapobadilishwa (kutoka kwa mfalme kwenda kwa jamhuri) au pale nchi mbili zenye madaraka kamili ya kujitawala zinapoungana.


  Lakini kuna sababu ya tatu ambayo inayoweza kusababisha kuandikwa kwa katiba mpya na ambayo ninaamini inatosha kabisa kwa Watanzania kuisimamia. Katiba yetu ya sasa inasema wazi kuwa “wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii” (Ibara ya 8.1a) Wananchi ndio msingi mzima wa madaraka yote; kwa maneno mengine asili ya madaraka (sovereignty) katika taifa letu iko na inabakia daima mikononi mwa wananchi. Hii ina maana gani? Maana yake kubwa ni kwamba wananchi wakiamua kutaka kubadilisha Katiba yao hawahitaji kibali cha Rais au serikali kwa sababu wao (wananchi) ndio asili ya madaraka. Wananchi ndio wanaoamua kama Katiba ya sasa inawafaa au wanataka kubadilisha. Kumbe basi sababu ya tatu inayoweza kusababisha Katiba mpya iandikwe ni maamuzi ya wananchi wenyewe kuona kuwa wanahitaji Katiba mpya kukidhi mahitaji yao ya sasa. Naamini kwa Tanzania hii ndio sababu kubwa naamini pasipo kutambua haki hii ya wananchi tutakiachia chama kimoja kuamua hatima ya taifa. Hili linatuleta kwenye kosa la mwisho la mzee Msekwa (yapo mengine nimeyaacha kwa wakati huu). Hili ni kushindwa kwa mzee Msekwa kuonesha uzito wa haja ya kuwa na Katiba Mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015. Mimi na wengine ambao tunaamini Katiba Mpya ni lazima iwepo kabla ya 2015 tunafanya hivyo kwa sababu tunajua kama taifa hatuwezi kwenda kwenye uchaguzi mkuu ujao chini ya Katiba hii ya sasa. Kama kwa miaka hamsini iliyopita tumekuwa na katiba ya sasa na ikiwa na mabadiliko mengi na malalamishi lukuki kwanini tuanze nusu karne ijayo na katiba hii hii. Kama kuna zawadi tunaweza kuwaachia watoto wetu wanaozaliwa mwaka huu (ambao miaka hamsini ijao ndio watakuwa watu wa wazima) basi ni zawadi ya katiba nzuri kabisa ambao inaona mbali.


  Hivyo, leo hii hatuna tena mjadala wa Katiba Mpya kwani hilo tumeshalimaliza. Sasa swali lililoko mbele yetu ni jinsi gani tuandike katiba hiyo, tuweke muda gani wa kukamilisha hatua gani na kwa vipi. Jambo kubwa la msingi kuanzia sasa ni kuweka mfumo utakaohakikisha tunakuwa na Katiba mpya kabla ya uchaguzi wa 2015 na binafsi nikiamini kuwa Kura ya Maoni ya Katiba Mpya ipigwe kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa 2014 ili kuanza kuona Katiba Mpya ikianza kufanya kazi mapema wakati huo. Katika hili sikubaliani na wale wanaosema ati tusiharakishe kuwa na Katiba Mpya; hatufanyi haraka lakini vile vile hatutakiwi kuchelewa. Tumeona Sudani ya Kusini waliamua kuwa na kura ya maoni miaka mitano iliyopita na sasa wamefanya hivyo. Na sisi ukiondoa suala la Katiba Mpya ninaamini ni lazima tuamue mojawapo ya masuala mazito ya Katiba yetu nalo ni suala la Zanzibar. Tayari watawala wetu wa sasa wameweka msingi wa Zanzibar kujitoa kwenye Muungano kwa hiyo ninaamini ni lazima tufikirie jinsi gani Zanzibar kama inataka kutoka kwenye Muungano itoke vipi. Nitazungumza zaidi hili siku nyingine zijazo lakini siamini kabisa kuwa tunaweza kutoka serikali mbili na kuwa serikali tatu na tukabakia kuwa kama Taifa. Ninaamini kama Baba wa Taifa alivyoamini mwelekeo ni kutoka serikali mbili kwenda serikali moja. Hapa ndio tutaona kuwa mjadala wa katiba basi ni mpana na unahitaji ratiba ya mambo ya kufanya ili hatimaye tuweze kuishi katika taifa ambalo sote tunalitaka.


  Lakini tukiwa na watu wenye mawazo ambayo ni kinyume kabisa na maslahi ya katiba mpya na wao ndio waliaminiwa kuwa wanauelewa wa Katiba tutaweza kweli kuwa na Katiba tunayoitaka. Kama hoja za mzee Msekwa zinakubaliwa na wana CCM wengi ina maana tunakazi kubwa kwanza ya kuwaelewesha wana CCM kwanza kuliko wananchi wengine. Maana hawa wasipoelewa watakuwa ni kikwazo cha matamanio ya Watanzania. Kizazi Kipya, Katiba Mpya kwa Taifa Jipya!


  Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com
   
Loading...